Saturday, March 27, 2010

Hii ni Saa ya Ufufuo na Uzima duniani kote!

Neno la Mungu katika kitabu cha Isaya 42: 22 linasema “ lakini watu hawa ni watu walioibiwa na kutekwa; wote wamenaswa katika mashimo, wamefichwa katika magereza; wamekuwa mawindo, wala hapana aokoaye; wamekuwa mateka wala hapana asemaye Rudisha.
Wapo watu wengi wamekufa katika mazingira ya kutatanisha huku ndugu zao, jamaa na marafiki wakadhania kuwa wamekufa kifo kilichopangwa na Mungu, wakidhani kuwa BWANA ametoa na BWANA ametwaa kumbe shetani kupitia washirika wake ndio waliotwaa. Ni kweli kuwa watu wote wamepangiwa muda wao wa kuishi duniani na muda unapofika hufa kifo cha ukweli. Hili halibishaniwi kibiblia, uu mavumbi wewe na mavumbini utarudi lakini iwe kwa mpango wa Mungu na sio mpango wa shetani akiwatumia wanadamu wachache waliojitoa kumtumikia shetani na ufalme wake wa giza ambao ni wachawi, waganga wa kienyeji, wasoma nyota au watabiri wa mambo ya nyota. Lakini wachawi, wafuga majini, wasoma nyota na waganga wa kienyeji hali wakimtumikia shetani ambaye ni muongo na baba wa huo, wamekuwa wakifanya mauzauza na kuua watu kwa kutumia nguvu za kishetani na kuwachukua watu hao kwenda misukuleni katika mashamba, katika mashimo, katika magereza ya kiroho, katika mapango na watu hao wamekuwa mawindo, wala hapana aokoaye; wamekuwa mateka wala hapana asemaye Rudisha. Lakini Yesu Kristo tunayemtumikia ameaumua kuwarudisha watu hao kutoka katika magereza na vifungo.

Yesu ndiye ufufuo na Uzima yeye anasema katika neno lake juu ya ufufuo wa Lazaro aliyekufa, akizikwa na kukaa kaburini muda wa siku nne na hatimaye kufufuliwa na Yesu “ Basi Yesu alipofika, alimkuta amekwisha kuwamo kaburini yapata siku nne. Na Bethania ilikuwa karibu na Yerusalemu, kadiri ya maili mbili hivi; na watu wengi katika Wayahudi walikuwa wamekuja kwa Martha na Mariamu ili kuwafariji kwa habari ya ndugu yao. Basi Martha aliposikia kwamba Yesu amekuja, alikwenda kumlaki na mariamu alikuwa akikaa nyumbani. Basi Martha akamwambia Yesu, Bwana, kama ungalikuwapo hapa ndugu yangu hangalikufa. Lakini hata sasa najua ya kuwa yoyote utakayomwomba Mungu, Mungu atakupa. Yesu akamwambia ndugu yako atafufuka. Martha akamwambia Najua ya kuwa atafufuka katika ufufuo siku ya mwisho. Yesu akamwambia Mimi ndimi huo Ufufuo na Uzima. Yeye aniaminiye mimi ajapokufa atakuwa anaishi(Yohana 11: 17-25).

Katika kizazi hiki kama ilivyo kawaida ya Mungu kuwapaka mafuta watumishi wake kwa wito na kazi mbalimbali za huduma; lakini kila mmoja wetu alipewa neema kwa kadiri ya kipimo cha kipawa chake Kristo: Naye alitoa wengine kuwa mitume na wengine kuwa manabii na wengine kuwa wainjilisti na wengine kuwa wachungaji na waalimu; kwa kusudi la kuwakamilisha watakatifu, hata kazi ya huduma itendeke, hata mwili wa Kristo ujengwe(Waefeso 4:7,11) ndivyo ambavyo Mungu pia hajatupungukia na katika kizazi cha ulimwengu huu wa leo chenye shingo ngumu, kizazi kilichojaa maovu, kizazi jeuri, Yesu Kristo Mungu tunayemtumikia amempaka mafuta kuhani wake, mtumishi wa Mungu, mtu wa vita tangu ujana wake Mchungaji Kiongozi Josephat Gwajima katika kuongoza mapambano ya kuzivunjavunja na kuzisambaratisha kambi zote za misukule na kuwarudisha wote waliokufa na kuchukuliwa misukule katika mazingira ya kutatanisha na kuitangazia kuzimu na mamlaka zake zote kuwa hii ni Saa ya Ufufuo na Uzima na ulimwengu wote ujue kuwa ile saa aliyoisema Yesu kuwa Amin, amin nawaambia Saa inakua na saa ipo, wafu watakapoisikia sauti ya mwana wa Mungu, na wale watakoisikia watakuwa hai (Yohana 5: 25) Hii ni saa ya ufufuo na Uzima duniani na Mungu wetu ajitwalie Utukufu sifa na heshima! Na itambulikane duniani kote kuwa hii ni saa ya Ufufo na Uzima!

Wednesday, March 17, 2010

Misukule warudishwa “fresh from Shamba”


Mmoja wa misukule fresh from shamba Mohamedi Mustapha, akioneshwa mbele ya maelfu ya watu na Mchungaji Josephat Gwajima katika ibada ya ijumaa ndani ya nyumba ya ufufuo na uzima.


Takribani wiki mbili zilizpopita Mchungaji kiongozi Josephat Gwajima wa Kanisa la Glory of Christ (T) Church maarufu kama “nyumba ya Ufufuo na Uzima” aliahidi kuwarudisha na hatimaye kulionesha kanisa misukule wakiwa katika hali yao ya kimsukule akitumia msemo wenye mchanganyiko wa lugha ya kiingereza na Kiswahili “misukule fresh from shamba” ili kuweka msisitizo kuwa misukule hao wamerudishwa kwa nguvu na uweza wa jina la Yesu.
Maelfu ya watu katika nyumba ya Ufufuo na Uzima wakiwa katika bonde la kukata maneno kwa mfululizo wa siku tatu, jumatatu, jumatano na ijumaa za tarehe 8, 10 na 12 mwezi Machi 2010 walipata fursa ya kuwashuhudia misukule waliorudishwa kutoka kwa wachawi waliokuwa wakiwashikilia.
Misukule hao waliokuwa wamekatwa ulimi kipindi walipokuwa msukuleni huku watu wakidhania kuwa hawataweza kuongea tena ila BWANA Yesu aliwaponya na mara baada ya kufanyiwa maombezi misukule hao walianza kuongea na kuelezea kwa kina ni nani aliyewachukua, chakula walichokuwa wakila na mahali walipokuwa wakitumikishwa waliopokuwa misukule. Watu hao waliorudishwa kutoka msukuleni ni pamoja na Jeremiah, Charles Nduru na Mohamedi Mustapha.

Bibi Kizee mchawi atunguliwa na makombora ya Ufufuo na Uzima


Bibi kizee mchwawi aliyedondoshwa na makombora ya kiroho yenye nguvu na uweza wa Yesu katika Nyumba ya Ufufuo na Uzima akihojiwa na Mchungaji Kiongozi, Josephat Gwajima, mara baada ya kudondoka. Bibi huyo alidai kuwa yeye hakwenda kuwanga hapo kanisani isipokuwa alikuwa akipita katika anga la mahali hapo kwenda kuwanga sehemu nyingine lakini akajikuta akipatwa na ajali na kudondokea ndani ya kanisa hilo. Siku iliyofuata bibi huyo aliamua kuleta zana zake za kazi ili zichomwe moto na yeye ampatie Yesu maisha yake, au kwa kifupi aokoke na kuacha kazi za kichawi na unganga wa kienyeji.