Saturday, March 10, 2012

Maelfu wajazwa Roho Mtakatifu katika kilele cha Semina ya Bonde la Baraka

Maelfu wa watu leo katika Nyumba ya Ufufuo na Uzima iliyopo Kawe, Tanganyika packers wamejazwa Roho Mtakatifu katika semina maalumu ya Kufunga na Kuomba iliyoanza Machi 7 mwaka huu na kuisha Machi 10 ikiongozwa na Mpakwa mafuta wa BWANA Mchungaji Kiongozi Josephat Gwajima. Ibada hiyo ilikuwa kilele cha semina ya maombi maalumu ya kufunga na kuomba yaliyochukua muda wa siku nne, ibada inakadiriwa kuhudhuriwa na watu zaidi ya elfu 40 kwa mara moja!

Akihubiri na kufundisha neno la uzima, Mch. Josephat Gwajima alisema kuwa baada ya mfungo huo, tutarajie kuingia katika bonde la Baraka (Tekoa) sawa sawa na neno la BWANA alilonena katika kitabu cha mambo ya 2 Nyakati 20: 26 " Hata baada ya siku nne wakakusanyika katika bonde la Baraka; maana ndipo walipomkaribia BWANA; kwa hiyo jina lake mahali pale pakaitwa Bonde la Baraka hata leo"

Hivyo ibada ya kesho asubuhi Jumapili Machi 11, 2012 ni ibada ya Kuchota Baraka katika Bonde la Baraka hapa Tanganyika packers, kawe baada ya kufunga na kumwomba BWANA siku nne mfululizo bila kukoma.