Sunday, September 23, 2012

UJUMBE: NYOTA KIBIBLIA

Mchungaji Kiongozi: Josephat Gwajima 23.9.2012

UTANGULIZI:
Huu ni mwendelezo wa somo la Nyota na Maisha mtu aliyonayo. Mathayo 2:1; Kama tulivyoona tangu mwanzo kuwa nyota ni kipawa, uweza, hatma au hali ya mtu ya baadaye. Tukaona nyota ya Yesu ilionekana kabla Yesu hajazaliwa na mamajusi wa mashariki walimwona kama Mfalme.

MAANA YA NYOTA:
Kama tulivyooa sehemu ya kwanza kuwa nyota ni kiashiria cha rohoni, kinachoonesha mtu atakuwa nani baadaye, mafanikio ya mtu au hatma ya mtu. Viashiria hivi ndivyo vinavyoitwa nyota.

NYOTA KATIKA BIBLIA:
Hesabu 24:14-17 Baraki alikuwa mfalme, na alipoona kuwa wanaisrael wanakuja ili kushambulia ufalme wake, akamtafuta Balaam amtabirie. Hayo ni maneno ya Balaamu aliyoona, Hivyo Balaamu alipoangalia taifa la Israel akaona nyota, kimsingi nyota ya mtu inaonyesha jinsi mtu atakavyokuwa baadaye. Hivyo balaamu aliweza kumuona Yesu tangu mwanzo na ndio maana mamajusi wa mashariki nao pia walimwona Yesu kama nyota.

Nyota yaweza kuonyesha kusudi la maisha ya mtu, na ndio maana ingawa Suleimani alizaliwa na mke wa Huria ambaye Daudi alimuua mumewe ili ampate lakini kwasababu nyota ya kujenga hekalu ilikuwa juu yake (yaani Suleimani), Mungu alimchagua kujenga Hekalu. Daudi alikuwa na watoto wengine wengi, lakini aliyechaguliwa kujenga ni Suleimani kwasababu ndio mwenye nyota ya kujenga yaani tangu anazaliwa

Isaya 47:8-12; Hapa biblia inataja neno “wajuao Falaki”, hii ni elimu inayohusu mambo ya nyota ambayo wachawi husoma. Katika Mathayo 2:1- Biblia inataja mamajusi, wao ni wasomaji wa nyota ambao waliiona nyota ya Yesu kabla ya Yesu hajazaliwa. Nyota ya Yesu iliwafanya mamajusi kumfuata kutoka mbali, na wakati huohuo Herode alifadhaika. Kumbe nyota ya mtu ikionekana watu wanaweza kuifuata na kukuletea unalohitaji. Watu wengi wapo katika vifungo mbalimbali kwasababu nyota zao zimefunikwa.

MAMBO 15 AMBAYO UTAYAONA KAMA NYOTA YA MTU HAIPO:
·        Umahiri na utendaji kazi wa mtu hauonekani; kama mtu hana nyota ule umahiri wa wake na utendaji kazi hauwezi kuonekana. Hata ajitahidi kufanya kazi kwa bidii umahiri hawezi kuonekana.

·        Hawezi kuwa mbunifu katika maisha; nyota huleta ubunifu sasa kama haipo basi ubunifu wa mtu hautaonekana. Mtu huyo atakuwa anashindwa kubuni kitu cha kufanya ili kupata mafanikipo katika maisha.

·        Hawezi kufanya kazi zake kwa ufanisi; nyota huleta ufanisi katika kazi, mtu akikosa nyota basi ule ufanisi wake hauwezi kuonekana, mtu huyo atakosa ufanisi katika kazi zake.

·        Hukosa mvuto; nyota huleta mvuto hivyo mtu nyota yake haipo, anakuwa anakosa mvuto hata wa watu kuomuona tena.

·        Hukosa kibali; nyota humfanya mtu awe na kibali hivyo mtu anapochukua nyota, kimsingi anakuwa amechukua kibali chako.

·        Huwezi kusikilizwa katika jamii; kwasababu nyota huleta kusikilizwa, mtu akichukuliwa nyota hawezi kusikilizwa katika jamii.

·        Hawezi kuthubutu;

·        Anakosa uthubutu wa kutenda;

·        Anakosa ujasiri wa kusema; mtu akikosa nyota anakosa ujasiri wa kusema.

·        Anakosa uthubutu wa kutoa maamuzi magumu; mafanikio ya mtu ni matokeo ya maamuzi magumu aliyowahi kuyafanya.

·        Anakosa ujasiri wa kudai unachojua ni kweli;

·        Huwezi kutumia hata kile ulichonacho; ndio maana ya lile andiko utajenga nyumba na mtu mwingine atalala ndani yake”.

·        Anakuwa na matatizo;

·        Anakuwa na hofu ya kutenda mapenzi ya Mungu; nyota ikichukuliwa mtu aweza kuwa na hofu ya yajayo, yaliyopo au yaliyopita.

·        Kukosa uaminifu kwenye mambo ya Mungu.

Kwahiyo wachawi au waganga wanapochukua nyota yako kimsingi, mambo hayo yanakuwa hayapo kwenye maisha yako.

JINSI WACHAWI WANAVYOCHUKUA NYOTA NA MATUMIZI YAKE:
Utajiuliza ni wakina nani wenye uwezo wa kuiona nyota; biblia inathibitisha kuwa waganga na wachawi wana uwezo wa kuiona nyota na kuifuata. Na kama nyota haina ulinzi wa Mungu waganga wanaweza kuichukua nyota. Kuna watu wanadhania kuwa uchawi haupo na kutokujali uwepo wake, lakini uchawi upo kwasababu biblia imetaja kuwa uchawi upo.

Wanachuaje; kwasababu wachawi wanaweza kuiona nyota ya mtu na kuifuata, hivyo wakigundua kuwa nyota ni nzuri wanaweza kuichukua na kumuuzia mtu mwingine; na ndio maana mtu anaweza kuzaliwa nyota ya uongozi, ujasiri, upendeleo, ubunifu au kupata kibali mbele za watu, alafu ikachukuliwa na kupewa mtu mwingine. Na ndio maana kuna watu ni matajiri kwasababu ya nyota za watu; na wakati huohuo mtu Yule ambaye nyota yake oimechukuliwa anaanza kuwa na matatizo; kile kibali au upendeleo aliokuwa nao awali hawezi kuwa nao tena.

Mtu aliyechukuliwa nyota; anakuwa na mafanikio mwanzoni lakini ghafla yanabadilika baada ya kuchukuliwa nyota. Kimsingi; Mungu akikupa kutu huwa kinadumu lakini kama maisha ya mtu yanaashiriwa na nyota pale nyota inapochukuliwa mtu huyo upendeleo wake unaanza kuondoka. Rudisha nyota yako kwa Jina la Yesu.

Maombi ya kuamuru aliyechukua Nyota yako arudishe:
Baba katika Jina la Yesu leo nimetambua kuwa nina nyota, nayo yaweza kuchuliwa na kunitia katika matatizo; hivyo ninaamuru ila aliyechukua nyota yangu arudishe katika Jina la Yesu. NInapokonya nyota yangu iliyochukuliwa katika Jina la Yesu, naamuru mahali popote ilipowekwa na kutumika ninaamuru irudi kuanzia sasa katika Jina la Yesu.

Ninaamuru umahiri wangu, ufanisi, uwezo wangu wa kutenda na uwezo wa kuthubutu ninaurudisha katika Jina la Yesu. Ninaamuru kibali, afya, ujasiri na mvuto wangu urudi katika Jina la Yesu; nataka nyota yangu katika Jina la Yesu.

UFUFUO NA UZIMA {THE GLORY OF CHRIST (T) CHURCH}
TANGANYIKA PACKERS,
KAWE, DAR ES SALAAM.

Sunday, September 16, 2012

NYOTA YA MTU NA MAISHA ALIYONAYO

Na Mchungaji Josephat Gwajima 16.9.2012

Utangulizi:
Biblia imeeleza kuhusu nyota ya Yesu ilivyoonekana  kutoka mashariki,(Mathayo2:1); Hii inadhihirisha wazi kuwa kila mtu ana nyota yake. Hivyo katika mfulilizo wa somo hili tutaona maana ya nyota, kazi ya nyota, nyota yaweza kufunikwa kichawi, madhara ya kuishi bila nyota, dalili za kuchukuliwa nyota, nyota yaweza kurudishwa na namna ya kutambua nyota yako. Hapa hatuzungumzii kuhusu kusoma nyota au utabiri wa nyota bali tunaangalia nyota kama ilivyo katika Biblia.

MAANA YA NYOTA:
Nyota katika Biblia inawakilisha kipawa, hatma ya mtu, lengo lililomfanya Mungu akulete  hapa duniani na kusudi lako la maisha. Hivyo tunaposema nyota yako ipo au imechukuliwa maana yake hayo mambo yamechukuliwa au yapo. Kimsingi hakuna mtu asiye na maana tangu kuzaliwa kwake, kwasababu kila mtu aliye duniani amekuja kwa kusudi lake.
Kuna tofauti kati ya elimu na nyota; elimu sio nyota lakini elimu yaweza kunoa nyota. Na si kwamba kujifunza kunaleta nyota bali nyota ipo kwa wote lakini elimu inainoa nyota; na ndio maana ni rahisi kumwona mtu hana elimu lakini anamafanikio mahali fulani. Ukisoma Mhubiri 9:11 Biblia inasema wakati na bahati huwapata wote na sio swala la elimu au ujuzi tu.

KAZI YA NYOTA:
 •        Nyota humfanya mtu kuwa mahiri katika utendaji kazi wake. (Effectiveness)
 •        Nyota huleta ubunifu katika maisha ya kila siku (Creativity)
 •        Nyota inamfanya mtu anatenda kwa ufanisi (Efficiency)
 •        Nyota huleta mvuto kwa watu kutoka mbali ili kuleta vitu kwa ajili yako. (Attraction)
 •      Nyota humfanya mtu awe na maisha yenye mwelekeo na kibali mbele za watu. (Acceptance  and Favor)
 •        Nyota humfanya mtu kusikilizwa katika jamii.
Kuna vitu ambavyo mtu anaweza kuvipata kwasababu nyota yake imeonekana. Nyota yaweza kuvuta zawadi yaani vile vitu ambavyo hujavitaabikia, na ndio maana Yesu alipokuwa mdogo aliletewa zawadi na mamajusi wa mashariki. (Mathayo 2:11) kwahiyo nyota ikichukuliwa maana sahihi ni kwamba hayo mambo hapo juu yote hayapo.
Mathayo 2:1-2; Wakati Yesu anazaliwa kulikuwa na watu wanaitwa mamajusi, ambao walikuwa na uwezo wa kusoma nyota. Hivyo katika ulimwengu wa roho waweza kuona watawala wajao, maisha yajayo au yale yatarajiwayo.  Na ndio maana Mamajusi wa mashariki ya mbali waliweza kuifuata nyota ya Yesu.
Nyota inapoonekana inaweza kufuatwa, yaani watu waona zile kazi zake na kumfuata mtu. Kimsingi tunaposema mtu hana nyota maana yake umahiri, ufanisi na kibali vimechukuliwa. Lakini nyota ikionekana  maana yake haya mambo yote yamerudishwa na hapo utamwona mtu anafanikiwa hata kama elimu yake sio kubwa.

NYOTA ILIYOCHUKULIWA/ ILIYOFUNIKWA KICHAWI:
Nyota ikifunikwa au kuchukuliwa kichawi maana yake mvuto, umahiri, ufanisi na uwezo unakuwa umechukuliwa au umefunikwa. Na ndio maana kuna watu wanahangaika kuanzisha kampuni, kujenga nyumba, kulima, au kufanya biashara kama nyota imefunikwa au kuchukuliwa kichawi huwezi kupokea mafanikio ya sahihi kwenye maisha. Watu wengi wanahangaika kuonekana au kukubalika lakini kumbe tatizo lipo kwenye nyota yaani imefunikwa au imechukuliwa kichawi.
Wachawi wanaweza kuona nyota ya mtu na kuifunika ili isionekane; na kwa namna hii watu wengi wanaonekana hawana mafanikio katika maisha kumbe nyota zao zimefunikwa. Hivyo ni muhimu kupambana Kwa Jina la Yesu ili nyota yako ionekane.

MADHARA YA KUISHI BILA NYOTA YAKO:
 •   Kwa kuwa nyota ndiyo inamwezesha mtu kuwa na kila kitu, ndio kusudi la mtu, upendeleo wa mtu; hivyo madhara ya kutokuwa na nyota ni kutokuwa navyo vyote vile.
 •   Siku zote unakuwa unatenda chini ya kiwango (Under performance). Na kwa namna hiyo hakuna mtu anakubali kile unachotenda; yaani elimu na maarifa yote yakuwa chini ya kiwango.
 •   Utapata na kuibiwa; unapata kazi baadaye unaibiwa au unapata mchumba baadaye anaibiwa. Kimsingi huwezi kudumu na haya mambo.
 •   Unapata lakini anatumia mtu mwingine.

DALILI ZA NYOTA ILIYOFUNIKWA:.
 •   Maisha kukosa mwelekeo; mtu akikosa nyota hata kama akiwa na elimu kama nyota haipo lazima mtu huyo atakosa mwelekeo.
 •   Kukwama kibiashara na kuishi maisha kwenye madeni.
 •   Unafanya kazi lakini hupati maendeleo. Yaani mtu anapata mshahara mzuri lakini anakosa mafanikio halisi kwasababu ya nyota iliyofunikwa au kuibiwa.
 •   Wewe ni kiongozi lakini jamii haikutambui.
 •   Ukichangia hoja za mijadala mbalimbali hakuna anayekusikiliza.
 •   Umesoma lakini hupati kazi, na ukipata kazi haiendani na elimu yako
 •   Maisha ya upweke na hakuna anayekujali katika familia.
 •   Unatenda kazi kwa bidii lakini hupandi cheo.
 •   Kama ni binti  sifa zote lakini hakuna anayekuchumbia maana huonekani.
 •   Kuandamwa na mabalaa na mikosi.
 •   Kupotelewa na watu wa muhimu
NYOTA YAWEZA KURUDISHWA:
Hatua ya kwanza kama hujaokoka unatakiwa kuokoka; kuokoka ni kumpokea Yesu awe Bwana na Mwokozi wa maisha yako ili upate uwezo wa kushindana, hivyo ukigundua nyota imechukiliwa unatakiwa umpokee Yesu ndani ya moyo wako. Ni kitu cha kushangaza kuhitaji msaada wa Yesu halafu yeye humtaki kimsingi kuokoka ni hatua ya kwanza ya kurudisha nyota.
Hatua ya pili ni kushindana kwa maombi; kama mtu anayetaka kurudisha nyota yake ni lazima achukue hatua  ya kushindana katika maombi. Hivyo baada ya kuokoka hatua inayofuata ni kushindana ili nyota irudi. Nyota yaweza kurudishwa kwa kuomba katika Jina la Yesu Kristo.

UTAJUAJE NYOTA YAKO NI IPI:
Usithubutu kwenda kwa mganga wa kienyeji au kusoma kwenye magazeti ili kujua nyota yako.  Ni muhimu kujua kilichoibiwa ni kipi katika maisha yako. Isaya 47:13Umechoka kwa wingi wa mashauri yako; basi, na wasimame hao wajuao falaki, wazitazamao nyota, watabirio kila mwezi mambo ya mwezi huo, wakakuokoe na mambo yatakayokupata.FALAKI ni elimu juu ya mambo ya nyota; biblia inataja kuwa kuna watu wanaojishughulisha na usomaji wa nyota. Lakini kuna mambo kadhaa yanayoweza kukuonyesha nyota yako ni ipi:-
Moyo wako, akili zako na mawazo yako yanakuwa katika hilo jambo AMBALO NI NYOTA YAKO. Mfano kama nyota yako ni biashara basi utakuta moyo wako upo kwenye biashara, basi lazima nyota yako ni k biashara. Kama nyota ni kuimba au siasa lazima moyo utakupeleka kwenye kuimba na siasa. Hivyo tambua kuwa kwenye nyota yako ndipo kuna Baraka zako.
Jambo ambalo ni nyota yako utalitenda bila kupambana; Yaani hutatumia nguvu kwenye kulitekeleza jambo hilo.

MAOMBI YA KURUDISHA NYOTA:

Kurudisha nyota Iliyoibiwa:
Baba katika Jina la Yesu, nimetambua kuwa nyota yangu yaweza kufunikwa na kuibiwa; na leo ninaamua kuirudisha kwa Jina la Yesu kila nyota yangu iliyoibiwa, nyota ya kukubaliwa, ufanisi, umahiri, biashara, kazi au nyota ya hatma njema naamuru irudi kwa Jina la Yesu Kristo. Ninaamuru nyota yangu ikombolewe kwa damu ya Yesu, ninaamuru iachiliwe katika Jina la Yesu.Kufunua nyota iliyofunikwa:
Katika Jina kuu la Yesu ninasafisha nyota yangu iliyofunikwa; nyota ya mafanikio ninaisafisha kwa Jina la Yesu. Katika torati kila kitu husafishwa kwa Damu nami natumia Damu ya Yesu kusafisha nyota yangu katika Jina la Yesu. Ninatakasa nyota yangu iliyochafuliwa katika Jina la Yesu.  Ninang’arisha nyota yangu katika Jina la Yesu.

Kuangamiza wasimamizi wa nyota:
Ninasimama kinyume na kila mashetani, wachawi na waganga wa kienyeji wanaoshikilia nyota yangu katika Jina la Yesu. Waliofunika nyota ninawaangamiza katika ulimwengu wa roho, ninateketeza wote walioiba nyota yangu kwa Jina la Yesu. Katika Jina la Yesu niharibu kazi na utawala wa mashetani wanaoiba nyota yangu katika Jina La Yesu.

Kukiri ushindi:                           
Ninatangaza kurudishwa kwa nyota yangu katika Jina la Yesu; ninatangaza maisha yangu kung’arishwa katika Jina la Yesu. Mafanikio yangu yamerudi katika Jina la Yesu. Nimeshinda  kwa damu ya Yesu.

UFUFUO NA UZIMA (THE GLORY OF CHRIST (T) CHURCH)
TANGANYIKA PACKERS,
KAWE, DARES SALAAM.

Sunday, September 9, 2012

UJUMBE: MIKATABA YA DAMU

Na Mchungaji Kiongozi: Josephat Gwajima. 9.9.2012

UTANGULIZI:
Katika mfululizo wa masomo haya tayari tumekwisha kujifunza kuhusu kafara ya damu na tukaona pia kuhusu Kafara ya mwanakondoo ambaye ni Yesu kristo. Leo tunaangalia kuhusu mikataba inayoweza kusababishwa na damu iliyomwagika.

TABIA ZA DAMU KATIKA BIBLIA:
Mwanzo 4:10; Adamu alikuwa na watoto wawili mmoja aliitwa Kaini na mwingine Habili; Kaini alipomuua Habili; Mungu akamwambia Kaini, Damu ya ndugu yako inanililia. Kumbe damu yaweza kulia na inaweza kuongea pia.

Kumbukumbu 12:23 Mungu anasema kuwa “…damu ni uhai”. Kumbe damu ina uhai; kwa namna hiyo kuna tabia kadhaa za damu:
i)                   Damu ina sauti
ii)                 Damu yaweza kulia
iii)               Damu inaleta laana
Na ndio maana Mungu amekataza kula au kunywa damu, hii ni kwasababu hizi tatu Kumbukumbu7:27; Walawi 17:10,12

DAMU INA SAUTI (INANENA):
Damu iliyomwagika chini inaweza kunena mema au yaweza kunena mabaya,damu inenayo mema ni ya Yesu peke yake, Waebrania 12:24 inasema, “na Yesu mjumbe wa agano jipya, na damu ya kunyunyizwa, inenayo mema kuliko ile ya Habili.Kumbe kuna damu inayonena mema (damu ya Yesu Kristo) na pia kuna damu inayonena mabaya (damu ya wanyama,ndege hata watu)

Damu yaweza kuongea mabaya juu ya mtu; damu ikimwagwa hunena na ndio maana hata nchi yaweza kuingia kwenye matatizo kwasababu ya damu inenayo iliyomwagika.

Mambo ya Walawi 19:26 Msile kitu cho chote pamoja na damu yake; wala msifanye kuloga, wala kutumia utambuzi. Mungu amekataza kula nyama pamoja na damu kwasababu damu ni uhai, na ina sauti. Na ukiangalia katika biblia kila mahali ambapo damu imekatazwa na uchawi pia umetajwa. Kwa maana hiyo tunajifunza kuwa uchawi upo na unaushirikiano wa karibu na matumizi ya damu.

MAFUNDO YA KICHAWI:
Ukisoma Ayubu 15:26 Humshambulia na shingo ngumu,  Kwa mafundo makubwa ya ngao zake;mafundo yapo na wachawi ndio wanayo yafunga. Wachawi wanaweza kuloga katika kufunga mafundo, hivi ni vifungo vya kichawi ambavyo hutumia kudumisha maisha ya watu. Kumbukumbu 18:11 wala mtu alogaye kwa kupiga mafundo, wala mtu apandishaye pepo, wala mchawi, wala mtu awaombaye wafu. Kuna mafundo ya aina mbalimbali mojawapo ni mafundo ya maamuzi; yaani mtu anashindwa kuwa na maamuzi, na ndio maana watu wengi wanashindwa kupiga hatua kwenye maisha kwasababu wamefungwa katika maamuzi.

Wachawi pia hutumia mafundo haya kufunga matumbo ya kina mama ili wasipate watoto; na ndio maana ya maandiko yale yanayosema Amin, nawaambieni, yo yote mtakayoyafunga duniani yatakuwa yamefungwa mbinguni; na yo yote mtakayoyafungua duniani yatakuwa yamefunguliwa mbinguni.Mathayo 18:18. Kwenye ulimwengu wa mwili mtu anaweza akaonekana anaumwa au ana matatizo lakini katika ulimwengu wa roho anakuwa amefungwa. Luka 13:16 huyu mwanamke alionekana amepooza kumbe shetani alikuwa amemfunga.

DAMU INAVYOTENDA KAZI:
Sasa kwa kujua kuwa kila damu iliyomwagwa inauwezo wa kusema, wachawi hutumia tabia hiyo ya damu kufunga maisha ya watu. kwahiyo wanachofanya wachawi au waganga ni kuchukua mnyama na kumchinja yule mnyama na kuinuizia inene tatizo lako. Kimsingi; hii damu iliyomwagwa ndiyo inayoitwa madhabahu ya tatizo lako. Na ndio maana waganga wa kienyeji huagiza kuku, mbuzi au ng’ombe ile ni kwa ajili ya kumwaga damu ili inene  mabaya juu ya mtu.

Damu inapomwagwa inatoa sauti; yaani katika ulimwengu wa roho ni sauti kubwa ili mtu akae katika tatizo; kinachotokea pale damu inaponena mashetani husikia rohoni na kwa njia hiyo mashetani yanapata mlango wa kuingia kwenye maisha ya mtu. Hivyo mashetani huja ili kutekeleza sauti ya ile damu inayonena. Kwa njia hiyo shetani amefunga maisha ya watu na kifungo kinakuwa kikubwa kulingana na wingi wa damu iliyomwagwa

DAMU INAYOTOKANA NA KUCHANJWA CHALE:
Biblia iko wazi sana kuhusu kuchanja chale kwenye miili ya watu. Mambo ya Walawi 19:28 Msichanje chale yo yote katika nyama ya miili yenu kwa ajili ya wafu, wala msiandike alama miilini mwenu; mimi ndimi Bwana. Mambo ya Walawi 21:25; Yeremia 48:37 Yaani; mtu huyu sio kwamba imemwagwa damu ya mnyama kwa ajili yake bali anakuwa amechanjwa mwenyewe kwenye mwili na ameitoa damu yake mwenyewe. Kimsingi; mganga anapokuwa anachanja chale huwa ananena maneno ambayo huwezi kuyaelewa. Yale maneno ndio sauti ya ile damu iliyo mwagwa.

Utajiuliza kwanini Mungu anakataza watu kupigwa chale; kimsingi damu inayomwagika ni uhai wako, kwa lugha rahisi ni kwamba unapochanjwa  chale unakuwa umeacha uhai wako kwa mganga wa kienyeji. Hivyo mganga anaweza kukuona na kukufuatilia kirahisi, hivyo akiamua kukufanya urudi kwake anaweza kukurudisha kirahisi kwasababu uhai wako umeuacha kwake.

DAMU YA YESU KRISTO:                                                                                                            
Unaweza ukajifunza kwanini Yesu alipokuja duniani asingekufa kwa kuumwa au njia nyingine ambayo haimwagi damu, Siri kuu ya kuja Yesu duniani ni kwa ajili yetu sisi tufunguliwe na kutoka kwenye vifungo kwa damu ya Yesu ambayo yenyewe hunena mema daima.

Yaani Mungu alipoaamua kumkomboa mwanadamu ikamlazimu kuvaa mwili ili aje kuukomboa ulimwengu. Na ndio maana aliitwa Immanuel yaani Mungu pamoja nasi, naye alipokuja duniani akaenda msalabani ili atengeneze madhabahu yake kwa njia ya kumwaga damu. Na nguvu ya damu ya Yesu ni kuwa hakutenda dhambi hivyo damu yake ina nguvu dhidi ya madhabahu zote za giza.
Wakati wao wanaitia damu za mafahari na mbuzi sisi tunanena damu ya Yesu, inayonena mema. Kwa kutumia damu ya Yesu twaweza kunyamazisha damu nyingine za giza.

Ibada ilimalizika kwa maombi:
Baada ya kujifunza somo hapo juu omba hivi;
Kamata kuhani wa madhabahu:
Ninakamata kuhani wa madhabahu  kwa jina la Yesu. Kila wachawi na waganga wote wanaosimama kama kuhani wa madhabahu, ninawakamata kwa jina la Yesu. Ninaharibu kazi zao katika jina kuu la Yesu Kristo. Imeandikwa mtakalolifunga duniani na mbinguni litakuwa limefungwa; ninawakamata na kuwafunga wote Katika Jina La Yesu.


Bomoa Madhabahu:
Katika jina lenye Nguvu la Yesu Kristo ninaharibu kila madhabahu za kishetani kwa Jina La Yesu. Ninabomoa madhabahu zinazoleta vifungo kwenye maisha yangu katika Jina La Yesu. Madhabahu za magonjwa, mikosi na laana ninazibomoa na kuzisambaratisha katika Jina la Yesu. Ninateketeza madhabahu zote katika Jina La Yesu.

Nyamazisha damu yoyote iliyomwagwa inayonena mabaya kwa ajiliya maisha yako:
Nanyamazisha damu zote zinazonena mabaya juu yangu katika Jina la Yesu, Nanyamazisha damu ya mbuzi na damu zote za wanyama kwa Damu ya Mwanakondoo. Ninaamuru damu yoyote inayonena mabaya juu yangu inyameze Kwa Damu ya Yesu Kristo. Imeandikwa Damu ya Yesu inanena mema nami kwa Damu hiyo ninanyamazisha kila damu za mashetani na damu ya Yesu inene mema kuanzia sasa.

UFUFUO NA UZIMA {THE GLORY OF CHRIST (T) CHURCH}
TANGANYIKA PACKERS,
KAWE, DAR ES SALAAM.
Sunday, September 2, 2012

UJUMBE: MIKATABA INAYOTOKANA NA KAFARA Tar. 2.9.2012

Na Mchungaji Kiongozi Josephat Gwajima

Utangulizi:
Wakristo wengi huwa hawazungumzii neno kafara kwasababu wanahisi kuwa ni la waganga wa kienyeji, lakini hili neno limeandikwa kwenye biblia mara nyingi sana. Hii ni kuonyesha kuwa  wapo watu wanatoa kafara.

KAFARA KWENYE BIBLIA:
Baada ya Yoshua na wana wa Israeli kuangusha ukuta wa Yeriko, Yoshua aliweka agano kuwa atakayeamua kujenga ukuta ataanza kwa kufiwa na mwanawe wa kwanza na akasema akimaliza atafiwa na mwanae wa pili. Yoshua 6:20-27. Lakini miaka mingi baadaye mtu mmoja akatoa kafara ya wanawe ili aweze kujenga ngome ya Yeriko kwa upya, Kumbe kafara yaweza kutolewa kwa ajili ya kujenga kitu duniani. Imeandikwa katika  1Wafalme 16:38.  

2Wafalme 3:20-27, Hapa tunaona habari ya Huyu Mfalme ambaye baada ya kuona anashindwa vita dhidi ya wana wa Israeli, akaamua kumtoa kafara mwanaye na hilo jambo likawa hasira juu ya Israeli na kashinda vita. Kumbe kafara inaweza ikamwezesha mtu kushinda vita. Ukisoma maandiko haya kwa haraka hutoweza kuelewa lakini ukikaa ukatafakari utaona kuna jambo la muhimu  sana hapo.

Kafara ya mtu kwenye biblia; 2Wafalme17:17,“Wakawapitisha watoto wao, waume na wake, motoni, wakapiga ramli, wakafanya uchawi, wakajiuza nafsi zao wapate kufanya yaliyo maovu machoni pa Bwana, hata kumkasirisha” kumpitisha mtoto motoni ni kumchoma moto kama kafara yaani ukisoma biblia ya kingereza inatumia neno “sacrifices “ Ezekieli 16:20-21, kumbe jambo la kafara lipo kwenye biblia,na hapa Ezekieli anasema wakawatoa kafara wanao kuwa chakula; na pia neno hili limeoneka na pia katika kitabu cha Ezekieli 20:31-32.

KWELI KUHUSU KAFARA:
Mtoto au mtu akitolewa kafara anakuwa ameuwawa Mwili na kupewa majini au mashetani, katika biblia shetani anayehusika na mambo ya kafara, Mambo ya Walawi 18:21;  ukisoma biblia ya Kiswahili unaweza ukahisi moleki ni mtu lakini tuangalie kwenye biblia ya kingereza “do not give out your children to be sacrifices..” Mambo ya Walawi 20:2 “who sacrifices..  kumbe inawezekana unaumwa na upo kwenye ugonjwa kumbe ndio unatolewa kafara hivyo..

Kumbe sasa waweza  kumwona mtu amekufa na ugonjwa Fulani kumbe ni kafara, mwingine anatoa kafara kwa ajili ya utajiri. Mambo ya Walawi 20:3, pia tunaona kuwa kumbe wachawi hawa wanatoa ndugu na si mtu ambaye hamjui. Yaani kama una ndugu wa karibu au wa mbali ambaye ni mchawi, Yule ndiye anayeweza kukutoa kafara, na kwenye kitabu cha Mambo ya walawi  shetani aliyekuwa anahusika na kafara aliitwa Moleki. Walawi 20:4,5  2Wafalme 20:10

Hayo maandiko ni ya agano la kale lakini pia katika agano jipya jambo hili limetajwa pia; 2Wakorintho 10:20.

KWANINI WATU WANATOA KAFARA:
Ukiangalia habari ya Nuhu baada ya kutoka kwenye safina nuhu alimtolea Mungu sadaka na ile harufu ilipofika kwa Mungu; akasema hatailaani nchi tena kumbe ile harufu ina maana sana kwenye ulimwengu wa roho; vivyo hivyo wanapo mtolea shetani kafara wanalenga kumpa ile harufu na ile harufu inamfanya shetani awa tekelezee wanayohitaji. Mtu anamtoa mwanawe ili kuwapa kafara mashetani, wamtekelezee anacho hitaji kama utajiri n.k.

Mambo ya Walawi 2:12 Vitu hivyo mtavisongeza kwa Bwana kuwa ni malimbuko; lakini visifike juu ya madhabahu kuwa ni harufu ya kupendeza.” Utajiuliza hii harufu na sadaka; hapa ni kafara inayotolewa kwa mashetani. Mambo ya Walawi 3:15, 16, Hesabu 5:17, Sadaka ya vinywaji hii ni baadhi ya mila hapa kwetu ni pale mtu anakunywa pombe alafu anawapulizia watu, hii ndio inaitwa sadaka ya vinywaji inayotolewa. Sasa hii inapotolewa kwa mashetani kwenye ulimwengu wa roho wanakuja mahali pale. Hesabu 15:10; 17:24; 18:7

KUWA MAKINI NA KAFARA ZILIZOTOLEWA KWA MASHETANI:
Kumbe shetani anaweza kutolewa kafaraza aina mbalimbali inaweza kuwa ya vinywaji, uji, nafaka, harufu, watoto au watu wazima; na ni muhimu kuwa makini sana na kuhudhuria sherehe ambazo si za ki Mungu kwasababu waweza kujikuta unashiriki kwenye sadaka hiyo. Kuna watu ambao matatizo yao yamewaanza baada ya kushiriki chakula cha kafara jambo hili biblia imekataza kwasababu ya madhara yake.

Ufunuo 5:8; 8:3 hapa biblia inataja sadaka ya harufu, na ndio maana ukienda kwenye maduka mengi utakuta wameweka vitu vinaitwa ubani; Hii ni sadaka au kafala ya kuteketezwa kwa majini, Isaya 43:23; Yeremia 6:20; 17:26, Ubani na Udi ni sadaka ya kuteketezwa, kimsingi; ile harufu ndiyo inayoifanya iitwe sadaka ya kuteketezwa, kwahiyo mtu unayemuona anachoma ubani ni anakuwa anatoa kafara ya ubani. Nehemia 13:9.. sadaka za unga na sadaka za ubani. Kimsingi watu tuliookolewa hatutoi sadaka za ubani kwasababu biblia inasema maombi ya watakatifu ndio sadaka ya harufu kwa Mungu. (Yohana 19:39)

Kumbe unapoona mahali au duka ukakuta wanachoma udi kimsingi ni kwamba wanaita Mashetani ambayo yanawasaidia kuleta wateja. Na ndio maana maduka mengi yana kuwa na vitu hivi ambavyo ni kafara au sadaka ya harufu; ili majini yaite wateja. Na ndio maana watu wengi wenye majini wanapenda ubani kwasababu kile ndio chakula chao.

KAFARA YA NCHI:
Kuna uwezekano nchi ikawekewa kafara ili wananchi wasiongee, yaani kunakuwa na matatizo katika nchi lakini kumbe ni kwasababu ya kuwaita mashetani ili kufanya wananchi wasidai haki yao. Na ndio maana kuna vitu ambavyo vinapitishwa kwenye nchi ambavyo kwa hakika ni kafara ya harufu kwa shetani. Mambo kama mwenge unaopita ni sadaka kwa mashetani kwa ajili ya nchi, kama unahitaji kujua ukweli wa jambo hili muombe Mungu akuonyeshe; katika ulimwengu wa roho, utajua wazi kuwa ni kafara kabisa kwa ajili ya nchi nzima.

Biblia iko wazi kuhusu kafara inayotolewa kwa ajili ya nchi; Katika biblia Kumbukumbu La Torati 32:43Furahini, enyi mataifa, pamoja na watu wake; Kwa maana atatwaa kisasi kwa damu ya watumwa wake, Atawatoza kisasi adui zake,  Tena atafanya kafara kwa nchi yake, na watu wake.” Kumbe kuna uwezakano wa nchi kutolewa kafara yaani mtu anatoa sadaka ili kuita mashetani kwenye nchi. Ni muhimu unapokuwa unaomba uwe unavunja na kusambaratisha kafara zilizo tolewa katika nchi. Nchi ya Tanzania inatakiwa ikombolewe kutoka kwenye kafala.

NGUVU YA KAFARA:
Unaweza ukajiuliza kafara inafanyaje kazi; kimsingi; sadaka au kafara ya vinywaji, damu au vyote tulivyoona ni chakula cha mashetani. Na kimsingi mashetani yapo katika ngazi mbalimbali kuanzia majoka mpaka kwenye majini majini madogo; kwahiyo wachawi au washirikina huita mashetani kulingana na ukubwa wa kafara kama ikitolewa kafara ya kuku anakuja shetani wa ngazi ndogo. Na ikitolewa kafara kubwa kama ya mtu inaliita shetani la ngazi ya juu sana. Hivyo kama mtu hajaokoka ni rahisi kutolewa kafara kwasababu anakuwa hana ulinzi wa Mungu.UFUFUO NA UZIMA {THE GLORY OF CHRIST (T) CHURCH}
TANGANYIKA PACKERS,
KAWE, DAR ES SALAAM.