google.com, pub-4324601895065941, DIRECT, f08c47fec0942fa0

Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

UJUMBE: MIKATABA YA DAMU

Na Mchungaji Kiongozi: Josephat Gwajima. 9.9.2012

UTANGULIZI:
Katika mfululizo wa masomo haya tayari tumekwisha kujifunza kuhusu kafara ya damu na tukaona pia kuhusu Kafara ya mwanakondoo ambaye ni Yesu kristo. Leo tunaangalia kuhusu mikataba inayoweza kusababishwa na damu iliyomwagika.

TABIA ZA DAMU KATIKA BIBLIA:
Mwanzo 4:10; Adamu alikuwa na watoto wawili mmoja aliitwa Kaini na mwingine Habili; Kaini alipomuua Habili; Mungu akamwambia Kaini, Damu ya ndugu yako inanililia. Kumbe damu yaweza kulia na inaweza kuongea pia.

Kumbukumbu 12:23 Mungu anasema kuwa “…damu ni uhai”. Kumbe damu ina uhai; kwa namna hiyo kuna tabia kadhaa za damu:
i)                   Damu ina sauti
ii)                 Damu yaweza kulia
iii)               Damu inaleta laana
Na ndio maana Mungu amekataza kula au kunywa damu, hii ni kwasababu hizi tatu Kumbukumbu7:27; Walawi 17:10,12

DAMU INA SAUTI (INANENA):
Damu iliyomwagika chini inaweza kunena mema au yaweza kunena mabaya,damu inenayo mema ni ya Yesu peke yake, Waebrania 12:24 inasema, “na Yesu mjumbe wa agano jipya, na damu ya kunyunyizwa, inenayo mema kuliko ile ya Habili.Kumbe kuna damu inayonena mema (damu ya Yesu Kristo) na pia kuna damu inayonena mabaya (damu ya wanyama,ndege hata watu)

Damu yaweza kuongea mabaya juu ya mtu; damu ikimwagwa hunena na ndio maana hata nchi yaweza kuingia kwenye matatizo kwasababu ya damu inenayo iliyomwagika.

Mambo ya Walawi 19:26 Msile kitu cho chote pamoja na damu yake; wala msifanye kuloga, wala kutumia utambuzi. Mungu amekataza kula nyama pamoja na damu kwasababu damu ni uhai, na ina sauti. Na ukiangalia katika biblia kila mahali ambapo damu imekatazwa na uchawi pia umetajwa. Kwa maana hiyo tunajifunza kuwa uchawi upo na unaushirikiano wa karibu na matumizi ya damu.

MAFUNDO YA KICHAWI:
Ukisoma Ayubu 15:26 Humshambulia na shingo ngumu,  Kwa mafundo makubwa ya ngao zake;mafundo yapo na wachawi ndio wanayo yafunga. Wachawi wanaweza kuloga katika kufunga mafundo, hivi ni vifungo vya kichawi ambavyo hutumia kudumisha maisha ya watu. Kumbukumbu 18:11 wala mtu alogaye kwa kupiga mafundo, wala mtu apandishaye pepo, wala mchawi, wala mtu awaombaye wafu. Kuna mafundo ya aina mbalimbali mojawapo ni mafundo ya maamuzi; yaani mtu anashindwa kuwa na maamuzi, na ndio maana watu wengi wanashindwa kupiga hatua kwenye maisha kwasababu wamefungwa katika maamuzi.

Wachawi pia hutumia mafundo haya kufunga matumbo ya kina mama ili wasipate watoto; na ndio maana ya maandiko yale yanayosema Amin, nawaambieni, yo yote mtakayoyafunga duniani yatakuwa yamefungwa mbinguni; na yo yote mtakayoyafungua duniani yatakuwa yamefunguliwa mbinguni.Mathayo 18:18. Kwenye ulimwengu wa mwili mtu anaweza akaonekana anaumwa au ana matatizo lakini katika ulimwengu wa roho anakuwa amefungwa. Luka 13:16 huyu mwanamke alionekana amepooza kumbe shetani alikuwa amemfunga.

DAMU INAVYOTENDA KAZI:
Sasa kwa kujua kuwa kila damu iliyomwagwa inauwezo wa kusema, wachawi hutumia tabia hiyo ya damu kufunga maisha ya watu. kwahiyo wanachofanya wachawi au waganga ni kuchukua mnyama na kumchinja yule mnyama na kuinuizia inene tatizo lako. Kimsingi; hii damu iliyomwagwa ndiyo inayoitwa madhabahu ya tatizo lako. Na ndio maana waganga wa kienyeji huagiza kuku, mbuzi au ng’ombe ile ni kwa ajili ya kumwaga damu ili inene  mabaya juu ya mtu.

Damu inapomwagwa inatoa sauti; yaani katika ulimwengu wa roho ni sauti kubwa ili mtu akae katika tatizo; kinachotokea pale damu inaponena mashetani husikia rohoni na kwa njia hiyo mashetani yanapata mlango wa kuingia kwenye maisha ya mtu. Hivyo mashetani huja ili kutekeleza sauti ya ile damu inayonena. Kwa njia hiyo shetani amefunga maisha ya watu na kifungo kinakuwa kikubwa kulingana na wingi wa damu iliyomwagwa

DAMU INAYOTOKANA NA KUCHANJWA CHALE:
Biblia iko wazi sana kuhusu kuchanja chale kwenye miili ya watu. Mambo ya Walawi 19:28 Msichanje chale yo yote katika nyama ya miili yenu kwa ajili ya wafu, wala msiandike alama miilini mwenu; mimi ndimi Bwana. Mambo ya Walawi 21:25; Yeremia 48:37 Yaani; mtu huyu sio kwamba imemwagwa damu ya mnyama kwa ajili yake bali anakuwa amechanjwa mwenyewe kwenye mwili na ameitoa damu yake mwenyewe. Kimsingi; mganga anapokuwa anachanja chale huwa ananena maneno ambayo huwezi kuyaelewa. Yale maneno ndio sauti ya ile damu iliyo mwagwa.

Utajiuliza kwanini Mungu anakataza watu kupigwa chale; kimsingi damu inayomwagika ni uhai wako, kwa lugha rahisi ni kwamba unapochanjwa  chale unakuwa umeacha uhai wako kwa mganga wa kienyeji. Hivyo mganga anaweza kukuona na kukufuatilia kirahisi, hivyo akiamua kukufanya urudi kwake anaweza kukurudisha kirahisi kwasababu uhai wako umeuacha kwake.

DAMU YA YESU KRISTO:                                                                                                            
Unaweza ukajifunza kwanini Yesu alipokuja duniani asingekufa kwa kuumwa au njia nyingine ambayo haimwagi damu, Siri kuu ya kuja Yesu duniani ni kwa ajili yetu sisi tufunguliwe na kutoka kwenye vifungo kwa damu ya Yesu ambayo yenyewe hunena mema daima.

Yaani Mungu alipoaamua kumkomboa mwanadamu ikamlazimu kuvaa mwili ili aje kuukomboa ulimwengu. Na ndio maana aliitwa Immanuel yaani Mungu pamoja nasi, naye alipokuja duniani akaenda msalabani ili atengeneze madhabahu yake kwa njia ya kumwaga damu. Na nguvu ya damu ya Yesu ni kuwa hakutenda dhambi hivyo damu yake ina nguvu dhidi ya madhabahu zote za giza.
Wakati wao wanaitia damu za mafahari na mbuzi sisi tunanena damu ya Yesu, inayonena mema. Kwa kutumia damu ya Yesu twaweza kunyamazisha damu nyingine za giza.

Ibada ilimalizika kwa maombi:
Baada ya kujifunza somo hapo juu omba hivi;
Kamata kuhani wa madhabahu:
Ninakamata kuhani wa madhabahu  kwa jina la Yesu. Kila wachawi na waganga wote wanaosimama kama kuhani wa madhabahu, ninawakamata kwa jina la Yesu. Ninaharibu kazi zao katika jina kuu la Yesu Kristo. Imeandikwa mtakalolifunga duniani na mbinguni litakuwa limefungwa; ninawakamata na kuwafunga wote Katika Jina La Yesu.


Bomoa Madhabahu:
Katika jina lenye Nguvu la Yesu Kristo ninaharibu kila madhabahu za kishetani kwa Jina La Yesu. Ninabomoa madhabahu zinazoleta vifungo kwenye maisha yangu katika Jina La Yesu. Madhabahu za magonjwa, mikosi na laana ninazibomoa na kuzisambaratisha katika Jina la Yesu. Ninateketeza madhabahu zote katika Jina La Yesu.

Nyamazisha damu yoyote iliyomwagwa inayonena mabaya kwa ajiliya maisha yako:
Nanyamazisha damu zote zinazonena mabaya juu yangu katika Jina la Yesu, Nanyamazisha damu ya mbuzi na damu zote za wanyama kwa Damu ya Mwanakondoo. Ninaamuru damu yoyote inayonena mabaya juu yangu inyameze Kwa Damu ya Yesu Kristo. Imeandikwa Damu ya Yesu inanena mema nami kwa Damu hiyo ninanyamazisha kila damu za mashetani na damu ya Yesu inene mema kuanzia sasa.

UFUFUO NA UZIMA {THE GLORY OF CHRIST (T) CHURCH}
TANGANYIKA PACKERS,
KAWE, DAR ES SALAAM.




Post a Comment

2 Comments

  1. Asante kwa Ujumbe huu wenye kufungua macho na kufahamua MIKATABA KATIKA DAMU. Mungu akubariki sana Mtumishi

    Maxwell Shimba

    ReplyDelete