Sunday, November 18, 2012

UJUMBE: MIAKA YA MAISHA YETU


Na. Mch. Mwangasa (Resident Pastor)
Mchungaji Mwangasa (Resident Pastor) akihubiri kanisani
Ufufuo na Uzima, Dar es Salaam

Mwanzo 47:7-12
9* “Yakobo akamjibu Farao, Siku za miaka ya kusafiri kwangu ni mia na thelathini; siku za miaka ya maisha yangu zimekuwa chache, tena za taabu, wala hazikufikilia siku za miaka ya maisha ya baba zangu katika siku za kusafiri kwao.” Haya yalikuwa ni mazungumzo baina ya Yakobo na Farao baada ya Yusufu kwenda kumtambulisha babaye kwa Farao. Lakini kitu cha kushangaza Farao akamuuliza Yakobo, siku za maisha yako ni ngapi? Na hilo ndilo lilikuw jibu ya Yakobo kwa Farao.Jibu la Yakobo linatupa jambo muhimu la kujifunza, ukifuatilia maisha ya Yakobo utagundua kuwa ni kweli yalikuwa ya kusafiri sana, ukianzia tangu alipozaliwa, baadaye alimkimbia Essau na kwenda kwa Labani, haikutosha akarudi kupatana na Essau, bado taarifa za mauaji ya Yusufu nayo yalichangia kufanya maisha yake yawe ya tabu. Na ndio maana alipoulizwa na Yusufu siku za maisha yake ni ngapi, ikabidi atenge muda aliosafiri yeye na maisha yaliokuwa wameishi wazee wake yaani (Ibrahimu na Isaka).

Mch. Bihagaze akimkaribisha Mch. Mwangasa
madhabahuni
Tukitaka kufuatilia maisha ya Yakobo alipokuwa kwa Labani, tunaweza kufahamu kupitia andiko hili Mwanzo  31:38-41, haya ni maelezo ya Yakobo kwa Labani, baada ya Labani kumpekuwa kutokana na upotevu wa miungu yake. Ndio maana hapo Yakobo anasema alikuwa anafanya kazi mchana na usiku, alibadilishiwa mishahara mara kumi kwasababu kila hasara ililopatikana ilirudishwa kwa Yukobo. (Mwanzo 30:25-44) pamoja na yote hayo, bado Labani alimdhulumu Yakobo, hivyo maisha ya Yakobo yalikuwa yamejaa tabu na dhulumiwa.

Wakati Labani akiwa amevuruga makubaliano yale, Yakobo akamtazama Mungu, na hapa ndipo tunaona jambo la ajabu pale Yakobo alipoweka fito kwenye maji, na wale wanyama walipokunywa wakapata mimba. Hapa tunajifunza jambo kuwa hata kama wanadamu wamekudhulumu, Mungu anaweza kukusaidia nawe utaneemeka kuliko waliokudhulumu. Hili jambo lilitokea wakati Labani ametorosha madume yote ili Yakobo asipate uzao kwa wanyama wale. Ukiokoka unakuwa na Mungu, hakuna haja ya kusikitika kuwa umebaki peke yako, kuna Mungu ambaye hawezi kukuacha.

Maelfu ya Watu wakimwabudu Mungu Jumapili hii
Ufufuo na Uzima
Imeandikwa Kwa maana kila kitu kilichozaliwa na Mungu huushinda ulimwengu; na huku ndiko kushinda kuushindako ulimwengu, hiyo imani yetu.” Yohana 5:4. Ukiokoka Mungu anakuwa pamoja na wewe, yaani umezaliwa na Mungu, na kila kilichozaliwa na Mungu huushinda ulimwengu. Na hapa kwa Habari ya Yakobo, Mungu alikuwa anataka ile ahadi aliyomuahidi Ibrahimu itimie kwa Yakobo.

Inawezekana kwenye maisha yako, unaishi kama Yakobo, maisha yaliyojaa kusafiri ena huku ukipapasa papasa bila kujua unakoelekea. Inabidi ujue jambo hili kuwa ukimpata Mungu unakuwa umepata jibu la maisha yako. Imeandikwa, Utajiri na heshima ziko kwangu,  Naam, utajiri udumuo, na haki pia.” Mithali 8:18. Mtafute Mungu ndipo utakutana na Utajiri na Heshima. Wewe ndio unajua siku za miaka yako ni mingapi, unajua mambo gani magumu unayopitia, lakini Mungu anakuuliza siku za maisha yako ni ngapi.

Hata katika habari ya mwana mpotevu, aliposemezana na baba yake kuhusu maisha aliyopitia, alirudishiwa yote (Luka 15:17-23). Leo mwambie Mungu miaka ya maisha yako. Mungu anasema “Unikumbushe, na tuhojiane; eleza mambo yako, upate kupewa haki yako.” Isaya 43:26. Kuna haja ya kuhojiana na Mungu, usiwambie watu mwambie Mungu. Yesu akamwambia Yule mwanamke kwenye kisima, kuwa yeye ndio maji yaliyo hai, kama unakiu ya jambo lolote mwambie Yesu Kristo (Yohana 4:14). Mungu kwetu sisi ni Mungu wa kuokoa na njia za kutoka mautini zina yeye!!!!!

The Glory Of Christ Tanzania Church
Ufufuo na Uzima
Dar es Salaam
Tanzania

No comments:

Post a Comment