Sunday, December 30, 2012

UBATIZO WA KIBIBLIA KUFANYIKA TAREHE 1 JANUARI 2013


Na Mchungaji Kiongozi Josephat Gwajima

Kila mtu aliyeokoka ni askari wa jeshi la Yesu, hivyo kama askari wa Yesu tunatakiwa kufuata kile ambacho Mungu anatuagiza, 1Timotheo 2:4; sisi ni wanajeshi wa jeshi la BWANA, Filemoni 1:2; Hivyo mkristo mwenzako aliyeokoka ni askari mwenzako.  Ndio maana katika biblia kila mahali Mungu alipojitambulisha alitumia jina la BWANA wa Majeshi. 1Samwel 15:2; 2Samweli 7:8. Utajiuliza majeshi haya ni yapi; haya ni majeshi ya Yesu ambayo ndio sisi tuliookoka. Mambo ya Nyakati17:7; Isaya 1:24;3:15; 10:24; 14:13;

Mara tu unapookolewa Yesu ambaye ni Bwana wa majeshi anatuagiza kutii amri yake.  Malaki 3:17; 4:3;  Mathayo 28:18-19, hapa BWANA wa majeshi anatoa Amri ya kuifuata. Kumbe kuwabatiza watu ni amri ya BWANA wa majeshi, hivyo tuna jukumu la kutii amri ya Yesu Kristo. Na unapookolewa Mungu anakutarajia utii amri ya mkuu wa majeshi Yesu Kristo.

MAANA YA NENO UBATIZO
Neno “ubatizo” linatokana na neno la kigiriki linaitwa “babto” au zamisha; hili neno Babto limetumika mara nyingi sana katika biblia Yohana 13:26.  Yesu alisema ambaye nitachovya naye tonge ndiye atakaye nisaliti” kumbe kuzamisha tonge katika mboga ndio mana rahisi ya kubatiza yaani chovya au kuzamisha. Kwahiyo kutokana na maana ya neno ubatizo tunaweza kujua kuwa ili mtu abatizwe anatakiwa awe kwenye maji tele.

UBATIZO WA KIBIBLIA
Yohana 3:23; kwa maana hiyo ya ubatizo ndio maana tunaona Yohana alibatiza mahali penye maji tele. Huwezi kuzamisha mtu ndani ya bakuli au birika, ni lazima maji yawe tele ili mtu aweze kuzama. Hivyo ubatizo wa kibiblia ni wa kumzamisha mtu ndani ya maji.  Na ndio maana katika kitabu cha Matendo ya mitume 8:26; hivyo ubatizo wa Kibiblia wote wawili hutelemka majini, hapo unaweza ukajiuliza je ulipobatizwa wote wawili mlitelemka majini? Kama sivyo basi ujue haukuwa ubatizo wa Kibiblia.
Na jambo lingine la kuangalia huyu towashi alihubiriwa, akaamini na kubatizwa. Unaweza ukalinganisha kama ulipobatizwa uliamini kwanza na je wote mliingia majini, na ndio maana mstari wa 29” unasema “kisha walipopanda kutoka majini” kumbe ubatizo wa kibiblia hutelemka majini na kupanda kutoka majini.

KWANINI WATU WANABATIZA NDANI YA BAKULI AU BIRIKA
Watu wengi wanayapindisha maandiko, lakini biblia inatuagiza kutumia neno la Mungu kwa halali, 2Timotheo 2:15. Na ndio maana utaona watu leo wanatumia maandiko vibaya kuwabatiza watu katika bakuli, bila kutelemka majini. Haya ndio maandiko ambayo watu huyatumia kupindisha ukweli, Hesabu 8:5-7; Mungu alimwambia Musa anyunyize maji ya utakaso, lakini huu si ubatizo bali ni utakaso. Na watu wengi waliokuwa wamefanyiwa hivi ni wale waliokuwa wameshika maiti, ilikuwa mtu ashikapo maiti anakuwa najisi mpaka amwagiwe maji ya farakano. Kimsingi huu haukuwa ubatizo wa kibiblia, bali ulikuwa utakaso tu na si ubatizo wa kibiblia.

MTU YUPI ANAYETAKIWA KUBATIZWA
Huyu ni mtu aliyetubu dhambi, kama hujatubu dhambi ubatizo wako si wa kibiblia. Matendo ya Mitume 2:37, hivyo kanuni ya Mungu ni kwamba mtu anatubu kwanza ndipo anabatizwa, lakini maeneo mengi watu hubatizwa wakiwa watoto wachanga ambao hawawezi kutubu. Hivyo kama ulibatizwa ukiwa mtoto mchanga, huo sio ubatizo wa kibiblia. Marko 16:15-16, Na ndio maana Yesu aliagiza kwa kusema aaminiye na kubatizwa, kumbe kinachoanza ni kuamini alafu unabatizwa.

Tumeona mambo kadhaa yanayoendana na ubatizo wa kibiblia, yaani unatubu kwanza, ndipo unabatizwa. Matendo ya Mitume 8:12, Biblia inaendelea kusema kuwa wakaamini wakabatizwa, huwezi kusema umebatizwa kama hujaamini bado. Matendo ya Mitume 8:35-38, katika biblia hakuna aliyebatizwa bila kuamini kwanza, na ndio maana Filipo alimwambia Yule towashi kwa habari ya ubatizo “ukiamini inawezekana” kumbe ubatizo wa kibiblia unaamini kwanza ndipo inawezekana kubatizwa. Ni swali la kujiuliza kuwa ulipobatizwa uliamini kwanza.  Matendo ya mitume 19:1-…

UBATIZO UNAWEZWA KUFANYWA KWA MTOTO MCHANGA
Mtoto mdogo hawezi kuamini, na kwa maana hiyo hawezi hata kutubu dhambi zake. Mama au baba wa ubatizo hawezi kutubu kwa niaba ya mtoto, huu ni usanii na si ukweli kabisa. Mtu anatakiwa asikie mwenyewe na atubu mwenyewe pasipo kujibiwa na mtu. Kwahiyo jibu la swali hili kuhusu ubatizo kwa watoto wadogo ni kwamba hakuna ubatizo kwa watoto wadogo, kwasababu hawezi kuamini, na pia ukimzamisha mtoto katika maji unaweza ukamuua.

Kwa maana hiyo; kama ulibatizwa ukiwa mtoto mchanga, huo haukuwa ubatizo. Na hata ukiamua kubatizwa ubatizo wa KIBIBLIA sio kwamba unabatizwa kwa mara ya pili bali ni mara ya kwanza, ule wa kwanza haukuwa ubatizo. Katika biblia mama au baba awezi kumuaminia mwanaye imeandikwa,Ezekieli 18:20. Kuwa baba hawezi kuchukua uovu wa mwanaye. Hata hivyo dhambi ya mtoto haihesabiwi kwasababu akili yake haijaweza kuitambua sheria bado, hivyo dhambi inaweza kuwepo lakini haijaanza kuhesabiwa kwasababu hawaijui sheria bado.

Kwa asili, mtoto anakuwa amezaliwa na asili ya dhambi, lakini haihesabiwi, Warumi 5:12-13 kumbe dhambi haisebawi kwa mtoto kwasababu haijui sheria na wala haijawa wazi kwake. Warumi 4:15. Matendo 2:38; Biblia inasema kwa siku moja walibatizwa wakiwa na umri tofauti tofauti.  Hivyo sio lazima kubatizwa ukiwa na umri kama wa Yesu bali awe mtu mwenye uwezo wa kuijua sheria.

NANI AKUBATIZE
Katika biblia waliobatizawalikuwa ni wanafunzi wa Yesu, na si wa musa mfano: Wasabato ni wanafunzi wa Musa na si wa Yesu. Kama ulibatizwa katika kanisa ambalo si la watu waliookoka maana yake ulibatizwa na mtu ambaye sio mwanafunzi wa Yesu. Hivyo huo haukuwa ubatizo wa kibiblia. Ubatizo wa kibiblia hufanywa na mwanafunzi wa Yesu na si  vinginevyo.

UWEZEKANO WA KUBATIZWA MARA MBILI AU ZAIDI
Ubatizo wa kibiblia unafanya mara moja tu, hivyo kama ulishawahi kubatizwa ubatizo wa kibiblia unafanyika mara moja tu. Lakini kuna mtu alibatizwa kabla ya kuamini, kibiblia hujawahi kubatizwa na ukibatizwa unakuwa ni mara ya kwanza. Mfano ulibatizwa ukiwa mtoto mchanga au ulibatizwa na mtu ambaye si mwanafunzi wa Yesu ule haukuwa ubatizo, lakini ukibatizwa sasa unakuwa umebatizwa kwa mara ya kwanza.

Unapoamiua kubatizwa leo unakuwa umebatizwa kwa mara ya kwanza kwasababu hakuna ubatizo kwa mtu ambaye alikuwa hajaokoka bado, hajaamini au alikuwa bado mtoto.

MAANA YA KIROHO YA UBATIZO
Ø  Ni kufa, kuzikwa na kufufuka pamoja na Bwana Yesu Wakolosai 2:12; hivyo katika ubatizo tunazikwa na kufufuliwa pamoja na Yesu Kristo.
Ø  Ni kutimiza haki yote; Na ndio maana Yesu alikuwa Mungu lakini alipokuja duniani alikwenda kubatizwa, hakustahiri kubatizwa lakini alibatizwa ili awe kielelezo kwetu. Ili sisi tumfuate yeye, unapokuwa umebatizwa unakuwa umetimiza haki yote ila kama hujabatizwa utakuwa hujatimiza haki yote
Ø  Ni ishara ya kumkiri Yesu hadharani. Kuna tofauti kati ya kumwamini na kumkiri Yesu Yohana 12:41-42. Lakini unapobatizwa ni kumkiri Yesu kuwa BWANA na mwokozi.

Maswali
Utajiuliza mbona yule mwizi msalabani alimwamini Yesu akaenda mbinguni bila kubatizwa?. Jambo la kujiuliza hapa je wewe upo msalabani, na haujapata nafasi ya kubatizwa?, Yule mwizi hakupata nafasi ya kubatizwa ndio maana alienda mbinguni lakini kwasasa una nafasi ya kubatizwa unatakiwa ubatizwe kibiblia.

Ukibatizwa lazima ubadilishe jina?
Kimsingi kuna majina ambayo ni lazima  ubadili mfano, tabu, makoye, sikuzani n.k lakini kama jina lako lina maana nzuri hakuna haja ya kubali jina. Na ndio maana katika biblia watu wa Mungu wengi walibadilishiwa majina yao.

No comments:

Post a Comment