Sunday, January 27, 2013

UJUMBE: MATUKIO YA KICHAWI


Na Mch. Kiongozi: Josephat Gwajima                                       Jumapili 27th January 2013

Mch. Kiongozi wa kanisa la Glory of Christ (T) Church
Josephat Gwajima
Kuna matukio ambayo yanaweza kutokea kwenye maisha yako na ukaona kuwa ni kawaida, lakini tambua kuwa matukio mengi huanzia rohoni. Matukio ya kishetani yanayoanzia rohoni yanaitwa matukio ya Kichawi. Tutajifunza somo hili kwa kuangalia kwa undani kuhusu Ayubu. Ayubu 1:1-... ; kitabu cha Ayubu kinaanza kwa kusema palikuwa na mtu mmoja katika nchi ya Usi…. Ayubu alikuwa anamcha BWANA, si mwenye dhambi…

Shetani akamwambia Mungu umembariki Ayubu ndio maana anakucha wewe, Mungu akamwambia, Katika Mstari wa 12’ “tazama yote aliyonayo yapo mikononi mwako lakini usinyooshe mkono juu yake mwenyewe” jambo la ajabu linatokea, mara tu baada ya Mungu kumruhusu shetani, jambo la kwanza shetani alianza kwa kuharibu mali zake (Ayubu 1:13…). Na katika kila tukio alilofanya shetani, alibakisha mtu mmoja wa kumpelekea habari Ayubu. Hii ni kwasababu shetani alitaka Ayubu asijue kuwa ni shetani bali Waseba ndio walioua na kuchukua mifugo wake ili amuhamishe mtazamo asifahamu kuwa ni jambo la kishetani,ndivyo amabavyo shetani anatenda kazi ahata leo.

Tukio la kwanza, Ayubu 1:13-15 Waseba waliwavamia watumishi wa Ayubu, unaweza ukawachunguza Waseba katika mitazamo miwili. Upande mmoja ni kwamba waseba ni mashetani waliovaa miili au ni watu walioingiliwa na mapepo kuharibu wanyama wa Ayubu. Tukio la pili limetajwa katika mstari wa 16’ kwamba moto ulishuka kutoka mbinguni, mtoa taarifa anaita moto wa Mungu, lakini katika kitabu cha (Ufunuo 13:13) inasema shetani anaweza kushusha moto pia. Huyu mfanya kazi aliita moto wa Mungu ili kwa njia hiyo shetani amdanganye Ayubu aache kuangalia shetani bali awaze kuwa ni matukio ya kawaida kutokea. Ndio maana katika waebrani 11:34, biblia inasema kwa imani walizima nguvu za moto, kwasababu kuna moto ambao waweza kuletwa na shetani. Haijalishi unapitia moto gani kwenye maisha yako, moto wa mikosi, kushindwa, umaskini na kila moto wa maisha yako uzime katika Jina la Yesu Kristo usiite ni matukio ya asili.

Tukio la tatu linawahusu Wakaldayo, katika mstari 17’ wameunda vikosi vitatu vitatu, nao ni watu ambao wameandaliwa na shetani ili kutekeleza yale maongezi ya mwanzo ya Mungu na shetani. Kumbe ni muhimu kuangalia matukio kwa namna ya rohoni, liwe tukio la kukosa umeme au nchi kuwa maskini liangalie kwa namna ya rohoni. Nguvu ya shetani ni kukufanya uwaze kuwa ni tukio la kawaida au la kiasili lakini kumbe kuna nguvu ya shetani nyuma yake. Tukio la nne ni upepo uliotokea na kuangusha nyumba waliokuwepo watoto wa Ayubu waliokuwa kwenye sherehe. Cha ajabu ni kwamba watoto wote wa Ayubu walikufa kwa maana ndio walikuwa walengwa,ila Yule mtoa taarifa hakufa kwasababu si mtoto wa Ayubu na pia hakuwa amelengwa yeye. Kumbe unaweza kuwepo mtego wa kichawi  nao unakuwa umemlenga mtu husika, na ndio maana katika Biblia inataja mitego ya ibilisi, yaani ibilisi anaweza kumtega mtu katika kitabu 2Timotheo 2:26 “wapate tena fahamu zao, na kutoka katika mtego wa ibilisi…..” hivyo alikuwa anabakishwa mmoja kwasababu lile tego halimuhusu, maana tego humlenga mtu au watu husika.

Usione ni kawaida, matukio kama hayo yanapotokea katika maisha yako, mfano, unaanza saluni halafu haifanikiwi kumbe ni kwasababu ya shetani, cha kufanya unatakiwa uingie rohoni kushughulikia. Pigo la Ayubu kubwa la kumwekea majipu katika mwili na magojwa, unaweza kuhangaika hospitali kama hujajua kuwa kimeanzia rohoni, hospitali wataita jipu au cancer lakini kumbe limeanzia rohoni. Na ndio maana unaweza kuona meli zinazama hadi hazionekani kumbe ni kazi za adui shetani, ni muhimu kujua kila unapoona matukio duniani kuna matukio ya kishetani ama yameletwa na shetani au yamesukumwa kuwepo na shetani. Na ndio maana ni muhimu unapoingia kwenye hatari au ajali ukailiitia Jina la Yesu ambalo ndilo pekee tulilopewa kuokolewa kwalo.

1Thesalonike 2:18 “ Nalitaka kuja kwenu….. lakini shetani akatuzuia” shetani anaweza kumzuia mtu, na mara nyingi kwenye kuzuia shetani hutumia watu wa kawaida ili usimtambue. Huwezi kukutana naye macho kwa macho kwasababu anatumia waseba, wakaldayo au upepo. Na ndio maana unaweza ukawa unataka kusafiri lakini ukazuiwa na mtu anayetakiwa akupe viza. Ni muhimu kujifunza kuangalia matukio kwa jicho la rohoni. Kwasababu kama hujui waweza kumchukia mtu, kumbe shetani ndio yupo ndani ya mtu anayekuzuia. Matendo ya Mitume 10:38, Shetani anaweza kumuonea mtu, pia anaweza kumwingia mtu maana aliwahi kuingia ndani ya Yuda, na wakati huo usijue kuwa ni shetani kumbe anatumia mtu. Kabla hujapambana na mtu anza na rohoni kwanza.

Luka 13:16 “…ambaye shetani amemfunga…” kumbe shetani anaweza kumfunga mtu, mapato, ndoto, matumaini au mafanikio. Unapomtaja shetani lazima ujue kuwa ana watumishi wake. Mungu ana watoto wake na shetani pia ana watoto wake, wale wanaotenda mapenzi ya shetani ni watoto wa ibilisi 1Yohana 3:10. Yohana 8:44 “…ninyi ni wa baba yenu ibilisi….” Wachawi na waganga ni wana wa ibilisi hivyo hitekeleza kazi za ibilisi duniani, na hawa ndio wanaoleta matukio mbalimbali. Shatani hushambulia eneo ambalo Mungu amekubarikia, ili usilitumie kukuletea mafanikio kwenye maisha yako.

Jambo la Muhimu ni kwamba; unatakiwa uangalie kila tukio linalotokea katika maisha yako kwa jicho la rohoni, matukio mengi huanzia kwa wakala wa shetani na wachawi. Jambo la muhimu ni kuwa unapookoka unapokea mamlaka dhidi ya shetani na wakala zake. Ni muhimu kuchukua nafasi yako kushughulika na shetani na wakala zake kwa njia ya maombi (katika ulimwengu wa roho). Ukifanikiwa kuharibu chanzo cha tatizo unakuwa umemaliza tatizo asilimia mia moja. 

No comments:

Post a Comment