Thursday, January 24, 2013

UJUMBE: SHERIA YA DHAMBI


Mch. Josephat Gwajima (SNP)

UTANGULIZI:

Warumi 8:1-2 “Sasa, basi, hakuna hukumu ya adhabu juu yao walio katika Kristo Yesu. Kwa sababu sheria ya Roho wa uzima ule ulio katika Kristo Yesu imeniacha huru, mbali na sheria ya dhambi na mauti.” Katika huu mstari wa pili tunaona sheria tatu ambazo Biblia inazitaja, kwanza sheria ya uzima, sheria ya dhambi na sheria ya mauti. Dunia hii inaongozwa na sheria (principles) na ndio maana kuna katika ulimwengu wa kawaida kuna sheria mbalimbali. Mfano sheria ya mvutano (gravitation force) na ndio maana ukichukua jiwe ukalirusha juu litakwenda lakini baada ya muda litarudi chini tena. Na kimsingi huwezi kubishana na sheria hiyo, na ukitaka kuibishia jaribu kwenda gorofani ujirushe lazima utaanguka chini sio kwasababu huna upako bali ni kwasababu ya sheria ya mvutano inayovuta vitu kuja chini.

DUNIA YA KAWAIDA NA SHERIA ZILIZOPO:

Kwa kawaida sheria huwa hazibadiliki, kwa mfano sheria inayosema unavyopanda kwenda juu baridi linaongezeka, hii sheria haibadiliki na ndio maana katika mlima kuna baridi zaidi kwasababu ya sheria ambazo zipo. Na vilevile sheria tulizoziona katika Biblia (warumi 8:2) ni bayana yaani hazitanguki. Na kwa maana hiyo hata nchi ili iwe na amani ni lazima ziwepo sheria na kanuni. Na ili watu wafuate sheria wamewekwa polisi, mahakama na magereza kwaajili ya kuhakikisha zile sheria zinafuatwa.

Unapofanya kosa lolote, unaingia kwenye matatizo kwasababu ya sheria iliyopo, kwa namna hiyo polisi watakukamata na kukupeleka mahakamani unapogundulika una makosa unafungwa, hii yote ni kwasababu ya sheria iliyopo.

MAISHA YA KIROHO NA SHERIA YA UZIMA, DHAMBI NA MAUTI:

Kama tulivyoona sheria za nchi zinazosimamia maisha ya wananchi ndivyo sheria hizi za rohoni zinavyotenda kazi. Kimsingi unapovunja sheria ile sheria inakushusha chini bila ya wewe kujua. Na ndio maana biblia inasema “kwa maana mshahara wa dhambi ni mauti bali karama ya Mungu ni uzima wa milele” Kuna tofauti kati ya mshahara na zawadi, kwasababu unapotenda kazi ni lazima upokee mshahara wake, upende usipende na ulieusilie.

Kimsingi, wewe unaweza ukawa unatenda vitu na hakuna anayekuona, unaweza ukawa umeokoka lakini unatenda mambo mabaya au dhambi katika ulimwengu wa siri. Siku utakayopokea mshahara kila mtu atajua isipokuwa hatojua umepokea hilo kutoka katika kazi dhambi gani uliyotenda. Unaweza kumuona mtu alikuwa wa Mungu lakini akafa ghaflaghafla watu wakasikitika na kumbe umepewa mshahara wa matendo yake ya sirini. Maisha yako ya sirini ni muhimu sana.

SHERIA YA DHAMBI:

Warumi 6:23: “Kwa maana mshahara wa dhambi ni mauti; bali karama ya Mungu ni uzima wa milele katika Kristo Yesu Bwana wetu.”

Ezekieli 18:4: “Tazama, roho zote ni mali yangu; kama vile roho ya baba ni mali yangu, ndivyo ilivyo roho ya mwana mali yangu; roho ile itendayo dhambi itakufa.”

Nini maana ya maneno haya?; hapo mwanzo sheria alikuwa mbinguni, akifikia kipindi akafanya yaliyomaovu na kuasi hivyo akafukuzwa mbinguni. Na alipotupwa duniani akaanzisha utawala wake katika kila mtaa wa  dunia hii ili kutenda kazi kila mahali. Haya majeshi ya pepo wabaya yapo kwaajili ya kuwapa watu mishahara ya matendo mabaya wanayoyatenda.

Kwasababu shetani alikuwa mbinguni, anaifahamu biblia anajua kanuni za Mungu, hivyo, unavyotenda lililoovu shatani anajua kuwa umekosea na amekaa tayari kugawa mshahara. Kumbe mshahara huu hautoki kwa Mungu bali shetani ndiye alipaye. (Yohana 10:10) yaani shetani hatendi kazi isipokuwa kuharibu, kuchinja na kuharibu. Unapotenda uovu kwa siri, mashetani hukaa mahali ili kugawa mshahara wa uovu ile. Na kwa muda ambao mashtaka yapo na hayajakanushwa kwa kutubu, mtu huyo atajikuta anafia dhambini. Kwa namna hiyo watu wengi wanaishi kwenye magonjwa na matatizo yanayotokana na maisha yao ya sirini ambayo hakuna anayejua.

Kiukweli hakuna dhambi ndogo wala kubwa, hivyo dhambi iliyondogo sana yaweza kumpeleka mtu Jehanamu. Dhambi ambazo watu huzidharau na kuziita ndogo ndizo zipelekazo watu Jehanamu bila hata ya wao kujua. Jifunze kutubu kila unapojikuta unamkosea Mungu.

Ni muhimu kutafuta mahali ulipouacha upendo wako wa kwanza, uhurudie na ukatubu. Mungu ni mwenye rehema atakusamehe kabisa na hatoyakumbuka makosa yako tena. Tengeneza maisha yako ya rohoni.

No comments:

Post a Comment