Friday, February 8, 2013

UJUMBE: KUPAONDOA HAPO AKAAPO SHETANI


Na Mch. Frank Andrew (RP)                                                   8th Feb. 2013Ufunuo 2:13-14 “napajua  ukaapo…. Hapo akaapo shetani” Yesu anaongea na kanisa kuwambia kuwa hapo ukaapo ndipo akaapo shetani; anaendelea kwa kusema “nawe walishika sana jina langu,wala hukuikana imani” kuna watu wanaishi wanamjua Mungu lakini bado mahali wakaapo ndipo penye makao ya shetani. Baada ya somo hili utaweza kujua na kuangamiza na kupaondoa kila mahali pa maisha yako ambapo shetani anakaa.

Dalili za akaapo shetani (Ufunuo 2:13-15):
1. Kuna mafundisho ya Balaamu.
2. Kuna mafundisho ya ukwazo.
3. Mafundisho ya kulaani watu wa BWANA.
4. Vitu vilivyotolewa sadaka kwa sanamu.

Dalili ya nne inataja sanamu, utajiuliza kwanini Mungu anakataza sana kwa habari ya sanamu mara kwa mara katika Biblia?. Jibu ni kwamba nyuma ya kila sanamu kuna roho, tunaweza kujifunza kitu kupitia Danieli 3:13-23 hii ni habari ya Shedraka, Meshaki na Abednego, Mfalme alisimamisha sanamu ili watu wote waibudu. Lakini watu hao wa Mungu watatu hawakukubali kuitumikia wala kuibudu sanamu kwasababu walijua kuwa nyuma ya ile sanamu kuna roho ambayo si Mungu JEHOVA yaani (miungu inayotumikiwa). kumbe shetani alikuwa amekaa nyuma ya ile sanamu na ndiye aliyekuwa anataka kuabudiwa.

Kama mtu uliyeokoka ni muhimu ukapajua mahali ambapo shetani anakaa katika maisha yako. Ili shetani akae mahali ni lazima kuwe na kiti chake cha enzi, ama wewe mwenyewe umepaweka kwa kupenda au watu wengine wamekuwea. Na shetani amekuja na kutawala maisha na kazi yake ni kuchinja, kuharibu na kuiba (Yohana 10:10) na ndio maana pepo wachafu wengi huwa wanasema “kiti wangu kiti wangu” ni kwasababu shetani katika ulimwengu wa roho amekaa katika maisha ya mtu huyo.

Kiti cha kwanza cha shetani ni dhambi (hii ni kumtengenezea kiti shetani mwenyewe), kuna tabia ndani ya mtu ambazo zinaweka kiti cha enzi cha shetani kwenye maisha yako. Tabia ya kiburi, mfano wa Naamani kiti chake cha enzi kilikuwa kwenye kiburi (2Wafalme 5:1-12) kiburi kilitaka kumkosesha muujiza wake. Alipokuwa na ukoma akamwendea nabii Elisha, naye akamwambia akajichovye kwenye mto wa Yordani uliokuwa na matope, lakini mwanzoni Naamani akajibu kwa dharau kuwa ameacha “mito bora kuliko yote ya Israeli kule alikotoka”. Hiko ndicho kinaitwa kiburi kwa kiti hicho shetani ameendelea kukaa katika maisha ya watu wengi, ni muhimu kujua kuwa Mungu hutenda kazi kupitia mambo madogo na hata Musa alikutana na Mungu katika kichaka, hivyo kuna viti vingine vinaondoka kwa kuamua kujishusha na kusikiliza kile watumishi wa Mungu wanachokwambia aua neno la Mungu linachokwambia.

Kimsingi, kuuleta utakatifu ni kumchafulia shetani mji; Paulo alipomtoa pepo wa utambuzi ndani ya kijakazi, wakamwita “anayechafua mji”. Kuna dhambi inatendwa ndani ya mtu na dhambi inayotendwa nje ya mtu. Watu wengi hutubu dhambi za nje kwa urahisi bali wengi husahau kutubu dhambi za ndani (moyoni) ambazo ni mbaya kama vile kutokusamehe, uchungu na wivu. Hizi ni hatari kwasababu hazijawahi kutubiwa. Dhambi za namna hii zinaleta madoa madoa katika vazi la utakatifu na wakati huohuo, Biblia inasema hakuna chenye madoa wala mawaa kitakachoingia mbinguni. Ili kujisafisha ni muhimu kutubu dhambi hizi na kunena kwa lugha muda wa kutosha ili kumruhusu Roho mtakatifu aombe ndani yako.

Pia, kiti cha enzi kingine cha kujiwekea ni pale unapoamua kwenda kwa mganga wa kienyeji ili kupokea makombe, kupigwa chale au kutoa kafala. Mizimu na waganga huweka viti vya enzi kwenya maisha ya watu. Pia, katika sherehe za arobaini za misiba kunakuwa na ibada kamili kabisa ambazo zinaweza mpa shetani kiti cha enzi katika maisha yako. Kwa namna hii shetani anapata nafasi kabisa katika maisha ya watu wengi bila ya wao kujua yaani unampa shetani mamlaka kamili juu ya maisha yako.

Vipo viti vya Enzi vya kuwekewa; ama na wachawi au waganga. Hawa ni pepo wachafu wanaotumwa kwenye maisha yako ili watende kazi ya kufunga maisha yako na kuweka mateso aidha ndani yako au kwenye familia. Unakuta mtu anamatatizo ya ndoa, matatizo ya shule, woga, wizi au tabu mbalimbali kwasababu ya kiti cha enzi cha shetani kilichowekwa kwenye maisha yake.

Viti vya enzi vingine ni vya familia au ukoo, havi husimamia tabia zinazofanana. Pia mara nyingi ukoo ulio chini ya kiti cha enzi hicho, watu wake huwa wanakufa vifo vinavyofanana na matatizo yanayofanana. Katika ukoo wa namna hii unakuta wanaukoo wote ni maskini, hawaoi, hawaolewi, au wakiolewa waume wao wanakufa; hii yote ni kazi ya kiti cha enzi cha shetani katika ukoo. Ndio maana ni muhimu kuwa makini na sherehe za koo na kimila. Ili kukomboka ni lazima umuondoe aliyekaa kwenye kiti cha enzi hiko kwa kutumia Jina La Yesu.

Bomoa pale akaapo shetani katika jina la Yesu, viti vya enzi vyote kama hirizi, na dawa za kiganga sambaratisha katika Jina la Yesu kristo. Tumepewa mamlaka ya kuwashinda waganga, wachawi na wote wanaofunga maisha yetu. Mungu akuweke huru katika Jina la Yesu.

-Frank Andrew-
Resident Pastor

No comments:

Post a Comment