google.com, pub-4324601895065941, DIRECT, f08c47fec0942fa0

Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

UJUMBE: MATUKIO YA KICHAWI (sehemu ya pili)

Na Mchungaji Kiongozi: Josephat Gwajima                                      03 Februari, 2013



Josephat Gwajima
SENIOR PASTOR G.C.T.C
UTANGULIZI:

Watu wengi wanajiuliza kwanini tunazungumzia uchawi mara nyingi, hii ni kwasababu shetani hutumia wachawi katika kutenda kazi duniani; na ndio maana katika Biblia kuna maandiko mengi yanayotaja uchawi na wachawi kama ifuatavyo:- Hesabu 23:23 24:1; 1Wafalme 9:22; 2Wafalme 17:17; Isaya 47:9,12; Mika 1:12; Nahumu 3:4; Matendo ya Mitume 8:9; 18:11; Wagalatia 5:20; 3:1; Ufu 9:21. Ni kweli tumepewa mambo yote na Mungu kama vile afya na mafanikio lakini shetani kupitia wachawi amekuwa akizuia, hivyo tunatakiwa kushughulika nao katika ulimwengu wa roho.. Katika sehemu ya kwanza ya somo hili tuliona kwa habari ya Ayubu ambapo shetani alipata ruhusa ya kugusa maisha yake. Shetani hakumtokea Ayubu kwa namna ambayo angemfahamu kuwa ni shetani, lakini alimjia kwa njia ya matukio, kumbe waweza kuwa unapitia kwenye hali mbaya kumbe ni matukio yanayosababishwa na wachawi.



Wakristo walio wengi wanapambana na shetani bila kujua nguvu za adui wanae pamaba nae. Nchi ya Japani ilipokuwa haijui kuwa Marekani wana bomu la nyuklia; waliwachokoza wakidhania kuwa watashinda, Lakini matokeo yake walishindwa kwasababu walikuwa hawajui nguvu ya wanayeshindana naye. Mara nyingi watu wengi hupambana na shetani bila kujua nguvu zake na matokeo yake wengi huishia kushindwa. Huwezi kupambana na adui usiyemjua,  vivyohivyo ili uweze kumshinda shetani ni lazima uanze kwa kutafuta maarifa kuhusu yeye.



MAFURIKO YA KICHAWI:

Ufunuo 12:13-16 Yule Joka alikuwa shetani, Biblia inasema Yule joka akatoa maji kama mto; kwa kawaida ingeonekana kama mafuriko ya maji dhidi ya yule mwanamke. Kumbe kuna matukio yanaweza kutokea kwenye maisha yako au kwenye nchi, na kumbe yamesababishwa na wachawi. Si kila moto au mafuriko ni ya kiasili, mengi huwa yanasababishwa na shetani ili kuua watu ili awashushe kuzimu. Kuna matukio yanatokea unadhania kuwa ni ya kawaida kumbe yameletwa na wachawi ili kuangamiza watu. Ni muhimu kujifunza kuyaangalia matukio kwa jicho la rohoni.



BIASHARA ZA KICHAWI:

Ezekieli 28:16, 18. “kwa wingi wa uchuuzi wako; watu walikujaza udhalimu” shetani mfanya biashara naye hutenda kazi pamoja na wachawi na waganga wa kienyeji. Kwa njia hii shetani anafunga maisha ya watu, na ndio maana  kuna watu wanafanya biashara za kichawi, Yaani wanamwendea shetani halafu wanamuomba aiwezeshe biashara yao kwa kumpa shetani ama damu au kafara. Wachawi wanapokuwa wanatoa kafara, huwa wanakuwa wanafanya biashara na shetani. Ufunuo 18:1- mstari 5” “wafanya biashara wa nchi wamepata mali kwasababu ya kiburi chake” mstari 11” “nao wafanya biashara wa  nchi walia na kuomboleza maana hapana mtu anunuaye bidhaa zao tena” mstari 13  biashara ya roho na miili ya wanadamu. Kumbe biashara nyingi unazoona watu wanafanya duniani, ni biashara za kichawi. Yaani mtu anafanya biashara lakini ndani yake kuna uvuvio wa kishetani, Nahumu 3:4. Ndio maana biashara za watu wengi hazifanikiwi wakati huohuo watu wanaomtegemea shetani wanafanikiwa kwa haraka ni kwasababu wameuza roho zao kwa shetani.



Matendo ya Mitume 16:16-17; 19:24 “aliyewapatia bwana zake faida nyingi” biashara hizi zipo kabisa, na ndio maana unaweza kufanya biashara lakini wenzako wanauza zaidi kuliko wewe hata kama wote mnauza bidhaa ileile, kumbe wenzako wamenuiza ili wao wauze na wewe usiuze. Ni vizuri kuanza kufanyabiashara na BWANA, yaani kabla ya kuanza biashara ni muhimu kufanya maombi kwanza ili kuiweka biashara yako katika ulinzi wa Mungu. Unapotaka kuanza biashara fanya na BWANA.



MAGONJWA YA KISHETANI:

Kuna watu ni wagonjwa sasa kwasababu ya wachawi. Magonjwa mengi sana husababishwa na wachawi. Unaweza kuwa unasumbuliwa na magonjwa yasiyopona kwasababu ya chanzo chake ni cha rohoni. Na ndio maana unapooumwa hata kama utaenda hospitali unatakiwa usiache maombi kwasababu shetani anaweza kusababisha magonjwa, hata Ayubu aliumwa majipu mabaya ambayo kimsingi yalisababishwa na shetani.



BIBLIA NA MATUKIO YA KICHAWI:

Mathayo 9:32 “tazama walimletea mtu bubu mwenye pepo, na yule pepo alipotolewa alinena” huyu ni mtu ambaye watu walipomuangalia walimuona ni bubu. Cha ajabu Yesu alipomuona hakushughulika na ububu bali alishughilika na pepo kuonyesha kwamba ule ububu ulisababishwa na pepo. Kuna mambo mengi ambayo yanasababishwa na shetani, hivyo unatakiwa kuyashughulikia.

Mathayo 13:10-15 “alikuwa na pepo wa udhaifu kwa muda wa miaka kumi na nane…” 15” “na huyu mwanamke aliye uzao wa Ibrahimu ambaye shetani shetani amemfunga” watu walishamzoea kumwona kuwa ni mama mwenye kibiyongo yaani hawezi kujinyoosha kabisa lakini Yesu alipomtoa pepo Yule mama alipona.



Wachawi wapo na watu wengi wanalogwa, Kumbukumbu la Torati 18:11; watu wanalogwa na wanalogeka, matatizo ya watu wengi yanasababishwa na shetani kupitia matukio ya kichawi. Marko 9:17; kuna magonjwa ambayo yanakuja kwenye maisha ya mtu kwasababu ya kulogwa. Katika utendaji kazi wa shetani anaweza akaingia ndani ya mtu na kumfunga, lakini pia shetani anaweza kumkandamiza mtu akiwa nje ya mwili na ndio maana kwa watu waliokoka lakini hawapigani vita ya rohoni wanaweza kujikuta wanakandamizwa na shetani akiwa nje yao. 1Wathesalonike 2:18, Paulo hakuwa amepagawa na pepo lakini shetani alimzuia. Zekaria 3:1. Shetani anaweza kukuzuia kutokea nje, yaani unahitaji kwenda nje ya nchi lakini shetani anakuzuia kupitia mtoa pasi ya kusafiria. Matendo ya Mitume 13:6 hata wachawi hupambana pia ili kukuzuia, ni muhimu kuishi maisha huku ukijua kunakushindana rohoni. 



JINSI YA KUSHINDA DHIDI YA MATUKIO YA KICHAWI

Mpokee Yesu kwanza; huwezi kushindana na shetani kama hujaokoka, ni muhimu umpokee Yesu kwanza ili akuwezeshe kupigana katika vita dhidi ya shetani. Jifunze kuomba mwenyewe; baada ya kuokoka kuna amani ya mwanzo unayoipata ile isikufanye ukasahau kuwa tupo vitani, kama tulivyoona hapo juu wanaoshindana nawe wanaweza kuwa ndani yako au nje yako. Katika hali hiyo unachotakiwa kufanya ni kujifunza kuomba mwenyewe kwasababu hata ukitegemea kuombewa kila siku, kuna muda utakuwa mwenyewe, na hapo unatakiwa usimame mwenyewe. Mtu uliyeokoka unatakiwa uhame kwenye ule wokovu wa kuombewa uhamie kwenye wokovu wa maarifa na kupambana kwa kutumia Jina la Yesu Kristo.


-Josephat Gwajima-

Senior Pastor G.C.T.C
 

Post a Comment

0 Comments