Sunday, March 17, 2013

UJUMBE: KUVUKA

Na Mch. Frank Andrew                                               17/3/2013

Inawezekana unapita katika hali ngumu ambayo umewekewa vizuizi ili usifikie mpenyo wa maisha yako.  Inawezekana kuna mambo ambayo katika maisha yako unahitaji kuvuka; ndio maana kuna watu wanasema “nikivuka katika hili nitamtukuza Bwana”. Kwasababu hiyo Mungu ametupa neema ya kujifunza leo kuhusu kuvuka. Mara zote katika biblia neno kuvuka limefuatana na kumiliki. Ukisoma katika Kumbukumbu 4:14, 23; 9:23; 11:11; 30:18, Maandiko hayo yote yanaonyesha kuwa hatma ya kuvuka ni kumiliki. Watu wengi hushindwa kumiliki kwasababu ya kushindwa kuvuka.

Wana wa Israeli walipokuwa wanataka kumiliki nchi ambayo Bwana aliwaahidia iliwapasa kuvuka mto Yordani kwanza, Kumbukumbu 9:1Basi fahamu ya kuwa siku hii ya leo, Bwana Mungu wako ndiye atanguliaye kuvuka mbele yako kama moto uteketezao; atawaangamiza, tena atawaangusha mbele yako; ndivyo utakavyowafukuza na kuwapoteza upesi, kama alivyokuambia Bwana.

Yesu alipoona kuwa makutano wamemzunguka aliwaamuru wanafunzi wake kuvuka hata ng’ambo, Mathayo 8:18. Hapa siongelei bahari ya  mwilini bali naongelea hali ya kiroho ambayo katikati umewekewa mpaka. Wachawi wamekuwekea mpaka kwenye mafanikio yako, umewekewa mipaka katika masomo yako, mipaka katika mahusiano yako au mipaka katika maendeleo yako. Mpaka huo umekuwa kama bahari katika ulimwengu wa roho ikuzuiayo kuvuka kwenda katika mafanikio yako.


Maisha ya Yesu yalionekana tangu mwanzo kabla hajazaliwa yaani aliwekewa kufanya hayo. Kwanza, maisha ya Yesu yalionekana kupitia nyota yake; pili, maisha ya Yesu yalionekana kupitia mambo aliyoandikiwa na manabii kabla hajazaliwa. Kumbe maisha ya mtu yaweza kuandikiwa na watu rohoni, vivyohivyo kuna watu ambao wameandikiwa mistari ya rohoni ili usivuke na kumiliki. Wachawi na waganga wanaweza kukuwekea mipaka ya rohoni ili usiweze kumiliki, unaweza kuwekewa mpaka wa mahusiano yaani unapata mtu wa kukuoa lakini hauwezi kufikia hatma ya ndoa. Lakini jambo la muhimu kujua ni kuwa yupo Mungu aliye mkuu kuliko waweka vizuizi hivyo.

Wakati mwingine shetani anaona kuwa akikuachia ufanikiwe, utawasaidia wengine sasa hapo anakuwekea kizuizi ili familia au ukoo wako wote ubaki chini. Lakini haijalishi ni mizimu au mababu wa ukoo ndio walioweka mpaka lakini tuna amri moja ya kuvuka. Pamoja na mpaka uliowekewa ofisini kwako ili usivuke hapa kuna neno moja tu, Utavuka. Kuvuka ni haki yako.

VIZUIZI VYA KUVUKA:
1.Kuambatana na Mtu mwenye ugomvi na Bwana
Mfano wa Yona:
Neno la BWANA lilimjia Yona kumtaka aende Ninawi, lakini Yona akakataa akaamua kupanda meli iliyokuwa imebeba shehena kwenda Tarshishi. Kwasababu ya kumbeba Yona kwenye meli yao wakalazimika kumwaga shehena yote. Ni kweli wafanyabiashara hawa wangepata faida baada ya kuvuka lakini kwasababu ya Yona wakajikuta wanapata hasara. Hapa tunajifunza kuwa wakati mwingine unaweza kushindwa kuvuka kwasababu ya kuwa karibu na mtu mwenye ugomvi na bwana. Unaweza ukawa haufanikiwi katika biashara yako kumbe ni kwasababu umembeba Yona katika biashara hiyo. Kizuizi cha kuvuka chaweza kuwa ni pepo wachafu, mikoba ya kichawi au hirizi za waganga wa kienyeji.

2.Hofu
Kizuizi kingine cha kuvuka ni hofu; hili tunaliona kwa wanafunzi wa Yesu walipohitaji kuvuka kwenda ng’ambo. Hofu ni adui mkubwa wa kuvuka kwasababu mwishowe hofu hutengeneza lawama. Marko 4:35-41, Yesu Aliwaambia wanafunzi wake wavuke ng’ambo, lakini wakiwa katika kuvuka wakakutana na dhoruba baharini. Wanafunzi wakaingiwa na hofu wakaanza kupiga kelele, na kulaumu lakini Yesu alipoamka akakemea ule upepo. Hapa tunajifunza kuwa kwenye kuvuka katika hatma njema ya maisha yako lazima ukutane na upepo wa kukuzuia. Hofu yaweza kukufanya ushinde au usishinde kuvuka na kufika kwenye hatma yako. Na mara zote ukishindwa kuvuka kwasababu ya hofu hutengeneza lawama.

Inawezekana wanaokuzuia kumiliki ni watu wengine, lakini ahadi ya Mungu ni kwamba ukifanikiwa kuwapiga wanaokuzuia kumiliki lazima umiliki. Wana wa Israeli walipowapiga wanaowazuia waliwateka nyara na kuwamiliki wao na mali zao. Anayekuzuia kumiliki cheo chako basi jua kuwa utachukua chake. Bidii na nguvu yako ya kuvuka ndio haraka ya kumiliki, baada ya kuokoka unapokea mamlaka ya kuvuka. Na ukifanikiwa kuvuka utavuka na nyumba yako pia.

Matendo 16:8-9 “Wakapita Misia wakatelemkia Troa. Paulo akatokewa na maono usiku; alimwona mtu wa Makedonia amesimama, akimsihi, na kumwambia, Vuka, uje Makedonia utusaidie.” Kuna watu wanaohitaji uvuke ili uwasaidie, baada ya kuvuka vusha na wengine. Kuna watu ambao Mungu aweita wamtumikie au wana ndoto ya kutumikia Mungu, lakini kutokana na vizuizi wamejikuta wakikatishwa tamaa. Lakini leo kuna habari njema kuwa ukipambana utavuka na kumiliki. Vuka mstari waliokuchorea waganga na wachawi katika ulimwengu wa roho kwa Jina la Yesu Kristo!!!


Mchungaji Fank Andrew akitoa maneno ya uzima kanisani Ufufuo na uzima Kawe katika  ibada ya jumapili


Mchungaji Frank wa Ufufuo na Uzima akifundisha Kuhusu kuvuka katika maeneo mbali mbali ya maisha katika ibada ya jumapili iliyofanyika kanisani Kawe

Muimbaji wa nyimbo za Injiri Enock Jonas akiimba katika ibada ya jumapili kanisani Ufufuo na uzima

Muimbaji wa nyimbo za Injiri Enock Jonas akiimba wimbo wa Wema wa Mungu


Mchungaji Maximillian Machumu maarufu kama Mwanamapinduzi akiimba wimbo wake wa mapinduzi ya rohoni katika ibada ya Jumapili kanisani Ufufuo na Uzima


Platform choir wakiongoza kusifu na kuabudu katika Ibada ya Jumapili kanisani Ufufuo na Uzima 


Baadhi ya waimbaji wa Platfotm Saraphiner Urio(mwenye kipaza sauti),Omega Mwangela(mwenye gitaa),Pastor  Amosi (kwenye kinanda)na Pastor Peter wakongoza Ibada ya sifa kanisani Ufufuo na Uzima


Baadhi ya waimbaji wa platform wakimsifu Mungu


Waimbaji wa Platform wakiliinua jina la Bwana kanisani Ufufuo na UzimaKuna watu wanatakiwa kuvuka kwenda mahali fulani kwenye maisha yao lakini wanashindwa kuvuka kwasababu wamewabeba akina Yona(watu wenye ugomvi na Bwana) katika maisha yao
Pastor Frank Andrew

No comments:

Post a Comment