Sunday, March 31, 2013

KUTANGULIA KWENDA GALILAYA


Na Mch. Frank Andrew (RP)                                                                    31/3/2013


Mchungaji Frank Andrew (Resident Pastor)
Mathayo 28:1-7; Kama unavyojua Yesu aliposhtakiwa, mashtaka yake makubwa hayakuwa na vithibitisho vya kuonekana bali yalisimamia katika yale waliyosema. Kwa mashtaka hayo, wayahudi walimsulubisha. Maneno kama “mfalme wa wayahudi” “mkilibomoa hekalu nitalijenga ndani ya siku tatu” lakini pamoja na maneno yote aliyowahi kusema, kuna siku Yesu alisema “atafufuka baada ya siku tatu, watangulie kwenda Galilaya”. Na ndio maana wale Mafarisayo walimwendea Pilato kuomba walinzi wa kulinda lile kaburi ili wanafunzi wasiuibe mwili wake (Mathayo 27:62-66).

Ukifuatilia kwa makini utagundua kuwa Yesu walimshtaki kwa maneno yake, kwasababu hii tunajifunza kuwa maneno anayosema mtu yana nguvu sana.  Katika kitabu cha Yoeli 3:10 “Yafueni majembe yenu yawe panga, na miundu yenu iwe mikuki; aliye dhaifu na aseme, Mimi ni hodari.” Kumbe unapokuwa katika udhaifu hutakiwi kukiri udhaifu huo, Unachokitamka kina nguvu sana. Kuna watu wanaishi katika maisha ambayo sio sawa kwasababu ya kutamkiwa maneno na watu.

Pia katika Mwanzo 1:1-.. Utaona kuwa hata mbingu na nchi ziliumbwa na Mungu kwa neno lake, Mungu alisema na ikawa kama vile alivyosema. Kuna nguvu katika kusema, kwasababu mtu aliyeokoka nyuma yake kuna nguvu ya kulitimiza lile neno. Kuna nguvu ya ajabu sana katika kusema, ndio maana katika kumsulubisha Yesu wayahudi walipaza sauti kusema na sauti zao zikashinda sauti ya Pilato. Maneno yana nguvu.

Inawezekana kuna watu wamepatana kwa ajili ya kukuangamiza wewe, usikate tamaa maana hata wakati wa Yesu Herode na Pilato walipatana ili kumsulubisha Yesu (Luka 23:8-12). Inawezekana upo kwenye matatizo leo kwasababu ya maneno uliyowahi kuyasema, mfano; walisikia ukitamka kujenga wakaamua kukuendea kwa waganga ili usifanikiwe. Inawezekana ulitamka kufaulu na adui zako wakaamua kupatana ili kukufelisha. Ni muhimu kujua kuna watu walipatana kumuua Yesu ili kwa njia hiyo awasambaratishe wapatanao kinyume nawe.

Kusema kwa imani ni nguvu ya kuuleta muujiza wako; maana hata yule mama aliyetokwa na damu alianza kwa kusema moyoni mwake kuwa nikiigusa pindo la vazi lake nitapona. Ingawa Yesu alikuwa njiani tu akitembea lakini mwanamke yule alipokea muujiza wake pale pale. Kumbe uponyaji wa mwanamke yule ulipatikana kwa njia ya kutamka. Ni muhimu kujua kila mtu aliyeokoka ana Roho Mtakatifu ndani yake ambaye hulivalisha mwili kila neno linalotamkwa. Ukitamka uzima Roho Mtakatifu atatia uzima, ukitamka ushindi Roho atalivika neno lile ushindi ndani ya maisha yako.

Unalotamka kwa Jina la Yesu, lazima litimie, pokea uponyaji uliousema katika jina la Yesu. Pokea neema ya kutimiza ulichokisema. Maneno yako yana nguvu, unachokitamka kina nguvu nyuma yake. Yesu alisema atafufuka siku ya tatu, na baada ya siku tatu alifufuka kama alivyosema. Pamoja na walinzi kulinda kaburi lakini hawakuweza kuzuia neno la Yesu kutimia. Vivyohivyo leo hakuna wa kuzuia utakachotamka kwa imani. Ndio maana sherehe ya ukweli ya pasaka ni kuwatoa watu kutoka katika magereza na vifungo vyao ambavyo vimekaa kama kaburi kwao. Kama vile Yesu alivyofufuka kutoka kaburini vivyohivyo kwa kutamka utatoka gerezani leo (Matendo ya Mitume 12:1-5).


Pasaka ilianza pale wana waisraeli walipotoka kutoka Misri, Kutoka 12:31-36 “Akawaita Musa na Haruni usiku, akasema, Ondokeni tokeni katika watu wangu, ninyi na wana wa Israeli; enendeni, kamtumikieni Bwana kama mlivyosema. Twaeni kondoo zenu na ng'ombe zenu kama mlivyosema, enendeni zenu, mkanibariki mimi pia. Wamisri nao wakawahimiza watu, kuwatoa katika nchi kwa haraka, maana walisema, Tumekwisha kufa sote. Watu wakauchukua unga wa mikate yao kabla haijatiwa chachu, na vyombo vyao vya kukandia wakavitia ndani ya nguo zao mabegani. Wana wa Israeli wakafanya kama neno lile la Musa; wakataka kwa Wamisri vyombo vya fedha na vyombo vya dhahabu, na mavazi. Bwana akawajalia kupendelewa na Wamisri hata wakawapa kila walichokitaka. Nao wakawateka Wamisri nyara.Na wana wa Israeli walipotoka Misri hawakutoka utumwani mikono mitupu bali walitoka na mali nyingi. Waliokuweka katika kifungo wataona unatoka  na unaondoka na mali zao. Walikuzuilia cheo chako, unatoka na unachukua cheo chake. Ni kutamka tu kuwa “nataka”

Usijiulize yatakuaje mambo haya; kwasababu miaka mingi iliyopita Yesu alisema kuwa siku ya tatu nitafufuka na kuwatangulia Galilaya. Tumepewa mamlaka ya kusema na kutimia katika Jina la Yesu.
No comments:

Post a Comment