Monday, March 4, 2013

UJUMBE: VIFUNGO VYA TABIA


Na Mch. Josephat Gwajima                                                                 04.03.2013

Utangulizi:
Shetani hajabadilika na silaha zake ni zilezile; na jambo kubwa linaloshangaza watu ni kwamba silaha za shetani ni zilezile lakini bado zinatenda kazi kwenye maisha ya watu. Moja ya kifungo kinachosumbua watu ni kifungo cha tabia.  

Mara nyingi kupata urafiki au uhusiano ni rahisi lakini ili uweze kuendelea kuwa karibu na watu hao unatakiwa uwe na tabia nzuri. Hivyo shetani anaweza kukuacha usonge mbele na kazi ya Mungu lakini akakuzuia kupitia vifungo vya tabia. Kwasababu hii Roho Mtakatifu ametaka leo tujifunze kuhusu vifungo vya tabia:

KIPAWA NA TABIA YA MTU:
Kuna vitu kadhaa vya kuangalia kama mtu wa Mungu unayehitaji kufanikiwa, cha kwanza ni kipawa na pili ni tabia ya mtu.

Mithali 18:16 “zawadi ya mtu humpatia nafasi, humleta mbele ya watu wakuu; ” hili neno zawadi kwenye Biblia ya kingereza linaitwa “GIFT” au kwa Kiswahili kipawa. Sasa basi kipawa cha mtu chaweza kumfikisha mbele za watu wakubwa na kujulikana. Mfano mtu anaweza kuwa na kipawa cha uwimbaji lakini anakaa kijijini na umaskini, ila kile kipawa chake kikionekana kinaweza kumleta mtu huyo mjini hii ndio maana ya sehemu ya kwanza ya andiko hilo. Kwasababu hiyo kila mtu aliyepo duniani amepewa kipawa na Mungu ambacho kwa hicho anaweza kufika kwenye hatua ya juu zaidi.

Sasa basi kipawa cha mtu humleta mtu kwenye mafanikio yake, tatizo linakuja pale mtu anapokuwa na kipawa lakini tabia yake si nzuri. Hivyo tabia ndio ambayo inakubakiza katika sehemu uliyopo. Mtu anaweza kuwa na macho ya rohoni au upako lakini kama tabia yake ni mbaya hakuna mtu atakayetamani kuwa karibu naye. Ili Mungu akutumie kwa kiwango cha juu ni muhimu kuanza kwa kubadili tabia yako.

TABIA ZA KIMUNGU NA TABIA ZA ASILI:
Biblia imeainisha tabia za aina mbili, yaani tabia ya Kimungu na tabia ya kiasili au ya mwilini. Katika 1Wakoritho 2:14 “Basi mwanadamu wa tabia ya asili hayapokei mambo ya Roho wa Mungu; maana kwake huyo ni upuzi, wala hawezi kuyafahamu, kwa kuwa yatambulikana kwa jinsi ya rohoni.” 1Wakorintho 3:1 kuna tabia za rohoni na tabia za mwilini. Hivyo anachosema Mtume Paulo ni kwamba unapoongea na watu inabidi ujue ama mtu huyo ana tabia za rohoni au za mwilini. Mfano mtu anaweza kuwa mwimbaji mzuri lakini ana tabia ya uongo; Mtu mwingine anaweza kuwa na kipawa kitakachomfanya apate mchumba; lakini kama tabia yake ni mbaya ama uongo, au umbeya au uzinzi inaweza kumfanya kuachwa na mchumba wake sio kwasababu hapendwi bali kwasababu ya tabia. Tabia ya Kimungu ni tabia njema na nzuri lakini tabia ya kibinadamu ni tabia mbaya aliyonayo mtu.

Shetani akitaka kuharibu kipawa cha mtu anaanzia kwenye tabia yake; kwa maana hiyo tabia ya kibanadamu au ya mwilini ndio hiyohiyo Biblia inaiita tabia ya kishetani. Ukisoma katika Yakobo 3:15 “Hekima hiyo siyo ile ishukayo kutoka juu, bali ni ya dunia, ya tabia ya kibinadamu, na Shetani.” Unaona kumbe tabia mbaya ya kinadamu ndio hiyo inaitwa tabia ya kishetani. Mhubiri 10:1 “Mainzi mafu huvundisha marhamu ya mwuza marashi;  Kadhalika upumbavu haba ni mzito kuliko hekima na heshima.” Hili ni neno la hekima la Mfalme Suleimani kusema mainzi wanaweza kuharibu marhamu nzuri; ikimaanisha unaweza kupata mpenyo katika maisha lakini tabia mbaya inaweza kukupeleka mbali kabisa na upenyo wako.

Ndio maana waweza kumkuta mtu ni mwombaji au anatenda miujiza lakini tabia yake ikawa mbaya kwasababu ya asili. Jambo hili ndlo linalosabisha watu wengine kusema “kama ulokole ndio huu sitaki kuokoka” kumbe mtu huyo aliwahi kumuona mtu ambaye ameokoka na ananena au anaombea watu lakini ni mwongo au mzinzi. Katika Biblia, Samson alikuwa mnadhiri wa Mungu na alikuwa amepakwa mafuta tangu tumboni mwa mamaye. Japokuwa alikuwa mpakwa mafuta lakini alikuwa na tabia mbaya ya kutaka wasichana wa kifilisti ambao Mungu alikataza tangu mwanzo. Hii ni sawa na mtu kung’ang’ania kufungwa nira na mtu asiyeamini. Kwa njia hii Samson akakutana na Delila ambaye lengo lake halikuwa upendo bali ni kumharibia kipawa chake kwa kuijua siri yake. Vivyohivyo shetani amewaangamiza watu wa Mungu wengi kwa kuwafanya waoe au kuolewa na watu wasiomjua Kristo na matokeo yake kile kipawa cha Kimungu kilichokuwa ndani yao kinashindwa kuonekana tena.

KUBADILI TABIA:
Tabia mbaya ya mtu huondoka kwa kuamua mwenyewe, hata kama mchungaji akuombee mara zote kama tabia yako ni mbaya kwa asili inakulazimu kuamua kuibadili mwenyewe. Ni kweli tabia yako inaweza kuwa imeshakupotezea kibali kwa watu au imeshakupotezea upenyo katika maisha lakini ukiamua kuanza upya na BWANA na kuacha zile tabia mbaya Mungu wetu ni wa nafasi ya pili. Mungu wetu anatoa nafasi ya pili biblia inasema, “usifarahi ee adui yangu niangukapo mimi nitasimama tena”

Leo naongea na watu ambao walikuwa waombaji leo hawaombi tena, walimuhofu Mungu lakini leo hawana hofu, walikuwa watakatifu lakini leo ni waovu wakubwa Mungu anayo nafasi ya pili kwaajili yako. Amua kutubu na kuacha dhambi na tabia hiyo mbaya; Mungu atakuwezesha tena kama alivyomwezesha Samson kuwaangamiza wafilisti wote. Hivyo uamuzi wa kwanza ni kuamua mwenyewe kuacha tabia hiyo.

No comments:

Post a Comment