Sunday, March 10, 2013

UJUMBE: WALIONIFUNGA WALIISHIA KUPIGWA


Na Mch. Maximillian Machumu                                                       10.03.2013
Mchungaji Maximillian Machumu (RP) akihubiri
jumapili hii
Waamuzi 15:9-16: Samson alikuwa mnadhiri wa Mungu na aliwekwa kuwaangamiza wafilisti, kwasababu ya kuwaangamiza Wafilisti ndugu zake wakaamua kumfunga na kumkabidhi kwa wafilisti ili wasije kulipa kisasi kwa wao. Katika kumfunga Samsoni, ndugu zake wapatao elfu tatu walitumia kamba mbili; kuna mambo mengi ya kujifunza kupitia habari hii ya Samsoni:KWANINI NDUGU WALIMFUNGA: kama tulivyosoma katika kitabu cha Waamuzi 15:9-16, ndugu zake ndio waliohusika kumfunga Samsoni. Hapa tunajifunza kuwa mara nyingi adui (shetani) anapotaka kumfunga mtu hupitia kwa watu wake au wanaomjua mtu huyo vizuri. Kifungo kinachotokana na watu wako wa karibu ni kibaya zaidi kwasababu wanaujua udhaifu wako; muda gani unaomba na muda gani huombi.

Ndio maana hata Mtume Paulo aliwahi kutegeshewa nyoka kwenye kuni (Matendo ya Mitume 28:3). Nyoka ni yule mtu wa karibu anayejua siri na mambo unayoyafanya, kwasababu hiyo inakuwa rahisi kwa shetani kuwatumia kukuangamiza. Nyoka hakuonekana mwanzoni kwa Paulo kwasababu alijifanya kama kuni, na watu wa karibu ni vivyohivyo huwezi kuwatambua kwa urahisi. Furaha ni kuwa Mungu hakuruhusu yule nyoka kumwangamiza Mtume Paulo.KWANINI WALITUMIA KAMBA MBILI: Ndugu wa Samsoni walikuwa elfu tatu lakini jambo la ajabu ni kuwa walibeba kamba mbili tu; Utajiuliza nini siri ya hizi kamba mbili?. Yesu mwenyewe aliainisha kamba mbili kuu ambazo shetani anazitumia kuwaangamiza na kuwafunga watu duniani. Ukisoma katika Ufunuo 1:18 “na aliye hai; nami nalikuwa nimekufa, na tazama, ni hai hata milele na milele. Nami ninazo funguo za mauti, na za kuzimu.” Kumbe zile kamba mbili zina maana ya mauti na kuzimu. Kuzimu inaleta magonjwa na matatizo mbalimbali lakini mauti inaleta kifo. Kamba mbili mpya ni mauti na kuzimu. Kwa kuzimu na mauti shetani amekuwa akiwaangamiza na kuwatesa watu wa Mungu. Inawezekana na wewe ni mmoja wa watu wanaoteseka kwasababu ya kamba hizi leo kuna habari njema kuwa Yesu aweza kukata kamba hizo.MATOKEO YA KIFUNGO CHA SAMSONI: baada ya kumfunga, ndugu zake wakamkabidhisha kwa wafilisti yaani adui zake. Jambo la ajabu likatokea, mara baada ya kukabidhiwa. Imeandikwa, “Alipofika Lehi, Wafilisti wakapiga kelele walipokutana naye; ndipo roho ya Bwana ikamjia kwa nguvu, na zile kamba zilizokuwa juu ya mikono yake zikawa kama kitani iliyoteketezwa kwa moto, na vile vifungo vyake vikaanguka mikononi mwake.” Waamuzi 15:14 kupitia kifungo kile Mungu akamtumia Samsoni kuwaangamiza wafilisti wote. Kumbe waweza upo katika kifungo ambacho Mungu alikiruhusu ili upate ushindi ulio mkamilifu.MUNGU ANAWEZA KUKATA KAMBA ZILIZO KATIKA MAISHA YAKO: Wachawi na waganga wanaweza kuwa wajanja mbele ya macho yetu lakini Bwana anawaona, na kamba zao zinaonekana mbele ya macho ya BWANA. Hata mfalme Daudi aliwahi kuwa katika kamba hizo ukisoma katika Zaburi 119:61 “Kamba za wasio haki zimenifunga, Sikuisahau sheria yako.” Upo uwezekano wa mtu kufungwa, Mwilini unajiona ni mtu asiye na mafanikio au asiye na mwelekeo lakini rohoni unakuwa umefungwa na kamba kabisa. Zaburi 18:1->…  “…Kamba za mauti zilinizunguka, Mafuriko ya uovu yakanitia hofu. Kamba za kuzimu zilinizunguka, Mitego ya mauti ikanikabili. Katika shida yangu nalimwita Bwana, Na kumlalamikia Mungu wangu. Akaisikia sauti yangu hekaluni mwake, Kilio changu kikaingia masikioni mwake…” Mungu anaweza kukutoa katika kamba za matatizo unayopitia. Daudi alipokuwa katika kamba hizo aliliitia jina la BWANA.Yesu alipofufuka akatangaza kuwa anazo funguo za mauti na kuzimu, Hata kama aliyekufunga awe mtu wa karibu kiasi gani lakini zipo funguo za kufungua kamba zilizokufunga. Kama alivyofanya kwa Samsoni; baada ya kukufungua kinachofuata ni kipigo kwa wale wote walioshiriki kukufunga. Mungu anaweza kukutofautisha; shida na mateso yote unayopitia si kitu mbele za Mungu wetu kwasababu yeye anaweza kukuweka huru. Mpokee Yesu upate uhuru mkamilifu, kwasababu dunia ya leo haipo salama kama haupo ndani ya Yesu.

No comments:

Post a Comment