Monday, April 22, 2013

UJUMBE: KESHO ILIYOPIGWA KONA


Na Mch. Kiongozi Josephat Gwajima  22.4.2013

Kitabu cha Petro ni waraka wake kwa watu wote; ukisoma, 2 Petro 1:3 “kwa kuwa uweza wake wa Uungu umetukirimia vitu vyote vipasavyo uzima na utauwa kwa kumjua yeye aliyetuita kwa utukufu wake na wema wake mwenyewe” ukisoma kwa haraka waweza usijue siri iliyopo katika andiko hili. Andiko hili linamaanisha kuwa uweza wa Mungu umetupatia vitu vyote, kwa kumjua yeye.  Kumbe hapa tunapata kujua kuwa ni mapenzi ya Mungu tuwe na vitu vyote, na uweza huo wa Kiungu umeshatupa tayari “has given us” kila kitu kitupasacho kuishi.

Maana ya andiko hilo ni kuwa hapo kabla ya maisha yetu kuanza Mungu alikuwa ameshatukirimia mambo yote. Twaweza pata ufahamu mzuri zaidi kutoka kwenye habari ya Yeremia; Ukisoma “Yeremia 1:4-…” andiko linaanza kwa kusema “kisha neno la Mungu likamjia Yeremia…” Biblia inapotaja neno inamaanisha “Mungu” kwasababu katika (Yohana 1:1-5) Biblia inathibitisha kuwa neno hilo ni Mungu mwenyewe. Yesu Kristo ndio neno lililokuwa linawajia manabii hapo kabla, na ndio maana mara zote Yesu alipokuwa duniani alitumia maneno kama “Amini amini nawambia” au “Musa alisema hivi na mimi nasema hivi” Yesu alikuwa na mamlaka hiyo kwasababu yeye ndiye neno lenyewe haijaandikwa popote kuwa neno la Mungu likamjia Yesu, bali yeye alitamka neno kwa kuwa ndiye neno mwenyewe. Hivyo kwa habari ya Yeremia, biblia inapotaja “neno” inamaanisha Yesu mwenyewe alimjia Yeremia.  

Yesu alipomjia Yeremia akamwambia, (Yeremia 1:5) “kabla sijakuumba katika tumbo nalikujua, na kabla hujatoka tumboni, nalikutakasa;” Kumbe Yesu alimjua Yeremia kabla ya kuumbwa tumboni. Kimsingi, Hakuna mtu ambaye anaweza kukumbuka kipindi yupo tumboni wala kabla ya kuwa tumboni, lakini Mungu alikujua kabla ya kuwepo tumboni na alikukirimia vitu vyote. Swali la kujiuliza kama Mungu alikujua tangu huko mwanzo, na alikukirimia kila kitu; kwanini maisha yako yapo hivyo? Jibu la swali hilo litatoka katika ujumbe wangu wa leo “KESHO ILIYOPINDISHWA”. Tukirudi kwa habari ya Yeremia, Mungu aliongea na Yeremia akiwa kijana mdogo tu kuwa yeye amewekwa kuwa nabii wa mataifa (Yeremia 1:5). Kumbe kabla hujazaliwa Mungu alikwishakuweka katika njia njema ya maisha yako kama Yeremia; Jiulize nini kimetokea hadi leo upo kwenye njia nyingine? Mungu alikuwekea mafanikio tangu mwanzo, lakini jiulize nini kimetokea hadi leo upo katika hali hiyo mbaya?

Yawezekana wewe ni maskini leo, lakini unatakiwa ujue pia Mungu hakuiti kwa jina la umaskini bali anakuita kwa jina ambalo ndio kusidi lako. Warumi 8:29-30 “maana wale aliowajua tangu asili, aliwachagua tangu asili wafananishwe na mfano wa mwana wake, ili yeye awe mzaliwa wa kwa kwanza miongoni mwa ndugu wengi. Na wale aliowachagua tangu asili, hao akawaita na wale aliowaita; na wale aliowaita, hao akawahesabia haki, hao akawatukuza” kumbe tunaona kuwa Mungu amekwisha kuchagua tangu asili na tangu asili unatajwa kuwa mshindi. Na ukifanikiwa kupekuwa kwenye mipango ya Mungu juu yako, hutaona kuwa unatakiwa kuharibu mimba, au matatizo ya ndoa, au mateso ya umaskini, au kutokufanikiwa au magonjwa ambayo yanayokusumbua sasa.

Naweza fananisha jambo hili na mfano wa Treni na reli, mara zote treni hutembea katika reli yake. Vivyo hivyo maisha yako ni sawa na Treni, yana reli au njia ya Kiungu ya mafanikio yako, tatizo ni kuwa haupo kwenye reli na wewe wafikiri upo kwenye reli; kwasababu hata Treni isipopita kwenye reli yake itatembea kwa tabu baadaye itakwama; ndivyo ulivyo sasa unavyodhania kuwa maisha yako ndivyo yalivyo sivyo, unajiona na gari moja sio sahihi ulitakiwa uwe na kampuni! Kwasababu kama ungeona kusudi la Mungu katika maisha yako usingeishi maisha unayoishi sasa. Kuna mtu anasoma ujumbe huu akiwa kijijini lakini kumbe mpango wa Mungu, ulitakiwa uwe Uingeleza sasa hivi.

Kuna mambo makuu na makubwa ambayo Mungu anakuwazia katika maisha yako lakini hayajamilika kwasababu njia uliyotakiwa kupita imepindishwa (Waefeso 3:20). Ndio maana malaika alipomtokea Gideoni alimwita kwa jina la “shujaa”. Japokuwa Gideoni  alikuwa mtu wa kawaida kwa wakati ule bado kumbe tangu tumboni aliitwa shujaa na alitakiwa kuwa shujaa. Tatizo ni maisha yaliyomzunguka yalimfanya asiujue ukweli huu kuwa yeye ni shujaa. Pamoja na yote jina lile halikubadilika mbele za Mungu kuwa yeye katika ulimwengu wa roho anaitwa shujaa. Je wajua kuwa kabla ya kuzaliwa ulikuwa kwenye mapafu ya Mungu yaani ulikuwa pumzi ya Mungu, ulikuwa pamoja na Mungu ndio maana biblia inakuita “mwana wa miungu” (Zaburi 82:6), hiyo ndio asili yako. Rudi kwenye asili yako leo, asili yako sio uzinzi na uasherati, sio madeni, sio magonjwa, sio kushindwa. Amua kurudi kwenye asili yako kwasababu tupo duniani na kusudi la Mungu “mission” huwezi kufa ukiwa kwenye njia ya Mungu mpaka mission yako ikamilike, wakunyweshe sumu wakuloge hutokufa mpaka ukamilishe mission yako.

Kuna watu, kwasababu ya maisha wanayopitia wamejikuta wakijiuliza kuwa Mungu yupo kweli? Unawaza kama Mungu angekuwepo usingepitia kwenye mateso yako? Ni muhimu kujua Mungu alishakukirimia vitu vyote tatizo ni kwamba watu wengi hawapo katika asili yao. Biblia inasema Mungu ametukirimia vyote kwa kumjua yeye, sasa unachotakiwa kufanya ni kurudi katika njia, kwa kuanza kusoma neno, kufanya maombi yaani unatakiwa ubadilishe staili yako ya maombi na uhamie kwenye maombi ya kushindana ili kurudisha asili ya maisha yako. Kuna mashetani na wachawi ambao wapo katika ulimwengu wa roho ili kubadili njia yako ambayo Mungu alikuwekea ili uiishi. Inawezekana Mungu alikuweka kuwa kiongozi mkubwa na mwenye kukubalika lakini wachawi na mashetani waweza kukuhamisha kutoka katika njia ya Mungu aliyokuitia. Amua kurudi katika njia yako ambayo Mungu alikuita kwayo.

Warumi 8:19-21 Yaani hata viumbe vinavyoishi duniani vimetiishwa chini ya uharibifu yaani vimehamishwa kutoka katika asili yao. Viumbe navyo vyajua kuwa havipo katika asili yake, ndio maana navyo vinatarajia kufunuliwa kwake Kristo Yesu ili virudi katika asili yao. Hata Hana aliposumbuka miaka mingi pasipo kupata mtoto alimwomba BWANA akasema ukinipa mtoto atakuwa mjakazi wako, hapo ndipo Mungu alipomuingiza nabii Samweli kwenye tumbo la Hana. (1Samweli 1:11) Nabii Samweli ni nabii aliyekuwa na nguvu za Mungu, ambaye Mungu alimtumia sana; kumbe asili yake ni ile iliyotajwa na Hana akiwa kwenye maombi kabla hata ya Samweli kuzaliwa. Amini usiamini maisha unayoishi, sio ambayo Mungu alikupangia wewe uishi; hata wewe mwenyewe ni shahidi kuwa maisha hayo siyo uliyotaka kuishi. Kuna mashetani wamepindisha asili yako na kukupa maisha mengine na bahati mbaya zaidi umekubali maneno ya watu kukwambia “vumilia vumilia”. Kuna muda unatakiwa uamue kuchukua hatua ya kupambana ili urudi kwenye asili yako. Ndio maana watu ambao hawachukui hatua ya kuomba maombi ya kushindana wanajikuta wanahama kila kanisa bila mafanikio kumbe unatakiwa ufanye maamuzi ya kushindana na falme za giza. Huu ni wakati wa kuamua kurudi kwenye asili yako uliyopangiwa na Mungu.

Sikuzote shetani hufanya vita na watu ambao tangu asili waliitiwa maisha mazuri, yeye (shetani) huwa hamisha na kuwafanya wawaze kuwa wanavyoishi ndivyo Mungu anavyowataka kuishi. Leo amua kurudi katika asili yako, pambana na mamlaka za giza. Imeandikwa kwa maana kushindana kwetu sisi si juu ya damu na nyama bali ni juu ya falme na mamlaka za giza. Kataa kuishi maisha hayo na uamue kurudi kwenye asili yako aliyokupangia Mungu. Mungu hakukupangia mateso hayo unayopitia, Leo rudisha asili yako ambayo Mungu amekupangia. Mungu na akurudishie asili ya maisha yako!!!

No comments:

Post a Comment