google.com, pub-4324601895065941, DIRECT, f08c47fec0942fa0

Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

KAMA BADO UPO HAI LIPO TUMAINI


Na Mchungaji  Maximillian Machumu (RP)

Ujumbe huu ni ujumbe ambao waweza kubadilisha maisha yako kama utaamua kufungua moyo wako, kwasababu mwenendo wa maisha waweza kukufanya uhisi kuwa hakuna matumaini lakini leo baada ya kusoma somo hili unaenda kuona mwanga mpya kwenye maisha yako.

Ezekieli 37:11 "kisha akaniambia, mwanadamu mifupa hii ni nyumba yote ya Israeli tazama wao husema mifupa yetu imekauka matumaini yetu yametupotea, tumekatiliwa mbali kabisa" 
Ukiendelea kufuatilia kwa karibu kwa habari ya Ezekieli utagundua sababu ya Mungu kumleta katika bonde lile lililojaa mifupa. Kwanza, Imani ya Ezekieli ilikuwa imani yenye matumaini. Ingawa hali halisi ya mifupa ilikuwa imekwisha kauka, yeye alibaki na tumaini kuwa mifupa ile yaweza kuishi.

Hatua kubwa sana ya kudhihirisha kuwa mtu anamjua Mungu, ni ile ambayo mtu mmoja katikati ya vita, au hali za kukatisha tamaa, au hana analolitegemea katika maisha yake lakini bado anataja mambo yajayo, anataja matendo makuu ya Mungu.

Mungu hapendi ukate tamaa, wala umkufuru yeye katikati ya magumu na kwa taarifa yako tu ni kuwa watu wakubwa katika biblia hata walioitwa na Mungu, walipitia magumu lakini katikati ya magumu hayo walitamka maneno ya ushindi. Pia, kutamka maneno ya matumaini katikati ya magumu kunakufanya utoke mapema kwenye hali mtu aliyoko.

Inawezekana unapitia katika hali ngumu kwa sasa, lakini utakalolinena ukiwa katika dhiki hiyo itakufanya ama utoke ukiwa shujaa au aliyeshindwa. Na ndio maana hata Ezekieli alipowekwa mbele ya mifupa mikavu na kuulizwa 'je mifupa hiyonyaweza kuishi?' Naye alijibu kuwa 'wewe Bwana wajua', akionyesha kuwa hakuna jambo la kumshinda Bwana. Na ndio maana hata alipopewa nafasi ya kutamka neno alitamka uzima. Ni muhimu kujua maneno ya kutamka pindi unapopitia katika hali ngumu.

Ni muhimu kujua unachokiongea leo ndicho utakachokiishi kesho; wengine hujikuta wanaongea maneno mabaya juu yao wenyewe, huku wakisahau kuwa ni shetani ambaye anawafanya waongee maneno hayo ili apate nafasi ya kuharibu maisha yao baadaye.

Isaya 57:10 "ulikuwa umechoka kwaajili ya urefu wa njia yako, lakini hukusema hapana matumaini, ulipata kuuhishwa nguvu zako, kwasababu hiyo hukuugua" kumbe watu hawa, hali yao halisi iliwafanya wakate tamaa ya kufika wanapokwenda lakini pamoja na urefu wa njia bado walikiri kuwa matumaini yapo. Na kwasababu ya ukiri huo walipewa nguvu mpya. Usikiri udhaifu, Mungu anayetenda miujiza yupo na ukimkimbilia yeye, ataiondoa aibu yako na kukuvika kicheko.

Ukifuatilia habari ya Yusufu ambaye maisha yake yalianza kwa kuuzwa na ndugu zake kwa wamisri. Na alipouzwa waliigawa kanzu yake maana yake aliuzwa bila mavazi, lakini akiwa Misri na matumaini yakaanza kuja likatokea jambo jingine la kukatisha tamaa. Mke wa potifa akamsingizia kuwa anataka kumbaka, hivyo akatupwa gerezani maisha katiaka hali hiyo ni dhahiri kuwa Yusufu alikata tamaa kabisa. Lakini alipotoka gerezani Yusufu akawa waziri mkuu, jiulize, Mungu aliyemfanya kuwa waziri mkuu alikuwa wapi kipindi anauzwa? Au jiulize alikuwa wapi kipindi anawekwa gerezani? 

Ni muhimu kujua kuwa sio kuwa kwa unayopitia hali ngumu ukahisi Mungu amekuacha, si kweli; Mungu bado yupo pamoja na wewe na matumaini bado yapo. Yesu Kristo ni tumaini la kutosha kwenye maisha yako. Leo sikia sauti yake hii ikisema BADO YAPO MATUMAINI. Pata muda kuingia kwenye maombi na Mungu anakupa tumaini jipya leo. Inawezekana unapitia shida za ndoa, matatizo kazini, vita shuleni, roho ya kukataliwa mpaka umejihisi hakuna kesho ile uliyoiwaza. Leo tambua kuwa hata Ayubu katikati ya dhiki kuu hakuwahi kumkufuru Jehova bali aliweka tumaini lake kwake na kwa saa sahihi matumaini makuu yalionekana.

Hata kama ndoto yako inaonekana inataka kuzimika, inawezekana ulikuwa na ndoto za kusoma katika maisha yako lakini sasa unaona muda umeenda nakwambia bado lipo tumaini. Inawezekana madktari walikwambia kuwa mwisho wa kuzaa ni miaka 45 na wewe sasa unajiona unaelekea huo umri ukiwa hauna mtoto lakini nakwambia neno ambalo Yesu amenituma kwalo kuwa USIKATE TAMAA BADO YAPO MATUMAINI!!!!!

Mchungaji Maximillian Machumu (RP) 12/6/2013

Post a Comment

0 Comments