google.com, pub-4324601895065941, DIRECT, f08c47fec0942fa0

Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

HATUA ILIYOCHELEWESHWA

Na Mch. Josephat Gwajima (SNP) | GCTC; Dar es Salaam, Tanzania; 23.08.2013

UTANGULIZI:
Kwa asili, Mungu ni Mungu wa hatua kwa hatua, yeye huwapa watu hatua baada ya hatua. Na pia, kwa desturi; maisha ni hatua kwa hatua; siku kwa siku; na ndio maana mafanikio ya mtu hayapo katika kuokota almasi au kubahatisha tu bali ni hatua kwa hatua kuelekea katika utele. Katika hali kama hiyo, upo uwezekano hatua ya mtu ya kimaisha kucheleweshwa na kujikuta yupo kwenye hatua ambayo Mungu hakumkusudia kuwa tangu mwanzo.

Mwanzo 15:13, Hapa tunaona kuwa Mungu aliongea na Abrahamu kwamba, uzao wake (wana wa Israeli) watakaa utumwani kwa muda wa miaka mia nne. Lakini jambo la kushangaza ni kuwa, wana wa Isarel wakakaa katika nchi ya utumwa, Misri kwa muda wa miaka mia nne na thelathini (Kutoka 12:40-41) hapo tunapata kujua kuwa mafanikio ya mtu ya rohoni au mwili yanaweza kucheleweshwa na mambo fulani iwapo hajaamua au hajapata ufahamu wa kuyachukulia hatua.

MAANA YA HATUA:
Ili uweze kuelewa maana ya Hatua, naweza kutumia mfano huu kuwa; katika maisha tunayoishi inawezekana mtu akaanza katika kipato cha chini, kumtosha yeye peke yake, lakini baada ya muda mtu huyo anapata kazi nyingine yenye kipato zaidi na baadaye kupanda cheo, anafikia kujenga nyumba ya kwanza, ya pili na baadaye kupata safari za nje na kujenga magorofa n.k. Hizo ni hatua ambazo Mungu amewapa watu wazipitie kwa kadri wanavyoendelea kuishi. Kwa mfano huyo sasa tunajua kuwa, HATUA ni maisha ya mtu ya kimaendeleo ambayo Mungu alimwekea kuyaishi duniani.

Ni muhimu kujua Mungu amemwekea kila mtu hatua ambayo kwa hiyo, atafikia maendeleo na mafanikio katika maisha yake. Ndio maana Mfalme Daudi alisema kuwa, “Uzielekeze hatua zangu kwa neno lako, uovu usije ukanimiliki” Zaburi 119:133; Mfalme Daud alijua kuwa Mungu hutoa hatua kwa kila mtu na upo uwezekano wa hatua hizo kucheleweshwa.

UWEZEKANO WA HATUA YA MTU KUCHELEWESHWA:
Ukisoma katika Yeremia 25:11-12 “…nayo mataifa haya watamtumikia mfalme wa Babeli kwa miaka sabini…” kutoka hapo tunaona kuwa Mungu aliwaambia wana wa Israeli kuwa kipimo cha kuishi utumwani ni miaka sabini lakini swali ni kuwa, je walikaa utumwani kwa miaka sabini? Jibu tunalipata hapa, Danieli 9:2; Biblia inasema, Daniel kwa kusoma vitabu akagundua kuwa muda wa kukaa utumwani umeisha. Na baada ya kugundua, Danieli alichukua hatua ya kufunga na kuomba. Vivyo hivyo maisha ya mtu yaweza kucheleweshwa ili asifikie katika hatma yake njema; ndio maana mtu aweza kuitwa aliyefanikiwa katika miaka ishirini na mwingine miaka sabani; kimsingi wote wamefanikiwa lakini mmoja amecheleweshwa.

Upo uwezekano wa Mtu, Tabia au shetani kuchelewesha hatua au maendeleo ya mtu ya kimaisha. Ndio maana hata wana wa Israeli walipokuwa wakitoka Israel, walikuwa na uchaguzi wa njia ama fupi na njia ndefu. Lakini wana wa Israel walipitishwa njia ndefu ya miaka arobaini jangwani kwasababu ya kukwepa vita. Maisha ya wana wa Israeli ni kivuli cha maisha yetu ya rohoni; yaani waweza kufanikiwa baada ya miaka mingi kwasababu ya kukwepa kuvipiga vita vya rohoni. Ndio maana mtu aweza kuolewa lakini akiwa na miaka sitini au umejenga nyumba ukiwa na miaka sabini hata muda wa kuikaa kwenye hiyo nyumba haupo, kwasababu tu shetani au tabia kukuchelewesha.

SHETANI ANAVYOCHELEWESHA HATUA:
Kuna visababisho vingi vya kuchelewesha hatua za mtu, navyo vyaweza kuwa Ndugu wa karibu, Tabia za mtu (mfano, uvivu, wivu, dhambi n.k) au shetani. Leo tunaanza kwa kuangalia jinsi shetani anavyoweza kuchelewasha hatua za Mtu. Katika kitabu cha Daniel 10:1-14; Hapa tunaona Daniel aliamua kufunga na kuomba bila majibu, lakini katika siku ya 21 malaika Gablieli akaja na kumpa taarifa kuwa, “usiogope, Daniel; kwa maana tangu siku ile ya kwanza ulipotia moyo wako ufahamu, na kujinyenyekeza mbele za Mungu wako, maneno yako yalisikiwa…” ukiendelea kusoma, utaona malaika anamwambia kuwa majibu yake yalizuiwa na mkuu wa anga la Uajemi.

Kumbe wapo watu wanamwomba Mungu lakini bila kujua kuwa kuna shetani yupo mahali naye anazuia wasipokee kile ambacho Mungu amewaahidia kwa wakati. Mithali 16:9; Mungu ndiye aongozaye hatua za mtu na pasipo yeye shetani aweza kuchelewesha hatua hizo. Kimsingi Mungu amekuleta duniani na kukupa hatua ambazo ulipaswa kuzipitia lakini kwasababu ya shetani unajikuta hata maisha unayoishi sasa si sawa na hatua ambayo Mungu alitaka uwe nayo. Kisoma, Zaburi 73:2 “…hatua zangu zilikuwa karibu na kuteleza” Biblia inaonyesha kuwa kuna uwezekano wa mtu kuteleza katika hatua zake. Hizi si hatua za miguu ya kawaida bali ni maisha ya mtu ya kiroho au kimwili katika kuelekea maendeleo.

MFANO WA ALIYECHELEWESHWA NA SHETANI KATIKA BIBLIA:
Katika biblia kuna mtumishi wa Mungu mmoja aliyecheleweshwa Marko 5:6-20, Kimsingi, mtu huyu mwenye pepo ndani yake alikuwa na kazi na wito ya kumtumikia Mungu kwa kuhubiri injili; na ndio maana baada ya kufunguliwa akaenda kuhubiri injili katika Dekapoli lakini alikaa katika makaburi kwa miaka mingi ambayo angeweza kuitumia kumtumikia Mungu. Ndio maana leo waweza kuwakuta watu wana wito wa kumtumikia Mungu, lakini shetani anawaletea mawazo kinyume na kumtumikia Mungu na mwisho wanakuja kugundua kuwa, wamepoteza miaka mingi wakiwa wamecheleweshwa.

Hivi ndivyo shetani anavyoweza kuchelewesha maisha ya mtu katika masomo, biashara, mafanikio, maendeleo, mahusiano n.k Hii inaweza kutokea pale pepo wachafu wanapomwingia mtu na kuzuia hatua za mtu za mafanikio na kama mtu huyo akikosa ufahamu kuwa shetani ndiye anayefunga maisha yake; ataishia kulaumu na kukata tamaa bila mafanikio.

FANYA UCHAGUZI SAHIHI:
Ili kumiliki hatua zako kwa wakati inabidi uamue mwenyewe kushindana katika ulimwengu wa roho. Ndio maana kuna watu wameokoka na wengine hawajaokoka ambao waliwahi kutolewa unabii na kunenewa mambo mengi na watumishi wa Mungu, lakini hadi leo hayajatimia kwao; hii ni kwasababu ya kutokuamua kupigana katika ulimwengu wa roho. Na ndio maana Daniel alipogundua kuwa siku za kukaa utumwani zimeisha aliamua kuomba na kufunga ili kumiliki zile hatua ambazo Mungu amempangia.

Ni muhimu kujua kuwa Mungu akikuahidia kitu sio lazima kitimie kwa wakati, unaweza ukachelewa maana yupo azuiaye. Danieli aliomba kwa siku ishirini na moja bila majibu na inawezekana alianza kumlaumu Mungu kwa kutomjibu maombi yake lakini kumbe tatizo lilikuwa katika wakuu wa anga. Vivyo hivyo, usipoamua kushindana na wakuu wa anga na shetani unaweza ukajikuta unapambana katika maisha bila mafanikio. Ni muhimu kutumia mamlaka ambayo Yesu Kristo alituachia pale msalabani, kumsambaratisha shetani anayejaribu kuchelewesha mafanikio yako katika Jina la Yesu Kristo.

Information Ministry, GCTC


Post a Comment

0 Comments