google.com, pub-4324601895065941, DIRECT, f08c47fec0942fa0

Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

Mch. Gwajima: Mkutano wa Moshi utakuwa wa maajabu makubwa sana.

Mchungaji Josephat Gwajima ambaye ni Mchungaji kiongozi wa kanisa la Glory Of Christ Tanzania Church maarufu kama Nyumba ya Ufufuo na Uzima lenye makao yake makuu Kawe, jijini Dar es Salaam; amefanya mahojiano na Mtangazaji wa Radio Sauti ya Injili iliyopo mjini Moshi asubuhi ya leo. Mahojiano hayo ambayo yalidumu kwa muda wa saa nzima yalilenga kuelezea juu ya umuhimu wa neno la Mungu kwa kanisa la leo na pia kujua undani wa mkutano wa Injili unaotarajiwa kuanza jumapili hii mjini Moshi.

Mahojiano ya Mch. Josephat Gwajima na Deo Mosha wa Radio Sauti ya Injili - Moshi.

Mtangaziji huyo aitwaye Deo Mosha aliandaa mada ambayo kwayo ilimpatia wasaa mzuri kwa Mchungaji Josephat Gwajima kuelezea kwa undani juu ya umuhimu wa neno la Mungu kwa wakristo. Akieleza kwa undani juu ya umuhimu wa neno la Mungu, Mch. Gwajima alieleza historia fupi ya Ukristo kuanzia kipindi cha Martin Luther hadi kipindi hiki cha kunena kwa lugha. Alisema, injili ilitoka ulaya na kuja Afrika lakini katika kipindi hiki cha mwisho waafrika ndio watakao kuwa risasi ya mwisho ya injili kutoka katika bunduki ya Mungu.


Akieleza changamoto alizokutana nazo katika mkutano wa Injili wa Arusha, Mch. Gwajima alisema kuwa changamoto zipo, kwasababu ya ukweli kuwa mkutano wa injili ni mjumuiko wa mambo mengi sana. Akitolea mfano wa Mkutano wa kanisa hilo jijini Arusha, Mch. Gwajima alisema, "tumesafirisha vyombo vya mziki roli mbili na mabasi yaliyobeba wachungaji wapatao mia mbili kutoka Dar es Salaam waliokuja kwa ajili ya kuhudumia watu, kwa maana hiyo hizo gharama zote ni changamoto kwetu" Pia alisema, "kanisa la Ufufuo na Uzima linajitegemea katika mikutano yake bila kutegemea wafadhili kutoka nje ya nchi kwa maana hiyo changamoto bado ni kubwa kwetu."

Akiongelea Mkutano wa Moshi unaotarajiwa kuanza tarehe 20 hadi 27 Oktoba, alisema kuwa mkutano huo utakuwa wa maajabu na miujiza ya kupita kawaida, na akawaasa watu wa Moshi kujitokeza kwa wingi kuja kushuhudia waliokuwa msukuleni wakirudishwa na waliokufa kurudi kwenye uhai wao tena.

Mchungaji Josephat Gwajima akifanya mahojiano na mtangazaji Deo Mosha.

Alipoulizwa kwa habari za Misukule na kufufua watu waliokufa; Mch Gwajima alisema kuwa kazi hii si ya mtu mmoja bali ni kazi ya Bwana Yesu ambayo Mtu yeyote wa Mungu atakayeamua kufufua na kurudisha; Mungu atamtumia kwa nguvu ile ile. Akitoa andiko kutoka katika kitabu cha Mathayo 10:8; alisema kuwa Biblia iko wazi sana kwa habari ya kufufua watu waliokufa; na kusema kuwa tatizo la waafrika wengi ni vile wanashindwa kuthamini kitu kikubwa ambacho Mungu anakianzisha kwao.

Mwisho, alitoa wito kwa wachungaji vijana kwa kusema kuwa "yatupasa kuifanya kazi ya BWANA kungali bado asubuhi maana saa inakuja ambayo hatoweza mtu kuifanya" kwa maneno hayo aliwaasa vijana kuifanya kazi ya Mungu wangali vijana kwasababu mtu akianza kazi ujanani anapata muda mzuri wa kusahihisha makosa yake lakini akianza kazi uzeeni atakosa muda wa kusahihisha makosa na hivyo kushindwa kufanya vizuri.

Post a Comment

0 Comments