Sunday, January 12, 2014

MAELFU YA WATU WA MUNGU WAANZA MAISHA MAPYA KATIKA IBADA YA JUMAPILI NA MCHUNGAJI JOSPHAT GWAJIMA

Ibada ya Jumapili ya Tarehe 12.01.2014 katika Nyumba ya Ufufuo na Uzima Kawe yawa ya Manufaa makubwa sana kwa Maelfu ya watu waliofika Ibadani, ni Baada ya Mchungaji Kiongozi Josephat Gwajima kutangaza rasmi kuwa ni siku ya, kufanya maombi na watu kujiweka huru dhidi ya matatizo na laana za familia.SOMO: MATATIZO YA FAMILIA/UKOO
Na. Mch Josephat Gwajima

1 Mambo ya Nyakati 1:1-54
Ni kitabu cha kushangaza sana kwenye biblia sababu kinaelezea tu Fulani akamzaa Fulani, ni kitabu kilichokuwa inanipa taabu sana kukisoma kwenye biblia sababu majina mengine ni magumu hata kuyatamka, nikawa najiuliza hiki kitabu kinamaanisha nini na kwanini kimeandikwa kwenye biblia, nilikuwa sielewi ni nini mtu unaweza kujifunza kwa kuambiwa huyu akamzaa huyu.

Niliposoma kwenye 2 Timotheo 3:16 nikaona kila andiko lililoandikwa lafaa kwa mafundisho, nikajiuliza sasa haya majina ya watu kwenye hiki kitabu yanatufundisha nini? Nilipokuwa natafakari kitabu cha mambo ya nyakati nikapata shock (mshtuko) baada ya kusoma Mathayo 1:1-17 nikaona kitabu hiki kimeanza kwa kuandikwa hiki ni kitabu cha ukoo wa Bwana yesu, nikajiuliza hee hivi Yesu tena ana ukoo.


Nilipoanza kufuatilia huyu Mungu anataja ukoo tena kwanini, 2 Wakorintho 5:17 hata imekuwa mtu akiwa ndani ya kristo amekuwa kiumbe kipya, sasa haya mambo ya ukoo nini tena, niliposhuka kidogo nikaona haya ndiyo makabila 12 ya Yakobo, nikashangaa zaidi kumbe Mungu anajishughulisha na makabila tena. Hapo ndipo nikaanza kujifunza maisha ya mtu anayoishi leo, kama hauishi maisha yanayo mpendeza Mungu maisha yako yatakuwa sawasawa na kabila au ukoo anaotoka. Nikagundua kumbe kuelezea mambo ya familia hakuna tatizo maana hata Mungu yeye mwenyewe ameelezea sana kwenye biblia.
Nikaanza kufuatilia baadhi ya familia nikaona hata usome vipi huwezi kupata upenyo wa maisha, hata Mungu akikuinua kukupeleka ulaya litatokea jambo Fulani litasababisha urudi tu sababu familia hii hawaruhusiwi kupenya, familia hawaruhusiwi kutajirika, familia hawaruhusiwi kumuriki nyumba, familia hawatakiwi kumiriki magari.


Unaweza kuwa umeokoka, lakini kama hujadili na haya mambo ya familia utaingia mbinguni ukiwa umechoka, umekung’utwa kwelikweli, umeokoka lakini unaishi maisha magumu kweli,  unajiuliza mbona kwenye Mathayo 11:28 imeandikwa njooni kwangu ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo nami nitakupumzisha, unashangaa mbona mimi sipumziki, kumbe unatoka ukoo wa taabu wenye kulemewa na mizigo na laana (huo ni ukoo wa kutokupumzika).

Hebu jaribu kuangalia maisha ya baba yako na namna alivyo/anavyo malizia maisha yake, kama hakuna jitihada za ziada na wewe utamalizia maisha vile vile. Yesu alikuja ili tukatae kuwa na maisha kama waliyonayo baba/babu zetu, wewe umemuamini Yesu ili akuondolee yale maisha aliyoishi baba yako. Usiseme ukoo wetu sio ukoo wa viongozi, ukoo wetu hatufanikiwagi, ukoo wetu wanakufaga na umri mdogo, usiseme maneno hayo. Useme mama yangu alimaliza hivi lakini mimi nasimama na Bwana Yesu naamua kwenda beyond average, naamua kwenda mbele Zaidi. Usifuate kawaida wewe ukishakuwa umeokoka hauendi kwa kawaida za binadamu.


Ndio maana tunavoanza kuomba tunasema Mungu wa Ibrahimu, Isaka na Yakobo hapa tunakuwa tunajiungamanisha na utajiri na Baraka zote za Ibrahimu, Isaka na Yakobo. Kabla ya Ibrahimu kulikuwepo na kina Serugi, Tera na kina Nahori lakini hatuanzii huko maana Serugi alikuwa na matatizo yake, Ibrahimu alitengwa na jamaa zake akaambiwa aende kwenye nchi atakayokabidhiwa. Wokovu ni kutengwa, kutengwa na taratibu za ndugu, jamaa, umasikini na mabalaa ya familia. Hivyo ukishaokoka tu maana umetengwa, hupaswi kuwa kama alivyokuwa mama yako au baba yako au babu yako uende extra mile na pale walipoishia walipokutangulia.
 

Sababu itakayokufanya ukimbie kwa nguvu zote kwenda mahala pengine

Mwanzo 9:18-26

“…Hamu ndiye baba wa kanaani…”, “…Hamu baba wa kanaani akauona uchi wa baba yake, akawaeleza ndugu zake wawili waliokuwa nje…”


Ukisoma hayo maandiko utaona Hamu amefanya kosa na baba yake akamlaani kanaani na kizazi chake, na ukiendelea kusoma biblia utaona hiyo laana inavyozidi fuatilia kizazi cha kanaani. Kumbe hata leo kuna matatizo ambayo mtu unaweza kuwa nayo, sio kwamba yamesababishwa na maisha yako unayoishi leo hapana, bali yamesababishwa na makosa waliyo fanya babu wa ukoo, hiyo laana waliyolaaniwa ndiyo inayoendelea kukutafuna hii leo.


Nuhu akalevuka kutoka katika ulevi wake akamlaani kanaani, kanaani analaaniwa kwa kosa la baba yake, aliyeona uchi wa baba ni Hamu lakini laana ikamuangukia kanaani ambaye ni motto wa Hamu. Hapa tunajifunza kile kilichofanyika na mababu kina sambaa kwenye ukoo na vizazi vyote vijavyo, kama ni laana itasambaa kwenye kizazi chote, kama ni Baraka itasambaa kwenye kwenye vizazi na vizazi.

Hebu tuangalie maisha ya watoto waliozaliwa na kanaani

Mwanzo 10:15-19

Ukisoma hapo utaona kabila za wakaanani zikatawanyika na hata sodoma na gomora ilitokea hapo kwenye ukoo wa kanaani, unajiuliza hawa watu wa sodoma na gomora kwanini wanatenda uovu huu, kumbe ni laana ambayo imeendelea kuwafuatilia, hata kuteketea.

Kutoka 3:17

Mungu anasema atawapandisha watu wake kutoka katika mateso ya misri na kuwaingiza katika nchi ya mkaanani nchi iliyojaa asali na maziwa. Utagundua hapo, hawa wakaanani wananyang’anywa nchi yao na watu wa Mungu.

Kutoka 23:23 atawakatilia mbali wa Yebusi, unajiuliza hawa watu wamekosa nini mpaka wapate mateso yote haya, tunagundua ni lile kosa la Hamu kuona uchi wa baba yake, kosa hawakufanya hawa ukoo wa Kanaani lakini ndio laana inaendelea kuwafuatilia.

Kutoka 33:2 “…Nitawafukuza…” Kumbe kufukuzwa ni dalili ya laana

Kumb 20:17

Lakini uwaangamize kabisa Mhiti, na Mwamori, na Mkaanani, na Mperizi, na Mhivi, na Myebusi kama alivyokuamuru Bwana Mungu wako. Utaona hapa laana inawafanya hawa watu waangamizwe kabisa, wengine hata hawajui kulikuwa na Hamu ambaye alitenda kosa, lakini laana inaenda nao, na kamwe haiwaachi. Nawe ndivyo ilivyo kuna laana inakufuatilia ambayo leo lazima tuifanyie kazi.

1 Petro 1:18 “…Mwenendo wenu usiofaa mliupokea kutoka kwa baba zenu…” Kumbe kuna mambo yasiyofaa yanayowapata watu leo yalitoka kwa baba zao.

Mambo yaliyokupata kwenye maisha yasikuzuie kupaa kwenda kwenye kesho yako, yote yaliyokupata yalikuwa ni kukunoa uwe upanga mkali kwa ajili ya kesho yako.

Inawezekana leo una laana sababu ya makosa waliyofanya babu zako, babu yako alitesa wenye haki, babu yako alifanya mauaji akalaaniwa na laana inaendelea kwako hadi leo, leo ujitenge na laana za familia, Ibrahimu alitengwa na jamaa na ndugu zake akatangaziwa Baraka na kizazi chake chote hata kuzaliwa kwa Bwana Yesu.

Tanzania maeneo ambayo Mungu asiye Yehova alipoabudiwa kwa muda mrefu ndio masikini kuliko maeneo yote, hiyo ni kwa sababu ya laana ya kuabudu miungu mingine “Biblia inasema usimuabudu Mungu mwingine ila mimi Zaburi 81:9” laana hiyo inakufanya uwe replaced Mungu anakutoa na kumpa mwingine. Unapomuabudu Mungu mwingine ambaye sio Yesu unashangaa watoto wako wanaanza kuondolewa, watoto wako wanaondolewa ni laana hiyo, wakati mwingine unaamua wewe mwenyewe kuacha wenzako wanamiriki.Namna nzuri ya kutoka kwenye ukoo ni kutoka kama alivyofanya Ibrahimu akaambiwa toka leo kwa jamaa na ndugu zako nenda mpaka nchi nitakayokuonyesha. Kutoka kwetu leo kwenye familia sio kukataa familia, tunatoka kwa namna ya rohoni, tunajitenga na laana zote za familia, unapofanya hivyo mashetani waliotawala familia yako kwa muda mrefu wanakosa nguvu ya kukufuatilia.

Kila unapokataa kwenye ulimwengu wa roho unavunja kitu, unabomoa kitu, na mashetani waliotumwa kulinda ukoo wanakimbia wanajua huyu mtu katukataa.
 
Leo ukatae na kuhama kwenye ukoo wa laana, ukoo wa umasikini, ukoo wa balaa, uhamie ukoo wa Ibrahimu, Isaka na Yakobo, ukoo wa Bwana Yesu. Jitenge na mikosi yote, umasikini kwa jina la Yesu. Ufanye hivyo kwa kumaanisha, na hakika yake utabadirika, hutakuwa kama ulivyo kwa jina la Yesu.