Monday, May 26, 2014

SOMO: LAANA YA WACHAWI
MCHUNGAJI KIONGOZI JOSEPHAT GWAJIMA
Na Mchungaji Kiongozi Josephat Gwajima, 25 Mei 2014

Utangulizi

Aina za laana;

·   Laana ya wanadamu ,hii inaweza kuwa laana inayotokana na wazazi kwa mfano Nuhu alipomlaani mjukuu wake Kaanani  , tukajifunza kwamba anayekulaani siyo kwamba  lazima akuambie nimekulaani bali anaweza  akasema tutaona kama utafanikiwa hiyo ni laana tayari .
·         Laana ya Mungu, kwenye kitabu cha Malaki  Mungu anasema umelaaniwa kwa kumuibia Mungu sadaka zake.
·    Laana ya uchungu , mtu anaweza kuwa na uchungu moyoni hata baadaye ukaleta laana maishani mwake.
·  Laana ya majira ya kupanda na kuvuna, hii inatokana na  matendo ya mtu anayotenda  kama ni mema atapokea mema  na kama ni maovu baadaye yatampata mabaya.
·     Laana ya shetani , shateni naye anaweza kumlaani mtu kupitia wakala wake mfano wachawi.


Wachawi wanaweza kumlaani mtu na akalaaniwa, kwa maana  wanalaani kwa kutoa kafara inayoimarisha laana hiyo. Hesabu 25:1-25 (Tunaona watu  walitoa sadaka kwa miungu),  Kumbukumbu 32:17( watu walitoa sadaka kwa pepo), 1Samwel 26:19 ( walitoa kafara na ujira kwa mizimu), 1korintho 10:20( hata agano jipya tunaona watu wanatoa kafara kwa mashetani).  Kwa hiyo tunajifunza kuwa wachawi wanaweza kumlaani mtu kwa kutoa kafara,  kwa hiyo ni muhimu sana kujua  silaha zao na mbinu za wachawi ili nasi tuweze kuwadhibiti kwa  jina Yesu, maana ndiyo wametuzunguka katika maisha yetu.

Hesabu 22:1- 25,
 Tunaona Balaki Mfalme wa Moabu anakwenda  akiwa na ujira,  kumkodi Balamu mganga ili aweze kuwalaani wana wa Israel, ili atakapopigaana nao apate ushinda. Hii inatufundisha kuwa mtu hawezi kushinda vita akiwa amelaaniwa. Lakini Balamu alipotaka kuwalaani wana wa Israel alipanda mlimani na kuwaona vyema wana wa Israel. Hii inaonyesha kuwa ili mtu alaani, lazima akae pembe fulani, maana siyo kila eneo unaweza kutoa laana ikampata mtu.

Balamu alipotaka kuwalaani Israel Mungu  iligeuza kinywa chake, na akaanza kuwabariki wana wa Israel badala ya kuwalaani. Hii inatufundisha kuwa laana za wachawi haziwezi kuwapata watu waliookoka. Kwa hiyo tunaona mtu asiyekupenda anaweza kwenda kwa mganga na kumpa sadaka na kumwambia akulaani. Mganga baada ya kupokea ujira/sadaka ndipo anapoanza kutuma mashetani yanayoweza kumdhoofisha mtu rohoni na baadaye kushindwa kunatokea mwilini. Leo kwa jina la Yesu kila mchawi anayerusha laana katika ulimwengu wa roho naamuru imrudie mwenyewe kwa jina la Yesu.

Kwanini waganga wa kienyeji wanataka ujira wa kuku au mbuzi  ili wapate kumlaani mtu. Waganga wanapopokea kuku au mbuzi wanachinja na kumwaga damu , na damu hii ni uhai, kwa hiyo  inapomwagwa na  maneno ya laana yanatamkwa ndipo  damu inayabeba  hayo maneno na kuanza kuyaongea kila mara. Kwa hiyo  mashetani wanaposikia sauti ya damu ndipo wanaanza kwenda kumfuatilia yule mtu aliyetamkiwa maneno ya laana ili wayatimize. Kwa hiyo mahali hapa watu wengi wana matatizo mengi kwa maana wamelaaniwa na kuna damu mahali inaendelea kutamka hiyo laana katika madhabahu za wachawi. Usione watu wengi wamefanikiwa mwilini siyo kuwa wamefanikiwa tu bali kuna kitu kimefanyika katika ulimwengu wa roho. Na sisi watu wa Mungu tunakuja kanisani ili katika ulimwengu wa roho tupate kuharibu kila kazi za ibilisi kwenye maisha yetu.

Ukiri:
Kwa jina la Yesu naiteketeza laana yoyote iliyatamkwa juu yangu na kafara ya damu iliyomwagwa mahali popote kwa ajili yangu nainyamazisha kwa jina la Yesu.

Imeandikwa mwana wa Adamu alidhihirishwa apate kuzivunja kazi za ibilisi , kwa jina la yesu leo nasafiri katika ulimwengu wa Roho mahali popote zinapotokea laana za kuwalaani watu naziharibu kabisa kwa Jina la Yesu. Imeandikwa Roho wa Bwana yu juu yangu kwa maana amenitia mafuta kuwatangazia wafungwa kufunguliwa kwao.

 Nawatangazia watu wote walionilaani niko  huru kwa jina la Yesu na mashetani wa laana nawateketeza kwa jina la Yesu.  Kwa maana damu ya Yesu imemwagika ili wafungwa wa rohoni wapate kuwa huru , na leo nayavunja magereza yote ya magonjwa , laana, mikosi, kukataliwa kwa jina la Yesu.

Hapa duniani hakuna kitu kinachoweza kutokea bila kichocheo hasa katika ulimwengu wa  roho. Kwa hiyo usidhani matatizo uliyonayo yametokea yenyewe, hapana kuna laana mahali inayokufuatilia. Kwa mfano mtu anaweza kubaki kazini muda mrefu bila kupata promosheni  lakini akafikiri kuwa ni kawaida siyo kawaida maana wafanyakazi wenzake wanaweza kumlaani ili abaki pale bila kupanda cheo. Kwa jina la Yesu leo naamuru mtu yeyote  aliyefanya ushirikina au kumwaga damu kwa ajili yangu  vimrudie mwenyewe  kwa jina la Yesu.

Damu inapomwagwa mahali inaendelea kunena siku zote na mashetani wanakuwa wanaitii sauti ya hiyo damu na kumfuatilia yule mtu. Kwa hiyo ili mtu ashinde kwenye matatizo yake lazima anyamazishe ile damu ndipo mashetani wanakosa nguvu na kumwachilia mtu.  Tunaweza kunyamazisha damu za kafara kwa damu ya Yesu kwa maana imeandikwa nao wakamshinda kwa damu ya Mwanakondoo.

Maombi
Kwa jina la Yesu, baba leo nakata kamba zote za laana zilizo kwenye maisha yangu. Imeandikwa nao wakamshinda kwa damu ya Mwanakandoo , kwa damu ya Yesu nainyamazisha damu ya mabaya, mikosi, kuachwa,umasikini kwa jina la Yesu. Imeandikwa bomoeni bomoeni hata msingini leo kwa jina la Yesu nabomoa madhabahu zote ambapo kafara za damu zilimwagwa kwa ajili yangu kwa damu ya Yesu. Imeandikwa twaeni upanga wa roho ambao ni neno la Mungu nami natwaa upanga nawafyeka mashetani wote walioutumwa  kutoka kwenye madhabahu za laana za wachawi kuja kuniangamiza kwa jina la Yesu.
 Ewe damu unayenena mabaya  juu yangu nyamaza kwa jina la Yesu, imeandikwa kwa maana kushindana kwetu siyo juu ya damu na nyama bali ni juu ya falme mamlaka   wakuu wa giza na majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho . kwa jina la Yesu nakwenda rohoni  pande zote na mahali popote ilipotamkwa laana juu yangu  naiharibu kwa jina la Yesu. Naweteka nyara makuhani wote wa giza na kuwachinja  na madhabahu zazo zote nazibomoa kwa jina la Yesu.

Imeandikwa je kuna shirika gani kati ya nuru na giza? Kwa jina la Yesu kila mtu aliyepeleka jina langu kwenye madhabahu za wachawi leo naliondoa jina  langu kwa jina la Yesu.  Naliondoaa jina langu kwenye madhabahu ya aibu, madhabahu za umasikini, madhabahu za magojwa na kuliweka katika madhabahu  ya Yesu  Kristo ambayo ni madhabahu ya ushindi. Najitenga na maneno yote yaliyotamkwa kwa ajili yangu kwenye madhabahu za wachawi kwa jina la Yesu. Imeandikwa kila pando asilolipanda baba yetu wa mbinguni litang’olewa kwa jina la Yesu nawaamuru mashetani wote waliondani yangu kama wasimamizi wa laana kuniachia kwa jina la Yesu.


No comments:

Post a Comment