Sunday, September 21, 2014

KUNA NGUVU KATIKA MSALABA WA YESU.


IBADA YA JUMAPILI YA TAREHE 21-09-2014

NA MCHUNGAJI KIONGOZI JOSEPHAT GWAJIMA

SOMO:  NGUVU YA MSALABA

Nguvu ya Kanisa imeanzia katika msalaba wa Yesu Kristo ndio maana utaona kila mahali hapa duniani kuna alama ya  msalaba .  Kuna maandiko mengi ambapo Yesu Kristo aliongea kuhusiana na msalaba.

Mathayo 26:4

4 wakafanya shauri pamoja, ili wamkamate Yesu kwa hila na kumwua.

Mathayo 27:32, 42

32 Hata walipokuwa wakitoka, wakamwona mtu Mkirene, jina lake Simoni; huyu wakamshurutisha auchukue msalaba wake.

42 Yeye ni mfalme wa Israeli; na ashuke sasa msalabani, nasi tutamwamini.

Waefeso 2:16

16 Akawapatanisha wote wawili na Mungu katika mwili mmoja, kwa njia ya msalaba, akiisha kuufisha ule uadui kwa huo msalaba.

Wagalatia 2:14

14 Lakini mimi, hasha, nisione fahari juu ya kitu cho chote ila msalaba wa Bwana wetu Yesu Kristo, ambao kwa huo ulimwengu umesulibishwa kwangu, na mimi kwa ulimwengu.

Kimsingi unapoongea ukristo unaongelea mambo makuu matatu ambayo ni:

Ø Nguvu ya damu ya Yesu

Ø Kaburi wazi (Nguvu ya ufufuo)

Ø  Maneno aliyoongea Yesu msalabani.

Yesu alipokuwa msalabani akikaribia kukata roho alisema maneno saba. Kawaida mtu bila kujali alikuwa anaishije anapokaribia kufa huongea maneno ya maana na yenye uzito sana. Leo tunaangalia maneno saba aliyosema Yesu wakati anakaribia kufa na umuhimu wake. Lakini je, ni kwa nini alisema maneno saba wala sio kumi au mia moja?

 

Haya ni baadhi ya maandiko ambayo yanaonyesha kujirudia kwa namba saba mara kwa mara katika biblia;

Mwanzo7:2

2 Katika wanyama wote walio safi ujitwalie saba saba, mume na mke; na katika wanyama wasio safi wawili wawili, mume na mke.

Nuhu alipotaka kuchinja alichukua wanyama saba

Mwanzo 7:4

4 Kwa maana baada ya siku saba nitainyeshea dunia mvua, siku arobaini mchana na usiku; na kila kilicho hai nilichokifanya juu ya uso wa nchi nitakifutilia mbali.

Mwanzo21:28

28 Ibrahimu akaweka wana kondoo wa kike saba peke yao.
29 Abimeleki akamwambia Ibrahimu, Hawa wana kondoo wa kike saba, uliowaweka peke yao, maana yake nini?
30 Akasema, Hawa wana kondoo wa kike saba utawapokea mkononi mwangu, wawe ushuhuda ya kuwa ni mimi niliyekichimba kisima hiki.

Ibrahimu aliwaweka wanakondoo saba kama ushuhuda wa yeye ndiye aliyekichimba  kisima  kisichobishaniwa. Namba saba ni namba isiyo bishaniwa.

Zaburi 119:164

164 Mara saba kila siku nakusifu, Kwa sababu ya hukumu za haki yako.

Daudi alikuwa anamwabudu Bwana mara saba kwa siku.  

Namba saba ni namba ya utimilifu na ukamilifu. Msalaba wa Yesu Kristo kupitia maneno saba aliyoyasema Yesu akiwa pale ni ishara ya ukamilifu na utimilifu wa maisha yetu sisi tuaminio habari za msalaba.

 

MANENO SABA ALIYOONGEA YESU MSALABANI

1.     MUNGU WANGU MBONA UMENIACHA
Mchungaji kiongozi Josephat Gwajima

Watu wengine wanatumia sentensi hii kupotosha kwa kusema kuwa kama Mungu alimuacha pale msalabani basi sio mwana wa Mungu. Ni kweli aliachwa kwasababu ya dhambi zetu.  Alionekana mwenye dhambi si kwa kutenda bali kwa kubeba dhambi zetu na baba yake kwa sababu ya utakatifu wake alimpa mgongo. Alipopigwa magonjwa yako yaliadhibiwa katika mwili wa Yesu ndio maana Isaya 53:5 inasema  kwa kupigwa kwake sisi tumepona. Yesu alikataliwa ili sisi tupate kukubaliwa na Mungu baba.

 

       2. BABA WASAMEHE KWA KUWA HAWAJUI WATENDALO

Wakati Yesu anasema maneno haya alikuwa katikati ya mateso na maumivu makali lakini bado aliweza kusamehe. Kawaida mtu anapoumizwa hushindwa kusamehe mara moja; mwingine husema nitasema maumivu yakipoa au mwingine atakuambia nitakusamehe ila sitakusahau. Kuna watu wamekufa leo na wengine wana magonjwa yasiyotibika kwa sababu ya kutokusamehe. Unaposhindwa kusamehe Mungu naye hawezi kukusamehe hivyo sio rahisi kupata uponyaji wako kwa sababu Mungu huponya baada ya kukusamehe. “Akusamehe dhambi zako zote akuponye magonjwa yako yote.”

Marko2: 1-5

1 Akaingia Kapernaumu tena, baada ya siku kadha wa kadha, ikasikiwa ya kwamba yumo nyumbani.
2 Wakakusanyika watu wengi, isibaki nafasi hata mlangoni; akawa akisema nao neno lake.
3 Wakaja watu wakimletea mtu mwenye kupooza, anachukuliwa na watu wanne.
4 Na walipokuwa hawawezi kumkaribia kwa sababu ya makutano, waliitoboa dari pale alipokuwapo; na wakiisha kuivunja wakalitelemsha godoro alilolilalia yule mwenye kupooza.
5 Naye Yesu, alipoiona imani yao, akamwambia yule mwenye kupooza, Mwanangu, umesamehewa dhambi zako.

 Biblia inasema mkiwasamehe wawakoseao na Baba yenu wa mbinguni atawasamehe, kumbe basi hata msipowasamehe Baba wa mbinguni hatawasamehe pia. Unapokuwa husamehi kunakuwa na mapepo yanayopata mwanya kuingia ndani yako na kupandikiza roho ya uchungu ambayo huzaa presha, magonjwa ya moyo na kisukari.

Waebrania12:1

1 Basi na sisi pia, kwa kuwa tunazungukwa na wingu kubwa la mashahidi namna hii, na tuweke kando kila mzigo mzito, na dhambi ile ituzingayo kwa upesi; na tupige mbio kwa saburi katika yale mashindano yaliyowekwa mbele yetu,

Ile dhambi ikuzingayo ya kutokusamehe iweke kando. Unapoamua kusamehe wale mashetani wanaokaa ndani yako wanahama ndani yako na unapona magonjwa yako yote.

 

3. AMINI AMINI NAKWAMBIA LEO HII TUTAKUWA WOTE PEPONI

Yesu hakuwa na shaka na alipokuwa anakwenda. Alijua anakwenda wapi. Yesu alimwambia yule mwizi aliyemwamini pale msalabani kuwa hakika leo hii tutakuwa wote mbinguni. Msalaba wa Yesu unatupa hakika ya mafanikio yetu, unatupa uhakika juu ya uwepo wa mbingu na haki yetu ya kuishi huko. Duniani zimejaa taarifa nyingi za kubahatisha ila wewe uliyeokoka msalaba wa Yesu ni uhakika wa kwenda mbinguni. Biblia inasema “amini amini nawaambia yeye aniaminie mimi amepita kuingia mbinguni” Tazama nabisha mlangoni mtu atakayeisikia sauti yangu na kunikaribisha nitaingia ndani yake na atakuwa na uzima wa milele. Mbinguni ni kwetu na msalaba wa Yesu kristo ni uhakika wa kwenda Mbinguni na Yesu ndiye njia, kweli na uzima.

Yohana 14:1

1 Msifadhaike mioyoni mwenu; mnamwamini Mungu, niaminini na mimi.
2 Nyumbani mwa Baba yangu mna makao mengi; kama sivyo, ningaliwaambia; maana naenda kuwaandalia mahali.
3 Basi mimi nikienda na kuwaandalia mahali, nitakuja tena niwakaribishe kwangu; ili nilipo mimi, nanyi mwepo.
4 Nami niendako mwaijua njia.

Msalaba ni uhakika wa kuolewa kwako, hakika ya promosheni, hakika ya kazi yako, hakika ya  safari yako, hakika ya maisha yako. Kristo alikuwa na uhakika wa wapi aendako na nini anaenda kufanya, kuandaa makao kwa ajili yetu.

 

4.  MAMA TAZAMA MWANAO NA MTOTO TAZAMA MAMA YAKO

YOHANA 19:26-27

26 Basi Yesu alipomwona mama yake, na yule mwanafunzi aliyempenda amesimama karibu, alimwambia mama yake, Mama, tazama, mwanao.
27 Kisha akamwambia yule mwanafunzi, Tazama, mama yako. Na tangu saa ile mwanafunzi yule akamchukua nyumbani kwake.

Msalaba unaweza kuleta upatanisho, msalaba ni nguzo ya upatanishi. Inawezekana kuna migogoro kati yako na ndugu zako au wafanyakazi wako lakini leo kuna msalaba wa upatanishi. Leo mataifa yanapigana kwasababu hakuna mapatano, Baba na Mama wanagombana, hawapatani. Yesu alipokuwa msalabani mkono wake mmoja alimshika Mungu Baba na mkono mwingine akawashika wanadamu huku akiwa anakata roho  akapiga kelele akisema pataneni! Leo Yesu anaitwa daraja la upatanisho kati ya wanadamu na Mungu.

 

 

5. EE BABA MIKONONI MWAKO NAIWEKA ROHOO YANGU

Kumbe Roho inaweza kuwekwa kwenye mikono, yaweza kuwa ya Mungu Baba au mungu wa dunia hii ambaye ni shetani. Msalaba wa Yesu kristo unaweza kukabidhi Roho zetu mikononi mwa Mungu. Yesu akatuonyesha kwamba Roho yake ameiweka mikononi mwa Mungu Baba. Leo hii  Roho za watu ziko kwa wachawi, nyingine ziko kwa waganga wa kienyeji. Msalaba unatupa uhakika wa mahali pa kuwekwa roho zetu. Biblia inasema msimwogope yeye  awezaye kuua mwili bali mwogopeni yeye awezaye kuiua Roho na mwili.

 

 

6. NAONA KIU

Yohana  19:28

28 Baada ya hayo Yesu, hali akijua ya kuwa yote yamekwisha kumalizika ili andiko litimizwe, akasema, Naona kiu.

Ni jambo la kushangaza mtu aliye katika hatua ya kufa  kuhitaji maji. Haya maneno hakuwa akiwaambia wale waliomsulibisha  bali baba yake wa mbinguni; kwamba pamoja na taabu niliyonayo bado ninaona kiu ya kutimiza mapenzi yako. Yesu alikuwa msalabani tangu asubuhi na hapa alisema, “naona kiu” Msalaba wa Yesu unatupa kiu ya uponyaji, kufufua, miujiza, utoaji, kufunga, kuomba. Inawezekana kuna wakati  ulikuwa una kiu ya kuomba lakini leo umekuwa mkavu lakini upo msalaba wa yesu unatupa kiu ya kuyatimiza mapenzi ya Mungu katika maisha yetu.

 

7. IMEKWISHA

Yesu  hakuuwawa bali aliitoa Roho yake ili aitwae tena. Shetani hakujua kama Yesu alikuja ili afe ndio maana aliingia kwa watu wamhukumu kifo lakini. Yesu alikuwa mtii hata mauti ili atimize mapenzi ya baba yake. Alipokuwa msalabani Yesu aliangalia kama ametimiza yote yaliyompasa kufanya, akaangalia akaona uponyaji upo, ufufuo upo na maandiko yote juu yake yametimia ndipo akapiga kelele kusema imekwisha.

Baada ya Yesu kukata roho yakafuatia matukio yafuatayo:

Tukio la kwanza, Dunia yote ikawa Giza. Mungu akazima jua lake na Dunia ikawa giza “MSALABA NI MSALABA WA MATUKIO”

 Tukio la pili, miamba ikapasuka. Msalaba unapasua miamba. Je, kuna mtu ofisini au kwenye familia yako amefanyika mwamba? Mkutanishe leo na msalaba wa Yesu wenye uwezo wa kupasua miamba.

Tukio la tatu, makaburi yakafunguka. Hapo ndipo penye nguvu ya Ufufuo na Uzima yaani Yesu mwenyewe.

 Tukio la nne, dunia ikatikisika.

Tukio la tano, wanawake wakajipigapiga vifuani wakimaanisha wanamtafuta Yesu.

Tukio la sita, pazia la hekalu likapasuka maana yake kila mmoja wetu anayo ruhusa ya kuomba moja kwa moja kwa baba bila kupitia mtu yoyote.

Tukio la saba, kwenye msalaba  pakawekwa anuani maana yake anuani ya mahali unakoelekea kwa makusudi ya Mungu  ipo msalabani.

 Tukio la nane, yule aliyekuwa anaongoza usulubishaji akasema “hakika mtu huyu alikuwa ni mwana wa Mungu.”

Tukio la tisa, ilipofika jioni walienda kuwavunja miguu waliosulubiwa maana kwa sheria ya kiyahudi hairuhusiwi mtu kuwa hai juu ya msalaba sabato inapoingia. Akiwa hajafa hukatwa miguu ili afe kwa kuishiwa damu. Walikuta Yesu amekwishakufa lakini mmojawapo wa wale wanajeshi alimchomi mkuki ubavuni ndipo ilipotoka damu na maji. Hiki ni kithibitisho hakika kuwa Yesu alifia msalabani.

Yesu alipokufa kabla ya kufufuka alikwenda kuzimu ambako kulikuwa na dhima wakishangilia kumshinda Yesu.Yesu alimfuata shetani palepale kwenye kiti chake kuzimu akamkanyaga kichwa chake mbele ya malaika zake. Tena zaidi ya hayo akamnyanganya funguo za kuzimu na mauti.

 

MAOMBI:

Tunawafuata adui zetu palepale walipo, tunawatokea kwenye ulimwengu wa Roho na kuwakanyaga na kuwanyanganya mali zetu na vitu vyetu vyote kwa nguvu ya msalaba wa Yesu kristo.

Kwa jina la Yesu nimepewa mamlaka ya kukanyaga nyoka na nge na nguvu zote za yule adui kwa jina la Yesu. Kwa nguvu ya msalaba ninawafuata wachawi, waganga wa kienyeji na adui zangu wote katika ulimwengu wa roho waliokaa kikao kinyume na mimi, ninawaponda vichwa kwa jina la Yesu. Imeandikwa wakamshinda kwa damu ya mwanakondoo, ninawashinda kwa damu ya Yesu. Ninazikanyaga mamlaka zote za giza kwa damu ya mwanakondoo. Kwa nguvu ya msalaba, kwa damu ya mwanakondoo ninawashambulia wote mnaotumia nyota yangu, ninauponda uzao wa joka katika jina la Yesu. Ninawashambulia mashetani katikati ya uzao wa wanadamu kwa jina la Yesu.  Kwa damu ya mwanakondoo, ninavifuatilia vipawa vyangu vilivyofichwa katika mashimo kwa jina la Yesu. Ninaitumia nguvu ya msalaba kwa jina la Yesu, waliofichwa kwenye mashimo, kwenye mapori, baharini, kwenye mwezi, kwenye,  nyota, kwenye anga  ninawarudisha kwa damu ya Yesu.  Kwa jina la Yesu Kristo ninaamuru warudishwe, natumia nguvu ya msalaba kwa damu ya Yesu kristo, biashara zilizofungwa, kazi zilizofungwa ninazifungua kwa jina la Yesu.

Nakwenda msalabani, msalaba wa furaha, msalaba wa ukombozi, msalaba wa ushindi, msalaba wa nguvu, msalaba wa maarifa nakata rufaa  hapo kwa jina la Yesu.

Asante Bwana Yesu kwa ajili ya kunifia msalabani, asante kwa ajili ya nguvu iliyomo ndani ya msalaba. Asante kwa ukombozi, uponyaji na msamaha wako. Amen.

 


 Maelfu wakiwa ndani ya ufufuo na uzima kawe

Nguvu ya msalaba.


No comments:

Post a Comment