Monday, October 27, 2014

NGUVU YA IMANI


JUMAPILI YA TAREHE 26_10_2014

MCHUNGAJI JOSEH JONES 
 
 NA MCHUNGAJI KIONGOZI JOSEPHAT GWAJIMA
 
SOMO: NGUVU YA IMANI
 

Mchungaji kiongozi Josephati Gwajima akiwa na Mchungaji Joseph Jones

Kama raia wa Tanzania unahitaji upate fedha ya Tanzania ambayo ni shilingi ili uweze kuishi ndani ya nchi hii. Utaihitaji kupanda daladala, kununua chakula  na kugharamia maisha kwa ujumla. Lakini wewe kama mtu aliyeokoka ni zaidi ya raia wa Tanzania, wewe ni raia wa mbinguni. Kama ilivyo kwa nchi ya Tanzania, raia wa mbinguni pia wana fedha ambayo ni imani. Biblia inasema mwenye haki wangu ataishi kwa imani. Hatuwezi kumpendeza Mungu wala kuingia katika ufalme wa Mungu bila imani.

“Kwa maana mmeokolewa kwa neema, kwa njia ya imani; ambayo hiyo haikutokana na nafsi zenu, ni kipawa cha Mungu;”  Waefeso 2:8

“Basi imani ni kuwa na hakika ya mambo yatarajiwayo, ni bayana ya mambo yasiyoonekana. Lakini pasipo imani haiwezekani kumpendeza; kwa maana mtu amwendeaye Mungu lazima aamini kwamba yeye yuko, na kwamba huwapa thawabu wale wamtafutao.” Waebrania11:1

Kama unataka kumpendeza Mungu lazima uishi kwa imani; ndani ya maisha ya imani kuna uponyaji, wokovu, amani, nguvu. Pasipo imani huwezi kamwe kupokea baraka hizi. Lakini imani huendana na uvumilivu.

“Kwa maana haki ya Mungu inadhihirishwa ndani yake, toka imani hata imani; kama ilivyoandikwa, Mwenye haki ataishi kwa imani.” Warumi1:17

Imani inakuja kwa kusikia neno la Mungu, hiyo ndiyo njia pekee unayoweza kupokea imani. Unahitaji kusoma neno la Mungu, kulitafakari na zaidi kulitenda ndipo upokee imani. Kama ambavyo leo ungeenda kwenye ATM ya  benki mojawapo ya Tanzania kuchukua fedha; nenda kwenye ATM ya Mungu ambayo ni biblia ukachukue imani. Neno la Mungu ni mbegu; Yesu alitoa mfano huu wa mpanzi:

 Akawaambia, Hamjui mfano huu? Basi mifano yote mtaitambuaje?  Mpanzi huyo hulipanda neno.  Hawa ndio walio kando ya njia lipandwapo neno; nao, wakiisha kusikia, mara huja Shetani, akaliondoa lile neno lililopandwa mioyoni mwao.  Kadhalika na hawa ndio wapandwao penye miamba, ambao kwamba wakiisha kulisikia lile neno, mara hulipokea kwa furaha;  ila hawana mizizi ndani yao, bali hudumu muda mchache; kisha ikitokea dhiki au udhia kwa ajili ya lile neno, mara hujikwaa.  Na hawa ndio wale wapandwao penye miiba; ni watu walisikiao lile neno,  na shughuli za dunia, na udanganyifu wa mali, na tamaa za mambo mengine zikiingia, hulisonga lile neno, likawa halizai.  Na hawa ndio waliopandwa penye udongo ulio mzuri; ni watu walisikiao lile neno na kulipokea, na kuzaa matunda, mmoja thelathini, mmoja sitini, na mmoja mia.  Akawaambia, Mwaonaje? Taa huja ili kuwekwa chini ya pishi, au mvunguni? Si kuwekwa juu ya kiango? Kwa maana hakuna neno lililositirika, ila makusudi lije likadhihirika; wala hakuna lililofichwa, ila makusudi lije likatokea wazi.  Mtu akiwa na masikio ya kusikilia, na asikie.” Marko4: 13  

Neno la Mungu ni mbegu ambayo siku zote hutenda kazi. Tunalipanda neno la Bwana ndani ya mioyo yetu. Baada ya muda mbegu hii hukua ndani ya mioyo yetu na kuzaa matunda. Je, ni nani aliyepanda viazi akavuna mahindi? Hayupo. Vivyo hivyo basi mtu akitaka kuishi maishi ya imani lazima apande mbegu ya imani ambayo ni neno la Mungu.

Tunaposoma neno la Mungu au kusikiliza mahubiri hiyo ni mbegu inakuwa inapandwa. Baada ya kusikia mara kwa mara kwa muda fulani mti wa imani huanza kukua. Ili kuyaona matunda ya mti wa imani inatupasa kuwa wavumilivu.

“Kwa hiyo wekeeni mbali uchafu wote na ubaya uzidio, na kupokea kwa upole neno lile lililopandwa ndani, liwezalo kuziokoa roho zenu. Lakini iweni watendaji wa neno, wala si wasikiaji tu, hali mkijidanganya nafsi zenu.  Kwa sababu mtu akiwa ni msikiaji wa neno tu, wala si mtendaji, mtu huyo ni kama mtu anayejiangalia uso wake katika kioo.  Maana hujiangalia, kisha huenda zake, mara akasahau jinsi alivyo.” Yakobo1:21

Kukombolewa kwetu kunatokana na lile neno tunalolipokea. Kazi yetu sisi ni kulisikia neno, kulitafakari na kulitenda. Kazi ya Mungu ambaye ndiye mpanzi ni kulikuza hilo neno ili lizae matunda..

“Lakini yanenaje? Lile neno li karibu nawe, katika kinywa chako, na katika moyo wako; yaani, ni lile neno la imani tulihubirilo.  Kwa sababu, ukimkiri Yesu kwa kinywa chako ya kuwa ni Bwana, na kuamini moyoni mwako ya kuwa Mungu alimfufua katika wafu, utaokoka.  Kwa maana kwa moyo mtu huamini hata kupata haki, na kwa kinywa hukiri hata kupata wokovu.” Warumi10: 8

Imani ni kuamini kwa mioyo yetu na kukiri kwa midomo yetu. Unapookoka watakuwepo watu watakaokueleza habari mbalimbali za wokovu wakati kanisa nalo linajitahidi kukufundisha habari za wokovu. Wote hawa wanajaribu kupanda mbegu ndani yako. Utakachokiamini ndani ya moyo wako na kukiri kwa midomo yako hicho kitakuwa.

Imani yaweza kuelezewa kwa mfano wa ujauzito. Ili mama awe mjamzito ni lazima iwepo mbegu ambayo inapandwa ndani ya tumbo lake. Hawezi kuamka tu siku moja akajikuta ana tumbo kubwa. Wakati wa ujauzito zipo adha mbalimbali ambazo mama huyu atazipitia. Hata muda wa kujifungua unapowadia mama huyu hujua kuwa muda wake umefika bila hata kuambiwa. Zile dakika chache kabla ya kujifungua kwake huwa ni za mateso na maumivu makali sana lakini hufuatiwa na furaha isiyoelezeka baada ya mama huyu kumuona mwanaye kwa mara ya kwanza. Ndivyo ilivyo imani; lazima neno lipandwe, na hakika zitakuwepo adha nyingi utakazopitia wakati wa ujauzito wako wa imani. Na kabla tu imani yako haijazaa matunda kutakuwa uchungu ambao hufuatiwa na ule muujiza ambao ndilo tunda la imani yako. Beba ujauzito wa imani leo kwa jina la Yesu.

Mtu anaweza kuwa anajidanganya kuwa ana imani kwa kukiri maneno ya ukombozi. Lakini kama unatamka maneno hewa bila kuwa na neno ulilopanda ndani ya moyo wao huwezi kuwa na imani wala huwezi kuzaa matunda ya imani. Biblia inaiita imani ya namna hii imani iliyokufa. Kama wewe ni mgonjwa na unang’ang’ana  kusema nimepona, nimepona bila kuwa na neno la kusimamia hakika imani yako imekufa.  Unatakiwa kusema , “Imeandikwa kwa kupigwa kwale mimi nimepona, nimepona kansa kwa jina la Yesu.” Kama unataka ulinzi unasema, “Mabaya hayatanipata mimi wala tauni haitakaribia hemani mwangu, hakuna uchawi juu ya Yakobo wala uganga juu ya Israeli.” Imani ya namna hii hakika itazaa kwa wakati wake. Biblia inasema ukiwa na imani ndani yako chochote utakachokisema utakipata  sawa sawa na imani yako kama usemavyo.

Inawezekana unasema mimi ninaamini lakini siwezi kukisema ninachokiamini kwa sababu kama kisipotokea nitachekwa. Watu wengi huwa na mtazamo huu. Lakini kama huu ni muamala basi bila kutamka kile ulichopanda ndani ya moyo wako muamala huu haujakamilika. Ni lazima usikie neno ili lipandwe ndani yako halafu ukiri  kile unachokiamini.

Baada ya kupanda mbegu ya imani upo muda wa kusubiri ili mbegu hii iweze kumea, kukua na kisha kuzaa matunda. Hakuna mkulima apandaye mahindi leo na kutegemea kuvuna kesho; wala hakuna mama atungaye mimba leo akitegemea mtoto kesho. Ipo miezi tisa ya kusubiri mimba kugeuka mtoto. Watu wengi hukata tamaa wanapokosa kuona matunda ya imani yao mapema. Ili uweze kuzaa unahitaji kuwa mvumilivu kusubiri imani yako izae.

Monday, October 20, 2014

SHERIA MBILI ZA ROHONI.


SOMO: SHERIA MBILI ZA ROHONI

TAREHE: 19/10/2014

NA MCHUNGAJI KIONGOZI: JOSEPHAT GWAJIMA
Mchungaji kiongozi Josephat Gwajima

 Ulimwengu tunaoishi umegawanyika kwenye sehemu mbili; ulimwengu wa roho na ulimwengu wa mwili. Mambo huanzia kwenye ulimwengu wa roho na kisha hudhihirika katika ulimwengu wa mwili. Mtu anapofanikiwa rohoni baadae anafanikiwa mwilini. Unapopatwa na matatizo mfano magonjwa elewa kuwa matatizo hayo yameanzia rohoni. Unapoanza kuomba na kushambulia lazima utambue kuwa unashindana na ulimwengu wa roho. Imeandikwa;

Kwa maana kushindana kwetu sisi si juu ya damu na nyama; bali ni juu ya falme na mamlaka, juu ya wakuu wa giza hili, juu ya majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho.”   Waefeso 6:12
Mama mchungaji Grace Gwajima

Kumbe kabla ya udhihirisho wa baraka katika maisha yako lazima ubarikiwe rohoni. Ulimwengu wa roho ni dhahiri kabisa, hivyo kama ambavyo tunaona miji katika ulimwengu wa mwili ndivyo ilivyo katika ulimwengu wa roho. Hivyo ukibarikiwa kwenye mji wa Dar-es-salaam rohoni baadae utabarikiwa kwenye mji huo katika ulimwengu wa mwili. Kujua mistari mingi ya biblia sio ishara ya kuwa mtu ni wa kiroho zaidi, Mungu ni roho hivyo ni lazima tumwabudu katika roho na kweli. Imeandikwa.

Viumbe ambavyo makazi yake nikatika ulimwengu wa roho ni Mungu, malaika, mashetani ambao ndio wale malaika walioasi. Viumbe wa kimwili ni kama wanadamu, kuku, simba, miti.

Katika ulimwengu wa roho, kuna sheria mbili zinazouongoza. Mambo yote huanzia katika ulimwengu wa roho, hasa katika ndoto. Zipo sheria mbili, zinazoongoza ulimwengu wa roho.

Mchungaji Kiongozi Josephat Gwajima Akifundisha Sheria mbili za Rohoni
 

1.   UWEZO WA KUBADILI MAUMBO.

Ili mawakala wa shetani ambao ni wachawi waweze kwenda kuroga lazima watoke ndani ya miili yao na kuvaa umbo jingine ili wasitambulikane. Kwa kuwa anakuwa rohoni anaweza kuvaa umbo lolote, kugeuka kuwa kitu chochote mfano paka, mbwa, kunguru. Furaha ya mchawi ni kukusikia ukiendelea kusema jana kulikuwa na paka analia kama mtoto kwenye dirisha langu.  Imeandikwa;

“Baada ya hayo akawatokea watu wawili miongoni mwao, ana sura nyingine; nao walikuwa wakishika njia kwenda shamba.”  Marko 16:12

Yesu aliwatokea wanafunzi wake akiwa na sura nyingine, lakini kwa kuwa alikuwa rohoni, alionekana kuwa na sura nyingine. Yesu ana sura nyingi, kama umezoea kumuona kama daktari leo ana sura nyingine. Akitaka kukutokea kama mmea atakutokea kama ua la sharoni, akitaka kukutokea kama mnyama atakutokea kama simba wa kabila la Yuda, akitaka kukutokea kama kinywaji atakutokea kama maji ya uzima. Lazima utambue kuwa Mungu anaweza kukutokea kwa sura nyingine tofauti na ile uliyoizoea.

Mchungaji Gwajima akimsifu na kumwabudu Mungu.
 

UKIRI

Leo, katika jina la Yesu; Yesu unitokee kwa sura nyingine. Nimezoea kukuona  kama mponyaji tu, leo nitokee kama mfariji, kama mfalme wa wafalme, kama mwamba wa kale. Leo Yesu nitokee kwa sura nyingine sawasawa na tatizo nililonalo. Amen.

 

 “Yesu akamwambia, Mama, unalilia nini? Unamtafuta nani? Naye, huku akidhania ya kuwa ni mtunza bustani, akamwambia, Bwana, ikiwa umemchukua wewe, uniambie ulipomweka, nami nitamwondoa.” Yohana 20:15

Ni rahisi sana watu wasiokufahamu kukuamini kuhusu mambo ya imani kuliko mtu aliyekuzoea mfano mama yako au ndugu uliokua nao. Hawawezi kuamini kirahisi; ndiyo maana Yesu alimtokea mama yake kwa sura nyingine kama mtunza bustani, ili aweze kumwamini. Aliweza kufanya hivyo kwa sababu alikuwa rohoni. Watu wamemzoea Yesu wa kuponya magonjwa tu lakini Yesu anatokea kwa sura nyingine nyingi ili mambo yaweze kutokea na watu wamwamini.

Hivyo ili uweze kufanya jambo la rohoni lazima uvae sura nyingine. Imeandikwa; 

“Mimi Yohana, ndugu yenu na mwenye kushiriki pamoja nanyi katika mateso na ufalme na subira ya Yesu Kristo, nalikuwa katika kisiwa kiitwacho Patmo, kwa ajili ya Neno la Mungu, na ushuhuda wa Yesu.
Nalikuwa katika Roho, siku ya Bwana; nikasikia sauti kuu nyuma yangu, kama sauti ya baragumu,” Ufunuo 1:9-10

Roho inaweza kuvaa sura yoyote ndiyo maana Yesu alimtokea Yohane katika sura nyingine kwenye kisiwa cha Patmo. Imeandikwa;

“Bwana akamtokea Ibrahimu karibu na mialoni ya Mamre, alipokuwa ameketi mlangoni pa hema yake mchana wakati wa hari.  Akainua macho yake akaona, na tazama, watu watatu wamesimama mbele yake. Naye alipowaona alipiga mbio kuwalaki kutoka mlangoni pa hema, akainama mpaka nchi,” Mwanzo18: 1-2

Kumbe roho inaweza kugeuka na kuwa kitu chochote, na kufanaya kazi kama wanadamu. Imeandikwa;

“Huwafanya malaika zake kuwa pepo, Na watumishi wake kuwa moto wa miali.” Zaburi 104:4

Unaweza ukakuta upepo mkubwa sana umevuma na ukaleta maafa makubwa. Wanasayansi wakauita janga la asili, wakalipa jina na kupima spidi yake na kutoa majibu ya maafa yaliyotokea. Lakini kumbe ndani ya upepo ule kulikuwa na mtu. Lazima utambue kuwa kuna upepo  unaosumbua hali ya maisha yako ndo maana unaona taabu na misukosuko; na yupo aliyejigeuza kuwa huo upepo.

Yesu aliposema na tuvuke ng’ambo, shetani aliyajua hayo na kutikisa chombo. Tambua hata wewe kwenye maisha yako ukiona umepanga kufanya jambo lolote la maendeleo na mara gafla matatizo yanaanza kuibuka jua yupo anayetikisa chombo chako. Usikubali, pigana maana ni upepo  uliotengenezwa ili usifike unakokwenda au usifanye unachotakiwaa kufanya. Imeandikwa;

 Ndipo Farao naye akawaita wenye akili na wachawi; na hao waganga wa Misri wakafanya vivyo kwa uganga wao.
Wakabwaga chini kila mtu fimbo yake, nazo zikawa nyoka; lakini fimbo ya Haruni ikazimeza fimbo zao.”
   Kutoka 7: 11-12

Hii haimanishi kuwa mashetani wana uwezo wa kutengeneza chura, au nyoka au fimbo ila tu waliagiza mashetani mengine yajigeuze kufanyika chura, nyoka au fimbo. Kama ambavyo malaika wa nuru wanavyoweza kuvaa maumbo,  mashetani pia wanaweza kuvaa sura na maumbo ya kitu na kutimiza kusudi. Imeandikwa;

“Wala si ajabu. Maana Shetani mwenyewe hujigeuza awe mfano wa malaika wa nuru.” 2Wakorintho 11:14
Wenye matatizo mbali mbali wanafunguliwa kwa jina la yesu.

 Aina Nne za Mashetani.

1.   Majoka amabao ni roho ya uovu walioanguka kutoka mbinguni baada ya uasi.

 

“Kulikuwa na vita mbinguni; Mikaeli na malaika zake wakapigana na yule joka, yule joka naye akapigana nao pamoja na malaika zake;” Ufunuo 12:7

 

2.   Mizimu. Haya ni mashetani waliotawala ukoo kwa muda mrefu. Sio roho za watu waliokufa kwenye ukoo bali ni mashetani ambayo yanaufahamu ukoo kwa undani.

3.   Miungu. Ni mashetani waliopewa makafara kwa muda mrefu na wakapewa nguvu na kuwa miungu

4.   Majini. Hawa ni mashetani wenye asili ya kiarabu. Hupatikana kwenye sehemu zenye tamaduni za kiarabu.

Imeandikwa;

  Nikaona roho tatu za uchafu zilizofanana na vyura, zikitoka katika kinywa cha yule joka, na katika kinywa cha yule mnyama, na katika kinywa cha yule nabii wa uongo.   Ufunuo 16:13

 Akalia kwa sauti kuu, akisema, Umeanguka, umeanguka Babeli ule mkuu; umekuwa maskani ya mashetani, na ngome ya kila roho mchafu, na ngome ya kila ndege mchafu mwenye kuchukiza;    Ufunuo 18:2

Nguvu kubwa ya mashetani ni ule uwezo wa kutokutambulikana. Wanapotoka ndani ya miili huwa wananuiza na kuvaa maumbo bandia. Wachawi huwa wanakaa na kukusikiliza  kama umewatambua, kutokuwatambua kwako ni furaha kwao maana wanajua kuwa kuna jambo limefanyika na wamefanikiwa.

Maelfu ya watu wakiwa ndani ya bonde la kukata maneno
 
UKIRI
 ''Kuanzia leo lazima kila atakayekuja kuniroga nitamuona kwa jina la Yesu. Kila aliyegeuza umbo naamuru nimuone katika umbo lake la asili kwa jina la Yesu.''

Wapo watu ambao ukiongea nao husema kuwa wanasikia miguu inawaka moto au misumari ndani ya masikio. Wasilolijua watu hawa ni kuwa mashetani yamevaa umbo la moto au misumari na kukaa ndani ya miili yao. Inawezekana, unajisikia kumtukana mume au mke wako  lakini baada ya kufanya tendo hilo wewe mwenyewe unashangaa ilikuwaje. Wameuvaa mdomo wako ndio maana. Inawezekana umeuwekea uso wako kila aina ya urembo lakini bado unaonekana kama babu. Yupo aliyevaa umbo la babu na kukaa kwenye uso wako. Ukiona nchi inayumbayumba lazima ujue kuna chanzo chake kiko katika ulimwengu wa roho. Ukishinda vita ya rohoni mwilini waweza kushinda bila hata kuwa na silaha rasmi.
 


 
MAOMBI

 Ewe jini, joka, mzimu, uliyegeuka umbo na kuja kwangu, lazima nikuone katika jina la Yesu. Ninaaamuru wapigwe katika jina la Yesu. Ninasimama kama askari  wa jeshi la Bwana, naangusha ngome za balaa, ngome za mikosi, ngome za magonjwa katika jina la Yesu. Mimi nakataa kutawaliwa na mashetani katika jina la Yesu.

Kuanzia sasa roho yoyote iliyogeuka na kuwa balaa, talaka, mikosi, magonjwa, naivunja katika jina la Yesu. Kwa jina la Yesu, kuanzia leo chochote kilichotumwa kwangu, nilichokinunua kwa fedha yangu ila ni shetani aliyevaa umbo, nakiangamiza katika jina la Yesu. Kitu chochote, au roho yoyote, iliyo ndani ya nyumba yangu naivunja, nairudisha ilikotoka katika jina la Yesu. Amen!

2.   UNAMFUMBA MTU ASIKUTAMBUE.

Sheria ya pili ni kuwafumba watu ili wasiwatambue. Yani, uendelee kuamini kuwa vitu uvionavyo kwa macho au ndotoni ndivyo vilivyo. Akili ya mtu ikifungwa mtu akiona hatambui kama ni wachawi au mashetani. Yawezekana kila ukilala na kuota ndoto ukiamka unaanza kusema uliyoyaota ambayo yako katika  sura bandia. Inatakiwa uwafunge ili wasijifiche wakija uwatambuae katika jina la Yesu.  Bila kuomba huwezi kupokea uwezo wa kuwatambua. Imeandikwa ;

“Nanyi mkiomba lo lote kwa jina langu, hilo nitalifanya, ili Baba atukuzwe ndani ya Mwana. Mkiniomba neno lo lote kwa jina langu, nitalifanya”  Yohana 14:13-14
Maelfu wakimsifu  Mungu katika bonde la kukata maneno..

MAOMBI

 Katika jina la Yesu namteketeza mtu yeyote aliyejigeuza sura ili anitese, ninamfyeka katika jina la Yesu.

Kila atakayekuja katika umbo lolote lazima nimjue katika jina la Yesu,  ninawafunga wasinitambue kama mimi nimewaona. Kuanzia leo naamka kutoka kwenye usingizi wa kiroho, akili yangu iwaze kutawala, iwaze biashara katika jina la Yesu . Kuanzia leo naanza kutambua kazi yangu, naanza kuelewa kazi ya kufanya, biashara ya kufanya, katika jina la Yesu.

Nawashambulia mashetani wote katika jina la Yesu, mashetani walioshikilia familia yangu, kazi yangu, ndoa yangu, biashara yangu katika jina la Yesu. Ninawaangamiza katika jina la Yesu. Nawaangamiza maadui zangu wote katika jina la Yesu. Natumia mamlaka aliyonipa Yesu, ninawafyeka wanaozuia kazi yangu ninawafyeka wanaozuia ndoa yangu, ninawafyeka wanaozuia huduma yangu katika jina la Yesu. Nawashambulia kwa damu ya mwanakondoo. Imeandikwa;

“Kila silaha itakayofanyika juu yako haitafanikiwa na kila ulimi utakaoinuka juu yako katika hukumu utauhukumu kuwa mkosa. Huu ndio urithi wa watumishi wa Bwana, na haki yao inayotoka kwangu mimi, asema Bwana.”  Isaya 54:17

 Nawafyeka katika jina la Yesu, mtu yeyote aliyesimama kwenye njia zangu kunizuia nisifanikiwe, kuzuia nisisonge mbele, kunizuia nisipate ajira, nafunga uwezo wako wa kujigeuza na kuwa balaa,  mikosi, kuwa matatizo ,kuwa mtego, nawashambulia katika jina la Yesu.

Naharibu uwezo wenu katika jina la Yesu, nang’oa madhabahu zenu katika jina la Yesu. Nawatiisha, nakata mamlaka zenu, kila kiumbe kinachotumika kuharibu maisha yangu nakishambulia katila jina la Yesu. Naharibu uweza wenu wote katika jina la Yesu.

Natangua yote mliyoyapanga katika jina la Yesu. Imeandikwa;

“yeye uyatangua mashauri ya wadanganyifu na mikono yao isipate kutimiza makusudi yao.”

Kila vibarua wa shetani mnaovaa sura bandia nawaangamiza katika jina la Yesu, navunja kila laana ya familia iliyonipata kupitia viumbe wa rohoni mnaojibadilisha sura na kuniroga. Ninawafyeka katika jina la Yesu.

Kila nguvu ya giza inayotawala maisha ninailaani katika jina la Yesu, kila balaa zinazotawala maisha yangu nazivunja katika jina la Yesu. Nakiri leo niko huru, maisha yangu yako huru katika jina la Yesu. Amen!
Hakika Mungu ni mwema kwa watu wanaomtumainia yeye.

Monday, October 13, 2014

HAIKUWA HIVYO TANGU ZAMANI


IBADA YA JUMAPILI YA TAREHE 12/10/2014

MCHUNGAJI JOSEPHAT GWAJIMA

SOMO: HAIKUWA HIVYO TANGU ZAMANI

Utangulizi
Mchungaji kiongozi Josephat Gwajima

 Kanisa leo limefanywa kuwa mahali pa kukutania baada ya uchovu wa wiki nzima. Lakini haikuwa hivyo tangu zamani; kanisa lilianzishwa kama mahali pa kutatua matatizo yaliyoshindikana ndani ya wiki nzima.
“Kwa maana viumbe vyote pia vinatazamia kwa shauku nyingi kufunuliwa kwa wana wa Mungu.
Kwa maana viumbe vyote pia vilitiishwa chini ya ubatili; si kwa hiari yake, ila kwa sababu yake yeye aliyevitiisha katika tumaini;
Kwa kuwa viumbe vyenyewe navyo vitawekwa huru na kutolewa katika utumwa wa uharibifu, hata viingie katika uhuru wa utukufu wa watoto wa Mungu.
Kwa maana twajua ya kuwa viumbe vyote  pia vinaugua pamoja, navyo vina utungu pamoja hata sasa.” Warumi 8:19-22

Kumbe kuna viumbe ambavyo vimebebeshwa utumwa wa aina fulani ambavyo vinategemea kuwekwa huru.
Ulimwengu tunaouendea utakuwa ni ulimwengu ambao sio wa kushinda kwa sababu ndugu yako ni mbunge, waziri ama raisi, bali utakuwa ni ulimwengu wa kushinda mambo yote kwa imani. Tunakiendea kizazi ambacho mwenye haki ataishi kwa imani.

“Mungu akawabarikia, Mungu akawaambia, Zaeni mkaongezeke, mkaijaze nchi, na kuitiisha; mkatawale samaki wa baharini, na ndege wa angani, na kila kiumbe chenye uhai kiendacho juu ya nchi.” Mwanzo1:28
Haya ni mamlaka ambayo Mungu alimpa mwanadamu zamani sana kabla nyumba hazijajengwa, kabla  mavazi hayajaanza kutengenezwa. Kwanza ni kuzaa na kuongezeka iwe mwilini au rohoni. Pili ni kutiisha kila kitu kwenye nchi; mapori, majangwa, milima. Tatu, kutawala kila kitu angani, baharini na nchi kavu. Hivi ndivyo ilivyokuwa tangu mwanzo, asili yetu kama wana wa Mungu ni kutawala sio kutawaliwa. Lakini leo wana wa Mungu wamekuwa watu wakuogopaogopa; sivyo ilivyokuwa. Tuliumbwa kutiisha na kutawala angani, baharini na kwenye nchi.
Mungu ni Mungu wa kusema. Kabla hajatenda huwa anaongea kwanza. Ndio maana biblia nzima imejaa ahadi za Mungu, anasema atatubariki, atatuinua. Hivyo inatupasa  na sisi kuongea na kuikiri asili yetu. Tunatawala kwa mujibu wa sheria ya kitabu cha Mwanzo ibara ya kwanza kifungu cha ishirini na nane. Biblia ni sheria ya Bwana wa Majeshi na sheria hii haiwezi kubadilika kizazi hata kizazi.

Kwa asili ya mwanadamu alitakiwa atawale majini, angani na katika nchi. Shetani alipoona mwanadamu amepewa mamlaka hiyo akamfuata Adamu ili aibe mamlaka hiyo. Kwa kuwa sisi nasi tulikuwa katika viuno vya Adamu wakati anatenda dhambi iliyomgharimu mamlaka yake tumehesabiwa dhambi kutoka kwake..
“Nanyi mlikuwa wafu kwa sababu ya makosa na dhambi zenu;
Ambazo mliziendea zamani kwa kuifuata kawaida ya ulimwengu huu, na kwa kumfuata mfalme wa uwezo wa anga, roho yule atendaye kazi sasa katika wana wa kuasi;

Ambao zamani, sisi sote nasi tulienenda kati yao, katika tama za miili yetu, tulipoyatimiza mapenzi ya mwili nay a nia, tukawa kwa tabi yetu watoto wa hasira kama na hao wengine” Waefeso 2:1-3
Ndio maana leo shetani anaitwa mkuu wa anga. Kabla ya Adamu na Eva hawajatenda dhambi walikuwa wanatiisha anga, nchi na bahari. Walipokosea walipoteza mamlaka yao ambayo ilichukuliwa na shetani. Shetani aliichukua anga na kuitawala ndio maana akaitwa mfalme wa anga.
“Nao wakamshinda kwa damu ya mwanakondoo, na kwa neno la ushuhuda wao; ambao hwakupenda maisha yao hata kufa.
Kwa hiyo shangilieni enyi mbingu, nanyi mkaao humo. Ole wan chi na bahari! Kwa maana yule ibilisi ameshuka kwenu mwenye ghadhabu nyingi, akijua ya kuwa ana wakati mchache.” Ufunuo12:11-2
Adamu alikuwa anamiliki anga, bahari na nchi. Shetani alipofanikiwa kumtoa Adam, akafanikiwa kumiliki vyote alivyokuwa anamiliki. Ndio maana sasa kuzimu ina sehemu kuu tatu; angani, baharini na kwenye nchi.
Kama wana wa Mungu ambao tunatakiwa kuishi kwa imani ili kumpendeza Mungu;  kutamka, kusema na kukiri ahadi za Mungu kabla hazijawa bayana katika ulimwengu wa mwili ni sehemu ya maisha yetu. Tamka kwa bidii yaliyomo ndani ya moyo wako kwa maana uweza wa uzima na mauti u ndani ya kinywa chako. Hii ndiyo imani itupasayo kuishi kwayo. Imani ina viwango vinne;

Ø Unachowaza
Awazavyo mtu moyoni mwake ndivyo alivyo. Ni muhimu kujua namna ya kuyatiisha mawazo yako ili yawe sawasawa na namna ambavyo Mungu anawaza kuhusu wewe.

Ø Unachosema
Chochote uwazacho baada ya muda fulani utakikiri kwa kuwa hii ndiyo asili yetu kutoka kwa Mungu; kusema kabla jambo halijatokea.

Ø Unachotenda
  Ukishawaza na kukiri ni lazima uanze kutenda kuelekea kwenye lile jambo ambalo unaloliamini.

Ø Tendo la Imani
Hili ni tendo ambalo unatenda ambalo huwa ni kinyume na hali halisi ya mambo katika ulimwengu wa mwili.
Pasipo Imani haiwezekani kumpendeza Mungu. Mungu ni Mungu wa makusudi, hivyo lazima ufahamu kusudi lako katika maisha. Maendeleo hayaji kwa kuota utakuwa unatembea ukaokota mamilioni ya fedha halafu ukafanikiwa, mafanikio yoyote huja kwa hatua za kuhifadhi kidogokidogo kile ulicho nacho. Pale ambapo kusudi lisipofahamika matumizi mabaya lazima yatokee.

Hivyo shetani alipomtoa Adamu kwenye utawala akakaa yeye kuwa mtawala wa anga, nchi, bahari na vyote vilivyomo. Kabla Adamu hajatenda dhambi, akiwa bado ni mtawala; sisi tulikuwa ndani ya viuno vyake hivyo tulionja utawala huo. Baada ya shetani kuuchukua utawala kutoka kwetu, ana uwezo wa kuvitiisha viumbe vyote baharini, angani na kwenye nchi. Anayo mamlaka ya kuamuru viumbe kama bacteria, virusi , protozoa kuingia ndani ya miili ya wanadamu na kusababisha magonjwa au hata mauti. Leo dunia ina kila aina ya magonjwa na nyuma ya kila ugonjwa kuna kiumbe. Lakini viumbe hivi vimetiishwa kwa ubatili na yule aibaye ambaye ameiba mamlaka yetu. Haikuwa hivyo tangu zamani.
Mwanzoni Adamu hakuwa na magonjwa kabisa kwasababu alikuwa anatawala anga na viumbe vyake vyote, nchi na viumbe vyake vyote bahari na viumbe vyake vyote. Hivyo viumbe vyote vilikuwa chini ya utiisho wake. Hii ndiyo asili ya mwanzo ya mwanadamu.
Kwa nini leo kila janga kubwa linatokea Afrika? Vita vya kikabila, siasa mbovu, umaskini uliopitiliza, magonjwa ya ajabu; ukimwi unaua sana Afrika, ebola, mafua ya ndege, mafua ya nguruwe, dengue. Ni nini kinatokea? Shetani hawapendi waafrika kwa sababu anajua kutokea kwao ndipo utakapotokea ule uamsho wa siku za mwisho utakaogeuza tawala zote kuwa tawala za mwanakondoo. Imani bado ipo Afrika.
Tangu mwanzo shetani amekuwa akiona dalili za Afrika kuwa jeshi la mwisho la Mungu ndio maana anainua vita juu yake. Wana wa Israeli waliishi Afrika kwa miaka mia nne na thelathini utumwani Misri, miujiza mingi ilitokea Afrika  kule Misri. Haitoshi  alipozaliwa Yesu, malaika alimtokea Yusufu akamwambia amchukue Mariamu mkewe na mtoto Yesu na kuwapeleka katika nchi ya Misri. Wakati wa kubeba msalaba, ilipofika hatua  Yesu hawezi kuubeba tena alitokea Simon mkrene (Krene ni Afrika mahali panapoitwa Libya leo.) akaubeba msalaba mpaka Kalvari. Hii ni kuonyesha kuwa injili ya siku za mwisho itabebwa na waafrika. Ndio maana biblia inasema kutakuwepo na madhabahu katika nchi ya Afrika ( Isaya 19:4) 4 Nami nitawatoa hao Wamisri na kuwatia katika mikono ya bwana mgumu; na mfalme mkali atawatawala; asema Bwana, Bwana wa majeshi.
Yesu alivyokuja duniani alikuja kuturudishia utawala wetu ulioibiwa na shetani. Basi kumbe leo shetani anatawala isivyo halali, sisi ndio watawala halali. Tunayo mamlaka ya kuvitiisha viumbe vyote viletavyo magonjwa  kukaa nje ya mipaka ya Tanzania kwa jina la Yesu na vikatii.
Ebola ni mpango wa kuzimu, ni hukumu ya kifo kwa waafrika ili kuipunguza nguvu yetu. Na sisi kama watawala leo tumegundua asili yetu na hila ya yule alaye. Hivyo inatupasa kuchukua hatua kama watawala kutiisha, kumiliki na kutawala.
 
 
Maelfu ya watu wakiomba ndani ya bonde la kukata maneno

MAOMBI.
Ninaamuru kama mtawala wa bakteria, virusi na viumbe vyote wa magonjwa hamna uwezo juu yangu kwa jina la Yesu. Hamna mamlaka juu ya Tanzania. Ninawatiisha viumbe wote wanaoonekana na wasioonekana wasababishao magonjwa kwa jina la Yesu, hamtaingia ndani ya Tanzania kwa jina la Yesu. Kwa mamlaka niliyonayo ninawafunga virusi wote wa mafua ya ndege, virusi wa mafua ya nguruwe, ebola  nje ya Tanzania kwa damu ya Yesu. Kemikali zote, bakteria, protozoa wote ninawatiisha kwa damu ya Yesu Kristo. Kwa mamlaka ya damu ya mwanakondoo, viumbe wote wa magonjwa ninaupiga ule uweza uliowekwa ndani yenu juu ya Tanzania, juu ya Afrika, juu ya maisha yangu, juu ya familia yangu; ninaamuru kuanzia sasa  hamtaingia ndani ya nchi ya Tanzania kwa jina la Yesu.Ninavimiliki na kuvitiisha viumbe vyote vinavyokaa kwenye anga, bahari, na nchi. Mimi ni mtawala wenu, hamna mamlaka ya kunitawala  haikuwa hivyo tangu zamani. Ninawaseta mrudi kuzimu mlikotoka kwa jina la Yesu. Ninaamuru kuanzia sasa hamtanidhuru kwa damu ya Yesu. Viumbe vyote vinavyoonekana na visivyoonekana hamna uwezo wa kunitawala kwa jina la Yesu Kristo. Ninabeba mamlaka kama mtawala, ninawateketeza na uwezo wenu wa kudhuru kwa damu ya mwanakondoo. Nimepewa amri juu ya pepo wachafu na viumbe vyote, ninaangamiza kila nguvu iliyo juu yenu ninyi viumbe wa kishetani na kichawi na waganga wa kienyeji, ninawakausha kwa damu ya Yesu Kristo. Niwaondolea ule uwezo wa kuidhuru Tanzania kwa mamlaka ya damu ya mwanakondoo. Ninaiachilia damu ya mwanakondoo kwenye mipaka yote ya Tanzania,  damu inenayo  mema, ninainyunyizia kwenye mipaka yote ya Taifa la Tanzania na juu ya watu wake wote. Iwalinde dhidi ya magonjwa yote kwa jina la Yesu. Kwa mamlaka ya Jina la Yesu kristo ninatawala viumbe vvyote  vilivyomo baharini,  angani na kwenye nchi kwa damu ya Yesu. Ninatawala uchumi wa nchi, utajiri wa nchi; ninautawala kwa jina la Yesu Kristo. Ninatawala kwa jina la Yesu Kristo, ninatawala na kuvitiisha viumbe vyote vya magonjwa kwa jina la Yesu Kristo. AMEN!
  

Sunday, October 5, 2014

MADHABAHU ZA KICHAWI ZINAZOWAFANYA WATU KUSHINDWA ZABOMOLEWA NA KUVUNJWA.


IBADA YAJUMAPILI TAREHE 05/10/2014

NA MCHUNGAJI MWANDAMIZI: ADRIANO MAKAAZI

SOMO: MADHABAHU YA KUSHINDWA
Mchungaji mwandamizi Adriano Makaazi

Madhabahu ni eneo linalojengwa na mtu au watu kwa ajili ya kutolea kafara.  Kafara hii yaweza kuwa mbuzi, ng’ombe au mwanadamu. Ziko madhabahu  maeneo mbalimbali zilizojengwa ili kila jambo atakalolifanya mtu fulani lisifanikiwe. Mtu anaweza kufungua duka halafu baada ya muda akalifunga kwasababu ya kutokufanikiwa kinyume na matarajio yake. Kila analolifanya linashindikana, anakuwa mtu wa kushidwa shindwa. Mtu wa aina hii anatakiwa kutambua kuwa kuna madhabahu ya kushindwa aliyotengenezewa. Madhabahu inaweza kuwaleta watu pamoja, kumwabudu  na kusema na Mungu wa mbinguni au shetani. Unaweza kufika madhabahuni pa BWANA ukiwa mgonjwa lakini ukaondoka mahali hapo ukiwa mzima. Na hii ni kwa kuwa, madhabahu ni daraja la kumkutanisha Mungu na mwanadamu.

 WATU WALIOMJENGEA MUNGU MADHABAHU KATIKA BIBLIA

IBRAHIMU

Ibrahimu, baba wa imani aliambiwa na Mungu atoke katika nchi aliyozaliwa ya uru wa wakaldayo na aende katika nchi ya mbali BWANA atakayomuonyesha, na amjengee BWANA madhabahu huko. Ibrahimu  alitii neno la BWANA na akamjengea  madhabahu. Imeandikwa;
Mchungaji Mwandamizi Baraka Thomas

 Bwana akamtokea Abramu, akasema, Uzao wako nitawapa nchi hii. Naye huko akamjengea madhabahu Bwana aliyemtokea.
8 Kisha akaondoka huko akaenda mpaka mlima ulio upande wa mashariki wa Betheli, akaipiga hema yake; alikuwa na Betheli upande wa magharibi, na Ai upande wa mashariki, akamjengea Bwana madhabahu huko, akaliitia jina la Bwana.
Mwanzo 12:7-8

Kupitia madhabahu hii aliyoagizwa kujenga Ibrahimu aliweza kuwasiliana na Mungu.

 Imeandikwa;

 Wakafika mahali pale alipoambiwa na Mungu, Ibrahimu akajenga madhabahu huko, akaziweka tayari kuni, kisha akamfunga Isaka mwanawe, akamweka juu ya madhabahu, juu ya zile kuni. Mwanzo 22:9

Ibrahimu alikuwa mtu aliyefanikiwa sana kutokana na madhabahu aliyoijenga. Kumbe madhabahu ni kiunganishi cha Baraka kutoka kwa Mungu anayeabudiwa kwenye madhabahu husika mpaka kwa anayeabudu. Hivyo ni dhahiri kuwa mikosi, balaa na matatizo mengine pia yana chanzo chake kutokea kwenye madhabahu. Kwa akili yako unaweza kuhisi kuwa kushindwa kwako ni kwasababu ya elimu yako ulionayo, au mtaji kidogo ulionao. Mawazo yako sio kweli wala sio sahihi, tambua kuwa kuna madhabahu imejengwa inayofanya kazi ya kupolomosha mambo yako. Leo kwa jina la Yesu tunabomoa kila madhabahu ya kushindwa kwako.

Katia nyakati tulizonazo leo, watu wanamjengea shetani madhabahu kwenye magari yao, ofisi zao na hata nyumba zao. Kutokana na madhabahu hizi, waweza kuona mtu anapandishwa cheo bila kustahili; wakati yule aliyestahili anahamishwa ofisi ghafla au anakufa. Ni madhabahu ya kushindwa imefanya kazi.
Mwimbaji John Lisu

Bwana akamtokea usiku uleule, akasema, Mimi ni Mungu wa Ibrahimu baba yako, usiogope, maana mimi ni pamoja nawe, nami nitakubarikia, na kuzidisha uzao wako kwa ajili ya Ibrahimu mtumishi wangu.
Akajenga madhabahu huko, akaliitia jina la Bwana. Akapiga hema yake huko, na watumwa wa Isaka wakachimba kisima huko.
Mwanzo26:24-25.

Utaona Isaka kama ilivyokuwa kwa baba yake, yeye pia anamjengea MUNGU Yehovah madhabahu. Ili uweze kuwa na uhusiano wa kudumu Mungu uweze lazima umjengee  madhabahu. Pia tunaona kuwa anachokifanya baba mara nyingi mtoto naye hukifanya; hivyo aliyeabudiwa na baba mara nyingi ndiye ambaye huabudiwa na mwana.

Madhabahu inaweza kuwa chanzo cha Baraka zako au shida yako. Hivyo madhabahu zilizojengwa na wazazi wako au watu wa kale katika ukoo wako yaweza kuwa ndio chanzo cha Baraka au kushindwa kwako leo. Mfano Gideoni, alikuwa amekuwa mtu dhaifu kwa sababu alikuwa ameteswa na madhabahu ya kishetani  iliyokuwa imejengwa na baba yake.

Kila madhabahu inayojengwa hujengwa kwa sababu maalum. Ipo madhabahu imejengwa mahali kwa jina lako ili ushindwe na kufa katika matatizo uliyonayo. Unyonge wako ni kwasababu ya madhabahu iliyojengwa  ili ikutese. Leo tutawaagiza malaika wa BWANA wazisake madhabahu za kushindwa   zilizokufunga  kwa muda mrefu sana.

   UKIRI: MIMI NI SHUJAA WA BWANA, KWA MSAADA WA BWANA NALIENDEA JESHI NA KULIKANYAGA. NALIPONDA NA KULIONDOSHA  KWA JINA LA YESU.

 

NUHU

 Nuhu mara baada ya kutoka kwenye safina alimjengea BWANA madhabahu na kuweka sadaka mbele zake. Unapotaka kumtolea Mungu unapashwa kumtolea kilichosafi. Ili madhabahu iwe na nguvu lazima kuwepo sadaka juu yake tena iliyosafi. Mfano Habili alimtolea Mungu sadaka nono na yakupendeza na Mungu akapendezwa nayo. Ni vizuri kujiuliza kwanza kabla ya kumtolea Mungu sadaka kuwa unatoa nini mbele za BWANA?

Mara baada ya sadaka ya Nuhu mbele za BWANA, Mungu akafanya agano na Nuhu kuwa hataiangamiza tena nchi kwa gharika kama lile, na akaweka ishara ya upinde wa mvua. Imeandikwa:

 Nuhu akamjengea Bwana madhabahu; akatwaa katika kila mnyama aliye safi, na katika kila ndege aliye safi, akavitoa sadaka za kuteketezwa juu ya madhabahu.Mwanzo 8:20

Unaweza kutafuta kwa taabu sana, hali ikawa nzuri baada ya taabu kubwa lakini kama kuna madhabahu ya kushindwa imejengwa kwa ajili yako utaishia kufa mara tu baada ya kupata. Tambua kuwa unapaswa kupigana na kushindana ndio amani ya maisha yako iweze kupatikana. Usisubiri kufarijiwa, faraja unatakiwa kuitafuta wewe mwenyewe kwa kupigana na kushindana juu ya ufalme wa giza. Imeandikwa:

Kwa maana kushindana kwetu sio juu ya damu na nyama…. Waefeso6:12

Tunatakiwa kushindana siku zote bila kuzimia mioyo. Wale waliokujengea madhabahu ya kushindwa wao pia hawakati tamaa. Hata pale wanapoona umeanza kuwa na bidii ya kuomba na kuhudhuria ibada. Wao pia huzidi kuimarisha madhabahu kwa kuzidi kutoa kafara ili kuendelea kukuweka katika hali ya kushindwa. Imeandikwa:

Naye mfalme wa Moabu alipoona ya kwamba ameshindwa vitani, alitwaa pamoja naye watu mia saba wenye kufuta panga ili wapenye hata kwa mfalme wa Edomu; wala hawakudiriki.   2Wafalme3:26

UKIRI: Nakataa  kushindwa, nakataa kukata tamaa kwa jina la Yesu. Kila madhabahu ya kushindwa iliyojengwa  kwa jina langu naibomoa kwa jina la Yesu, kila madhabahu iliyojengwa angani, baharini, ufukweni au bondeni  ili mimi nishindwe, leo naibomoa kwa jina la Yesu. Kila madhabahu ya kukataliwa, kuonewa naibomoa kwa damu  ya Yesu. Amen.

Zamani watu walikuwa wanatoa kafara ili washinde vita, hata ulimwengu wa sasa watu wengine wanatoa kafara kwa mashetani ili waweze kushinda katika nafasi za ushindani kama vile biashara, utawala, vyeo maofisini, au kataika kutafuta kazi. Nawe pia lazima uingie katika ulimwengu wa kushindana na upate kushinda. Lakini ushindani wako wewe ni kinyume na wao, yakupasa kushindana kwa Jina la Yesu. Mtu anapokushinda, ujue amekutolea kafara kwenye madhabahu ya kishetani. Lakini neno la Mungu linatuonyesha kuwa Yesu alitoa kafara ya damu yake yenye thamani kuliko damu zote ili tupate kushinda siku zote.  Imeandikwa:   

Nao wakamshinda kwa damu ya Mwana-Kondoo, na kwa neno la ushuhuda wao; ambao hawakupenda maisha yao hata kufa. Ufunuo 12:11

 

 

 

Kafara ya Madhabahu

Kafara hii mara nyingi huwa ni damu inayomwagika juu ya madhabahu husika. Ukiharibu damu iliyo kwenye madhabahu, madhabahu haina nguvu tena. Kafara inayo mwagwa juu ya madhabahu ya mashetani ndiyo inayowapa nguvu ya kutenda jambo lolote la uharibifu juu ya wanadamu. Waganga na wachawi wanapotaka ushindwe, ukataliwe, uwe mgonjwa au upatwe na tatizo lolote; kafara ya damu ndiyo inayotumiwa kutenda kazi.

 

UKIRI:  Leo kwa jina la yesu kila damu inayonifanya nisishinde, niwe mgonjwa, nionewe, nainyamazisha kwa jina la Yesu.

Imeandikwa :

 Akasema, Umefanya nini? Sauti ya damu ya ndugu yako inanililia kutoka katika ardhi. Mwanzo 4:10

Kisha mtu awaye yote wa nyumba ya Israeli, au miongoni mwa hao wageni wakaao kati yao, atakayekula damu, ya aina yo yote, nitakunja uso wangu juu ya mtu huyo alaye damu, nami nitamkatilia mbali na watu wake. Mambo ya walawi 17:10

Kumbe basi kama damu inaweza kulia, vivyo hivyo yaweza kuongea. Hivyo kwa kadri ile damu iliyomwagwa juu ya madhabahu ya kushindwa inazidi kunena ndivyo na wewe unavyozidi kuwa mtu wa kushindwa. Hii ndiyo sababu Mungu alikataza tusile damu, maana ndimo ulimo uhai.

UKIRI: Kila aliyetoa kafara kuharibu ndoa yangu, damu iliyotolewa juu ya madhabahu ilitolewa ili mimi nishindwe na kuangamia, leo naiponda damu hiyo na kuisambarataisha kwa jina la Yesu. AMEN

 

 

MAOMBI:

Katika jina la Yesu Mungu baba naomba msamaha kwa kila dhambi niliyokutenda kwa kujua au kutokujua. Naomba unisamehe uovu wangu na unitakase kwa ajili ya vita. maana imeandikwa Daudi akivitakasa vita. Naomba unitakase na unisafishe kwa ajili ya vita. Amen

Maelfu wakivunja madhabahu za kushindwa.
Kila madhabahu ya kushindwa iliyojengwa juu ya ukoo wetu ili uwe ukoo wa kushindwa au kufakufa, madhabahu iliyojengwa angani, mabondeni au milimani leo naibomoa kwa jina la Yesu.

Wewe uliyejenga madhabahu ya kukataliwa juu ya maisha yangu naiangusha leo kwa jina la Yesu. Imeandikwa: Nao wakamshinda kwa damu ya mwanakondoo na neno la ushuhuda wao. Ewe madhabahu nakushinda kwa jina la Yesu.  Wewe uliyenitesa kwa madhabahu yako leo nakupasua na naipasua na kafara yako kwa jina la Yesu. Kwa maana imeandikwa: Nimekuweka juu ya mataifa na juu ya falme ili kubomoa na kuvunja na kuharibu na kuangamiza katika jina la Yesu.

Kila madhabahu iliyojengwa ili niwe mtu wa kushindwa; kushindwa kwa familia, kushindwa kwa taifa langu ,ndoa yangu, masomo yangu  naibomoa kwa jina la Yesu. Nakuamuru kwa jina la Yesu toka ndani yangu, achia akili yangu, achia ufahamu wangu, achia  moyo wangu kwa jina la Yesu.

Kila madhabahu iliyojengwa juu ya familia ili tushindwe na kukataliwa naiangusha kwa jina la Yesu. Madhabahu iliyojengwa juu ya nchi yangu Tanzania naiangusha kwa jina la Yesu. Naamuru madhabahu ya kushindwa ipasuke kwa jina la Yesu na kafara ya madhabahu imwagike katika jina la Yesu.

Madhabahu zote njia panda, chini ya milima, mabondeni, nchi kavu naamuru zianguke  katika jina la yesu. Madhabahu iliyojengwa ili mimi niwe wa kupoteza, kuchanganyikiwa, maskini naivunja leo kwa jina la Yesu. Imendikwa: Mimi ni rungu la Bwana na silaha za BWANA za vita; naivunja madhabahu iliyojengwa juu ya mafanikio yangu, juu ya huduma yangu, madhabahu iliyojengwa ili nitumikishwe na mashetani au familia yangu naibomoa kwa jina la Yesu.

Madhabahu iliyojengwa kwenye mtaa wangu, kwenye ukoo wangu, kwenye mji wangu, kwenye nchi yangu naivunja na kuibomoa kwa jina la Yesu. Naipasua na kuiangamiza kwa jina la Yesu.

AMEN.