Monday, October 20, 2014

SHERIA MBILI ZA ROHONI.


SOMO: SHERIA MBILI ZA ROHONI

TAREHE: 19/10/2014

NA MCHUNGAJI KIONGOZI: JOSEPHAT GWAJIMA
Mchungaji kiongozi Josephat Gwajima

 Ulimwengu tunaoishi umegawanyika kwenye sehemu mbili; ulimwengu wa roho na ulimwengu wa mwili. Mambo huanzia kwenye ulimwengu wa roho na kisha hudhihirika katika ulimwengu wa mwili. Mtu anapofanikiwa rohoni baadae anafanikiwa mwilini. Unapopatwa na matatizo mfano magonjwa elewa kuwa matatizo hayo yameanzia rohoni. Unapoanza kuomba na kushambulia lazima utambue kuwa unashindana na ulimwengu wa roho. Imeandikwa;

Kwa maana kushindana kwetu sisi si juu ya damu na nyama; bali ni juu ya falme na mamlaka, juu ya wakuu wa giza hili, juu ya majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho.”   Waefeso 6:12
Mama mchungaji Grace Gwajima

Kumbe kabla ya udhihirisho wa baraka katika maisha yako lazima ubarikiwe rohoni. Ulimwengu wa roho ni dhahiri kabisa, hivyo kama ambavyo tunaona miji katika ulimwengu wa mwili ndivyo ilivyo katika ulimwengu wa roho. Hivyo ukibarikiwa kwenye mji wa Dar-es-salaam rohoni baadae utabarikiwa kwenye mji huo katika ulimwengu wa mwili. Kujua mistari mingi ya biblia sio ishara ya kuwa mtu ni wa kiroho zaidi, Mungu ni roho hivyo ni lazima tumwabudu katika roho na kweli. Imeandikwa.

Viumbe ambavyo makazi yake nikatika ulimwengu wa roho ni Mungu, malaika, mashetani ambao ndio wale malaika walioasi. Viumbe wa kimwili ni kama wanadamu, kuku, simba, miti.

Katika ulimwengu wa roho, kuna sheria mbili zinazouongoza. Mambo yote huanzia katika ulimwengu wa roho, hasa katika ndoto. Zipo sheria mbili, zinazoongoza ulimwengu wa roho.

Mchungaji Kiongozi Josephat Gwajima Akifundisha Sheria mbili za Rohoni
 

1.   UWEZO WA KUBADILI MAUMBO.

Ili mawakala wa shetani ambao ni wachawi waweze kwenda kuroga lazima watoke ndani ya miili yao na kuvaa umbo jingine ili wasitambulikane. Kwa kuwa anakuwa rohoni anaweza kuvaa umbo lolote, kugeuka kuwa kitu chochote mfano paka, mbwa, kunguru. Furaha ya mchawi ni kukusikia ukiendelea kusema jana kulikuwa na paka analia kama mtoto kwenye dirisha langu.  Imeandikwa;

“Baada ya hayo akawatokea watu wawili miongoni mwao, ana sura nyingine; nao walikuwa wakishika njia kwenda shamba.”  Marko 16:12

Yesu aliwatokea wanafunzi wake akiwa na sura nyingine, lakini kwa kuwa alikuwa rohoni, alionekana kuwa na sura nyingine. Yesu ana sura nyingi, kama umezoea kumuona kama daktari leo ana sura nyingine. Akitaka kukutokea kama mmea atakutokea kama ua la sharoni, akitaka kukutokea kama mnyama atakutokea kama simba wa kabila la Yuda, akitaka kukutokea kama kinywaji atakutokea kama maji ya uzima. Lazima utambue kuwa Mungu anaweza kukutokea kwa sura nyingine tofauti na ile uliyoizoea.

Mchungaji Gwajima akimsifu na kumwabudu Mungu.
 

UKIRI

Leo, katika jina la Yesu; Yesu unitokee kwa sura nyingine. Nimezoea kukuona  kama mponyaji tu, leo nitokee kama mfariji, kama mfalme wa wafalme, kama mwamba wa kale. Leo Yesu nitokee kwa sura nyingine sawasawa na tatizo nililonalo. Amen.

 

 “Yesu akamwambia, Mama, unalilia nini? Unamtafuta nani? Naye, huku akidhania ya kuwa ni mtunza bustani, akamwambia, Bwana, ikiwa umemchukua wewe, uniambie ulipomweka, nami nitamwondoa.” Yohana 20:15

Ni rahisi sana watu wasiokufahamu kukuamini kuhusu mambo ya imani kuliko mtu aliyekuzoea mfano mama yako au ndugu uliokua nao. Hawawezi kuamini kirahisi; ndiyo maana Yesu alimtokea mama yake kwa sura nyingine kama mtunza bustani, ili aweze kumwamini. Aliweza kufanya hivyo kwa sababu alikuwa rohoni. Watu wamemzoea Yesu wa kuponya magonjwa tu lakini Yesu anatokea kwa sura nyingine nyingi ili mambo yaweze kutokea na watu wamwamini.

Hivyo ili uweze kufanya jambo la rohoni lazima uvae sura nyingine. Imeandikwa; 

“Mimi Yohana, ndugu yenu na mwenye kushiriki pamoja nanyi katika mateso na ufalme na subira ya Yesu Kristo, nalikuwa katika kisiwa kiitwacho Patmo, kwa ajili ya Neno la Mungu, na ushuhuda wa Yesu.
Nalikuwa katika Roho, siku ya Bwana; nikasikia sauti kuu nyuma yangu, kama sauti ya baragumu,” Ufunuo 1:9-10

Roho inaweza kuvaa sura yoyote ndiyo maana Yesu alimtokea Yohane katika sura nyingine kwenye kisiwa cha Patmo. Imeandikwa;

“Bwana akamtokea Ibrahimu karibu na mialoni ya Mamre, alipokuwa ameketi mlangoni pa hema yake mchana wakati wa hari.  Akainua macho yake akaona, na tazama, watu watatu wamesimama mbele yake. Naye alipowaona alipiga mbio kuwalaki kutoka mlangoni pa hema, akainama mpaka nchi,” Mwanzo18: 1-2

Kumbe roho inaweza kugeuka na kuwa kitu chochote, na kufanaya kazi kama wanadamu. Imeandikwa;

“Huwafanya malaika zake kuwa pepo, Na watumishi wake kuwa moto wa miali.” Zaburi 104:4

Unaweza ukakuta upepo mkubwa sana umevuma na ukaleta maafa makubwa. Wanasayansi wakauita janga la asili, wakalipa jina na kupima spidi yake na kutoa majibu ya maafa yaliyotokea. Lakini kumbe ndani ya upepo ule kulikuwa na mtu. Lazima utambue kuwa kuna upepo  unaosumbua hali ya maisha yako ndo maana unaona taabu na misukosuko; na yupo aliyejigeuza kuwa huo upepo.

Yesu aliposema na tuvuke ng’ambo, shetani aliyajua hayo na kutikisa chombo. Tambua hata wewe kwenye maisha yako ukiona umepanga kufanya jambo lolote la maendeleo na mara gafla matatizo yanaanza kuibuka jua yupo anayetikisa chombo chako. Usikubali, pigana maana ni upepo  uliotengenezwa ili usifike unakokwenda au usifanye unachotakiwaa kufanya. Imeandikwa;

 Ndipo Farao naye akawaita wenye akili na wachawi; na hao waganga wa Misri wakafanya vivyo kwa uganga wao.
Wakabwaga chini kila mtu fimbo yake, nazo zikawa nyoka; lakini fimbo ya Haruni ikazimeza fimbo zao.”
   Kutoka 7: 11-12

Hii haimanishi kuwa mashetani wana uwezo wa kutengeneza chura, au nyoka au fimbo ila tu waliagiza mashetani mengine yajigeuze kufanyika chura, nyoka au fimbo. Kama ambavyo malaika wa nuru wanavyoweza kuvaa maumbo,  mashetani pia wanaweza kuvaa sura na maumbo ya kitu na kutimiza kusudi. Imeandikwa;

“Wala si ajabu. Maana Shetani mwenyewe hujigeuza awe mfano wa malaika wa nuru.” 2Wakorintho 11:14
Wenye matatizo mbali mbali wanafunguliwa kwa jina la yesu.

 Aina Nne za Mashetani.

1.   Majoka amabao ni roho ya uovu walioanguka kutoka mbinguni baada ya uasi.

 

“Kulikuwa na vita mbinguni; Mikaeli na malaika zake wakapigana na yule joka, yule joka naye akapigana nao pamoja na malaika zake;” Ufunuo 12:7

 

2.   Mizimu. Haya ni mashetani waliotawala ukoo kwa muda mrefu. Sio roho za watu waliokufa kwenye ukoo bali ni mashetani ambayo yanaufahamu ukoo kwa undani.

3.   Miungu. Ni mashetani waliopewa makafara kwa muda mrefu na wakapewa nguvu na kuwa miungu

4.   Majini. Hawa ni mashetani wenye asili ya kiarabu. Hupatikana kwenye sehemu zenye tamaduni za kiarabu.

Imeandikwa;

  Nikaona roho tatu za uchafu zilizofanana na vyura, zikitoka katika kinywa cha yule joka, na katika kinywa cha yule mnyama, na katika kinywa cha yule nabii wa uongo.   Ufunuo 16:13

 Akalia kwa sauti kuu, akisema, Umeanguka, umeanguka Babeli ule mkuu; umekuwa maskani ya mashetani, na ngome ya kila roho mchafu, na ngome ya kila ndege mchafu mwenye kuchukiza;    Ufunuo 18:2

Nguvu kubwa ya mashetani ni ule uwezo wa kutokutambulikana. Wanapotoka ndani ya miili huwa wananuiza na kuvaa maumbo bandia. Wachawi huwa wanakaa na kukusikiliza  kama umewatambua, kutokuwatambua kwako ni furaha kwao maana wanajua kuwa kuna jambo limefanyika na wamefanikiwa.

Maelfu ya watu wakiwa ndani ya bonde la kukata maneno
 
UKIRI
 ''Kuanzia leo lazima kila atakayekuja kuniroga nitamuona kwa jina la Yesu. Kila aliyegeuza umbo naamuru nimuone katika umbo lake la asili kwa jina la Yesu.''

Wapo watu ambao ukiongea nao husema kuwa wanasikia miguu inawaka moto au misumari ndani ya masikio. Wasilolijua watu hawa ni kuwa mashetani yamevaa umbo la moto au misumari na kukaa ndani ya miili yao. Inawezekana, unajisikia kumtukana mume au mke wako  lakini baada ya kufanya tendo hilo wewe mwenyewe unashangaa ilikuwaje. Wameuvaa mdomo wako ndio maana. Inawezekana umeuwekea uso wako kila aina ya urembo lakini bado unaonekana kama babu. Yupo aliyevaa umbo la babu na kukaa kwenye uso wako. Ukiona nchi inayumbayumba lazima ujue kuna chanzo chake kiko katika ulimwengu wa roho. Ukishinda vita ya rohoni mwilini waweza kushinda bila hata kuwa na silaha rasmi.
 


 
MAOMBI

 Ewe jini, joka, mzimu, uliyegeuka umbo na kuja kwangu, lazima nikuone katika jina la Yesu. Ninaaamuru wapigwe katika jina la Yesu. Ninasimama kama askari  wa jeshi la Bwana, naangusha ngome za balaa, ngome za mikosi, ngome za magonjwa katika jina la Yesu. Mimi nakataa kutawaliwa na mashetani katika jina la Yesu.

Kuanzia sasa roho yoyote iliyogeuka na kuwa balaa, talaka, mikosi, magonjwa, naivunja katika jina la Yesu. Kwa jina la Yesu, kuanzia leo chochote kilichotumwa kwangu, nilichokinunua kwa fedha yangu ila ni shetani aliyevaa umbo, nakiangamiza katika jina la Yesu. Kitu chochote, au roho yoyote, iliyo ndani ya nyumba yangu naivunja, nairudisha ilikotoka katika jina la Yesu. Amen!

2.   UNAMFUMBA MTU ASIKUTAMBUE.

Sheria ya pili ni kuwafumba watu ili wasiwatambue. Yani, uendelee kuamini kuwa vitu uvionavyo kwa macho au ndotoni ndivyo vilivyo. Akili ya mtu ikifungwa mtu akiona hatambui kama ni wachawi au mashetani. Yawezekana kila ukilala na kuota ndoto ukiamka unaanza kusema uliyoyaota ambayo yako katika  sura bandia. Inatakiwa uwafunge ili wasijifiche wakija uwatambuae katika jina la Yesu.  Bila kuomba huwezi kupokea uwezo wa kuwatambua. Imeandikwa ;

“Nanyi mkiomba lo lote kwa jina langu, hilo nitalifanya, ili Baba atukuzwe ndani ya Mwana. Mkiniomba neno lo lote kwa jina langu, nitalifanya”  Yohana 14:13-14
Maelfu wakimsifu  Mungu katika bonde la kukata maneno..

MAOMBI

 Katika jina la Yesu namteketeza mtu yeyote aliyejigeuza sura ili anitese, ninamfyeka katika jina la Yesu.

Kila atakayekuja katika umbo lolote lazima nimjue katika jina la Yesu,  ninawafunga wasinitambue kama mimi nimewaona. Kuanzia leo naamka kutoka kwenye usingizi wa kiroho, akili yangu iwaze kutawala, iwaze biashara katika jina la Yesu . Kuanzia leo naanza kutambua kazi yangu, naanza kuelewa kazi ya kufanya, biashara ya kufanya, katika jina la Yesu.

Nawashambulia mashetani wote katika jina la Yesu, mashetani walioshikilia familia yangu, kazi yangu, ndoa yangu, biashara yangu katika jina la Yesu. Ninawaangamiza katika jina la Yesu. Nawaangamiza maadui zangu wote katika jina la Yesu. Natumia mamlaka aliyonipa Yesu, ninawafyeka wanaozuia kazi yangu ninawafyeka wanaozuia ndoa yangu, ninawafyeka wanaozuia huduma yangu katika jina la Yesu. Nawashambulia kwa damu ya mwanakondoo. Imeandikwa;

“Kila silaha itakayofanyika juu yako haitafanikiwa na kila ulimi utakaoinuka juu yako katika hukumu utauhukumu kuwa mkosa. Huu ndio urithi wa watumishi wa Bwana, na haki yao inayotoka kwangu mimi, asema Bwana.”  Isaya 54:17

 Nawafyeka katika jina la Yesu, mtu yeyote aliyesimama kwenye njia zangu kunizuia nisifanikiwe, kuzuia nisisonge mbele, kunizuia nisipate ajira, nafunga uwezo wako wa kujigeuza na kuwa balaa,  mikosi, kuwa matatizo ,kuwa mtego, nawashambulia katika jina la Yesu.

Naharibu uwezo wenu katika jina la Yesu, nang’oa madhabahu zenu katika jina la Yesu. Nawatiisha, nakata mamlaka zenu, kila kiumbe kinachotumika kuharibu maisha yangu nakishambulia katila jina la Yesu. Naharibu uweza wenu wote katika jina la Yesu.

Natangua yote mliyoyapanga katika jina la Yesu. Imeandikwa;

“yeye uyatangua mashauri ya wadanganyifu na mikono yao isipate kutimiza makusudi yao.”

Kila vibarua wa shetani mnaovaa sura bandia nawaangamiza katika jina la Yesu, navunja kila laana ya familia iliyonipata kupitia viumbe wa rohoni mnaojibadilisha sura na kuniroga. Ninawafyeka katika jina la Yesu.

Kila nguvu ya giza inayotawala maisha ninailaani katika jina la Yesu, kila balaa zinazotawala maisha yangu nazivunja katika jina la Yesu. Nakiri leo niko huru, maisha yangu yako huru katika jina la Yesu. Amen!
Hakika Mungu ni mwema kwa watu wanaomtumainia yeye.

No comments:

Post a Comment