Monday, November 24, 2014

MADHABAHU ZA KICHAWI ZINAVYOLETA LAANA KWA WATU.


JUMAPILI YA TAREHE 23/11/2014

MCHUNGAJI KIONGOZI JOSEPHAT GWAJIMA

SOMO: MADHABAHU YA LAANA YA KICHAWI
Mchungaji kiongozi Josephat Gwajima

Neno mchawi limeandikwa mara nane kwenye Biblia tena kwa mkazo; neno wachawi limeandikwa mara ishirini, uchawi mara kumi na nne, uganga mara kumi na nane, waganga mara ishirini na moja na mapepo mara mia moja na arobaini na moja. Ni muhimu na lazima mambo haya yahubiriwe ili watu waweze kuyaelewa na waweze kuwa huru.

 “Tena mtu mume au mtu mke aliye na pepo, au aliye mchawi, hakika atauawa; watawapiga kwa mawe; damu yao itakuwa juu yao.” Walawi 20:27

 

Maana ya Laana

Laana ni zaidi ya kuwa mgonjwa. Ni pale ambapo maisha ya mtu yanakosa muelekeo; kila unalolianza hulimalizi, ikiwa asubuhi unatamani iwe mchana na mchana unatamani iwe usiku. Ukiwa huna watoto unawatamani ukiwapata unatamani usingekuwa nao. Hayo ndio maisha ya laana. Yaliyojaa misukosuko, kukosa amani na furaha kutoweka kabisa.

Laana inaweza kumpata mtu kutoka kwa mchawi au mshirikina ambaye anakuwa na wivu juu ya maisha yako. Ni vizuri ujue kuwa katika kila familia lazima kunakuwa na mtu mshirikina au mchawi. Na siku zote kamba za kufungwa na mtu anayekujua zinatenda kazi vizuri kuliko kamba za mtu asiyekujua.

Lakini laana pia yaweza kumpata mtu anapoacha kuisikiliza sauti ya Mungu. Biblia inaeleza kwa kirefu namna maisha ya mtu mwenye laana yalivyo.

“Lakini itakuwa usipotaka kuisikiza sauti ya Bwana, Mungu wako, usiyaangalie kufanya maagizo yake yote na amri zake, nikuagizazo hivi leo, ndipo zitakapokujia laana hizi zote na kukupata.  Utalaaniwa mjini, utalaaniwa na mashambani.  Litalaaniwa kapu lako na chombo chako cha kukandia.  Utalaaniwa uzao wa tumbo lako, na uzao wa nchi yako, maongeo ya ng'ombe wako, na wadogo wa kondoo zako.  Utalaaniwa uingiapo, utalaaniwa na utokapo,  Bwana atakuletea laana na mashaka, na kukemewa, katika yote utakayotia mkono wako kuyafanya, hata uangamie na kupotea kwa upesi; kwa ule uovu wa matendo yako, uliyoniacha kwayo.  Bwana atakuambatanisha na tauni, hata atakapokwisha kukuondoa katika nchi uingiayo kwa kuimiliki.  Bwana atakupiga kwa kifua kikuu, na kwa homa, na kwa kuwashwa, na kwa hari ya moto, na kwa upanga, na kwa ukaufu, na kwa koga; navyo vitakufukuza hata uangamie.  Na mbingu zako zilizo juu ya kichwa chako zitakuwa shaba, na nchi iliyo chini yako itakuwa chuma.  Bwana atafanya mvua ya nchi yako iwe vumbi na mchanga; itakujilia juu yako kutoka mbinguni hata uangamie.  Bwana atakufanya upigwe mbele ya adui zako; utawatokea juu yao kwa njia moja, lakini utakimbia mbele yao kwa njia saba; nawe utatupwa huko na huko katika falme zote za duniani.  Na mzoga wako utakuwa chakula cha ndege wote wa angani, na wanyama wote wa duniani, pasiwe na mtu wa kuwafukuza.  Bwana atakupiga kwa majipu ya Misri, na kwa bawasiri, na kwa pele, na kwa kujikuna, ambayo hupati kupoa.  Bwana atakupiga kwa wazimu, na kwa upofu, na kwa bumbuazi la moyoni;  utakwenda kwa kupapasa-papasa mchana, kama apapasavyo kipofu gizani, wala hufanikiwi katika njia zako; nawe sikuzote utaonewa na kutekwa nyara, wala hapatakuwa na mtu wa kukuokoa.  Utaposa mke na mume mwingine atalala naye; utajenga nyumba usiikae; utapanda mizabibu usitumie matunda yake.  Ng'ombe wako atachinjwa mbele ya macho yako, usile nyama yake; utanyang'anywa punda wako mbele ya uso wako kwa jeuri, usirudishiwe; kondoo zako watapewa adui zako, usipate mtu wa kukuokoa.  Wanao na binti zako litapewa taifa lingine, na macho yako yataangalia, na kuzimia kwa kuwatamani mchana kutwa; wala hapatakuwa na kitu katika uwezo wa mkono wako.  Matunda ya nchi yako, na taabu yako yote, vitaliwa na taifa usilolijua; utaonewa tu, na kupondwa chini daima;  hata uwe mwenye wazimu kwa yaonwayo na macho yako, utakayoyaona.  Bwana atakupiga magoti na miguu kwa jipu lililo zito, usilopata kupozwa, tokea wayo wa mguu mpaka utosi wa kichwa.  Bwana atakupeleka wewe, na mfalme wako utakayemweka juu yako, kwa taifa usilolijua wewe wala baba zako; nawe huko utatumikia miungu mingine ya miti na mawe.  Nawe utakuwa ushangao, na mithali, na dharau, kati ya mataifa yote huko atakakokuongoza Bwana.  Mbegu nyingi utazichukua nje shambani, lakini utavuna haba, kwa kuwa nzige watazila.  Utapanda mizabibu na kuitengeza, wala hutakunywa katika divai yake, wala kuichuma kwani italiwa na mabuu.  Utakuwa na mizeituni katika mipaka yako yote usijipake mafuta yake; kwa kuwa mzeituni wako utapukutika.  Utazaa wana na binti, lakini hawatakuwa wako wewe; kwa sababu watakwenda utumwani.  Miti yako yote, na mazao ya nchi yako, nzige watakuwa nayo.  Mgeni aliye kati yako atazidi kupaa juu yako; nawe utazidi kushuka chini.  Yeye atakukopesha, wala wewe usimkopeshe; yeye atakuwa ni kichwa, wewe utakuwa mkia.  Na laana hizi zote zitakujilia juu yako, zitakuandama na kukupata, hata uangamizwe, kwa kuwa hukuisikiza sauti ya Bwana, Mungu wako, kushika maagizo yake na amri zake alizokuagiza;  nazo zitakuwa juu yako kwa ishara na ajabu, na juu ya uzao wako milele;  kwa kuwa hukumtumikia Bwana, Mungu wako, kwa furaha na moyo wa kushukuru, kwa ajili ya ule wingi wa vitu vyote;  kwa hiyo utawatumikia adui zako atakaowaleta Bwana juu yako, kwa njaa, na kwa kiu, na kwa uchi, na kwa uhitaji wa vitu vyote; naye atakuvika kongwa la chuma shingoni mwako, hata atakapokwisha kukuangamiza.  Bwana atakuletea taifa juu yako kutoka mbali, kutoka ncha ya dunia, kama arukavyo tai; taifa usilolifahamu ulimi wake;  taifa lenye uso mkali, ambalo haliangalii uso wa mzee, wala halipendelei kijana;  naye atakula uzao wa ng'ombe wako wa mifugo, na uzao wa nchi yako mpaka utakapokwisha kuangamizwa; wala hatakuachia nafaka, wala divai, wala mafuta, wala maongeo ya ng'ombe wako, wala wana-kondoo wako, hata atakapokwisha kukuangamiza.  Naye atakuhusuru katika malango yako yote, hata kuta zako ndefu, zenye maboma, ulizokuwa ukiziamini, zishuke, katika nchi yako yote kila upande; naye atakuhusuru katika malango yako yote kila upande, katika nchi yako yote aliyokupa Bwana, Mungu wako.  Nawe utakula uzao wa tumbo lako mwenyewe, nyama ya wana wako na binti zako aliokupa Bwana, Mungu wako; katika mazingirwa na katika mkazo utakaokazwa na adui zako.  Mtu mume kati yenu aliye mwororo na laini sana, jicho lake litakuwa ovu juu ya nduguye, na juu ya mke wa kifuani mwake, na juu ya masalio ya wanawe waliosalia naye;  hata asitake wao mmojawapo apewe katika nyama ya wanawe atakaowala, kwa kuwa hana kitu kilichomsalia kwake; katika mazingirwa na mkazo utakaokazwa na adui yako katika malango yako yote.  Mwanamke kati yenu aliye mwororo na laini, ambaye hangehatirisha kuweka wayo wa mguu wake nchi kwa umalidadi na ulaini, jicho lake huyu litakuwa ovu juu ya mume wa kifuani mwake, na juu ya mwanawe, na juu ya binti yake,  na juu ya mchanga wake atokaye katikati ya miguu yake, na juu ya wanawe atakaowazaa; kwa kuwa atawala kwa siri, kwa uhitaji wa vitu vyote; katika mazingirwa na mkazo utakaokazwa na adui yako katika malango yako.  Kama hutaki kutunza kufanya maneno yote ya torati hii yaliyoandikwa katika kitabu hiki, upate kulicha jina hili la fahari na utisho, Bwana Mungu wako;
ndipo atakapofanya Bwana mapigo yako yawe ya ajabu, na mapigo ya uzao wako, mapigo makubwa kwa kweli, ya kudumu sana, na magonjwa mazito ya kudumu sana.  Naye atakurejezea maradhi yote ya Misri juu yako uliyokuwa ukiyaogopa, nayo yataambatana nawe.  Tena kila ugonjwa, na kila pigo yasiyoandikwa katika kitabu cha torati hii, atakutia nayo Bwana juu yako, hata utakapokwisha kuangamizwa.  Nanyi mtasalia wachache kwa hesabu, ninyi mliokuwa mfano wa nyota za mbinguni kwa wingi; kwa kuwa hukuisikiza sauti ya Bwana, Mungu wako.  Tena itakuwa, kama vile alivyokuwa akifurahi Bwana juu yenu kwa kuwatendea mema na kuwafanya kuwa wengi, ndivyo atakavyofurahi Bwana juu yenu kwa kuwapoteza na kuwaangamiza; nanyi mtanyakuliwa katika hiyo nchi mwingiayo kuimiliki.  Bwana atakutawanya katika mataifa yote, tokea ncha hii ya dunia hata ncha hii ya dunia; nawe huko utatumikia miungu mingine usiyoijua wewe wala baba zako, nayo ni miti na mawe.  Wala katika mataifa hayo hutapata raha iwayo yote, wala hutakuwa na kituo cha wayo wa mguu wako; lakini Bwana atakupa huko moyo wa kutetema, na macho ya kuzimia, na roho ya kudhoofika;  na uzima wako utakuwa na wasiwasi mbele yako; nawe utakuwa na woga usiku na mchana, wala hutaamini kamwe maisha yako;  asubuhi utasema, Laiti ingekuwa jioni! Na jioni utasema, Laiti ingekuwa asubuhi! Kwa kicho cha moyo wako utakavyokucha, na kuona kwa macho yako utakavyoona.” Kumbukumbu 28: 15-67

Unakuta unazaa watoto hata uwafundishe vipi hawaelewi, umekuwa mtu wa mashaka na kuonewa, kila ukianza biashara unakuwa unaishia na madeni na kufilisika. Chanzo ni laana hiyo, tauni inayoongelewa kwenye biblia ni magonjwa kama kifua, mgongo, homa zinakuwa haziishi, bumbuazi la moyoi unakuwa umeeduwaa tu; unaposa mchumba lakini mwingine anakuja kumwoa, unaanza mradi haufanikiwi, ngombe wako anachinjwa mbele ya macho yako maana yake unapigwa roba au kabari na kuibiwa huku unajiona,

Shida hizi zinaweza kuwa zinakupata na hujui kwa nini au nini chanzo chake. Chanzo cha yote haya chaweza kuwa ni laana ya wachawi.

Laana ya Kichawi

“Kisha wana wa Israeli wakasafiri na kupanga katika nchi tambarare za Moabu ng'ambo ya pili ya Yordani karibu ya Yeriko.  Na Balaki mwana wa Sipori akaona mambo yote ambayo Israeli wamewatendea Waamori.  Moabu akawaogopa hao watu sana, kwa kuwa walikuwa wengi; Moabu akafadhaika kwa sababu ya wana wa Israeli.  Moabu akawaambia wazee wa Midiani, Sasa jeshi hili la watu litaramba vitu vyote vinavyotuzunguka, kama vile ng'ombe arambavyo majani ya mashamba. Na Balaki, mwana wa Sipori, alikuwa mfalme wa Moabu zamani zile.  Basi akatuma wajumbe kwa Balaamu mwana wa Beori, hata Pethori, ulio kando ya Mto, mpaka nchi ya wana wa watu wake, kwenda kumwita, akisema, Tazama, kuna watu waliotoka Misri; tazama, wanaufunika uso wa nchi, tena wanakaa kunikabili mimi.  Basi, njoo wewe, nakusihi unilaanie watu hawa; maana wana nguvu kunishinda mimi. Labda nitawaweza, tupate kuwapiga, niwafukuze watoke katika nchi yangu, kwa maana najua ya kuwa yeye umbarikiye hubarikiwa, na yeye umlaaniye hulaaniwa.  Wazee wa Moabu, na wazee wa Midiani, wakaenda, wakichukua ujira wa uganga mikononi mwao; wakamfikilia Balaamu, wakamwambia maneno ya Balaki.  Akawaambia, Kaeni hapa usiku huu, nami nitawaletea jawabu kama Bwana atakavyoniambia; wakuu wa Moabu wakakaa na Balaamu.  Mungu akamjia Balaamu, akasema, Ni watu gani hawa ulio nao pamoja nawe?  Balaamu akamwambia Mungu, Balaki mwana wa Sipori, mfalme wa Moabu, amewatuma kwangu, akisema,  Tazama, kuna watu waliotoka Misri, wanaufunika uso wa nchi; basi njoo unilaanie watu hawa; labda nitaweza kupigana nao, na kuwafukuza.” Hesabu 22:1-11

Kumbe unaweza kuwa una nguvu ya kumshinda mtu lakini unapolaaniwa unakuwa hauna kitu tena. Unaweza kuwa una elimu lakini ukilaaniwa elimu yako haiwezi kukusaidia kuishi maisha mazuri. Wana wa Israeli walisafiri jangwani wakapata njaa Mungu akawapa mana kutoka mbinguni na mavazi yao hayakuchakaa kwa muda wa mika arobaini , wakapata kiu mwamba ukatoa maji jangwani, wakaugua naye yule nyoka wa moto akawatokea wakaponywa. Walipofika kwenye bahari ya Shamu, ikagawnyika wakavuka huku farasi na wapanda farasi wa majeshi  ya Farao akatupwa baharini. Balaki mwana wa Moabu alipoona wana wa Israeli wanaelekea kwenye nchi yao ya ahadi akamkodisha mchawi aje kuwalaani. Hata wewe leo wapo kina Balaki wa maisha yako ambao wameona umepita vikwazo na magumu mengi na sasa unakaribia kulifikia lile kusudi la Mungu katika maisha yako; wameazimia kuona unaharibikiwa hivyo wanakulaani kama wachawi au kama sio wanakodisha mchawi akulaani kwa niaba yao kama Balaki alivyomtumia Balamu kuwalaani wana wa Israeli..

Kwenye ulimwengu wa rohoni kuna viashiria vinavyoonyesha mtu atakuwaje siku zijazo na watu ambao hawakupendi wanapoona unaelekea kwenye mafanikio wanamkodisha mtu mchawi ili akulaani. Lakini sisi tuliookolewa kwa damu ya mwanakondoo Yesu Kristo tuna nguvu ya kuwashinda wao maana wao wanategemea hirizi, na kafara zao lakini sisi tunamtegemea Bwana wa majeshi.

Laana inapotumwa huruka na kwenda kuingia sehemu husika na inajua ingie kwa nani na isingie kwa nani.

“Balaamu akamwambia Balaki, Nijengee hapa madhabahu saba, ukaniandalie hapa ng'ombe waume saba, na kondoo waume saba.  Balaki akafanya kama Balaamu alivyonena. Balaki na Balaamu wakatoa sadaka, ng'ombe mume mmoja na kondoo mume mmoja juu ya kila madhabahu.  Balaamu akamwambia Balaki, Simama karibu na sadaka yako, nami nitakwenda, labda Bwana atakuja kuonana nami; na lo lote atakalonionyesha nitakuambia. Akaenda hata mahali peupe juu ya kilima.  Mungu akakutana na Balaamu; naye Balaamu akamwambia, Nimetengeneza madhabahu saba, nami nimetoa sadaka ng'ombe mume mmoja na kondoo mume mmoja juu ya kila madhabahu.  Bwana akatia neno katika kinywa chake Balaamu, akasema, Umrudie Balaki; ukaseme maneno haya.  Akarudi kwake, na tazama, amesimama karibu na sadaka yake ya kuteketezwa, yeye na wakuu wote wa Moabu pamoja naye.  Akatunga mithali yake, akasema, Balaki amenileta kutoka Aramu, Mfalme wa Moabu kutoka milima ya mashariki, Njoo! Unilaanie Yakobo, Njoo! Unishutumie Israeli.  Nimlaanije, yeye ambaye Mungu hakumlaani? Nimshutumuje, yeye ambaye Bwana hakumshutumu?” Hesabu 23: 1- 8

Mchawi Balaam alitataka madhabahu saba ili awalaani wana wa Israeli siku saba za wiki. Laana ya mchawi haina jumapili wala jumatatu bali ni siku zote. Pia tumeona amewatoa kondoo na ngombe kama kafara juu ya kila madhabahu. Katika wanyama watolewao kafara juu ya madhabahu ng’ombe ndiye mkubwa kuliko wote na kondoo mdogo kuliko wote. Hii inamaanisha kuwa kwenye mambo makubwa wanakulaani na kwenye mambo madogo pia.  

Kwa hiyo yule mtu ambaye hakupendi anamwendea mchawi halafu wanaandaa madhabahu na kuchinja mnyama ili damu ambayo ni uhai imwagike kwenye madhabahu. Mashetani huja kwenye ile madhabahu na kunywa ile damu inayomwagika na baadaye huelekezwa kwako  ili waje kukuwekea hiyo laana.

lakini, kama ilivyoandikwa, Mambo ambayo jicho halikuyaona wala sikio halikuyasikia, (Wala hayakuingia katika moyo wa mwanadamu,) Mambo ambayo Mungu aliwaandalia wampendao. Lakini Mungu ametufunulia sisi kwa Roho. Maana Roho huchunguza yote, hata mafumbo ya Mungu.  Maana ni nani katika binadamu ayajuaye mambo ya binadamu ila roho ya binadamu iliyo ndani yake? Vivyo hivyo na mambo ya Mungu hakuna ayafahamuye ila Roho wa Mungu.” 1 Wakorintho 2:9-11

Yapo mambo makubwa ambayo Mungu ameandaa kwa ajili ya maisha yako. Pale ulipo leo si kitu kabisa ipo sehemu njema unayoelekea kesho. Mahali ambapo hutatikisika tena na utasahau taabu yako. Wewe ambaye ni mbilikimo leo kesho utakuwa baunsa. Mungu tunaye mtumikia ni Mungu anayejua tutokako na tuendako. Ukikubali kumsikiliza Mungu hakika atasema na Balaam wa maisha yako kama alivyosema kipindi kile cha wana wa Israeli; kwamba “huweezi kumlaani aliyebarikiwa.”  Kama Mungu ndiye aliyekubariki sio mchawi wala mshirikina atakayeweza kukulaani. Lakini uwe na baraka kutoka kwa Mungu ambayo hupatikana kwa kuisikiliza sauti yake. Utakapolaaniwa na Mungu pia, hakuna atakayekubariki ukabarikiwa.

 

Balaam Alikuwa ni Mchawi si Nabii wa Bwana.

Kwa nini mchawi huyu Balaam anasikia sauti ya Bwana kama sio nabii wa Bwana? Ni kwa sababu mtu anapoingia kwenye ulimwengu wa rohoni anakuwa anawaona wote Mungu na malaika zake pamoja na shetani na mapepo yake. Hivyo Mungu aliingilia mawasiliano ya Balaam na shetani na kumpa maelekezo yake kwa kuwa alikuwa anawalinda wana wa Israeli. Balaam yeye atakuwa alidhani kuwa Mungu ni ngazi fulani ya juu katika utawala wa shetani ambao yeye hajafikia.

Baadaye huyu mchawi Balaam alikuja kufia mikononi mwa wana wa Israeli.

Balaamu naye, huyo mwana wa Beori, huyo mchawi, wana wa Israeli walimwua kwa upanga kati ya hao wengine waliowaua.” Yoshua 13:22

 

Madhabahu za Laana za Kichawi.

Wachawi hawawezi kuloga bila madhabahu. Ili waweze kuyatuma mashetani yafanyike laana kwenye maisha yako ni lazima madhabahu ijenge kwanza. Kisha lazima kafara itolewe juu ya madhabahu hiyo ili ule uhai ambao umo katika damu uyahuishe yale mashetani ambayo hufanyika laana. Pasipo hiyo madhabahu laana haiwezi kufanyika kwako. Hivyo ni muhimu kuzishughulikia madhabahu zilizoinuliwa ili wewe ulaanike. Zinapobomoka zile, wewe unarudi kwenye kusudi la Mungu juu ya maisha yako.

 

UKIRI:

Ninazivunja laana za wachawi na waganga wa kienyeji kwa damu  ya mwaanakondoo. Madhabahu saba zenye kafara saba zilizo juu yangu ninazivunja kwa damu ya Yesu. Kuanzia leo kila madhabahu ya kuzimu  ya Lucifer, nabii wa uongo ninaifyeka kwa damu ya Yesu, maaskari wa kishetani ninawafyeka na madhabahu zao kwa jina la Yesu Kristo. Ninasimama kinyume na kuzimu, ninateketeza nia ya kuzimu kwa jina la Yesu. Imeandikwa; “laana isiyo na sababu haimpati mtu”  Ninaibomoa madhabahu ya kila laana iliyo juu ya maisha yangu kwa jina la Yesu.

Kwa jina la Yesu ninabomoa madhabahu za laana za kichawi. Madhabahu za kushindwa, madhabahu za kuzimu zilizojengwa juu yangu, madhabahu za laana ya ukoo wangu; ninazivunja kwa jina la Yesu! Ninavaa silaha za vita, ninawafyeka wasimamizi wote wa laana za kichawi kwa jina la Yesu, ninawateketeza kwa damu ya mwanakondoo. Ewe laana uliy kwenye maisha yangu ninakufuta kwa jina la Yesu, ninateketeza laana za kishetani zilizotumwa kwangu na familia yangu kwa damu ya Yesu. Ninazivunja laana zote za kishetani zilizotumwa kwangu kwa jina la Yesu.

Ewe laana ya nchi uliyoishikilia nchi yangu ninakuamuru achia nchi yangu kwa jina la Yesu. Madhabahu za laana ya kushindwa, laana ya kukataliwa, laana ya kukosa mke/mume;  ninaibomoa kwa jina la Yesu. Ninazibomoa madhabahu zote za kichawi kwa jina la Yesu. Madhabahu za laana juu ya familia yangu ninazivunja kwa damu ya mwanakondoo. Kwa jina la Yesu ninavunja laana juu ya ndoa yangu kwa, ninavunja laana juu ya masomo yangu, ninazivunja madhabahu za kishetani zilizoshikilia laana juu ya biashara yangu kwa jina la Yesu. Kwa damu ya mwanakondoo, maneno ya laana yaliyotamka na wanadamu juu yangu na familia yangu ninayavunja kwa jina la Yesu. Imeandikwa; “ni nani asemaye neno ikiwa Bwana hakuliagiza likatendeka?” Hii laana haijaagizwa na Bwana, ninaibatilisha kwa damu ya mwanakondoo.

Ninawateketeza majini na mashetani wote mlioshikilia laana juu ya nchi na familia yangu kwa jina la Yesu. Ninavunja laana za majeshi ya pepo wabaya kwenye maisha yangu kwa jina la Yesu. Ninavunja madhabahu za wachawi zilizomwagiwa damu ya kafara inenayo laana juu ya maisha yangu; ninazivunja kwa damu ya mwanakondoo, katika jina la Yesu Kristo. AMEN!

 

 

 

 

 

 

No comments:

Post a Comment