Monday, December 1, 2014

MIKONO YA KICHAWI


JUMAPILI YA TAREHE 30/11/2014

MCHUNGAJI KIONGOZI JOSEPHAT GWAJIMA

SOMO: MIKONO YA KICHAWI/KISHETANI
Mchungaji kiongozi Josephat Gwajima.

Biblia inasema;

Mungu ni Roho, nao wamwabuduo yeye imewapasa kumwabudu katika roho na kweli.” Yohana 4:24

Lakini pamoja na kuwa Mungu ni roho, Mungu anayo mikono na vidole pia.

“Na mche ule ulioupanda Kwa mkono wako wa kuume; Na tawi lile ulilolifanya Kuwa imara kwa nafsi yako.” Zaburi 80:15

“Miongoni mwao waliokufa nimetupwa, Kama waliouawa walalao makaburini. Hao ambao Wewe huwakumbuki tena, Wametengwa mbali na mkono wako.” Zaburi 88:5

“Lakini, ikiwa mimi natoa pepo kwa kidole cha Mungu, basi ufalme wa Mungu umekwisha kuwajilia.” Luka11:20

Mkono wa Bwana hutumika kuokoa, kubariki na kuponya wanadamu.

“Bwana atawapa watu wake nguvu; Bwana atawabariki watu wake kwa amani.” Zaburi 29:11

Yesu alipokuwa akiwaambia wanafunzi wake anatoa pepo kwa kutumia kidole cha Mungu  alikuwa anamaanisha anatoa pepo kwa uwezo wa Roho mtakatifu. Roho Mtakatifu  ndiye kidole cha Mungu. Leo hii Mungu hutenda kazi kupitia mikono ya mawakala wake duniani ambao ni wachungaji na watumishi wengine wa Mungu aliye hai. Ndio maana watu wengi wanapomwabudu Mungu huimba wakisema, “Mungu niguse, niguse Bwana.” Watu hawa huguswa na Mungu kupitia watumishi wa Mungu waliojaa nguvu za Roho Mtakatifu.

Kama ambavyo Mungu ana mikono na vidole; shetani naye ana mkono wake na kidole chake.

“Kisha Bwana akamwuliza Shetani, Je! Umemwangalia huyo mtumishi wangu Ayubu? Kwa kuwa hapana mmoja aliye kama yeye duniani, mtu mkamilifu na mwelekevu, mwenye kumcha Mungu na kuepukana na uovu. Ndipo Shetani akamjibu Bwana, na kusema, Je! Huyo Ayubu yuamcha Bwana bure? Wewe hukumzingira kwa ukigo pande zote, pamoja na nyumba yake, na vitu vyote alivyo navyo? Kazi za mikono yake umezibarikia, nayo mali yake imeongezeka katika nchi. Lakini nyosha mkono wako sasa, uyaguse hayo yote aliyo nayo, naye atakukufuru mbele za uso wako. Bwana akamwambia Shetani, Tazama, yote aliyo nayo yamo katika uwezo wako; lakini usinyoshe mkono wako juu yake yeye mwenyewe. Basi Shetani akatoka mbele za uso wa Bwana. Ilitukia siku moja hao wanawe na binti zake walipokuwa wakila na kunywa divai katika nyumba ya ndugu yao mkubwa,  mjumbe akamfikilia Ayubu na kumwambia, Hao ng'ombe walikuwa wakilima, na punda walikuwa wakilisha karibu nao;  mara Waseba wakawashambulia, wakawachukua wakaenda nao; naam, wamewaua hao watumishi kwa makali ya upanga, mimi peke yangu nimepona, mimi tu, kukuletea habari.  Huyo alipokuwa akali akinena, akatokea na mwingine, na kusema, Moto wa Mungu umeanguka kutoka mbinguni na kuwateketeza kondoo, na wale watumishi, na kuwaangamiza; mimi peke yangu nimepona, mimi tu, kukuletea habari.  Huyo alipokuwa akali akinena, akatokea na mwingine, na kusema, Wakaldayo walifanya vikosi vitatu, wakawaangukia ngamia, wakaenda nao, naam, wamewaua wale watumishi kwa makali ya upanga; mimi peke yangu nimepona, mimi tu, kukuletea habari.  Huyo alipokuwa akali akinena, akatokea na mwingine, na kusema, Wanao na binti zako walikuwa wakila na kunywa divai katika nyumba ya ndugu yao mkubwa;  mara, tazama, upepo wenye nguvu ukatoka pande za jangwani, ukaipiga hiyo nyumba pembe zake nne, nayo ikawaangukia hao vijana, nao wamekufa; na mimi peke yangu nimepona, mimi tu, kukuletea habari. Ndipo Ayubu akainuka, akalirarua joho lake, kisha akanyoa kichwa chake, na kuanguka chini, na kusujudia;  akasema, Mimi nilitoka tumboni mwa mama yangu nili uchi, nami nitarudi tena huko uchi vilevile; Bwana alitoa, na Bwana ametwaa; jina la Bwana na libarikiwe.”  Ayubu 1:8-21

Tunajifunza hapa kuwa mtu anayependwa na Mungu ni yule mtu mkamilifu, mwelekevu, mweye kumcha Mungu na mwenye kuepuka uovu. Mungu hujivunia mtu wa namna hii.

Shetani anamwambia Mungu kwamba Ayubu anamcha kwasababu amembariki na kumwekea ulinzi. Mungu akampa ruhusa shetani anyooshe mkono wake juu ya vyote alivyo navyo Ayubu lakini asiuguse uhai wake. Shetani pia kama ambavyo Mungu alivyo na mawakala duniani; yeye pia anao. Hawa ndio wachawi na waganga. Hivyo shetani anapotaka kukugusa atakugusa kupitia wao.

Kuna watu ambao wana matatizo kwasababu wameguswa na mkono wa kichawi bila wao kujua. Kama ambavyo Ayubu alianza kupatwa na matukio baada ya shetani kupata kibali cha kumgusa ndivyo inavyokuwa kwa mtu anayeguswa na mikono ya kichawi leo. Shetani aliponyoosha mkono wake tu, wakatokea waseba (wezi) wakaiba mifugo na kuondoka nao. Ayubu hakuwa peke yake mwenye mifugo lakini wengine hawakuibiwa ila yeye. Kwa nini? Mkono wa shetani umemgusa. Baada ya kuguswa kila eneo la maisha yake Ayubu alianza kuchanganyikiwa. Kumbe unapoguswa na mkono wa shetani unaanza kuchanganyikiwa pia. Ayubu akaishia kumshukuru Mungu akisema Bwana alitoa Bwana ametwaa jina lake libarikiwe. Lakini mimi ni wewe ni mashahidi leo kuwa ni kweli Bwana alitoa kwa Ayubu lakini si kweli alitwaa tena alivyotoa. Aliyevitwaa alikuwa shetani. Kumbe yawezekana kabisa kuwa ulipewa vitu na Bwana lakini mkono wa kichawi ukavigusa na kuvitwaa.

Lakini lihimidiwe jina la Bwana kwa kuwa ipo mikono ya watumishi wa Mungu wa kweli itumikayo kugusa na kurudisha vyote ambavyo waseba walikuwa wameiba.Imeandikwa

 

“watashika nyoka; hata wakinywa kitu cha kufisha, hakitawadhuru kabisa; wataweka mikono yao juu ya wagonjwa, nao watapata afya.” Marko 16:18

 

Sisi tunaomtumikia Mungu tumepewa mamlaka ya kuweka miono yetu juu ya wagonjwa, walioibiwa, walioteswa na kuwarudishia afya zao na vyote walivyoibiwa na yule aliyekuja kuiba na kuharibu yaani shetani.

Inawezekana leo unapitia balaa na mikosi mbalimbali kwenye maisha yako ambayo chanzo chake ni kushikwa na mikono ya kichawi. Yamkini hawakuweza kukushika wewe lakini walishika nguo yako au kiatu chako au kitu chako chochote; na kwa kadri ambavyo unaendelea kukaa na kile kitu nyumbani kwako kinakuwa kiunganishi kati yako na ile laana au mkosi. Ni lazima ukate kile kinachokuungamanisha na yale matatizo yatokanayo na ile mikono ya kichawi..

Kila unapoamka, unapoomba unatakiwa uombe damu ya Yesu itakase mikono yako, uso wako na mwili wako kwa ujumla. Haupaswi  kuwaogopa na kuwakwepa, unatakiwa upambane nao kwa jina la Yesu. Kila aliyegusa nguo yako kwenye ulimwengu wa roho leo mrudishie vyote alivyokuwekea kwa jina la Yesu. Ruhusa uguswe na mkono wa Mungu kabla mikono ya kichawi haijakugusa, ukiguswa na Mungu ile nguvu inaingia mpaka kwenye mifupa  ndani ya mwili wako. Hapo nguvu ya mikono ya kichawi haitoweza kufanikiwa tena juu yako.

 

 

Maombi

Mikono ya wachawi waliowahi kugusa mikono yangu, nguo zangu, chakula change, mali zangu zote; kuanzia sasa kwenye ulimwengu wa roho ninafuta alama zao kwa jina la Yesu.

Mikono ya kichawi iliyogusa vitu vyangu, mwili wangu au kitu chochote ninavifuta kwa jina la Yesu. Alama za kichawi zilizoachwa ndani ya nguo zangu ninazifuta kwa damu ya Yesu. Mikono ya kichawi iliyogusa ndoa yangu, familia yangu, kazi yangu ninaiamuru kwa jina la Yesu ivunjike. Ninanyoosha mkono wa Mungu kuivunja na kuiteketeza mikono ya kishetani iliyonyooka juu ya maisha yangu; ninaivunja kwa jina la Yesu Kristo. Imeandikwa

 “nao wakamshinda kwa damu ya mwana kondoo” Ufunuo12:11

Kila mchawi aliyenyoosha mkono wake juu ya mwili wangu, nguo zangu, kichwa changu, kanisa langu, nchi yangu, ndoa yangu, ninaipoozesha kwa damu ya mwana kondoo.

Kila mkono wa kishetani ulionyooka ili kuleta maangamizo juu yangu, ninaupoozesha na kuuvunja kwa jina la Yesu Kristo. Ninatuma polio kwenye mikono yote ya kichawi iliyojipanga kugusa watoto wangu, biashara yangu, elimu yangu. Ninaipoozesha kwa damu ya Yesu Kristo, ninaivunja kwa jina la Yesu Kristo. Kila kazi iliyoanzishwa na mikono ya kishetani ninaibatilisha kwa jina la Yesu Kristo. Ninaamuru kwa mamlaka ya jina la Yesu, kila mkono wa kichawi ulionyooka kunigusa mimi na familia yangu upooze kwa damu ya Yesu Kristo. Ninaifyeka kwa jina la Yesu Kristo.

Mikono inayoleta utasa ninaivunja kwa jina la Yesu. Ewe mkono ulionyooka kuleta utasa kazini kwangu, utasa kwenye elimu ninakuvunja kwa jina la Yesu Kristo. Kila mkono wa kichawi uliotumwa kunigusa mimi na vyote nilivyonavyo leo ninakuvunja kwa jina la Yesu Kristo. Ewe shetani uliyenyoosha mkono wako kuniletea uoga wakati wa usiku na hofu wakati wa mchana leo ninakuvunja kwa jina la Yesu Kristo. Kila mkono ulionyooka juu ya watoto wangu, wazazi wangu, rafiki zangu, na ndugu zangu wote leo ninaondoa uweza wako wa kudhuru na kukuvika polio upooze, ninakufyeka kwa jina la Yesu Kristo. Ninaukata mkono ulionyooshwa ili nisiolewe kwa jina la Yesu. Ninaukata mkono ulionyooshwa ukagusa nguo zangu, mali yangu au chochote nilicho nacho kwa jina la Yesu; ninaukata mkono ulionyooshwa kugusa ajira yangu kwa jina la Yesu. Ninaukata mkono wa wachawi ulionyooshwa kugusa mapato yangu kwa jina ya Yesu. Mchawi mwanaume, mtoto, mwanamke, mzee ninaukata mkono wako uliounyoosha kunigusa mimi na mali zangu  kwa jina la Yesu Kristo. Amina!

 

 

 

 

 

 

No comments:

Post a Comment