google.com, pub-4324601895065941, DIRECT, f08c47fec0942fa0

Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

BWANA AMEKUCHAGUA

UFUFUO NA UZIMA CATHEDRAL
IBADA YA JUMAPILI 07.07.2024
ASKOFU DR JOSEPHAT GWAJIMA
SOMO: BWANA AMEKUCHAGUA

Kila mtu ameumbwa kipekee na Mungu, Mungu anapokuleta duniani wa aina yako unakuwa peke yako.

Kuna wanne wanaokujua wewe:

  • Watu wanavyokujua wewe
  • Mungu anavyokujua wewe
  • Wewe unavyojijua wewe
  • Shetani anavyokujua wewe

Mashujaa huwa hawachaguliwi huwa wanaandaliwa na Mungu.

“Kwa maana wewe u taifa takatifu kwa BWANA, Mungu wako; BWANA Mungu wako, amekuchagua kuwa watu wake hasa, zaidi ya mataifa yote walioko juu ya uso wa nchi.” Torati 7:6

Sote tunafanana ila nataka ujue kuna watu wamechaguliwa kwa ajili ya jambo fulani.

Ukisikia kitu kimechaguliwa na Mungu achana nacho. 

“Lakini wewe hutanijengea nyumba hiyo; ila mwanao atakayetoka katika viuno vyako, yeye ndiye atakayeijenga nyumba kwa jina langu.” 1 wafalme 8:19

Mungu anakuwa na jambo lake, lakini hana mikono, miguu, kinywa, anamchagua mtu ili jambo lake liweze kutimia, na Mungu akikuchagua anakupeleka kila mahali unapofika pana maana yake, hatua zako zinaongozwa na yeye, kila unachofanya kinaongozwa na yeye ukikosea kidogo ukaenda mbali anakurudisha pale pale.

Mungu huwachagua wale usiowategemea, na kuna wakati mtu amechaguliwa na Mungu hajijui kuwa yeye amechaguliwa, ila anakuwa anajiuliza mbona naona nampenda Mungu tu, kuna mambo ambayo aliyechaguliwa anaweza kuyafanya  hata kama usipompa pesa, kuna baadhi ya mambo ukiyafanya unataka kupewa pesa, lakini kuna baadhi ya mambo hata kama hujapewa pesa unafurahi, unaweza ukachaguliwa ukae Dar es salaam lakini sasa wewe uko liwale, Mungu akikuchagua hata kama unakaa nyuma ya jangwa atakuleta mjini.

Unaweza kuwa umechaguliwa na bado ukawa unaishi nyuma ya jangwa, maana yake unakaa pakavu kila jambo haliendi, unaweza ukawa uko peke yako kwenye familia huna msaada lakini Bwana amekuchagua, hakuna anaekuelewa kwenye ukoo wenu, wenzako wameolewa wewe unafanya nini wenzako wana kazi wewe unafanya nini, kwenye familia unaonekana wa ajabu ajabu, waambie Samweli hajafika, akifika kila kitu kitakuwa sawa.

Umechaguliwwa kabla ya kuwekwa misingi ya ulimwengu, mazingira yanakufanya kusukumwa mpaka nyuma ya jangwa lakini Mungu anakutengeneza uwe yule uliyeandaliwa kuwa, Mungu akikuchagua hazuiwi na watu, haijalishi wamekupeleka wapi, anaweza kukuita kutoka pande za mwisho za nchi kwa ajili ya kutimiza kusudi lake, mambo uliyoyapitia wala usihuzunike Mungu anakwenda kukuinua, kila mtu ana kusudi ambalo amechaguliwa kutimiza.

Kama Mungu  amekuchagua kwa kusudi fulani shetani akakubeba akupeleke mahali fulani ili kusudi Samweli akija asikukute, lakini lile kusudi lina maelekezo linakufaa wewe, na unapochaguliwa unahama kuwa mwanadamu anayefanya kazi ya mwanadamu unakuwa kiumbe cha ki-Mbinguni ambacho kinatimiza kusudi hilo la Mungu kukuleta duniani, Mungu ndiye aliyekuumba wewe anajua kazi yako, na makusudi yanatofautiana kuna watu wao ni kulia anaomboleza, tukiangalia kwenye biblia unakutana na Yeremia analia (anaomboleza).

Kuna wengine kama Eliya hawalii, wenyewe ni kujibu, Mungu akikuchagua anakupa na neema, neema ni uwezesho wa ki-Mungu wa kukuwezesha kufanya jambo ambalo uwezo wako na elimu yako ya kibinadamu haiwezi kufanya.

Kuna manabii kama Isaya, Isaya ni Nabii wa usahihi, anaona mambo ya mbele kabla hayajatokea, kila mtu anachaguliwa na Mungu kwa wakati wake, kwa aina yake na kusudi lake, mtu akichaguliwa na Mungu biashara imeisha. 

Mtu aliyepakwa mafuta kwa ajili ya kusudi husika ukishindana nae utaangukia pua, yale Maisha ya nyuma ya jangwa yana uhusiano sana na namna utakavyopenya kuingia kwenye kusudi lako. yatakufanya upate kibali mahali fulani na kusudi lako liweze kutimia.

Kwa nini Mungu ana tabia ya kuchagua yule na sio huyu, Mungu akikuchagua kwa ajili ya jambo anapanda kiu ndani yako, ukiona ukiingia baadhi ya sehemu mpaka upite dirishani ujue sio penyewe, ukiona unatumia nguvu kubwa lakini matokeo ni kidogo ujue sio sehemu yako.

“Wala si hivyo tu, lakini Rebeka naye, akiisha kuchukua mimba kwa mume mmoja, naye ni Isaka, baba yetu, (kwa maana kabla hawajazaliwa wale watoto, wala hawajatenda neno jema wala baya, ili lisimame kusudi la Mungu la kuchagua, si kwa sababu ya matendo, bali kwa sababu ya nia yake aitaye), aliambiwa hivi, Mkubwa atamtumikia mdogo. Kama ilivyoandikwa, Nimempenda Yakobo, bali Esau nimemchukia. Tuseme nini basi? Kuna udhalimu kwa Mungu? Hasha!  Maana amwambia Musa, Nitamrehemu yeye nimrehemuye, nitamhurumia yeye nimhurumiaye. Basi, kama ni hivyo, si katika uwezo wa yule atakaye, wala wa yule apigaye mbio; bali wa yule arehemuye, yaani, Mungu.”  Warumi 9:10-14

Duniani unapeleka sifa zako ndo unachaguliwa, kwa watu waliookoka unapewa sifa na unachaguliwa

Kila anayekusaliti anakutengeneza kuwa shujaa wa baadae, kusalitiwa kunakutengeneza kujua ulio nao ni kina nani, Mungu anaweza kukuletea matukio yenye kukuletea maumivu lakini mwisho wake unakuwa imara, Mungu akiamua kukuchagua wewe kwa ajili ya jambo hata kama watashindana na wewe kuanzia asubuhi mpaka jioni watavunjika migongo, ukiona mtu amechaguliwa kwa ajili ya jambo achana nae, ukipambana nae utaliwahisha lile jambo.

Utajuaje umechaguliwa juu ya jambo fulani?

Roho yako inakuwa inapepea akili yako inaweza kukataa, kuchaguliwa na Mungu ni Nungu anakuwa na ajenda yake duniani kwa kuwa hana sehemu ya kupitia duniani kwa hiyo anakuchagua wewe anaingia ndani yako ili kutimiza kusudi lake.

“Mna hila nyingi moyoni mwa mtu; Lakini shauri la BWANA ndilo litakalosimama.” Mithali 19:21

Alilolipanaga Bwana iwe wanakuletea ujanja ujanja, iwe ni wizi, kwa namna yoyote  ile lazima litasimama, kila mtu ana kusudi la Mungu ukiona mtu hana kusudi ujue kashafariki, Mungu amekuchagua  na katik lile jambo alilokuchagua haufi mpaka lile jambo limetima.

Post a Comment

1 Comments