UFUFUO NA UZIMA UBUNGO CATHEDRAL
IBADA YA JUMAPILI 2 APRILI 2023
ASKOFU BARAKA THOMAS TEGGE
SOMO: VITA YA KUMILIKI YALE ULIYOPEWA NA MUNGU.
Usipofahamu
namna ya kumiliki yale ambayo Mungu amekupa kamwe hutawezi kuyapata. Mungu
alishakupa mambo yote yakukufikisha kwenye hatima yako na Mungu huwa hadanganyi.
Mungu anapokuahidi jambo kuna kuwa na agano kati yake na aliyemuahidi na kila
upande kwenye agano kuna sehemu lazima itimize. Mungu anakupa kila kitu lakini
kuna sehemu lazima uifanye wewe la sivyo hutaweza kupata yale uliyopewa. Mungu
alivyokuwa anawaongoza wana wa Israeli kuna mataifa mengine alikuwa anawaambia
waacheni kwa kuwa hajawapa, ila kuna nchi na mataifa ambayo Mungu aliwapa.
“Ikawa
baada ya kufa kwake Musa, mtumishi wa BWANA, BWANA akamwambia Yoshua, mwana wa
Nuni, mtumishi wa Musa, akasema, Musa mtumishi wangu amekufa; haya basi,
ondoka, vuka mto huu wa Yordani; wewe na watu hawa wote, mkaende hata nchi
niwapayo wana wa Israeli. Kila mahali zitakapopakanyaga nyayo za miguu yenu, nimewapa
ninyi, kama nilivyomwapia Musa. Tangu jangwa hili na mlima huu, Lebanoni, mpaka
mto ule mkubwa, mto wa Frati, nchi yote ya Wahiti, tena mpaka bahari ile kubwa
upande wa machweo ya jua, hapo ndipo patakapokuwa mpaka wenu. Hapatakuwa mtu ye
yote atakayeweza kusimama mbele yako siku zote za maisha yako; kama nilivyokuwa
pamoja na Musa, ndivyo nitakavyokuwa pamoja na wewe; sitakupungukia wala
sitakuacha.” Yoshua 1:1-5.
Lazima
kuwe na mtu wa kukurithisha yale ambayo Mungu amekupa, Yoshua alikuwa na kazi ya
kuwarithisha wana wa Israeli nchi ya ahadi, ambayo Mungu aliyowaapia Baba zao. Wana
wa Israeli walikuwa ni kana kwamba wanahama hama ila kuna nchi waliyokuwa
wanaiendea ambayo Mungu aliwapa. Vivyo hivyo pia kuna mtu anaweza kuonekana kana
kwamba hana kitu, ana madeni, tabu n.k ila anakuwa njiani kuelekea pale ambapo
Mungu kamuandalia.
Pamoja
na ahadi waliyopewa na Mungu ya kumiliki nchi ya ahadi, wana wa Israeli
waliacha sehemu kubwa sana ambayo hawakuwa wameimiliki. Ahadi ya Mungu ni kweli
na hakika lakini kama usipopigana Mungu hana la kukusaidia.
“Basi
Yoshua alipokuwa mzee, na kwendelea sana miaka yake, BWANA akamwambia, Wewe
umekuwa mzee na kwendelea sana miaka yako, kisha inasalia nchi nyingi sana bado
kumilikiwa.” Yoshua 13:1.
Kuna
nchi kubwa sana ilisalia bila kumilikiwa na wana wa Israeli, baadhi ya makabila
wakawa wanakaa kwenye nchi za wenzao. Ulegevu ulipelekea haya yote kutokea.
“Kisha
mkutano mzima wa wana wa Israeli walikutana pamoja hapo Shilo, wakasimamisha
hema ya kukutania kuko; nayo nchi ilikuwa imeshindwa mbele zao. Zilisalia
katika wana wa Israeli kabila saba ambazo hazijagawanyiwa bado urithi wao.
Yoshua akawauliza wana wa Israeli, akasema, Je! Hata lini mtakuwa walegevu
katika kuingia kwenu na kuimiliki hiyo nchi, ambayo yeye BWANA, Mungu wa baba
zenu, amewapa?” Yoshua 18:1-3.
Ilibidi
wawaendee waliokuwa wamekaa kwenye nchi ya ahadi na kupigana nao ili wamiliki
nchi ambayo Bwana aliwapatia. Yoshua hakwenda kuwapigania, walienda wenyewe
kupigana. Wale unaodhani watakuja kukupigana, huo ulegevu utakufanya ushindwe
kuimiliki.
“Wakasema,
Haya, inukeni, twende tukapigane nao; kwa maana tumeiona hiyo nchi nayo ni nchi
nzuri sana; nanyi, je! Mwanyamaa tu? Msiwe wavivu kwenda, na kuingia, ili mpate
kuimiliki nchi hiyo.” Waamuzi 18:9.
Ili
umiliki kwenye agano jipya hakuna utofauti sana na agano la kale, ni lazima
upigane na majeshi ya shetani kwenye ulimwengu wa roho. Sheria ya kumiliki
alichokupa/ kuahidi Mungu ni lazima upigane kila wakati pasipo kuchoka.
“Hatimaye,
mzidi kuwa hodari katika Bwana na katika uweza wa nguvu zake. Vaeni silaha zote
za Mungu, mpate kuweza kuzipinga hila za Shetani. Kwa maana kushindana kwetu
sisi si juu ya damu na nyama; bali ni juu ya falme na mamlaka, juu ya wakuu wa
giza hili, juu ya majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho. Kwa sababu
hiyo twaeni silaha zote za Mungu, mpate kuweza kushindana siku ya uovu, na
mkiisha kuyatimiza yote, kusimama. Basi simameni, hali mmejifunga kweli
viunoni, na kuvaa dirii ya haki kifuani, na kufungiwa miguu utayari tupatao kwa
Injili ya amani; zaidi ya yote mkiitwaa ngao ya imani, ambayo kwa hiyo mtaweza
kuizima mishale yote yenye moto ya yule mwovu. Tena ipokeeni chapeo ya wokovu,
na upanga wa Roho ambao ni neno la Mungu; kwa sala zote na maombi mkisali kila
wakati katika Roho, mkikesha kwa jambo hilo na kudumu katika kuwaombea
watakatifu wote;” Waefeso 6:10-18.
Mambo ya kuzingatia kuhusu Mungu na kumiliki.
- Kuyafahamu mawazo ya Mungu.
Kuna
mawazo ambayo Mungu anayo kwa ajili ya kila mtu. Kila mtu kuna hatima kupewa na
Mungu. Kuna mawazo ya Mungu kwenye kila hatua na mambo ya maisha yako.
“Maana nayajua mawazo ninayowawazia ninyi, asema BWANA, ni mawazo ya amani wala si ya mabaya, kuwapa ninyi tumaini siku zenu za mwisho.” Yeremia 29:11.
- Njia za Mungu.
Njia za Mungu ni kwa namna gani mtu apate yale ambayo Mungu amemuwazia (ahadi za Mungu).
- Wakati wa Mungu.
Mungu
anawakati wake wakukufanyia jambo fulani, usiposubiri wakati wa Mungu kwa
haraka zako utaharibu na kukosea.
“Mdogo
atakuwa elfu, Na mnyonge atakuwa taifa hodari; Mimi, BWANA, nitayahimiza hayo
wakati wake.” Isaya 60:22.
Mambo
haya kuhusu kumiliki, ili wewe uyafahamu lazima roho mtakatifu akuelekeze.
“Lakini
Mungu ametufunulia sisi kwa Roho. Maana Roho huchunguza yote, hata mafumbo ya
Mungu. Maana ni nani katika binadamu ayajuaye mambo ya binadamu ila roho ya
binadamu iliyo ndani yake? Vivyo hivyo na mambo ya Mungu hakuna ayafahamuye ila
Roho wa Mungu.” 1 Wakorintho 2:10-11.
Mawazo
haya ya shetani yanaweza kuwa kupitia watu wako wa karibu na unaowaamini ambapo
shetani atawavuvia na kuwatumia wakushauri kinyume na mawazo, njia na wakati wa
Mungu ili ushindwe kuchukua hatua kuelekea hatima uliyopewa na Mungu. Petro
alitumika na shetani ili ajaribu kumzuia Yesu kutimiza kusudi lake alipewa na
Mungu.
“Tangu
wakati huo Yesu alianza kuwaonya wanafunzi wake ya kwamba imempasa kwenda
Yerusalemu, na kupata mateso mengi kwa wazee na wakuu wa makuhani, na
waandishi, na kuuawa, na siku ya tatu kufufuka. Petro akamchukua, akaanza
kumkemea, akisema, Hasha, Bwana, hayo hayatakupata. Akageuka, akamwambia Petro,
Nenda nyuma yangu, Shetani; u kikwazo kwangu; maana huyawazi yaliyo ya Mungu,
bali ya wanadamu.” Mathayo 16:21-23.
Hekima
ya kibinadamu ndio mawazo ya shetani, ambayo lazima yawe kinyume na mawazo ya
Mungu. Kuna muda hekima ya shetani inaonekana ni bora ila dhumuni lake ni
kuzuia kusudi na mawazo ya Mungu juu yako.
“Hekima
hiyo siyo ile ishukayo kutoka juu, bali ni ya dunia, ya tabia ya kibinadamu, na
Shetani.” Yakobo 3:15.
Kuna
mambo ya Mungu hutafanya kama utasikiliza ushauri wa kila mtu. Paulo anasema
injili aliyopewa haikuwa kwa namna ya kibinadamu na wala hakufanya shauri na
wanadamu ili ahubiri.
“Kwa
maana, ndugu zangu, injili hiyo niliyowahubiri, nawajulisha ya kuwa siyo ya
namna ya kibinadamu. Kwa kuwa sikuipokea kwa mwanadamu wala sikufundishwa na
mwanadamu, bali kwa ufunuo wa Yesu Kristo.” Wagalatia 1:11-12.
“alipoona
vema kumdhihirisha Mwanawe ndani yangu, ili niwahubiri Mataifa habari zake; mara
sikufanya shauri na watu wenye mwili na damu;” Wagalatia 1:16.
Na
kufuata mawazo na njia za Mungu haimaanishi kwamba umiliki wako utakuwa mwepesi
Hapana. Mawazo na njia za Mungu zinaweza kuwa ngumu lakini huko ndipo kwenye
umiliki wako na lazima upigane.
0 Comments