UFUFUO NA UZIMA CATHEDRAL
IBADA YA JUMAPILI 03.03.2024
ASKOFU DKT JOSEPHAT GWAJIMA
SOMO:
KINYWA CHA KICHAWI
Maneno yanayotamkwa yana nguvu ya kubomoa ama kujenga, Maneno yanapotamkwa yanakuwa angani yakisubiri muda ili yatimie. Wakati wana wa Israeli wameangusha ukuta wa Yeriko, Yoshua akasema maneno ya laana kwa atakaye kuja kujenga ukuta wa Yeriko.
“Naye Yoshua akawaapisha kiapo
wakati ule, akasema, Na alaaniwe mbele za BWANA mtu yule atakayeinuka na
kuujenga tena mji huu wa Yeriko; ataweka msingi wake kwa kufiliwa na mzaliwa wa
kwanza wake, tena atayasimamisha malango yake kwa kufiliwa na mtoto wake
mwanamume aliye mdogo.” Yoshua 6:26.
Baada ya kupita miaka karibu
mia tatu, akatokea mtu anaitwa Hieli Mbetheli akataka kuujenga ukuta, yale
maneno ya laana yakatimia.
“Katika siku zake, Hieli Mbetheli
akajenga Yeriko; akatia misingi yake kwa kufiwa na Abiramu mzaliwa wake wa
kwanza, na kuyaweka malango yake kwa kufiwa na mwana wake mdogo Segubu;
sawasawa na neno la BWANA alilolinena kwa Yoshua mwana wa Nuni.” 1 Wafalme
16:34.
Lakini pia maneno ya Yoshua
yalifanya maji ya Yeriko yawe machungu, yasiyofaa na yenye kufanya nchi kuzaa
mapooza.
“Watu wa mjini wakamwambia
Elisha, Angalia, twakusihi, mahali pa mji huu ni pazuri, kama bwana wangu
aonavyo; lakini maji yake hayafai, na nchi huzaa mapooza. Akasema, Nileteeni
chombo kipya, mtie chumvi ndani yake. Wakamletea. Akatoka akaenda mpaka
chemchemi ya maji, akatupa ile chumvi humo ndani, akasema, BWANA asema hivi,
Nimeyaponya maji haya; hakutatoka huko tena kufa wala kuzaa mapooza. Hivyo yale
maji yakapona hata leo, sawasawa na neno la Elisha alilolinena.” 2 Wafalme
2:19-22.
Ahabu alinenewa maneno ya laana
na Eliya kwa sababu alimuua Nabothi aliyemiliki shamba zuri la urithi ambalo
alikataa kumuuzia. Ahabu na mkewe Yezebeli wakatengeneza kisa ambacho kilifanya
Nabothi auwawe.
“Neno la BWANA likamjia Eliya
Mtishbi, kusema, Ondoka, ushuke, ukutane na Ahabu mfalme wa Israeli, akaaye
katika Samaria; yuko katika shamba la mizabibu la Nabothi, ndiko alikoshukia
ili alitamalaki. Ukamwambie, ukisema, BWANA asema hivi, Je! Umeua, ukatamalaki?
Nawe utamwambia, kusema, BWANA asema hivi, Mahali pale mbwa walipoiramba damu
ya Nabothi, mbwa watairamba na damu yako, naam, damu yako. Ahabu akamwambia
Eliya, Je! Umenipata, ewe adui yangu? Akamwambia, Nimekupata, kwa sababu
umejiuza utende yaliyo mabaya machoni pa BWANA. Angalia, nitaleta mabaya juu
yako; nami nitakuangamiza kabisa, nitamkatia Ahabu kila mume, aliyefungwa na aliyeachwa
katika Israeli. Kisha nitaifanya nyumba yako iwe kama nyumba ya Yeroboamu mwana
wa Nebati, na kama nyumba ya Baasha mwana wa Ahiya, kwa ajili ya chukizo
ulilonichukiza, hata kunighadhibisha, ukawakosesha Israeli. Tena BWANA alinena
habari za Yezebeli, akisema, Mbwa watamla Yezebeli katika kiwanja cha Yezreeli.
Mtu wa nyumba ya Ahabu afaye mjini, mbwa watamla, na yeye afaye mashambani
ndege wa angani watamla.” 1 Wafalme 21:17-24.
Pia Ahabu alinenewa maneno na
Mikaya Nabii ya kwamba asingerudi kutoka vitani lakini Ahabu aligoma
kumsikiliza Mikaya na kumfunga.
“Mfalme wa Israeli akasema,
Mchukueni Mikaya, mkamrudishe kwa Amoni mkuu wa mji na kwa Yoashi mwana wa
mfalme; mkaseme, Mfalme asema hivi, Mtieni mtu huyu gerezani, mkamlishe kwa
chakula cha shida, na maji ya shida, hata nitakaporudi kwa amani. Mikaya
akasema, Ukirudi kabisa kwa amani, BWANA hakusema kwa mimi. Akasema, Sikieni,
enyi watu wote.” 1 Wafalme 22:26-28.
Maneno yote aliyonenewa Ahabu
kutoka kwa Eliya (kuwa Mtu wa nyumba ya
Ahabu afaye mjini, mbwa watamla) na Mikaya (Mikaya akasema, Ukirudi kabisa kwa amani, BWANA hakusema kwa mimi) yakaja
kutimia. Pamoja na mbinu zote za kukwepa kuuwa lakini
maneno ya laana yaliyokuwa juu yake yakatimia. Neno lile lililonewa linatafuta
fursa litimie.
“Mtu mmoja akavuta upinde kwa
kubahatisha, akampiga mfalme wa Israeli mahali pa kuungana mavazi yake ya
chuma; kwa hiyo akamwambia mwendesha gari lake, Geuza mkono wako, unichukue
kutoka katika majeshi; kwa kuwa nimejeruhiwa sana. Pigano likazidi siku ile;
mfalme akategemezwa garini mwake, kinyume cha Washami, hata jioni akafa; damu
ikatoka katika jeraha yake ndani ya gari. Ikapigwa mbiu jeshini, jua likichwa,
kusema, Kila mtu aende mjini kwake, na kila mtu shambani kwake. Hivyo akafa
mfalme, akachukuliwa Samaria, wakamzika mfalme huko Samaria. Wakaliosha gari
penye birika la Samaria, na mbwa wakaramba damu yake; (basi ndipo walipooga
makahaba); sawasawa na neno la BWANA alilolinena.” 1 Wafalme 22:34-38.
Wachawi nao wanaweza kutamka
neno likawa. Wana wa Israeli wanatoka nchi ya ahadi na utiisho juu yao, wakawa
wanapita kwenye nchi ya Moabu, mfalme wa Moabu Balaki akawaogopa na hofu ikajaa
moyoni mwake. Balaki akaenda kwa mchawi Baalamu ili awalaani wana wa Israeli.
Mchawi anakinywa cha kutamka juu ya mtu ikawa maana Balaki anamwambia Baalamu
yeyote umlaanie lazima iwe.
Wewe nawe kuna maneno unaweza
kuwa umetamkiwa na kinywa cha kichawi. Ukitamkiwa maneno na kinywa cha kichawi
kama vile Mungu anavyoliangalia neno ili alitimize.
“Ndipo BWANA akaniambia, Umeona
vema, kwa maana ninaliangalia neno langu, ili nilitimize.” Yeremia 1:12.
Mashetani, mapepo, majini nao
wanaweza kulisimamia neno la kinywa cha kichawi mpaka litimie. Maneno
uliyotamkiwa kichawi yanaweza kutengeneza tabia, udhaifu nk, ambao utakufanya
ushindwe kufikia hatima yako.
Lazima mtu mwenye mamlaka na
kinywa cha ki Mungu yaani Baba atamke maneno mengine yatakayovunja maneno
yaliyotamkwa na kinywa cha kichawi.
0 Comments