UFUFUO NA UZIMA CATHEDRAL
SEMINA YA MAHUSIANO ALHAMISI 05.09.2024
ASKOFU BARAKA THOMAS TEGGE
SOMO: MAMBO YA KUZINGATIA ILI USIFANYE SEX KABLA YA NDOA 2
Kuna wakati mtu akiwa mjinga, Mungu ana namna ya kuyachukilia mambo kama hayaoni. Lakini kuna wakati mtu akishalijua neno na sheria ya Mungu, akakosea, Mungu atamuadhibu sawasawa na makosa yake.
“Basi, zamani zile za ujinga
Mungu alijifanya kama hazioni; bali sasa anawaagiza watu wote wa kila mahali
watubu.” Matendo ya Mitume 17:30
2. Epuka mambo yoyote yanayoamsha (kuchochea) hisia za mapenzi.
Kila mtu aliyemzima wa afya na
akili huwa anapata hisia za mapenzi. Mtu wa Mungu ili asifanye dhambi inabidi
ajilinde, na namna ya kushinda hisia za mapenzi ni kuepuka mambo yoyote ambayo
yataamsha hisia za mapenzi.
“Linda moyo wako kuliko yote
uyalindayo; Maana ndiko zitokako chemchemi za uzima.” Mithali 4:23
Mwili wa mtu aliyeokoka hauna
utofauti na mtu ambaye hajaokoka, kumbuka kinachozaliwa mara ya pili ni roho
sio mwili. Ni jukumu la mtu aliyeokoka kuudhibiti mwili wake kutenda mambo fulani.
“Twajua ya kuwa kila mtu
aliyezaliwa na Mungu hatendi dhambi; bali yeye aliyezaliwa na Mungu hujilinda,
wala yule wovu hamgusi.” 1 Yohana 5:18
Kuchezea hisia za mapenzi ni
sawasawa na mtu asiyetaka kuungua ila akacheza na moto. Hisia za mapenzi zipo
kwa kila mtu ila zinakuwa zimelala, na zikiwa zimelala usiziamshe.
“Nawasihi, enyi binti za
Yerusalemu, Kwa paa na kwa ayala wa porini, Msiyachochee mapenzi, wala
kuyaamsha, Hata yatakapoona vema yenyewe.” Wimbo ulio bora 2:7
Hisia za mapenzi ni kati ya hisia
zenye nguvu sana kwenye mwili wa mtu.
Ukiwa kwenye mahusiano inakuwa
hatari zaidi kwa kuwa ukishachochea hisia za mapenzi basi kuna mahali au mtu wa
kuelekezea hisia hizo. Kipindi cha hatari ni pale watu wanapoanza mahusiano kwa
kuwa wanakuwa na hisia za kuvutiwa na mwenzie. Hii hupelekea urahisi wa kuamsha
hisia za mapenzi kwa mwenzie.
Mambo yanayoamsha
hisia za mapenzi.
- Maneno unayosikia (oral) kuhusu mapenzi. Maneno yana nguvu sana kuchochea hisia za mapenzi. Kuna maneno kutoka kwa mtu unayempenda na kuvutiwa nae akikwambia kwenye mahusiano ya uchumba hisia zako za mapenzi zinaamshwa na kuchochewa.
- Maneno unayoandikiwa (written) kuhusu mapenzi. Maneno unayo andikiwa yana nguvu kwa maana hata ukisahau kuna sehemu unaweza kuyapata na kuyarudia.
Kwenye kuandikiana message au kuambiana maneno lazima kuwe na mipaka. Kuna maneno ambayo mtambiana kwenye ndoa ili kuepusha hisia za mapenzi wakati wa uchumba.
- Mambo unayoyaona. Epuka kuangalia picha au majarida machafu. Teknolojia imefanya mambo machafu yawe rahisi sana kuyapata sio kama zamani. Ukishaanza kuangalia hayo mambo machafu yanakutengeneza addiction (uraibu) ambapo huwezi kuangalia hizo picha chafu bila kuamsha hisia za mapenzi. Kama kweli una nia ya kuepuka mambo yanayoamsha hisia za mapenzi, epuka kuangalia picha chafu au filamu zenye maudhui ya mapenzi.
- Mazingira ya faragha. Mazingira ya faragha yanaruhusu kufanya sex, kuna watu wanakuwa kweli hawana dhamira ya sex ila kuwa kwenye mazingira ya faragha inapelekea kufanya tendo hili. Mazingira ya faragha hutengeneza uwezo wa kufanya mambo fulani ambayo ni ya siri na huwezi kufanya mbele ya jamii/ umma kama sex tena mkiwa na hisia za mapenzi. Sehemu ya faragha hutengeneza uwezo wa yale maneno ya kusikia na kuandikiwa kuhusu mapenzi au mambo unayoyaona, kufanya iwezekane kutenda sex maana hayo yote huamsha hisia za mapenzi. Hata ukidhamiria ila kuna mazingira ukiwepo inaweza hatarisha na ukafanya sex. Tamari alikuwa na dhamira ya kutokufanya sex na kaka yake yaani Amnoni lakini mazingira ya faragha yakapelekea kufanyika tendo hilo.
“Amnoni akamwambia Tamari, Kilete
chakula chumbani, nipate kula mkononi mwako. Basi Tamari akaitwaa mikate
aliyoifanyiza, akamletea Amnoni nduguye mle chumbani. Naye alipokwisha
kuileta karibu naye, ili ale, Amnoni akamkamata, akamwambia, Njoo ulale nami,
ndugu yangu. 12Naye akamjibu, La, sivyo, ndugu yangu, usinitenze nguvu;
kwani haifai kutendeka hivi katika Israeli; usitende upumbavu huu. Nami
nichukue wapi aibu yangu? Wewe nawe utakuwa kama mmoja wa wapumbavu wa Israeli.
Basi, sasa, nakusihi, useme na mfalme; kwa maana hatakukataza kunioa. Walakini
yeye hakukubali kusikiliza sauti yake; naye akiwa na nguvu kuliko yeye,
akamtenza nguvu, akalala naye.” 2 Samweli 13:10-14
Ili kushinda majaribu ya
mazingira ya faragha ambayo yatapelekea kuamsha hisia za mapenzi na kutenda sex
ni lazima udhamirie na kuepekuka mazingira hayo kabisa. Yusufu alikuwa na
dhamira ya kutokufanya sex na mkewe Potifa lakini pia alikimbia mazingira ya
faragha.
“Ikawa baada ya mambo hayo, mke
wa bwana wake akamtamani Yusufu, akamwambia, Lala nami. Lakini akakataa,
akamwambia mke wa bwana wake, Tazama, bwana wangu hajui kitu kilichowekwa
kwangu nyumbani, na vyote alivyo navyo amevitia mkononi mwangu. Hakuna
mkuu katika nyumba hii kuliko mimi, wala hakunizuilia kitu cho chote ila wewe,
kwa kuwa wewe u mkewe. Nifanyeje ubaya huu mkubwa nikamkose Mungu? Akawa
akizidi kusema na Yusufu siku baada ya siku, lakini hakumsikia alale naye, wala
aongee naye. Ikawa, siku moja, akaingia nyumbani atende kazi yake, wala
hapakuwa na mtu katika watu wa nyumbani humo ndani; huyo mwanamke
akamshika nguo zake, akisema, Lala nami. Yusufu akaiacha nguo yake mkononi
mwake, akakimbia, akatoka nje.” Mwanzo 39:7-12
Kushinda kufanya sex kabla ya
ndoa lazima uwe na misimamo binafsi kabla hujaingia kwenye ndoa. Kilichompa
ushindi Yusufu ni msimamo binafsi wa kukimbia mazingira ya faragha ambayo ni
rafiki kufanya sex.
"BONYEZA HAPA KUANGALIA SEMINA NZIMA YA MAHUSIANO"
0 Comments