google.com, pub-4324601895065941, DIRECT, f08c47fec0942fa0

Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MPENYO WA KIMBINGU

UFUFUO NA UZIMA CATHEDRAL
IBADA YA JUMAPILI 26.04.2026
ASKOFU DKT JOSEPHAT GWAJIMA
SOMO:  MPENYO WA KIMBINGU

Mungu anasema ameweka mbele yetu siku arobaini za kupenya kwenye magumu tuliyonayo. Maisha yamejaa vita; ushindi katika vita ndiyo uwezekano wa kupata unachokitaka. Kuna watu walipookoka na kumjua Yesu, wakaacha mambo wanayoyahitaji yajilete yenyewe.

Kumjua Yesu pekee haitoshi. Kuna vitu ili uvipate ni lazima upigane vita. Mungu anapenda kuona watoto wake wakipigana vita maana Yeye ni Mtu wa vita 

"BWANA ni mtu wa vita, BWANA ndilo jina lake." Kutoka 15:3.

Hakuna shamba, gari, nyumba au nafasi ambayo utaipata bure; kila kitu kinamilikiwa na mtu. Lazima upige mtu na lazima ufyeke mtu ili upate kitu chako; hujafyeka, hujatoboa. Ukiokoka zinapigwa.

Mungu akikuonesha kitu anakuambia hicho ni chako lakini ili ukipate vita lazima ipigwe kwanza. Ndani ya siku arobaini tunazozianza kuna wa kupiga na wa kupigwa, na mambo ni mawili tu, mshindi au mshindwa. Sisi ni majeshi ya Bwana na ni washindi sio washindwa, kwa maana “…Hata sasa Bwana ametusaidia.” (1 Samueli 7:12)

"liacha Uyahudi, akaenda zake tena mpaka Galilaya. Naye alikuwa hana budi kupita katikati ya Samaria. Basi akafika kunako mji wa Samaria, uitwao Sikari, karibu na lile shamba ambalo Yakobo alimpa Yusufu mwanawe. Na hapo palikuwa na kisima cha Yakobo. Basi Yesu, kwa sababu amechoka kwa safari yake, akaketi vivi hivi kisimani. Nayo ilikuwa yapata saa sita. Akaja mwanamke Msamaria kuteka maji. Yesu akamwambia, Nipe maji ninywe. Kwa maana wanafunzi wake wamekwenda mjini kununua chakula............. Yohana 4:3-29

Kutokujua ni tatizo. kuna wakati unakutana na mtu unamtendea jambo bila kujua ni nani kumbe ni mtu mwenye njia ya kupenya kwako. Mwanamke Msamaria alimuuliza Yesu kwa namna ya dharau bila kujua Yeye ndiye Masihi wanayemsubiri (Yohana 4:12).

Mwanamke Msamaria alikuwa na uelewa kuwa ilishatabiriwa zaidi ya miaka elfu moja mia mbili iliyopita kwamba Masihi atakuja, lakini hakujua kuwa anayeongea naye ndiye; alikuwa anauelewa kuhusu Isaya 6:8 na Isaya 53:5.

Kutoka Musa kuishi hadi Kristo yapata miaka kati ya elfu moja na mia mbili, na elfu moja na mia tano ambayo ilitabiriwa kuwa Masihi atazaliwa duniani ili aukomboa ulimwengu. Musa alitabiri ujio wa kizazi cha mwanamke atakayeponda Kichwa cha nyoka; uzao wa mwanamke alimaanisha Kristo Yesu.

Esau aliinua juu nyoka wa shaba ambaye, kwa yeyote amtazamaye alipata kuishi; hiyo ilikuwa ni Ishara ya ujio wa Kristo Yesu. Katika Torati, Mungu alisema atamuinua nabii mwingine aliyekama Musa; nabii huyo ni Kristo Yesu.

Kwenye maisha kuna watu huwa na taarifa kabla ya mtu au jambo halijatokea. Kuna mambo mambo yamefichwa machoni pa mtu; yampasa mtu kuomba ili afunuliwe. Imeandikwa katika 

"akisema, Laiti ungalijua, hata wewe katika siku hii, yapasayo amani! Lakini sasa yamefichwa machoni pako."Luka 19:42

Hadi leo Wayahudi/Israel wanasubiri Kristo aliyetabiriwa aje. Mariam alichukuliwa mimba kwa uwezo wa Roho Mtakatifu akiwa Nazareti, na mimba ilikuwa miezi tisa akiwa Nazareti. Yesu alizaliwa katika mji wa Bethlehem na akiwa mchanga akahamia Misri. Akiwa Misri aliishi mji wa Alexandria kandokando ya mto Nile.

Mto Nile unaanzia Tanzania, hivyo, Yesu alikunywa na kutumia maji yetu. Wakati Israel wanasubiri ujio wa Masihi, kuzaliwa na uwepo wa Yesu ulifunuliwa kwa watu wachache.

1. 1. Mariam

Baada tu ya kuchumbiwa na Yusufu, Mariam anatokewa na Malaika na kumjulisha kuwa atachukua mimba kwa uwezo wa Roho Mtakatifu na atazaa mtoto mwanamume mwenye jukumu la kimbingu. Mariam alikubali kuwa iwe kama alivyoambiwa

"Mariamu akasema, Tazama, mimi ni mjakazi wa Bwana; na iwe kwangu kama ulivyosema. Kisha malaika akaondoka akaenda zake"Luka 1:38.

Wakati Wayahudi wanaingia kwenye Masinagogi kuomba ujio wa Masihi, Mariam alijua ujio umefika lakini hakusema maana siyo rahisi kuamini kwa sababu manabii wote walimsubiri mpaka wakafa bila Masihi kuja.

Kuna baadhi ya mambo ukiwaambia watu hawatakuelewa lakini usikate tamaa songa mbele. Hakuna jambo gumu kama jambo ambalo dunia nzima inalisuburi lakini wewe uko nalo.

2.  2. Yusufu

Yusufu alisikia tetesi kuwa Mariam, mchumba wake, ni mjamzito. Yusufu alitaka kumuacha Mariamu kwa siribila kumuaibisha. Malaika alimtokea Yusufu na kumpa taarifa kuwa mimba ya Mariamu ni kwa uwezo wa Roho Matakatifu na ni kusudi la kimbingu la kuzaliwa Masihi atakayeukomboa ulimwengu.

Kuna wanawake wa mataifa mbali mbali lakini wameachwa wote akachaguliwa Mariamu ili tumbo lake litumike kuukomboa ulimwengu. Kuna jambo siyo la kila mtu. Kila mtu ana jambo alilopewa kutimiza hapa duniani. Hakikisha kusudi lako unalitimiza.

Wenye haki wakipewa jambo la mtu hawasemisemi. Mariamu alikuwa mchumba tu wa Yusufu lakini Malaika alimuita Mariamu kuwa mke wa Yusufu. Mwenye haki akichumbia tu mbingu zinajua aliyechumbiwa ni mke. Muujiza wako unaweza ukashukia kwa mchumba wako au mkeo au mumeo na ukiona hivyo usijiulizeulize, dandia upenye pamoja naye.

3.  3. Elizabeth

Alikaa nchi ya milima. Mariamu alimtembelea Elizabeth kumjulisha mimba ya Masihi. Elizabeth alikuwa na mimba kumzaa Yohana. Yohana alikuwa mtengeneza njia ya Yesu.

Mariamu na Elizabeth waliposalimiana tu, Yohana tumboni mwa Elizabeth akaruka kwa shangwe, na Elizabeth akajazwa Roho Mtakatifu.

4.  4. Simeoni

Kuna watu hawafi mpaka jambo waliloahidiwa na Bwana litimie. Unaweza ukakosa mambo mengi, mfano, chakula, fedha, nyumba ila hufi mpaka uone jambo ambalo Mungu alikuahidi. Nabii Eliya hakufa kwa mateso aliyopitia.

Kwa desturi ya Wayahudi, mtoto akifikisha siku nane hupelekwa hekaluni kutairiwa. Simeoni alipata shauku kwenda hekaluni siku ambayo Yesu alipelekwa. Roho Mtakatifu aliwaongoza wote kukutana hekaluni.

5.  5. Hana binti Fanueli

Alikuwepo hekaluni wakati Simeoni anakutana na Yesu akiwa na siku nane.

Hekima ya Mungu ina knockout Hekima za dunia. umeanza na bila kitu ila utamaliza na kila kitu. Mungu kama angetaka wewe kumaliza kama hivyo ulivyo ungekufa toka tumboni mwa mama yako au kwenye ile ajali uliyopona au kwenye ile shida iliyokuwa inakutatiza; ila kama uko mzima hadi muda huu basi hautamaliza kama hivyo ulivyo sasa.

Ujinga wako hauwezi kuzuia lile ambalo Mungu amelipanga juu yako. Mungu haangalii makosa wala kuanguka kwako; Yeye anaangalia kusudi aliloliweka ndani yako. Wakati wako wa baraka ukifika hupambani, wakati ukifika utaweka nguvu kidogo ila matokeo ni makubwa kama mlipuko wa volkano.

Kuna tofauti ya mtu aliyetumwa na Mungu akulete ujumbe na mtu aliyetoka kwa Mungu akuletee ujumbe.

6.  6. Mamajusi, Wachungaji wa Kondoo wa zamu, na Herode.

Hawa wote pia walipata taarifa za kuzaliwa Kristo Yesu. Wachawi wanao ujuzi wa kujua jambo lako hata kama wewe hujui; waliona Nyota wakajua Kristo amezaliwa. Mamajusi walimfahamisha Herode kuhusu taarifa za kuzaliwa Kristo Yesu.

Katika mpenyo wa kimbingu wa siku arobaini, wenye kuelewa haraka watapenya mapema sana lakini hakika ni kwamba siku ya mwisho majeshi yote ya Mungu tunavuka.

BONYEZA HAPA KUANGALIA IBADA YA JUMAPILI

Post a Comment

0 Comments