UFUFUO
NA UZIMA CATHEDRAL
IBADA
YA JUMAPILI 27.09.2026
BISHOP DR JOSEPHAT
GWAJIMA
SOMO:
MATUKIO YA KICHAWI
![]() |
Kila
tukio katika ulimwengu wa kawaida (secular episodes), lina chanzo chake katika
ulimwengu wa roho. Huu ndio msingi mkuu wa kutufumbua macho kuhusu
namna ulimwengu wa giza unavyofanya kazi kupitia "Matukio ya
Kichawi."
Maandiko katika kitabu cha Ayubu
(Ayubu 1) yanatupa picha kamili ya
jinsi ulimwengu unavyoratibiwa. Ayubu alikuwa mtu mcha Mungu, lakini pasipo
yeye kujua, kulikuwa na kikao cha kiroho kilichofanyika mbinguni ambapo Shetani
alipewa ruhusa ya kugusa mali na watoto wa Ayubu.
Duniani, matukio yalionekana ya
kiasili na ya kawaida kabisa: majambazi wa kabila la Waseba walivamia na
kuchinja watumishi wa Ayubu, moto ulishuka kutoka mbinguni ukachoma kondoo za
Ayubu, na upepo wa dhoruba ukapiga kona nne za nyumba ya Ayubu na kuua watoto wa
Ayubu. Kwa mtazamaji wa kawaida wa mwilini, hayo yalikuwa ni majanga ya asili
au ujambazi wa kawaida. Lakini ukweli wa kiroho ni kwamba, matukio yote hayo
yalikuwa ni matokeo ya maamuzi yaliyopitishwa kwenye kikao cha kiroho.
![]() |
Hata leo, adui
anafanya vikao vya siri chini ya bahari, njia panda, na kwenye madhabahu za
giza ili kupanga "Kalenda za Kichawi." Kwenye kalenda hizo, majina ya
watu huandikwa kulingana na kile adui anachokusudia: nani apate ajali miezi ya
mwisho wa mwaka, nani apewe talaka, nani afukuzwe kazi, na nani afe kabla ya wakati
wake. Hakuna jambo linalotokea mwilini bila kikao cha kiroho kutangulia.
Kama vile
serikali za mwilini zinavyokaa na kupitisha bajeti na mipango ya maendeleo,
ndivyo na mamlaka za giza zinavyokaa kwenye vikao kupitisha bajeti ya
uharibifu. Kila unachokiona kikiharibika mwilini, ujue kura yake ilishapigwa na
kalenda yake ilishapitishwa kwenye kikao cha kiroho. Wachawi hukaa vikao kila
siku. Kabla ya mtu hajalogwa, kuna kikao / vikao vilikaliwa na wachawi
kupitisha maamuzi dhidi yake. Asili ya maamuzi ni vikao; Mungu hukaa vikao, mfano ni Mwanzo 1:26. Vikao hufanyika rohoni.
Kutambuliwa kwa
taifa la Israeli 1948 ni mfano hai wa matukio ya kiroho yanavyozaa uhalisia wa
mwilini. Ezekieli
37:1-10 kuhusu bonde la mifupa mikavu, Mungu
alimpeleka Nabii Ezekieli kwenye bonde lililojaa mifupa iliyokauka sana,
ikimaanisha hali ya kukatisha tamaa, umaskini uliokithiri, au uharibifu
uliodumu kwa miaka mingi kiasi cha kupoteza matumaini ya kurejea. Nabii
Ezekieli akatabiri uhai kwa mifupa hiyo, na baada ya miaka mingi ikadhihirika
mwilini kwa kurudi kwa taifa la Israel na kutangazwa rasmi kuwa nchi huru mwaka
1948.
Mtu hufanikiwa /
hupanda juu kupitia upendeleo aliopewa na Mungu; Mungu alishatoa, hivyo ni
jukumu la mtu kumiliki. Hata hivyo, wachawi huiba upendeleo wa mtu. Mtu
aliyeiba upendeleo wa mwingine, atafanikiwa kwa sababu upendeleo huo unafanya
kazi vilevile kama ambavyo Mungu aliutoa.
Shetani hana uwezo wa kuumba;
kazi zake ni tatu tu, kuiba, kuua na kuharibu (Yohana 10:10),
na ana namna tatu kuu anazotumia kumtesa na kumdhibiti mwanadamu mwilini:
1. Kuingia
ndani ya mtu / Kupagawa (Possession): Hali hii hutokea pale roho chafu
(kama vile majini au vibwengo) inapoingia ndani kabisa ya mwili wa mtu na
kuanza kutumia viungo vyake, mfano mdomo, kuongea au kutenda mambo yaliyo
kinyume na uasili wake.
2. Kudhibitiwa
Kutokea Nje (External Hindrance): Hapa mtu anaweza akawa
amemwamini Mungu na ana Roho Mtakatifu ndani yake (hajapagawa), lakini adui
anasimama nje ya mazingira yake kuzuia fursa zake. Ni kama vile mtume Paulo anavyosema
alitaka kwenda kwa Wathesalonike mara mbili lakini "Shetani
alituzuia" (1 Wathesalonike
2:18), au jinsi adui alivyosimama upande wa kuume wa Kuhani Mkuu Yoshua ili
kushindana naye (Zakaria 3:1).
3. Kukandamizwa
Eneo Moja la Maisha (Oppression): Katika hali hii, mtu anakuwa na
furaha na mafanikio katika maeneo mengi, lakini eneo moja mahususi linakuwa
limegandamizwa kikamilifu, iwe ni ugonjwa sugu usioeleweka na madaktari, mikosi
ya kifedha, au utasa.
Kwa namna hizi
tatu, ni wazi kabisa kuwa Shetani hawezi kudhibitiwa katika ulimwengu wa kawaida (secular episodes),
isipokuwa, ni ulimwengu wa kiroho pekee ndiyo una mamlaka ya kumdhibiti
Shetani; imeandikwa katika Waefeso 6:12 kuwa “Kwa maana kushindana kwetu sisi si juu ya
damu na nyama; bali ni juu ya falme na mamlaka, juu ya wakuu wa giza hili, juu
ya majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho”
Huwezi kupigana vita vya rohoni
kwa kutumia akili, hekima, au mamlaka ya mwilini. Mambo ya rohoni yanahitaji
mamlaka ya kiroho.
Yapo matukio
mengine ni ya kawaida kabisa hata ndani ya familia baina ya wenza, lakini
vyanzo vyake ni kiroho. Moja ya mifano hai ya kiroho inayodhihirika mwilini
ni kile kinachoitwa "Kangaroo Lifestyle" (Maisha ya Kangaroo).
Mnyama kangaroo anajulikana kwa tabia yake ya kutosimama sehemu moja; yeye
hutembea kwa kuruka-ruka kutoka hatua moja kwenda nyingine na hawezi kutulia.
Katika ulimwengu wa mwili, roho
hii inapomvaa mtu, inamfanya kuwa wa kuruka ruka na asiyetabirika kimaisha,
katika mahusiano, au kazini. Mtu anakuwa hajatulia: leo yuko hapa, kesho yuko
kule; leo anaanzisha biashara hii, kesho anaiacha na kurukia nyingine; leo yuko
kwenye ndoa au mahusiano haya, kesho anaruka kwenda kwingine bila sababu ya
msingi. Watu wa nje wanaweza kudhani ni maamuzi yake binafsi au ni tabia tu ya
kawaida ya kutofanya maamuzi sahihi, lakini ukweli wa kiroho ni kwamba kuna mamlaka
ya giza inayomfanya aruke ruke kama kangaroo ili asipate utulivu wa kufanikiwa
na kuwahi hatua zake za maisha.
Kuna wakati changamoto za maisha
hazitokani na kile unachokifanya leo, bali zinatokana na kile ulichokibeba
kwenye meli ya maisha yako. Biblia inatupa mfano wa Yona (Yona 1), mtu aliyekuwa mbishi na mwenye msimamo mkali wa kukataa
maagizo ya Mungu. Wakati Yona alipoingia kwenye meli iliyokuwa inaenda
Tarshishi, dhoruba kali ilipiga baharini hadi shehena zote zikawa hatarini
kupotea.
Hii inawakilisha "Yona Lifestyle" (roho au ukoo mbishi). Ukibeba mtu,
tabia, au muundo wa kiroho wenye roho ya Yona kwenye biashara yako, ndoa yako,
au familia yako, dhoruba hazitaacha kupiga, meli itatikisika na utapoteza vitu
vya thamani si kwa sababu huna akili ya biashara, bali kwa sababu umebeba
"Ukoo Mbishi" usiotaka kutii sauti ya Mungu. Success comes because of
the decision you make; good or bad. Mshushe Yona.
Wakati mwingine, ulimwengu wa
giza huunda koo kabisa kupitia DNA ya kiroho (Luciferic DNA), kama ilivyotokea Mwanzo 6 ambapo malaika walioanguka walizaliana na binti za
wanadamu na kuzaa majitu (Nephilim).
Hawa walikuwa watu ambao tangu asili yao walikuwa wameharibika kiroho na
walihitaji uingiliaji maalum wa ki Mungu. Unaweza ukafanikiwa au ukaharibikiwa
kwa sababu ya kuingia katika ukoo fulani.
Ukombozi wa Ukoo:
Habari njema ni kwamba, Mungu ana
uwezo wa kuingilia kati historia ya ukoo na kuibadili kabisa bila kujali adui
alipanga nini. Mathayo 1:1 inatuonesha
kitabu cha ukoo wa Yesu Kristo. Katika ukoo huu, Mungu alichagua kwa makusudi
kuwaingiza wanawake wawili wenye historia tata: Rahabu (kahaba wa Yeriko) na
Ruthu (Mmoabi kutoka taifa lililolaaniwa).
Mungu alifanya hivi ili kuonesha
mantiki ya kiroho kwamba: Yeye haangalii historia ya aibu au laana ya ukoo
wako ulikotoka, bali anaangalia moyo wako wa utii wa sasa. Kupitia Rahabu
na Ruthu kuingia kwenye uzao wa Masihi, Mungu alivunja sheria zote za kiasili
na kiukoo ili kutengeneza njia mpya safi. Hii inamaanisha kuwa hata kama
ulizaliwa kwenye ukoo wa kichawi, uliolaaniwa, au ukoo unaoruka ruka kama
kangaroo, neema ya Mungu inaweza kukutoa huko na kukuingiza kwenye uzao wa
kifalme wa kiroho.
Ili kuvunja kalenda na matukio ya
kichawi yaliyopangwa dhidi ya familia yako, ndoa yako, au afya yako, unahitaji
kusimama imara katika Jina la Yesu (Yohana
14:13-14) na
kutumia damu ya Yesu kumshinda ibilisi na mashetani (Ufunuo 12:11). Tumia Upanga wa Roho ambao ni Neno la Mungu
kufyeka wachawi na adui zako (Waefeso
6:17). Wachawi ni watu; wapo watu si wa Mungu ila ni wa Shetani, lakini ni
watu. Imeandikwa katika 1 Yohana 3:10
kuwa, “Katika hili watoto wa Mungu ni dhahiri, na watoto wa Ibilisi nao. Mtu
yeyote asiyetenda haki hatokani na Mungu, wala yeye asiyempenda ndugu yake.”
tunapaswa kuwa miali ya moto (Zaburi 104:4) na kuamka usiku wa manane
kugeuza matukio yaliyopo hewani. Tunapoinuka kwa mamlaka na kukataa maisha ya
dhoruba za Yona au mtindo wa kuruka ruka wa kangaroo, ulimwengu wa roho
unalazimika kutengeneza matukio mapya ya utulivu na ustawi, na tutakuwa huru
kweli kweli (Yohana 8:36).

.jpeg)

0 Comments