google.com, pub-4324601895065941, DIRECT, f08c47fec0942fa0

Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MATUKIO YA KICHAWI

UFUFUO NA UZIMA CATHEDRAL
IBADA YA JUMAPILI 04.10.2026
BISHOP DR JOSEPHAT GWAJIMA
SOMO: MATUKIO YA KICHAWI

Kuelekea mwisho wa nyakati, matukio ya kutisha, majanga ya asili (kama mvua za kupitiliza, upepo, matetemeko, na vita) yataongezeka duniani. Dunia itayachukulia majanga haya kama mambo ya asili, lakini kimsingi yanatengenezwa kwenye ulimwengu wa giza ili kumtengenezea njia "Mpinga Kristo" kushika mamlaka ya dunia.

Mpinga Kristo hatakuwa pepo, bali ni kiongozi wa kibinadamu (kisiasa na kiuchumi) atakayekubalika na mataifa yote kwa sababu ataonekana kuwa na akili sana kuliko viongozi wengine na kuleta amani ya muda. Viongozi wa mataifa (Maraisi, Wafalme na Mawaziri wakuu) watasalimu amri kwake ili aiongoze dunia kwenye korongo lake. Itatokea, siyo kwa sababu Shetani ana nguvu, ni kwa sababu ya kalenda ya Bwana ambayo hata Shetani mwenyewe anatembelea hiyo.

Wakati ukiwadia, Kanisa litamtambua kama Mpinga Kristo wakati dunia itamwona kama mwokozi kwa sababu ya werevu na ujanja ujanja wake. Walio wa Bwana watatengwa na njia za Mpinga Kristo kwa maana Kanisa haliwezi kuchangamana au kufanya maelewano (compromise) na imani zingine; Sisi tumetengwa na watu wa dunia hii (2 Wakorintho 6:17).

Kama Kanisa Imani yetu ni moja tu, ili tufike kwa Baba (Mungu) njia ni moja tu; Yesu Kristo. Imeandikwa katika Yohana 14:6 kuwa, "… Mimi ndimi njia, na kweli, na uzima; mtu haji kwa Baba, ila kwa njia ya mimi."

Imani ya yetu (Kikristo) imesukwa / imeunganishwa na pamoja na mila na desturi za Kiyahudi; Anayeilaani Israeli amejilaani mwenyewe na anayeibariki Israeli amejibariki kulingana na sheria ya Mungu. Ni Mungu peke yake tunamwamini na kuisikiliza sauti yake.

Tangu Ibrahimu hadi wana wa Israeli wanavuka Bahari ya Shamu, hakukuwa na kitabu walichokisoma au kuwapa maelezo; Wao waliisikia sauti ya Mungu tu. Kitabu na Sheria kilianza wakati Wana wa Israeli wanatoka Misri kwenda Kanaani, na walipofika kwenye Mlima Sinai, Mungu akashusha amri kumi kwa Musa ziwaongoze Wana wa Israeli ambao walianza kumuuzi Mungu; Mungu alisisitiza (Kutoka 20:3) wasiwe na Mungu mwingine ila Yeye.

Ni ahadi ya ulinzi wa Mungu kwake / kwao wamtegemeao ya kuwa, katika hali yoyote, watakatifu wa Mungu wana ahadi ya kulindwa na hawatadhurika na majanga ya dunia. Sisi Ufufuo na Uzima hatutalegeza msimamo wetu kuhusu Mungu wetu kwa maana tunawakilisha serikali ya mbinguni. Hatufuati inayoitwa hekima ya mwanzi kuinama upepo ukivuma na kuinuka upepo ukipita; ile siyo hekima ni unafiki wa mwanzi. Tunafuata maelekezo ya Biblia kama yatuambiavyo mstari kwa mstari.

Kwa namna tunavyoamini katika Neno, hata utabiri wa kisayansi wa ujio wa mvua kubwa za Super El Niño zitakazosababisha kukatika kwa madaraja, ukosefu wa chakula, umeme na mlipuko wa magonjwa, tumaini na suluhisho la kweli halitotoka kwa akili za kibinadamu bali kwa Mungu asiyesinzia (Zaburi 121:3-4).

Ipo mifano mingi ambayo Mungu aliwalinda watu wake kwenye majanga makubwa:

1.   Mvua ya Mawe na Moto: Kutoka 9:22-26 – Mvua kubwa ya mawe na moto ilipiga Misri yote lakini katika nchi ya Goshen walikokaa wana wa Israeli haikuwako mvua hiyo.

2.   Pigo la Mainzi: Kutoka 8:21-23 – Mungu alitenga nchi ya Goshen ili mainzi wasiwepo huko, wakati Misri yote ilijaa mainzi.

3.   Vifo vya Wazaliwa wa Kwanza: Kutoka 11:4-7 – Malaika wa kifo aliua wazaliwa wa kwanza wote wa Misri, lakini kwa Waisraeli hakuna hata mbwa aliyetoa ulimi wake.

Ni desturi ya Mungu kuwatenga Wamisri na Waisraeli, yaani, waovu na wanaomcha Mungu. Kwanini wanaomcha Mungu hawaguswi? Jibu ni rahisi kabisa; tupo duniani kutimiza jukumu la Mungu mwenyewe ambalo angependa aje mwenyewe kulitimiza lakini akatutuma tumwakilishe kulitimiza, hivyo anatulinda tukamilishe.

Mwenye jukumu kubwa, anavita kubwa. Wachawi wanauwezo wa kuona lile jambo kubwa ambalo Mungu ameliweka ndani ya mtu, wakamzuia mtu asiliishi; kwa bahati mbaya sana Mungu anaweza akakuwekea kitu ndani yako lakini hata wewe ukawa hujijui. Kwa sababu hiyo, hata mataifa mengi yanakuwa ovyo kwa sababu watu wazuri (magenius na wenye nia njema) hawapo kwenye siasa. Walio kwenye giza wamewaaminisha watu wazuri kuwa siasa ni "mchezo mchafu" na kwamba isichanganywe na dini.

Ukweli kuhusu siasa ni kwamba, siasa siyo mchezo mchafu kwa sababu, wabunge, mawaziri na marais ndio wanaopanga kodi, sera za nchi, ulinzi, kuzalisha nafasi zote muhimu kwa ustawi wa nchi, na kuteua watu wa kushika nafasi hizo; siasa ni mchezo msafi kwa maana hata Bunge linapoanza huwa linamuomba Mungu, hivyo Mungu yupo bungeni. Kwahiyo, kumuachia mwana wa giza awe mwanasiasa ni kuleta mfumo wa giza ndani ya nchi.

Kuhusu Nyota na Hatima:

Kila mtu amezaliwa akiwa na "nyota" au mzigo/mission maalum kutoka kwa Mungu (iwe ya kibiashara, kijamii, au kisiasa).

Yusufu: Aliota ndoto ya nyota 11, jua na mwezi vikimwinamia, ikionyesha uongozi na hatima yake juu ya ndugu zake na wazazi wake.

Balaamu na Mamajusi: Mchawi Balaamu aliona nyota itakayotoka katika Yakobo). Mamajusi wa mashariki pia waliona nyota ya Yesu.

Yohana Mbatizaji na Eliya: Yohana alikuja kwa nguvu na roho ya Eliya, lakini Yohana mwenyewe alipoulizwa kama yeye ni Eliya alisema "hapana" kwa sababu alikuwa hajajitambua, japo walio nje pamoja na Yesu walijua; unawezakuwa na kitu kikubwa ndani yako lakini hujijui.

Uharibifu wa Kichawi: Wachawi wana uwezo wa kuona nyota za watu (kama nyota ya fedha, masomo, utawala, au ndoa) na kuziiba au kuzikandamiza kwa kutumia mapepo, magonjwa, au umaskini ili wao wafanikiwe huku mwenye nyota akiteseka.

Ukiidai nyota iliyoibiwa utaipata. Ukiipata, inarudi na mali iliyoitengeneza. Nyota haidaiwi kwa kwenda kwa waganga bali kwa kutumia mamlaka na amri katika Jina la Yesu. Imeandikwa katika Waefeso 6:12 kuwa, "Kwa maana kushindana kwetu sisi si juu ya damu na nyama; bali ni juu ya falme na mamlaka, juu ya wakuu wa giza hili, juu ya majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho."

Tunashinda kwa maana tumepewa amri ya kukanyaga nyoka na nge na nguvu zote za adui, na hakikisho letu ni dhahiri kuwa hakuna kitakachotudhuru. Vipo vingi vya muhimu lakini havirudishi nyota; kwa mfano, elimu. Elimu haihakikishii mtu mafanikio ya kiuchumi.

Ni ahadi ya Mungu kuturudishia miaka yote iliyoliwa na nzige (Yoeli 2:25). “The world offers you what you fight for.” Itake nyota yako, utaipata, kwa Jina la Yesu; Amina!

Maombi ya Kushindana:

Kwa mamlaka ya Jina la Yesu, ninaingia kwenye ulimwengu wa roho; Ninatuma Moto wa Roho Mtakatifu kwenye kila pango, kwenye kila shimo, kwenye kila mibuyu, kwenye kila pori, na chini ya madaraja yote ambako nyota yangu ilifichwa au kufungiwa kwenye chupa na vibuyu! Navunja kila chupa na chungu cha kichawi sasa hivi!

Ninaziamuru nyota zangu zote zilizochukuliwa tangu utotoni mwangu zirudi kwangu sasa:

Nyota yangu ya fedha na utajiri, NJOO!

Nyota yangu ya biashara na kazi, NJOO!

Nyota yangu ya ndoa na uzao wa tumbo langu, NJOO!

Nyota yangu ya kibali, ya uso, na kupendwa, NJOO!

Nyota yangu ya akili, elimu, na macho ya kuona fursa, NJOO!

Nyota yangu ya afya na nguvu, NJOO!

Kwa Jina la Yesu; Amina.

    BONYEZA HAPA KUANGALIA IBADA YA JUMAPILI

 

Post a Comment

0 Comments