JUMAPILI
YA TAREHE 21 – 12 – 2014
MCHUNGAJI
KIONGOZI JOSEPHAT GWAJIMA
SOMO:
UHAMISHO WA KIROHO
“Basi vizazi vyote
tangu Ibrahimu hata Daudi ni vizazi kumi na vinne; na tangu Daudi hata ule
uhamisho wa Babeli ni vizazi kumi na vinne; na tangu ule uhamisho wa Babeli
hata Kristo ni vizazi kumi na vinne.” Mathayo 1:17
“Yekonia alikuwa na
umri wa miaka kumi na minane alipoanza kutawala; akatawala miezi mitatu katika
Yerusalemu; na jina la mama yake aliitwa Nehushta binti Elnathani wa
Yerusalemu. Akafanya yaliyo mabaya machoni pa Bwana,
mfano wa yote aliyoyafanya baba yake. Wakati ule
watumishi wa
Nebukadreza mfalme wa Babeli wakakwea kwenda Yerusalemu, na mji
ukahusuriwa. Na Nebukadreza, mfalme wa Babeli,
akaufikilia huo mji, hapo watumishi wake walipokuwa wakiuhusuru. Na Yekonia, mfalme wa Yuda, akatoka akamwendea mfalme wa
Babeli, yeye na mama yake, na watumishi wake, na wakuu wa watu wake, na maakida
wake; mfalme wa Babeli akamchukua mateka katika mwaka wa nane wa kutawala
kwake. Akatoa huko hazina zote za nyumba ya Bwana, na
hazina za nyumba ya mfalme, akavikata-kata vyombo vyote vya dhahabu ambavyo
Sulemani, mfalme wa Israeli, alivifanya katika hekalu la Bwana, kama Bwana
alivyosema. Akawachukua mateka watu wa Yerusalemu wote
pia, na wakuu wote, na mashujaa wote, watu elfu kumi; na mafundi wote, na wafua
chuma wote; hapana mtu aliyebaki, ila waliokuwa wanyonge wa watu wa nchi.”
2Wafalme 24:8 – 14
Mfalme wa Israel
wakati ule alikuwa anaitwa Yekonia na alitawala miezi mitatu na kumtenda Mungu
dhambi, naye Mungu akaruhusu mfalme wa Babeli aende kwa mfalme wa Israeli na
kuitawala Israel. Kumbe katika utawala, mtawala haihitaji muda mrefu sana ili
kuharibu mambo; vivyo hivyo kwenye wokovu, mtu haihiitaji kuwa kwenye wokovu
muda mrefu ili amkosoe Mungu. Tunaona Mfalme Yekonia alitawala miezi mitatu tu
na kisha kumtenda Mungu dhambi. Pia tunaona Mungu alipoziona dhambi za Yekonia
akaliachia taifa adui la Babeli kulivamia taifa la Israel. Unapokuwa dhambini
Mungu ataruhusu adui zako wakupige na hakika watakushinda. Hakuna ushindi
katika dhambi. Na Mfalme
Yekonia alilitambua vema jambo hili.
Kwa kutambua
hilo, Yekonia akaamua kujisalimisha kwa mfalme Nebukadreza yeye pamoja na mama
yake, baraza lake la mawaziri, maakida pamoja na watu wengine muhimu katika
nchi wakiwemo matajiri wote. Pia, mfalme Nebukadreza alichukua vitu vya thamani
kutoka katika hekalu la Bwana ikiwa ni pamoja na sanduku la agano. Akachukua
majeshi, mafundi, wenye akili wote na wafua chuma ili wakaujenge ufalme wa
Babeli.
Mfalme Yekonia alijisalimisha
kwa kuwa alijua atashindwa vita kwa sababu ya hali yake mbaya kiroho, yaani
dhambi. Imeandikwa,
“Mpenzi
naomba ufanikiwe katika mambo yote na kuwa na afya yako, kama vile roho yako
ifanikiwavyo.” 3 Yohana 1:2
Hali yako ya kiroho
ikiwa imefanikiwa, “ukiwa hauna dhambi” mambo mengine ya mwilini yatafanikiwa
vivyo hivyo. Mfalme wa Babeli hapa ni alama ya shetani. Shetani huwa ana
kawaida ya kuwachukua wale watu wenye akili, uwezo na nguvu popote aingiapo na
kuondoka nao. Yawezekana ni katika nchi au hata familia. Hujawahi kusikia
msibani watu wakisema, “ni heri angekufa fulani na si huyu.” Kuna msemo kuwa
watu wazuri huwa hawadumu. Kwa nini? Shetani anajua kuwa watu wa namna hii ni
hatari kwa ufalme wake ndio maana anajitahidi kuwafanya mateka mapema wawe
misukule au wadhaifu kwa namna ambayo hawatakuwa tishio kwake tena.
Imeandikwa,
“Kabla sijakuumba katika tumbo
nalikujua, na kabla hujatoka tumboni, nalikutakasa; nimekuweka kuwa nabii wa
mataifa.” Yeremia 1:5
Kabla hujazaliwa
Mungu tayari alikuwa na mpango na maisha yako kwamba utakapokuja duniani, uje
kuujenga ufalme wa Mungu. Hivyo akakuwekea uwezesho wa namna fulani ambayo leo
tunauita nyota ya mtu. Yaweza kuwa ni nyota katika biashara, masomo, utawala au
nyota ya kupendwa na kuubalika. Nyota yako ilipokuwa inashuka kuingia kwenye
tumbo la mama yako, shetani pia aliiona. Ndio maana kuna watu matatizo yao
yalianza tangu wakiwa tumboni. Shetani anajaribu kuharibu ule mpango wa Mungu
juu ya mtu. Lakini Mungu wetu ni Mungu aokoaye, ni pale tunapokuwa tumejitenga
naye kwa dhambi zetu ndipo tunapompa mwanya wa kutufanya mateka.
Imeandikwa,
“Mungu ni Roho, nao
wamwabuduo yeye imewapasa kumwabudu katika roho na kweli.” Yohana4:24
Mungu ni roho na
kilichozaliwa na roho ni roho na huushinda ulimwengu. Tunamwita Mungu Baba
kwasababu ya Roho zetu. Sisi sio miili, bali ni roho zilizotoka juu mbinguni na
kuvaa miili. Biblia inasema atokaye juu yu juu ya yote hata mauti. Kama kuna
kitu cha kipuuzi na cha kijinga tena kisicho na thamani hapa duniani basi kitu
hicho ni mwili wa mwanadamu. Miili mingine ya wanyama kama kuku, ng’ombe, mbuzi
inapokufa inaweza kutunzwa na kutumika baadae kama chakula au manufaa mengine.
Lakini mwili wa mwanadamu unapokufa hauna thamani ni wa kutupa tu. Wanadamu
wamejiwekea utaratibu wa namna ya kuutupa mwili ambao wanauita mazishi. Lakini
ukweli ni kwamba wanachokuwa wanafanya ni kuutupa mwili husika. Roho zetu ndizo
zenye thamani maana hizo hazifi hata milele. Kama sio Yesu, mwili wako hauna
thamani kabisa. Paulo alijua hili ndio maana akasema, “Kwa maana si mimi
ninayeishi bali Kristo aliye ndani yangu, kufa ni faida na kuishi ni Kristo.
Imeandikwa,
“Amin, amin, nawaambia, Yeye alisikiaye neno langu na
kumwamini yeye aliyenipeleka yuna uzima wa milele; wala haingii hukumuni, bali
amepita kutoka mautini kuingia uzimani.” Yohana 5:24
“Mimi
nimewapa neno lako; na ulimwengu umewachukia; kwa kuwa wao si wa ulimwengu,
kama mimi nisivyo wa ulimwengu. Mimi siombi kwamba
uwatoe katika ulimwengu; bali uwalinde na yule mwovu. Wao
si wa ulimwengu, kama mimi nisivyo wa ulimwengu. Uwatakase
kwa ile kweli; neno lako ndiyo kweli. Kama vile
ulivyonituma mimi ulimwenguni, nami vivyo hivyo naliwatuma hao ulimwenguni.”
Yohana 17: 14
Mfalme Yekonia hakuwa
mjinga bali mtu mwenye hekima. Alipokubali kujisalimisha kwa Mfalme Nebukadreza
alikuwa akiwaza ni heri wapelekwe uhamishoni kuliko kuipoteza nchi kabisa. Japo
nchi ilibaki na watu wadhaifu tu, alikuwa anajua katika viuno vyake kulikuwa na
mtoto ambaye ndiye angewatoa uhamishoni hawa wana wa Israel waliopelekwa
uhamishoni.
“Na
baada ya ule uhamisho wa Babeli, Yekonia akamzaa Shealtieli; Shealtieli akamzaa
Zerubabeli; Zerubabeli akamzaa Abihudi; Abihudi
akamzaa Eliakimu; Eliakimu akamzaa Azori; Azori
akamzaa Sadoki; Sadoki akamzaa Akimu; Akimu akamzaa Eliudi; Eliudi
akamzaa Eleazari; Eleazari akamzaa Matani; Matani akamzaa Yakobo; Yakobo akamzaa Yusufu mumewe Mariamu aliyemzaa YESU aitwaye
Kristo.” Mathayo 1:12
Leo kanisa
limehamishwa kwenye ulimwengu wa kiroho kiasi cha kutoamini uweza na nguvu za
Mungu. Tumehamishwa kwenye miji ya kiroho ya uharibifu, tupo mashimoni. Lakini
tumebweteka na kuridhika kukaa huku uhamishoni. Tumelima mashamba na bustani,
tumeoa na kuolewa huku uhamishoni na pia tumezaa tukiwa uhamishoni. Ni wakati
wa kutambua kuwa pamoja na mashamba na bustani tulizotengeneza lakini tuko
uhamishoni na yatupasa kurudi kwenye asili yetu.
“Bwana amekufanya kuhani badala ya
Yehoyada, kuhani, ili mpate kuwa watumishi katika nyumba ya Bwana, kwa kila mtu
aliye na wazimu, na kwa kila mtu ajifanyaye kuwa nabii, umtie katika mkatale na
pingu. Mbona, basi, hukumkemea Yeremia wa Anathothi,
ajifanyaye kuwa nabii kwenu, ambaye ametuma watu kwetu katika
Babeli, kusema, Uhamisho huu ni wa siku nyingi; jengeni nyumba, mkakae ndani
yake; pandeni bustani, mkale matunda yake.” Ezekieli 29: 26
Kwenye
ulimwengu wa rohoni kuna miji ya kiroho kabisa ambayo mtu ambaye ni roho
anaweza kuchukuliwa na kupelekwa huko. Miji hiyo ina nyumba, magari na kila
kitu kama ilivyo kwenye ulimwengu huu. Iko miji ya kiroho ya Mungu ambayo ina
nuru kuu inayoangazwa na Yesu mwenyewe.
“Msifadhaike mioyoni mwenu; mnamwamini
Mungu, niaminini na mimi. Nyumbani mwa Baba yangu mna
makao mengi; kama sivyo, ningaliwaambia; maana naenda kuwaandalia mahali. Basi
mimi nikienda na kuwaandalia mahali, nitakuja tena niwakaribishe kwangu; ili
nilipo mimi, nanyi mwepo. Nami niendako mwaijua njia.” Yohana 14:1
“Na ukuta wa
mji ulikuwa na misingi kumi na miwili, na katika ile misingi majina kumi na
mawili ya wale mitume kumi na wawili wa Mwana-Kondoo. 23 Na
mji ule hauhitaji jua wala mwezi kuuangaza, kwa maana utukufu wa Mungu huutia
nuru, na taa yake ni Mwana-Kondoo.” Ufunuo 21: 14
“Nami sikuona hekalu ndani yake; kwa maana Bwana Mungu
Mwenyezi na Mwana-Kondoo, ndio hekalu lake. Na mji ule hauhitaji jua wala mwezi
kuuangaza, kwa maana utukufu wa Mungu huutia nuru, na taa yake ni Mwana-Kondoo.
Na mataifa watatembea katika nuru yake. Na wafalme wa nchi huleta utukufu wao
ndani yake.” Ufunuo 21:22-24
Pia,kuna miji
ya kiroho ya giza ambayo giza lake hutokana na giza la mtawala wake shetani.
Miji hii inaitwa miji ya uharibifu. Inaitwa miji ya uharibifu kwa sababu ndani
yake kunafanyika mambo ya uharibifu. Huko ndiko shetani huwaweka watu na mali
za watu alizoiba.
“Katika siku hiyo itakuwako miji
mitano katika nchi ya Misri itumiayo lugha ya Kanaani, na kumwapia Bwana wa
majeshi; mji mmoja utaitwa Mji wa uharibifu.” Isaya 19:18
“Macho yangu yamechoka kwa machozi,
Mtima wangu umetaabika; Ini langu linamiminwa juu ya nchi Kwa uharibifu wa
binti ya watu wangu; Kwa sababu watoto wachanga na wanyonyao, Huzimia katika
mitaa ya mji. Wao huwauliza mama zao, Zi wapi nafaka na divai? Hapo wazimiapo
kama waliojeruhiwa Katika mitaa ya mji, Hapo walipomiminika nafsi zao Vifuani
mwa mama zao.” Maombolezo2:11-12
Katika miji
hii shetani na mawakala wake hufanya kazi za giza pamoja na kuchukua watu walio
imara, wenye akili, wenye nguvu, wenye uelewa mkubwa wanaong’ara na kuwapeleka
kwenye miji yake ya kiroho iliyoko kuzimu. Huko watu hawa humtumikia yeye kwa
namna mbalimbali katika kuujenga utawala wake wa kuzimu.
Sio mpango wa
Mungu watu wake wakae uhamishoni. Ndio maana hata kipindi kile, baada ya muda
mrefu wa kukaa uhamishoni Babeli, Mungu alimuinua Mfalme Koreshi akawaruhusu
wana wa Israeli kurudi kwenye nchi yao. Naye mfalme Koreshi aliandika waraka
kwa wafalme wengine katika njia ambayo wana wa Israeli wangeitumia kupita ili
wawaruhusu kupita. Mungu anainua mfalme Koreshi kwa kanisa katika wakati huu na
waraka pia umekwishaandikwa na Bwana Yesu mwenyewe. Ni wakati sasa watu wa
Mungu tuhame kutoka uhamishoni katika ulimwengu wa Roho na kurudi kwenye asili
yetu chini ya kiongozi wetu Yesu Kristo. Ni kweli tumejenga, tumelima
uhamishoni lakini hatuna budi kuacha yote na kuirudia ile asili yetu.
Maelfu wakiwa ndani ya bonde la kukata maneno |
MAOMBI
Kwa mamlaka ya
jina la Yesu Kristo, ninarudi kwenye mtazamo wangu wa asili niliowekewa na
Mungu. Kwa jina la Yesu ninarudi kutoka uhamishoni, ninawafyeka wale wote
mnaonizuia nisirudi kwa jina la Yesu. Ninatoka uhamishoni kwa jina la Yesu,
ninahama kwenye uhamisho wa kiroho kwa jina la Yesu; wale wote mlionipandikizia
fikra na mitazamo ya kishetani ninawateketeza kwa moto wa Mungu. Kwa jina la
Yesu ninaangusha milima yote iliyo mbele yangu, wachawi wote mlionizuia
uhamishoni ninawateketeza kwa moto wa Mungu, ninawaangusha kwa jina la Yesu. Kwa
damu ya mwanakondoo, nawasha moto kwenye miji yenu, natoka narudi kwenye asili
yangu ya rohoni kwa jina la Yesu Kristo. Ninafungua njia ya kupita kutoka
kwenye utumwa kwa jina la Yesu Kristo, ninarudi nyumbani. Ninahama kwenye
ulimwengu wa roho kutoka utumwani, narudi uzimani kwa jina la Yesu; ninahama
kutoka mautini narudi uzimani kwa jina la Yesu, ninahama kutoka kwenye
kushindwa narudi kwenye kushinda kwa jina la Yesu, nahama kutoka kwenye kufeli,
kuhuzunika, kuogopa, ninarudi kwenye asili ya ujasiri, nguvu, uweza, uimara,
utajiri, mafanikio kwa damu ya mwanakondoo. Kila anayenizuia ninamsambaratisha
kwa jina la Yesu Kristo. Wote mnaonizuia nisihame kwenye vifungo vyenu ninawafyeka
kwa jina la Yesu. Ninarudi kwenye asili yangu ya kumiliki kutiisha na kutawala
kwa jina la Yesu Kristo mwana wa Mungu aliye hai. Amen!
0 Comments