UFUFUO
NA UZIMA CATHEDRAL
IBADA
YA JUMAPILI 13.09.2026
ASKOFU
DKT JOSEPHAT GWAJIMA
SOMO:
KESHO
KUBWA ILIYONASA NDANI YA MTU
![]() |
Hatima ya mtu haikuanza siku aliyozaliwa. Hatima ya mwanadamu haianzi siku anayotoka tumboni mwa mama yake. Mtu alikuwepo mbinguni kama roho kabla ya kuja duniani. Neno la Mungu linasema katika Yeremia 1:5, "Kabla sijakufanya katika tumbo nalikujua, na kabla hujatoka tumboni nalikutakasa; nimekuweka kuwa nabii wa mataifa." Hii ina maana kwamba mtu alikuwepo mbinguni kama roho kabla hajaletwa hapa duniani.
Mfano: Pasipoti
za wananchi wa Korea Kusini
huandikwa umri wa mtu kwa kurudisha nyuma miezi tisa; Serikali yao inatambua
kuwa mtu alikuwepo tangu mimba ilipotungwa. Tumbo la mama ni kama uwanja wa
ndege tu ambapo roho inatua ikitokea mbinguni, na mwili ni ubia tu kati ya
wazazi wa kimwili na Mungu aliyeitoa roho.
Mungu Yesu hakuanza siku
alipozaliwa; alikuwepo mbinguni tangu mwanzo. Mungu aliumba mbingu na nchi kwa
Neno lake, na badae Neno akavaa mwili, akaja duniani kwa njia ileile ya kuwa
duniani, yaani akazaliwa (Yohana 1:1-14).
Hatuko
duniani kwa bahati mbaya: Hakuna mtu aliyeko Dar es Salaam au Tanzania kwa
ajali; Mungu alituleta kwa kusudi lake maalum. Mfano, Yohana 1:6
inasema wazi kuwa Yohana alitumwa kutoka kwa Mungu. Hii inatufundisha kuwa
ukitumwa na Mungu, unazaliwa duniani; ukikamilisha kazi uliyotumwa, unarudi kwa
aliyekutuma (Mhubiri 12:7).
Tunatoka mbinguni kuja duniani
katika utimilifu wa wakati tu (Wagalatia
4:4) na hatufi mpaka tutimize jukumu lililotutoa mbinguni kama ilivyokuwa
kwa mzee Simeoni ambaye hakufa mpaka alipombeba mtoto Yesu (Luka 2:26-35). Mwenye jukumu hupewa
neema ya kutimiza jukumu hilo; hata hivyo kuna wakati kesho ya mtu inakuwa imenaswa ndani ya uhalisia wa kibinadamu
ikisubiri neno la ki Mungu na mafuta ya kinabii ili iachiliwe.
Maana ya "kunasa" kwa
kesho ya mtu: Mifano katika Mbegu ya Embe na Yai: Kokwa la
embe kwa macho ya kawaida ni mbegu, lakini ndani yake "kumenasa"
shina, matawi, majani, na magunia ya maembe yatakayovunwa kwa miaka mingi
ijayo. Ule uwezo mkubwa umefungiwa ndani ya mbegu ndogo tu. Yai limebeba kuku
lakini ni mpaka uwadie utimilifu wa wakati ili kuku huyo adhihirike.
Kwa mifano hiyo, tunang’amua kuwa
uwezo wa mtu uko ndani yake; kile
Mungu amepanga mtu awe, hakiko mbinguni bali Mungu ameshakiweka ndani ya mtu.
Kila kitu kwa ajili ya upenyo wa mtu kiko ndani yake, ila kimenaswa ili mtu
asiwe na kesho iliyoamuriwa na Mungu. Ni lazima tuinasue kesho iliyonaswa, kwa
jina la Yesu!
Mifano ya
“kesho iliyonasa” na ikanasuka kwa jina la Yesu:
Katika 1 Samueli 1:1-2,
Biblia inamtambulisha mtu mmoja aitwaye Elkana mwana wa Yohamu, aliyekuwa na
wake wawili, Hana (mke mkubwa) na Penina (mke mdogo). Imeandikwa, "… naye huyo Penina alikuwa na
watoto, lakini Hana hakuwa na watoto."
Penina alikuwa anazaa watoto kwa
wepesi sana, na alipata watoto saba. Lakini Hana, aliyependwa sana na mumewe, hakupata
mtoto. Penina alimsimanga na kumdhalilisha Hana kila siku, kwa maneno makali
kwa sababu Hana hakuwa anajua uchungu wa uzazi.
Biblia inasema katika 1 Samueli
1:5 kuwa Bwana alikuwa amefunga
tumbo la Hana. Hapa tunajifunza kuwa sio kila kuzuiliwa ni laana. Tumbo
la Hana lilishikiliwa na falme za giza zilizojua kuwa Hana akizaa, hatoi mtoto wa kawaida tofauti na Penina aliyekuwa
anazaa watoto wa kawaida tu (quantity); Hana alibeba hatima nzito (quality).
Ndani ya tumbo la Hana kulikuwa kumekwamia Nabii Samueli, na ndani ya Samueli
kulikuwa na wafalme wa Israeli.
Hana alipozidiwa na huzuni ya
kutopata mtoto, hakukimbilia kwa waganga; Hana alimimina roho yake mbele za
Bwana, na Bwana, kupitia mtumishi wake, Eli, alimwambia Hana katika 1
Samueli 1:17 kuwa, "Enenda
kwa Amani; na Mungu wa Israeli akujalie haja yako uliyomwomba." Biblia
inasema katika 1 Samueli 1:20
kuwa wakati ulipowadia, Hana akachukua
mimba, akamzaa mtoto mwanamume, akamwita jina lake Samueli.
Baada ya kumzaa Samueli, Hana
alipata watoto wengine watano, lakini Biblia haiwazungumzii wala haitaji majina
yao (1 Samueli 2:18-21). Mungu
alimchagua Samueli pekee kutoka kwenye tumbo la Hana kwa ajili ya taifa la
Israeli. Samueli akapa kibali kwa Bwana na kwa watu (1 Samueli 2:26). Hana akamtoa Samueli kwa Bwana.
Mungu alimuita Samueli akiwa bado
mtoto mdogo. Ili Mungu anene na mtu, ni lazima mtu huyo aisikie sauti ya Bwana
ikimuita na aitike. Baba wa kiroho wa Samueli alikuwa Eli, lakini Eli hakuwa
akisikia sauti ya Bwana ila alijua namna ya kuitika na alimfundisha Samueli.
Yatupasa kujua namna ya kuitika tutwapo na Mungu. Mungu alipomuita Samueli, Samueli
aliitika kwa kusema, "Nena, Bwana, kwa kuwa mtumishi wako
anasikia." (1 Samueli 3:10).
Baada ya kuitwa na Mungu akaitika,
kuanzia hapo Samweli aliisikia sauti ya Mungu katika maisha yake yote. Mungu
alimtumia kwa mambo mengi kwenye taifa la Israeli. Ukiitwa, ukaitika, Mungu
anakutumia. Bwana aliwaokoa Wana wa Israeli kupitia maombi na sadaka ya
Samueli, wakawashinda Wafilisti kwa radi na ngurumo zilizowasambaratisha (1
Samueli 7:10). Samueli alifanyika kiwanda cha kutengeneza wafalme wa
Israeli; ndani yake kulikuwa na pembe ya mafuta iliyobeba kesho ya Sauli na
Daudi.
Kuna wakati Mungu anaruhusu mtu
apoteze vitu vyake ili amkutanishe na mtu wa hatima yake. Sauli, kijana wa
kabila la Benjamini, alitumwa na baba yake kwenda kutafuta punda waliopotea. Akiwa
amezunguka miji mingi bila kuwapata punda na akakata tamaa na kutaka kurudi
nyumbani, mtumishi wake anamuongoza kukutana na muonaji mwenye kuheshimiwa ili
amuonee punda waliopotea (1 Samueli 9:6).
Imeandikwa
katika 1 Samueli 9:16 kuwa, "Kesho, wakati kama huu,
nitakuletea mtu kutoka nchi ya Benyamini, nawe mtie mafuta ili awe mkuu juu ya
watu wangu Israeli." Hapa tunajifunza kuwa Mungu ndiye aliwapoteza
wale punda wasipatikane kwa siku tatu ili kumpeleka Sauli mbele ya Samueli.
Mungu hutengeneza matukio ili mtu aifikie hatima yake. Siyo kila kupoteza
unakemea shetani; kuna kupoteza ili uipate hatima. Mungu akikuita, anaruhusu
Roho wake awe juu yako; Roho akikushukia unageuzwa na kuwa mtu mwingine kabisa.
Sauli aligeuzwa akawa mpaka mnenaji. Asingepatikana Samueli, Sauli naye
asingepatikana; hatima ya Sauli ilinasa tumboni mwa Hana.
Kukataliwa na Bwana haikuanza
leo. Badae Sauli aliasi na Mungu akamkataa. Mungu akamtuma tena Samueli kwenye
nyumba ya mzee Yese kumpaka mafuta Daudi. Imeandikwa katika 1 Samueli 16:1
kuwa, "Hata lini utamlilia
Sauli, ikiwa mimi nimemkataa asiwamiliki Israeli? Ijaza pembe yako mafuta,
uende, nami nitakupeleka kwa Yese, Mbethlehemi; maana nimejipatia mfalme katika
wanawe."
Baada
ya kukataliwa na Bwana, Sauli alijaribu namna nyingi kujinasua lakini hakuweza;
aliendelea kumchukiza Bwana. Mungu akikukataa, ukijaribu kujiokoa unaharibu
zaidi.
Katika familia ya mzee Yese, Daudi
alikuwa anachunga kondoo, na familia yake haikuona ufalme ndani yake. Kesho ya
Daudi kuwa mfalme ilikuwa imenasa ndani ya pembe ya mafuta aliyokuwa nayo Samueli.
Kuna matukio mengi ya kidunia yanayoweza kumchelewesha mtu kuifikia hatima
yake; hata ndugu ndani ya familia kuna mambo huchelewesha kwa kuangalia sura.
Mungu huangalia moyo ili kumchagua amtakaye. Mungu alimchagua Daudi kwa
kuangalia moyo. Mtu akichaguliwa na Bwana, husubiriwa atoke alikozuiliwa.
Dharau na kufichwa hakuzuii hatima kutimia.
Nyuma ya mafanikio ya Daudi, yupo
Goliati. Ili mtu afanikiwe, lazima apatikane Goliati wa maisha yake. Goliati ni daraja la mafanikio. Baada
ya Daudi kupakwa mafuta kwa siri Bethlehemu, ilibidi atokee Goliati wa kitaifa
ili mafuta ya Daudi yajulikane kitaifa / yadhihirike. Kuna matukio
yanatengenezwa na Mungu siyo yakuue, ila yakufanikishe. Mungu akikubariki hakupi hela, anakupa Goliati; changamoto, vita,
au dhiki anazopitia mtu leo hazijaja kumuua, zimekuja kujenga misuli yake ya
kiroho na kumtambulisha kwenye hatima yake.
Daudi
alimshinda Goliati na mafuta ya Samueli yakadhihirisha ushujaa wake. Pamoja na
laana za Goliati kwa Daudi kwa miungu yake (Dagon), Daudi alimshinda Goliati kwa
Jina la Bwana na kumkata kichwa kwa upanga wa Goliati mwenyewe. Fitina
zilizopangwa na adui zako dhidi yako ndizo zitakuwa silaha zako dhidi ya adui
zako; wageuzie uwashinde.
Vita kubwa unayopitia kwenye
familia yako, biashara yako, au afya yako ni thibitisho kuwa kuna "Kesho
Kubwa" imenasa ndani yako. Wewe ndiye uliyebeba ufunguo wa ukombozi wa
ndugu zako.
Kama vile Eli alivyomwambia Hana,
nami natamka: "Enenda kwa amani,
na Mungu wa Israeli akupe haja ya moyo wako." Kila kilichonasa
kikiwa cha kifedha, kibiashara, au kifamilia kianze kupenya sasa, kwa jina la
Yesu!
Maombi na Baraka za baba Yetu kwetu:
Baba mtakatifu, Muumba wa mbingu na nchi, Mungu
mkuu kuliko miungu yote ya Tanzania! Tazama mwanao ameinua mikono yake juu;
Kesho yake kubwa imenaswa mahali; Kazi yake, biashara yake, afya yake
imeshikiliwa; Kama vile maneno ya Eli Kuhani yalivyomkwamua Hana, nami natamka
leo: Mwanangu, enenda kwa amani! Na Mungu wa Israeli akupe haja ya moyo wako!
Ninaamuru upenyo usiokuwa wa kawaida kwenye maisha yako kuanzia sasa! Ninamwagiza Sauli na majeshi ya giza yaliyojipanga kukuangamiza yasambaratike kwa jina la Yesu! Kila Goliati aliyesimama mbele ya hatima yako aanguke sasa hivi! Kila utendalo kuanzia leo lifanikiwa; kazi imefanikiwa, biashara imefanikiwa, ndoa imefanikiwa, na afya yako inarejea kwa jina la Baba, na la Mwana, na la Roho Mtakatifu! Amina.
BONYEZA HAPA KUANGALIA IBADA YA JUMAPILI


0 Comments