google.com, pub-4324601895065941, DIRECT, f08c47fec0942fa0

Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

ADUI WA NJIA YA HATIMA

UFUFUO NA UZIMA CATHEDRAL
IBADA YA JUMAPILI 06.09.2026
ASKOFU DKT GERSHOM MWAKILA
SOMO: ADUI WA NJIA YA HATIMA 

Kila mwanadamu ana hatima (kusudi) na Mungu ameweka taratibu maalum za kuifikia hatima hiyo; huo utaratibu ndio "Njia". Kila njia ina adui zake. Njia ni Mtu. Njia ya hatima ya masomo, biashara, au mafanikio mara nyingi huwa ni mtu anayetumiwa na Mungu kukuvusha. Hivyo, adui wa hatima ni mtu anayeinuka kukuzuia usifikie kusudi lako.

Yesu ndiye Njia Kuu. Kulingana na Yohana 14:4-6 na Matendo 4:12, Yesu ndiye njia pekee ya kufika kwa Baba; njia nyingine zote za wanadamu kuelekea kwa Mungu zimefungwa. Siyo kila njia ni sahihi kwa kila mtu. Njia iliyo sahihi kwa mtu mmoja inaweza kuwa anguko la mwingine. Mfano: Bahari ya Shamu ilikuwa njia ya wokovu kwa Wana wa Israeli, lakini ikawa njia ya mauti na maangamizi kwa majeshi ya Farao.

Kwakuwa njia ni mtu na adui wa njia ni mtu, kuna maadui na mitego ya njiani:

Kuna njia ya majuto kwa mtu kuielekea hatima yake. Njia hii hutokea kwa namna ambayo watu wanakuja kama wajumbe wa ibilisi wenye sura njema, lakini mwisho wao huacha majuto kwenye kazi, ndoa, biashara au jambo jema la mtu. Muombe Mungu akufunulie kujua kama njia ni salama kwa maana imeandikwa katika Zaburi 139:24 kuwa, “Ukaone kama iko njia ya ubaya ndani yangu, Ukaniongoze katika njia ya milele”.

"Kwa jina la Yesu, mtu yeyote aliyebeba majuto aende mbali na asikaribie biashara zangu, kazi zangu, ndoa yangu, na miradi yangu. Ninamkatilia mbali kwa jina la Yesu!"

Mungu na Shetani Kupitia Watu: Mungu hufungua mambo kupitia mkono wa mtu mwenye nia ya Mungu, na Shetani huharibu, kuloga, au kuleta magonjwa kupitia mtu mwenye nia ya uharibifu. Imeandikwa katika Warumi 8:28 kuwa, “Nasi twajua ya kuwa katika mambo yote Mungu hufanya kazi pamoja na wale wampendao katika kuwapatia mema, yaani, wale walioitwa kwa kusudi lake.”. Kwahiyo, ukikutana na mtu aliyebeba nia ya Mungu, kimsingi umekutana na Mungu katika sura ya mtu, kwa maana Mungu hapendi kuwahuzunisha watu wake (Maombolezo 3:33). Hata hivyo, mara nyingi adui hutoka miongoni mwa watu wa nyumbani (Mika 7:6).

Kwa mantiki hii, mambo ya mtu hufunguliwa na kubarikiwa kwa mkono wa mtu, na mambo ya mtu uharibiwa na kufungwa kwa mkono wa mtu. Ukitaka kusafisha njia yako, anza na wale wanaokuzunguka. Njia za kuingia mautini ni mtu, na njia za kutoka mautini ni mtu pia. Ni imani yetu kuwa njia za kutoka mautini zina Yehova; Bwana amezinyoosha na hajamkabidhi mtu kwa maana anazo mwenyewe.

Sisi tulio na Kristo tunaimani thabiti kuwa mauti siyo mwisho. Tunayo imani ya kuziendea njia za kutoka mautini. Kupitia Roho Mtakatifu aliyemfufua Yesu, ndoa iliyokufa, biashara iliyokufa, miradi iliyokufa, vyote vinahuishwa na kufufuka. Ile roho iliyomtoa Yesu Kristo katika wafu kwa kuhuisha roho yake, ipo kuhuisha roho zetu. Roho hiyo inakaa ndani yetu kama ilivyoandikwa katika Warumi 8:11 kuwa, “Lakini ikiwa Roho wake yeye aliyemfufua Yesu katika wafu anakaa ndani yenu, yeye aliyemfufua Kristo Yesu katika wafu ataihuisha na miili yenu iliyo katika hali ya kufa, kwa Roho wake anayekaa ndani yenu.” Roho ya kuhuisha ikimuingia mtu, inamtoa kwenye mauti ya kila kilichokufa kwenye maisha yake.

"Ikiwa Roho aliyemfufua Kristo kutoka kwa wafu anakaa ndani yangu, ninamuru mwili wangu ulio katika hali ya kufa uhuishwe! Ninatangaza uzima kwenye figo zangu, seli zangu, na ubongo wangu. Ninaamuru biashara yangu iliyokuwa inakufa iamke tena, ndoa yangu iishi tena, na miradi yangu isimame tena, kwa jina la Yesu Kristo!"

Roho ya Amaleki (Unyonge na Uchovu): Amaleki anawakilisha adui anayevizia pale mwanadamu anapochoka au kuonyesha unyonge (Kumbukumbu la Torati 25:17-18). Ukielekea kwenye njia uliyopewa na Bwana, adui huibuka kwenye njia yako ili akuzuie. Adui akiona umechoka, anaibuka ili akumalize. Adui huyu hachapi kiongozi wa mbele, anapiga walio nyuma (wanyonge). Epuka kumuonesha adui yako kuwa umechoka; ulimwengu wa roho hautaki unyonge; kataa maneno kama "nimechoka" au "sisi wanyonge" kwani unyonge huvutia mapigo ya adui badala ya huruma kwa maana imeandikwa katika Ufunuo 21:27 kuwa “Na ndani yake hakitaingia kamwe chochote kilicho kinyonge, wala yeye afanyaye machafuko na uongo, bali wale walioandikwa katika kitabu cha uzima cha Mwana-Kondoo.”

Mungu anasema, yeye aliye dhaifu na aseme “mimi ni hodari (Yoeli 3:10). Ni kanuni ya rohoni kuwa, hata kama umechoka sema “nina nguvu” (Mithali 8:14, 18:21). Sema kinyume na udhaifu wako; Mungu atakutendea sawasawa na neno la kinywa chako (Zaburi 118:17). Adui wa njiani anavizia udhaifu wa mtu ili amuangamize (Ezra 8:31); batilisha maneno yote uliyojinenea udhaifu, kwa damu ya Yesu inenayo mema. Kuna watu wakiwa dhaifu hutia huruma, lakini wana wa Mungu hawapeani pole ila hutiana moyo kwa maneno ya Mungu yanayohuisha nguvu.

"Kwa jina la Yesu, ninafuta kila ukiri wa kinyume niliowahi kuutamka kwa kinywa changu. Ninakataa lugha ya unyonge na uchovu. Hata kama nilikuwa dhaifu, ninasema mimi ni hodari na nina nguvu! Nguvu ya Amaleki ya kunivizia kwenye uchovu wangu ninaitengulia sasa hivi, kwa jina la Yesu!"

Walinzi Wakali na Fomula za Kifamilia: Mamlaka za giza huweka walinzi wakali ili kuzuia na kuchepusha njia ya ustawi (Mathayo 8:28). Mtu aviziaye / anyemeleaye, haji waziwazi; Mungu humzuia yeye aviziaye. Elisha alimuokoa mfalme wa Israeli mara nyingi alipoviziwa na adui njiani. Adui hutengeneza fomula ya kumfunga mtu na kumuangusha kupitia vizazi hata vizazi. Mfano, kuwa na magonjwa ya kufanana, vifo vya kufanana na ukomo wa umri unaofanana. Adui awekapo fomula hiyo, njia za kuelekea mafanikio hulindwa sana na mamlaka za rohoni ili mtu asiendee wala asione. Zipo dalili zinazoashiria mtu analindwa sana, mfano ni kuwa na wasiwasi wa kuanza jambo kama biashara.

Kuelekea nchi ya Wagerasi, Yesu alipita kwa sababu njia zina yeye. Sisi tunamtanguliza Yesu; akipita na sisi tunapita. Vaa nia ya kupita kwenye njia; achia Upanga wa roho kuwafyeka walinzi wote wa njiani waondoke kwenye njia.

"Ninatoa upanga wa Roho kinyume na walinzi wote wakali waliokaa kwenye njia ya ustawi wangu, ndoa yangu, na promotion yangu. Ninawafyeka wote kwa jina la Yesu! Ninabatilisha kila mtego wa hasara, umaskini, kifo, au ajali uliotegwa njiani mwangu. Mitego hiyo ninairudisha kwa adui, wazame wao kwenye mashimo waliyochimba kwa jina la Yesu!"

Kufichwa, Kuzuiliwa, na Kupindishwa kwa Njia:

Njia ya mtu inaweza kufichwa (Isaya 40:27). Njia ni mtu; mtu akifichwa usionane naye, huwezi ukafika kule unatakiwa uende.

Njia inaweza ikazuiliwa (Warumi 1:13). Njia ni mtu; mtu anaweza akazuiliwa na mtu / watu wenye nia ya shetani. Mtume Paulo alijaribu mara nyingi kwenda Rumi kueneza injili lakini shetani akawa akizuia asiende. Kuzuiliwa kwa Paulo ni kuzuia hatima ya Warumi wengi ambao Paulo, kwa neno la Mungu, angewasaidia kufikia hatima zao.

Njia ya mtu inaweza ikapindishwa; Mungu anapoandaa hatima, anaandaa na namna ya mtu kuifikia hatima hiyo. Mafanikio ya mtu yapo kwenye hatima yake. Walimwengu huingilia njia ya mtu kuelekea mafanikio. Mtu hujikuta anapambana sana lakini hafiki kwa sababu ya hao walimwengu.

Njia za Mungu zimenyooka sana lakini wachawi, wenye kujaa hila, wana wa uovu wote, adui wa haki yote, wana wa Ibilisi na manabii wa uongo huzipindisha, na matokeo yake mtu hupambana sana kujishughulisha na hafikii mafanikio (Matendo ya mitume 13:6-10). Kama wapindishaji wasingekuwepo, mafanikio yangepatikana bila kupambana kwa maana njia za Bwana zimenyooka.

BONYEZA HAPA KUANGALIA IBADA YA JUMAPILI

Post a Comment

0 Comments