google.com, pub-4324601895065941, DIRECT, f08c47fec0942fa0

Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

KARAMA YA MUNGU HAINA MAJUTO – SEHEMU YA TATU

UFUFUO NA UZIMA CATHEDRAL
IBADA YA JUMAPILI 08.09.2024
ASKOFU DKT JOSEPHAT GWAJIMA
SOMO: KARAMA YA MUNGU HAINA MAJUTO – SEHEMU YA TATU

Mungu akikupa karama hakuna mwanadamu wa kuiondoa, akikupa amekupa. Shetani aliposhushwa kutoka Mbinguni, alishushwa na karama zake alizopewa ikionyesha kuwa Mungu akikushusha, karama na vipawa vyako vinabaki vilevile hakuna wa kukunyang’anya. 

“Fahari yako imeshushwa hata kuzimu, Na sauti ya vinanda vyako; Funza wametandazwa chini yako,Na vidudu vinakufunika.” Isaya 14:11

“Ulikuwa ndani ya Adeni, bustani ya Mungu; kila jiwe la thamani lilikuwa kifuniko chako, akiki, na yakuti manjano, na almasi, na zabarajadi, na shohamu, na yaspi, na yakuti samawi, na zumaridi, na baharamani, na dhahabu; kazi ya matari yako na filimbi zako ilikuwa ndani yako; katika siku ya kuumbwa kwako zilitengenezwa tayari.” Ezekieli 28:13

Mungu akikupa karama hawezi kukunyang’anya, hata kama unaitumia kwenye mambo mengine yasiyo ya ufalme wake. 

“Kwa sababu karama za Mungu hazina majuto, wala mwito wake” Warumi 11:29 

Biblia ya kiingereza inasema,

“For God’s gifts and his call can never be withdrawn.” Romans 11:29

Mungu akikupa kipawa hakuna mtu wa kuchukua kipawa hicho.

Wapo watu pia ambao wamepewa karama na Mungu, wanadhani hali yao ya sasa ya maisha itaamua mwisho wao. Lakini wito na karama upo pale pale, haufutiki.

Kuna watu ambao hawajakusudiwa na Mungu tangu kuwekwa kwa misingi ya ulimwengu, hawa ndio wale wana wa Ibilisi.

“Yule mnyama uliyemwona alikuwako, naye hayuko, naye yu tayari kupanda kutoka kuzimu na kwenda kwenye uharibifu. Na hao wakaao juu ya nchi, wasioandikwa majina yao katika kitabu cha uzima tangu kuwekwa misingi ya ulimwengu, watastaajabu wamwonapo yule mnyama, ya kwamba alikuwako, naye hayuko, naye atakuwako.” Ufunuo wa Yohana 17:8

Mungu anawatu wake aliowachagua duniani kabla hawajazaliwa na alivyowashusha walikuja na vipawa vyao kwa ajili ya kufanya kazi maalumu walioagizwa hapa duniani.

“Atukuzwe Mungu, Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, aliyetubariki kwa baraka zote za rohoni, katika ulimwengu wa roho, ndani yake Kristo; kama vile alivyotuchagua katika yeye kabla ya kuwekwa misingi ya ulimwengu, ili tuwe watakatifu, watu wasio na hatia mbele zake katika pendo.” Waefeso 1:3-4

Ni vizuri kutenda matendo mema ili kukukaa kwenye kusudi ambalo Mungu kakuitia ila pia lazima umwamini Yesu. Lakini kusudi la Mungu la kuchagua halipo kwenye wema au ubaya wa mtu anaoufanya.

“(kwa maana kabla hawajazaliwa wale watoto, wala hawajatenda neno jema wala baya, ili lisimame kusudi la Mungu la kuchagua, si kwa sababu ya matendo, bali kwa sababu ya nia yake aitaye),” Warumi 9:11

Mungu alikujua tangu asili yani yule wa ndani ambaye ni wa milele. Wewe ulikuwepo hata kabla misingi ya dunia haijawekwa. Asili yako sio dunia hii bali mbinguni kwa aliyeweka karama hio ndani yako.

Maana wale aliowajua tangu asili, aliwachagua tangu asili wafananishwe na mfano wa Mwana wake, ili yeye awe mzaliwa wa kwanza miongoni mwa ndugu wengi. Warumi 8:29

Kama vile Yesu amekuwepo kabla ya vyote, wewe pia ulikuwepo kabla ya vyote. Mungu alikuleta duniani ili uungane na wenzio wenye makusudi yanayofanana ili mfanye kazi maalumu mliopewa. 

“naye ni mfano wa Mungu asiyeonekana, mzaliwa wa kwanza wa viumbe vyote. Kwa kuwa katika yeye vitu vyote viliumbwa, vilivyo mbinguni na vilivyo juu ya nchi, vinavyoonekana na visivyoonekana; ikiwa ni vitu vya enzi, au usultani, au enzi, au mamlaka; vitu vyote viliumbwa kwa njia yake, na kwa ajili yake. Naye amekuwako kabla ya vitu vyote, na vitu vyote hushikana katika yeye.” Wakolosai 1:15-17

Wa nje anakula chakula, anachoka na mavumbini atarudi. Mtu wa nje ni wa udongo na unaweza kufanana na wazazi wake waliomzaa. Mwana wa Mungu ni yule wa ndani ambaye ni roho na huyo ndio wewe sio yule wa nje. 

Mtu wa kwanza atoka katika nchi, ni wa udongo. Mtu wa pili atoka mbinguni. Kama alivyo yeye wa udongo, ndivyo walivyo walio wa udongo; na kama alivyo yeye wa mbinguni, ndivyo walivyo walio wa mbinguni. 1 Wakorintho 15:47-48

Yesu alipomjibu shetani kuwa mtu hataishi kwa mkate alimaanisha mtu wa pili ambaye ni roho hatishi kwa mkate sio mtu wa kwanza ambaye ni udongo.

“Naye akajibu akasema, Imeandikwa, Mtu hataishi kwa mkate tu, ila kwa kila neno litokalo katika kinywa cha Mungu.” Mathayo 4:4

Wewe ni mtu mwenye mwili yaani wewe sio mwili. Anayeongozwa na roho yaani wa ndani yako anakuwa na nguvu zaidi maana wa ndani halali, hasinzii wala haoni njaa.

“Tena kuna miili ya mbinguni, na miili ya duniani; lakini fahari yake ile ya mbinguni ni mbali, na fahari yake ile ya duniani ni mbali.” 1 Wakorintho 15:40

Mungu anapokuleta duniani anakuwekea karama, wito na vipawa ili afanye kazi kupitia wewe yaani unafanya kwa niaba ya Mungu. Kwa hilo uliloitiwa huwezi kushindwa maana ni Mungu anafanya kazi kutimiza kusudi lake alilokuletea duniani.

Yale magumu na majangwa unayopitia leo yameandaliwa na Mungu ili kukuandaa na kukufundisha jinsi ya kupita kwenye majangwa na changamoto za maisha.

Wito ulioitiwa na Bwana hauwezi kubadilishwa kamwe, lazima uwe vile Mungu amekupangia. Hata kama umeenda mbali Mungu atakurudisha kwenye njia ikupasayo kuiendea na nguvu na karama zako zile zile.

Lipo kusudi lako ambalo Bwana amekuitia na atawaondoa wengine wasiostahili ili wewe upenye. Shetani mwenyewe hakunyang’anywa vipawa, basi hata wewe ile karama uliyopewa ipo pale pale, yale matukio yanayokupata yanakuwa yanakutengeneza.

Karama ambayo Mungu aliweka ndani yako haibadilishwi wala haiozi hadi kusudi la Mungu litimie kwenye maisha yako AMEN.

"BONYEZA HAPA KUANGALIA IBADA NZIMA YA JUMAPILI"

Post a Comment

0 Comments