UFUFUO NA UZIMA CATHEDRAL
IBADA YA JUMAPILI 01.12.2024
ASKOFU DKT JOSEPHAT GWAJIMA
SOMO:
WAKATI WAKO UMETIMIA
Mungu huwa anawaandaa watu kwa muda mrefu sana kwa ajili ya jukumu fulani ambalo linaweza kuwa la muda mfupi tu. Kila mtu kuna siku utakufa, Kifo ni nini? ni pale ganda la nje (mwili) linarudi mavumbini na wewe unamrudia Mungu aliyekutuma.
“Nayo mavumbi kuirudia nchi kama
yalivyokuwa, Nayo roho kumrudia Mungu aliyeitoa.” Mhubiri 12:7
Mara nyingi kwenye mazishi huzuni hutokana na kufikiria
yule mliyekuwa mnamuona ameondoka na kufukiwa. Wewe ulitoka mbinguni na hio ndio
asili yako umetoka kwa Mungu.
Kila mtu ana jukumu alilopewa na Mungu kutimiza
duniani, iwe siasa, tiba, uhandisi, biashara nk. Kazi ya shule ni kuendeleza
ufahamu, kipaji na karama ya mtu aliyopewa na Mungu.
Kwenye maisha ya mwanadamu Mungu huleta muda wa
maandalizi, maandalizi haya humjenga mtu kwa matukio mbalimbali ili kufanya
lile shauri aliloitiwa duniani kutimiza.
Yesu alivyokuja alikuja kwa jukumu la kutuokoa sisi
na dhambi zetu lakini maandalizi ya jukumu hilo yalikuwa ya muda mrefu. Jina
Yesu aliitwa na wazazi wake waliomsikia malaika kuwa ataitwa Yesu.
“Tazama, utachukua mimba na kuzaa
mtoto mwanamume; na jina lake utamwita Yesu.” Luka 1:33
Ili kujua namna Maisha ya mtu yanaweza kuwa na
maandalizi ya muda mrefu, tutamuangalia Bwana wetu Yesu. Tunaanza kumuona Yesu
akiwa na umri wa siku nane (8).
“Hata zilipotumia siku nane za
kumtahiri, aliitwa jina lake Yesu; kama alivyoitwa na malaika kabla
hajachukuliwa mimba. Kisha, zilipotimia
siku za kutakasika kwao, kama ilivyo torati ya Musa walikwenda naye hata
Yerusalemu, wamweke kwa Bwana.” Luka 2:21-22
Yesu alikuwa ameitwa kwenye na uchanga wake huo wa
umri wa siku nane.
Tunakuja kumona tena akiwa na umri wa miaka kumi na
miwili (12). Kutoka umri wa siku nane (8) hadi miaka kumi na miwili (12)
hatuoni anafanya nini, hii inaonyesha alikuwa ni mtu wa kawaida anaishi maisha
ya kawaida japo ni Mungu. Hutaona anaponya watu wala kuhubiri neno, hata hio
haikuweza kuondoa Uungu wake. Kwenye umri huu wa miaka kumi na miwili (12)
alishakuwa na ufahamu wa kujua nyumba ya Baba yake, maarifa ya kujua kuwa yeye
ni mwana wa Mungu.
Kile kitendo cha Yesu kutii wakubwa wake inaonyesha
hakuwa mtukutu au mjuaji japo alikuwa ni Mungu.
Baada ya miaka kumi na miwili (12) akaja kuibuka
tena akiwa na umri wa miaka thelathini (30) akaanza kuhubiri. Hapo katikati kutoka
umri wa miaka kumi na miwili (12) hadi thelathini (30) hatujui alikuwa anafanya nini tena.
Hii yote inaoonyesha miaka yote hio alikuwa
anaandaliwa tu, na hilo jukumu lenyewe akaja kulifanya kwa muda wa miaka mitatu
na nusu tu akaenda mbinguni.
“Na Yesu mwenyewe, alipoanza
kufundisha, alikuwa amepata umri wake kama miaka thelathini, akidhaniwa kuwa ni
mwana wa Yusufu, wa Eli..” Luka 3:23
Sasa swali ni, Je umri huo ambao Yesu hakuwa anajulikani
alikuwa anafanya nini, alikuwa anafanya nini? Biblia inasema alikuwa seremala,
watu walimfahamu ni jamaa wa kawaida tu aliyekuwa mtoto wa seremala na kuna
wengine aliwachongea meza, makochi nk.
“Akatoka huko, akafika mpaka nchi
ya kwao; wanafunzi wake wakamfuata. Na ilipokuwa sabato, alianza
kufundisha katika sinagogi; wengi waliposikia wakashangaa, wakisema, Huyu
ameyapata wapi haya? Na, Ni hekima gani hii aliyopewa huyu? Na, Ni nini miujiza
hii mikubwa inayotendeka kwa mikono yake? Huyu si yule seremala, mwana wa
Mariamu, na ndugu yao Yakobo, na Yose, na Yuda, na Simoni? Na maumbu yake
hawapo hapa petu? Wakajikwaa kwake.” Marko 6:1-3
Watu wakawa wanajiulizza hii miujiza na hekima
imetoka wapi. Watu walimjua Yesu tangu akiwa mtoto, familia yake na maisha ya
kawaida aliyoishi. Wakawa hawaamini kama atakuwa ndiye yule aliyemtabiri nabii
Isaya miaka mia saba (700) kabla.
“Na alipofika nchi yake,
akawafundisha katika sinagogi lao, hata wakashangaa, wakasema, Huyu amepata
wapi hekima hii na miujiza hii? Huyu si mwana wa seremala? Mamaye si yeye
aitwaye Mariamu? Na nduguze si Yakobo, na Yusufu, na Simoni, na Yuda? Na
maumbu yake wote hawapo hapa petu? Basi huyu amepata wapi haya yote? Wakachukizwa
naye. Yesu akawaambia, Nabii hakosi kupata heshima, isipokuwa katika nchi yake,
na nyumbani mwake mwenyewe. Wala hakufanya miujiza mingi huko, kwa sababu
ya kutokuamini kwao.” Mathayo 13:54-58.
Kuna sehemu mpaka ukazuka ugomvi kwamba kwanini watu
wanamsikiliza Yesu aliye na mapepo tena ana wazimu. Haya yote yalikuwa kwa
sababu Yesu hakufanania yule waliyemsubiri tangu kipindi cha nabii Isaya. Hii
inaonyesha kuwa kwenye maandalizi kwa ajili ya kusudi alilokupa Mungu kuna
kuitwa majina ya ajabu na watu.
“Kukaingia tena matengano kati ya
Wayahudi, kwa ajili ya maneno hayo. Wengi wao wakasema, Ana pepo huyu,
tena ana wazimu; mbona mnamsikiliza?” Yohana 10:19-20
Nabii Isaya alitabiri kuja kwa Yesu duniani miaka mia
saba (700) kabla hajaja duniani.
“Maana kwa ajili yetu mtoto
amezaliwa, Tumepewa mtoto mwanamume; Na uweza wa kifalme utakuwa begani mwake; Naye
ataitwa jina lake, Mshauri wa ajabu, Mungu mwenye nguvu, Baba wa milele, Mfalme
wa amani.” Isaya 9:6
Isaya alitabiri kana kwamba lile jambo limekwisha
tokea. Isaya alisema kwa maana mtoto amezaliwa wakati Yesu alikuwa bado
hajazaliwa. Isaya aliona mpaka wa kumtengenezea njia yaani Yohana.
“Sikiliza, ni sauti ya mtu aliaye, Itengenezeni
nyikani njia ya BWANA; Nyosheni jangwani njia kuu kwa Mungu wetu.” Isaya 40:3
Mungu anavyoona siku za tukio fulani zinazidi kukaribia
huwa anawaonyesha watu wake. Kuna watu wenyewe wito wao ni kusikia kutoka kwa
Bwana.
“Hakika Bwana MUNGU hatafanya neno
lo lote, bila kuwafunulia watumishi wake manabii siri yake.” Amosi 3:7
Kabla ya Yesu kuzaliwa kuna watu ambao kwa hakika
walijua kuwa yeye ni mwana wa Mungu, aliyekuja kuwaokoa wanadamu.
Wanaume
wanne waliojua kwa hakika muda atakao kuja Yesu mwana wa Mungu duniani.
1. Mzee Simeoni, aliandaliwa na Mungu asife mpaka
amuone aliyetabiriwa na nabii Isaya. Luka
2:25 Huyu mzee alijua kwa hakika hataweza kufa mpaka atakapomuona Yesu.
2. Yusufu. Yusufu alijua mpaka miezi ambapo masihi ataingia
duniani. Miriamu alibeba mimba kwa uweza wa roho mtakatifu, alijua kwa hakika
Mungu anatokea nyumbani kwake.
3. Yohana Mbatizaji. Yohana alijua kwa maana
alitumwa kutengeneza njia ya mtu, alipoona kuna kijana anasogea kwenye maji ili
abatizwe akajua tu kuwa yule ndiye.
4. Zacharia baba wa Yohana Mbatizaji. Alijuaje? kwa
maana mtoto wake Yohana alizaliwa ili aitengeneze njia ya Bwana yaani nitakaye
mzaa anakuja kwa ajili ya Bwana. Nikimuona mtengeneza njia nimemuona Bwana.
Wanawake
watatu waliojua kwa hakika muda atakao kuja Yesu mwana wa Mungu duniani.
1. Maria mama wa Yesu. Alijua kuwa kabeba ujauzito
wa Yesu aliye mwana wa Mungu, Bwana wetu.
2. Elizabeth mama wa Yohana mbatizaji.
3. Anna binti Fanueli. Luka 2:36 mtoto Yesu alipoingia ndani ya hekalu akajua
aliyeingia ndio masihi.
Hii yote inatuambia nini? kuna watu wametengwa na Mungu kuhusu mambo fulani na hawatakufa mpaka watimize hilo kusudi duniani.
0 Comments