google.com, pub-4324601895065941, DIRECT, f08c47fec0942fa0

Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

TATIZO NDANI YA TATIZO

 

UFUFUO NA UZIMA CATHEDRAL
IBADA YA JUMAPILI 08.02.2026
ASKOFU DKT GERSHOM MWAKILA
SOMO: TATIZO NDANI YA TATIZO

Watu wengi wamezungukwa na matatizo ya aina mbalimbali kama vile matatizo ya kibiashara, ndoa, kazi na mengine mengi. Kwa mfano, kuna mtu ana ndoa lakini bado anakabiliwa na matatizo, na kuna mwingine hana ndoa lakini pia ana matatizo. Hii inaonesha kuwa kila mtu ana changamoto zake, ingawa hutofautiana kulingana na sababu na mazingira ya kila mmoja.

Mtu anapokuwa na tatizo, asipokubali uwepo wa tatizo hilo, linaweza kuzaa tatizo lingine kubwa zaidi. Mfano wake ni Adamu na Hawa. Walipokula tunda walilokatazwa na Mungu, na walipohojiwa hawakukubali makosa yao bali walianza kujitetea. Kutokana na kosa hilo, walijificha mbali na uso wa Mungu, jambo lililosababisha laana juu yao. Hii inaonesha kuwa kutokukubali kosa ni chanzo cha matatizo makubwa zaidi.

kasema, Nalisikia sauti yako bustanini, nikaogopa kwa kuwa mimi ni uchi; nikajificha. Akasema, Ni nani aliyekuambia ya kuwa u uchi? Je! Umekula wewe matunda ya mti niliyokuagiza usiyale? Adamu akasema, Huyo mwanamke uliyenipa awe pamoja nami ndiye aliyenipa matunda ya mti huo, nikala. 13BWANA Mungu akamwambia mwanamke, Nini hili ulilolifanya? Mwanamke akasema, Nyoka alinidanganya, nikala. BWANA Mungu akamwambia nyoka, Kwa sababu umeyafanya hayo, umelaaniwa wewe kuliko wanyama wote, na kuliko hayawani wote walioko mwituni; kwa tumbo utakwenda, na mavumbi utakula siku zote za maisha yako; Mwanzo 3:10-14

Kila mtu ana tatizo moja au zaidi. Matatizo yenyewe siyo shida kubwa sana; bali maamuzi ya namna ya kulishughulikia tatizo hilo ndiyo jambo la msingi. Maamuzi hayo huamua kama tatizo litapata suluhisho au litazaa tatizo jingine.

Katika matatizo yako, Mungu anaweza kukuonesha njia na kukupa maelekezo ya jinsi ya kulitatua. Hata hivyo, uamuzi wa kutekeleza au kutotekeleza unabaki kuwa wa kwako.

Katika Biblia, Kaini alitoa sadaka ya mazao yasiyompendeza Mungu, na Mungu hakuipokea sadaka yake. Mungu akamwonya kwa kumwambia, “Dhambi inakuotea mlangoni; yapasa uishinde.” Lakini Kaini hakuitii sauti ya Mungu. Matokeo yake, tatizo hilo likazaa tatizo jingine kubwa zaidi la kumuua ndugu yake Abeli, na baadaye akasema uongo mbele za Mungu. Hivyo, tatizo lisipotatuliwa kwa mwongozo wa Mungu, huzalisha matatizo mengine makubwa zaidi.

“Kama ukitenda vyema, hutapata kibali? Usipotenda vyema dhambi iko, inakuotea mlangoni, nayo inakutamani wewe, walakini yapasa uishinde.” Mwanzo 4:7

Nyuma ya kila tatizo la mtu kuna chanzo chake. Laana ni maneno mabaya anayosemewa mtu, iwe ni kutoka kwa mtu mwingine au kama hukumu ya Mungu. Vivyo hivyo, baraka ni maneno mema anayosemewa mtu na Mungu au mtu mwenye mamlaka ya kiroho. Baraka humfanya mtu astawi na kumiliki.

Laana halali huwa na madhara makubwa, na inaweza kusababisha umasikini, mauti, kukataliwa, magonjwa, pamoja na kupata na kupoteza mara kwa mara.

Moja ya sababu zinazoweza kumfanya mtu asifanikiwe ni athari ya maneno mabaya aliyotamkiwa. Maneno yana uzito wa kiroho, hivyo ili kushughulikia maneno ni lazima kushughulikia kwa njia ya rohoni. Watu wengi huamini katika uchawi kwa sababu wanaamini kuwa uchawi unafanya kazi katika ulimwengu wa roho. Shetani anapotaka mtu asipone au asifunguliwe, huteteresha imani yake ili asiweze kuamini katika nguvu za Mungu.

Mungu amemuumba mwanadamu ategemee msaada kutoka katika ulimwengu wa roho. Roho ikiwa katika hali njema, mambo mengine ya maisha kama biashara, afya na ustawi pia huenda vizuri.

Hata hivyo, Mungu anahitaji uamuzi wako ili aweze kukutendea. Maamuzi yako ndiyo huamua tatizo lako litapata tiba gani. Ukichagua kumruhusu Mungu ashughulikie tatizo lako, utapata uponyaji na ufumbuzi.

Kuamini uchawi na ushirikina kunaweza kumwingiza mtu katika vifungo na laana. Laana inaweza kusababisha kushindwa kumiliki, kutostawi, kutofanikiwa, pamoja na kupata magonjwa na mikosi. Ni muhimu kuacha kutegemea uchawi na unganga, na badala yake kumtegemea Mungu, ili upate baraka katika kila eneo la maisha yako.

Post a Comment

0 Comments