google.com, pub-4324601895065941, DIRECT, f08c47fec0942fa0

Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

HATUNA CHA KUPOTEZA

UFUFUO NA UZIMA CATHEDRAL
IBADA YA JUMAPILI 15.02.2026
PASTOR YOHANA MAGINGA
SOMO: HATUNA CHA KUPOTEZA


Mungu hutenda kazi kupitia wanadamu ili kutimiza kusudi lake hapa duniani. Kwa hiyo, usimdharau mtu yeyote kwa sababu ya mwonekano wake, maana Mungu anaweza kumtumia mtu yeyote kutekeleza mapenzi yake. Mara nyingi Mungu huchagua watu wanaoonekana kuwa dhaifu au wasiothaminiwa ili kuonesha ukuu wa nguvu zake.

Katika andiko la Wafalme wa pili tunaona jinsi Mungu alivyowatumia wakoma wanne kuikomboa Samaria kutoka katika njaa kali. Ingawa walionekana hawafai na walitengwa na jamii, Mungu aliwatumia kuwa chombo cha wokovu kwa taifa zima. Hili linatufundisha tusijidharau wala kuwadharau wengine, kwa kuwa kila mtu anaweza kutumiwa na Mungu kwa wakati alioupanga ili kusudi lake litimie.

Tukisema, Tutaingia mjini, mjini mna njaa, nasi tutakufa humo; nasi tukikaa hapa, tutakufa vile vile. Haya! Twende tukaliendee jeshi la Washami; wakituhifadhi hai tutaishi; wakituua, tutakufa tu. Basi wakaondoka kabla ya mapambazuko, ili waende mpaka kituo cha Washami; na walipofika mwanzo wa kimo cha Washami, kumbe! Hapana mtu. Kwa maana Bwana alikuwa amewasikizisha Washami kishindo cha miendo ya magari, na kishindo cha farasi, kama kishindo cha jeshi kubwa; wakaambiana, Tazama, mfalme wa Israeli amewaajiri wafalme wa Wahiti, na wafalme wa Wamisri, waje wapigane nasi. 7Kwa hiyo wakaondoka, wakakimbia kungali giza bado, wakaziacha hema zao, na farasi zao, na punda zao, na kimo chao vile vile kama kilivyokuwa, wakakimbia wapate kujiponya nafsi zao. Basi wale wenye ukoma walipofika mwisho wa kituo, waliingia katika hema moja, wakala, na kunywa, wakachukua fedha, na dhahabu, na mavazi, wakaenda wakavificha; wakarudi, wakaingia katika hema ya pili, vile vile wakachukua vitu, wakaenda, wakavificha.” 2 wafalme 7:5-8

Imani ndiyo msingi wa kutimiza kusudi la Mungu. Mtu asipoamini neno la Mungu, hawezi kupokea yale aliyopangiwa katika mpango wake. Kile kinachomkwamisha mtu mara nyingi si ukosefu wa baraka, bali ni ukosefu wa imani. Usipoitanguliza imani, hutaweza kupata kile unachokihitaji maishani, ilhali Mungu anayajua mahitaji ya kila mmoja.

Ulipomkubali Yesu Kristo kuwa Bwana na Mwokozi wa maisha yako, uliingia katika familia ya Mungu na ukaitwa Mwana wa Mungu. Kwa kuwa mali na vyote vilivyomo ni vya Mungu, inakupasa kuwa na mawazo na mtazamo chanya. Maneno mema uyasemayo kwa imani hujenga msingi katika ulimwengu wa roho, na baadaye matokeo yake hudhihirika katika maisha yako.

Maandiko yanatufundisha kwamba Mungu anaweza kufanya mambo makuu kuliko yote tuyaombayo au kuyawaza, kwa kadiri ya nguvu itendayo kazi ndani yetu. Vilevile, pasipo imani haiwezekani kumpendeza Mungu. Hivyo, imani ni sharti la kupokea ahadi na baraka zake.

Hauhitaji kumtafuta Mungu kana kwamba yuko mbali, kwa maana anaishi ndani ya wale waliomwamini. Ushuhuda wa mambo uliyoyapata ni uthibitisho kwamba Mungu yupo na anatenda kazi ndani yako. Usimdharau mtu yeyote kwa sababu ya hali yake, kwa kuwa mwisho wa kila jambo anaujua Mungu pekee.

Kila baraka ina kiwango na wakati wake. Mungu hufungua mlango ambao hakuna awezaye kuufunga. Kwa hiyo, uwe mwaminifu katika kutimiza ahadi zako kwa Mungu, naye atakuwa mwaminifu katika kukubariki kulingana na mapenzi yake.

BONYEZA HAPA KUANGALIA IBADA YA JUMAPILI

 

Post a Comment

0 Comments