google.com, pub-4324601895065941, DIRECT, f08c47fec0942fa0

Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MATUKIO KATIKA DAMU KWENYE FAMILIA

UFUFUO NA UZIMA CATHEDRAL
IBADA YA JUMAPILI 29.03.2026
ASKOFU DKT GERSHOM MWAKILA
SOMO: MATUKIO KATIKA DAMU KWENYE FAMILIA


Familia ni muhimu sana katika taifa kwa sababu shetani akitaka kupiga taifa anaanza kwa kupiga familia; hivyo, ukitaka kuponya taifa lolote unatakiwa kuponya familia maana familia huleta taifa. Familia ikiwa na watu masikini hata taifa linakuwa masikini. Familia zikitajirika na taifa linatajirika.

Familia ni kundi dogo ndani ya jamii ambalo linatengeneza ukoo. Familia tofauti za damu moja zinatengeneza ukoo, na koo tofauti tofauti zikikusanyika zinatengeneza makabila ambayo kwa pamoja tunapata taifa.

Kila familia ina roho za familia ambazo zinaweza kufanana au kutofautiana kati ya famila moja na familia nyingine. Mfano wa roho za familia ni; roho za kukosa ndoa, roho za ugomvi, roho za damu, n.k. kuna wataalamu kabisa wanaojihusisha na damu katika familia.

Kuna familia ambazo, kwa sababu ya roho ya damu, hawajawahi kumiliki mali au kushika nafasi yoyote ya uongozi, hata ile ndogo kabisa katika jamii. Damu husafiri kutoka uzao mmoja hadi uzao mwingine ndani ya familia, vivyo hivyo matukio yanayoambatana na damu, mfano magonjwa.

Kuna matukio ndani ya familia ambayo yanawafuatilia wanafamilia. Matukio hayo yamezungumziwa katika Biblia Takatifu na katika vyanzo vya kisayansi.

Sayansi inasema kuna mambo hutoka kwa wazazi na kurithiwa na watoto, kwa mfano, rangi ya ngozi, kimo cha mtu, unene/wembamba wa mtu, tabia, n.k. Mambo haya yote husafiri kwa njia ya damu.

Damu ina seli na ute ute. Damu ina vitu visivyoonekana ambavyo kitaalamu vinaitwa vinasaba (DNA). Vinasaba ni visafirishaji vya matukio kutoka uzao mmoja kwenda uzao mwingine. Mambo yote yaliyotajwa juu yanarithishwa kwa njia ya vinasaba. Hivyo sayansi inakubaliana sawa na Biblia kuwa mtoto anaweza kurithi tabia kutoka kwa mzazi.

 “Baba zetu walitenda dhambi hata hawako; Na sisi tumeyachukua maovu yao.” Maombolezo 5:7

-      Neno hili linatufundisha kuwa watoto wanabeba maovu ya dhambi za wazazi wao.

 “Nanyi mfahamu kwamba mlikombolewa si kwa vitu viharibikavyo, kwa fedha au dhahabu; mpate kutoka katika mwenendo wenu usiofaa mlioupokea kwa baba zenu;” 1Petro 1:18

-      Watoto hupokea mwenendo kutoka kwa wazazi wao. Mwenendo ni tabia.

Matukio ya ukoo huwafuata wanaukoo kimya kimya kupitia damu. Mfano, mwenendo, muonekano na aina ya maisha wanayopitia wanaukoo kutoka kizazi hadi kizazi.

Matukio Ambayo Biblia Imeyasema Yamesafiri Kupitia Damu:

Biblia imetaja matukio mengi katika koo tofauti tofauti ambayo yamesafiri kutoka uzao mmoja hadi uzao mwingine.

1.    Tukio la uongo ndani ya familia.

i)             Familia ya Ibrahimu (Baba wa Imani)

Matukio katika familia ya Ibrahimu ambayo yanatajwa ni; alioa mwanamke mzuri, hofu na uongo.

“Basi kulikuwa njaa katika nchi ile; Abramu akashuka Misri, akae huko kwa muda maana njaa ilikuwa nzito katika nchi. Ikawa alipokuwa karibu kuingia Misri, akamwambia Sarai mkewe, Tazama, najua ya kuwa u mwanamke mzuri wa uso; basi itakuwa, Wamisri watakapokuona watasema, Huyu ni mkewe; kisha wataniua mimi na wewe watakuacha hai. Tafadhali useme, wewe u ndugu yangu, iwe heri kwangu kwa ajili yako, na nafsi yangu iishi kwa ajili yako.” Mwanzo 12: 10-13

Matukio ya Ibrahimu; -

-      Alipungukiwa chakula na kwenda kutafuta,

-      Ibrahimu alitambua kuwa mkewe Sara ni mzuri,

-      Ibrahimu aliingiwa hofu ya kuuawa,

-      Ibrahimu akaingia kwenye kudanganya (kusema uongo)

-      Uongo aliosema Ibrahimu ukasajiliwa kwenye damu ya Ibrahimu.

ii)            Isaka mtoto wa Ibrahimu

Kama ilivyokuwa kwa baba yake, Isaka naye alipitia matukio yale yaliyosajiliwa kwenye damu ya Ibrahimu.

“Isaka akakaa katika Gerari. 7Watu wa mahali hapo wakamwuliza habari za mkewe. Akasema, Ni ndugu yangu huyu maana aliogopa kusema, Ni mke wangu, watu wa nchi wasije wakamwua kwa ajili ya Rebeka; kwa maana alikuwa mzuri wa uso.” Mwanzo 26: 6-7

Matukio ya Isaka; -

-      Alimuoa Rebeka aliyekuwa mzuri,

-      Hakuwa na chakula akaenda kutafuta Gerari,

-      Aliingiwa na hofu ya kuuawa,

-      Alisema uongo kama baba yake kuwa Rebeka ni ndugu yake

Mfano katika maisha yetu; -

Kuna wakati mwanandoa anakuwa na mgogoro wa ndoa na mwenza wake kuhusu tabia fulani inayomlazimu kushitaki kwa wakwe zake bila kufahamu kuwa tabia husika imesafiri kwa njia ya damu kutoka kwa baba/mama mkwe wake kwenda kwa mwenza wake. Mara nyingi migogoro hiyo hukosa ufumbuzi.

iii)          Esau na Yakobo, Watoto wa Isaka.

Kwa Kadiri tabia inavyozidi kurithishwa ndivyo inaimarika na kuwa hatari zaidi. Kwa Yesu tabia hizo hukomeshwa bila kujali ukubwa wake.

Isaka akiwa mzee alitaka kumbariki mwanae mzaliwa wa kwanza, Esau. Yakobo, hali akiipata taarifa hiyo, alijiandaa kudanganya. Yakobo akijua Ngozi ya kaka yake (Esau) kuwa inavinyweleo, aliamua kutengeneza vazi la ngozi ili kufanana na Esau na kulivaa kufanikisha kudanganya. Yakobo alifanikiwa kudanganya kwa sababu baba yake (Isaka) alikuwa kipofu.

2.    Tabia kwa njia ya damu.

i)             Nyumba ya Ibrahimu – kila mzaliwa wa kwanza hapati/hafanikiwi.

Mzaliwa wa kwanza wa Ibrahimu aliitwa Ishmaeli aliyemzaa kwa kijakazi. Mzaliwa wa pili alikuwa Isaka. Mungu alifanya agano na mzaliwa wa pili wa Ibrahimu.

 “Ibrahimu akamwambia Mungu, Lau kwamba Ishmaeli angeishi mbele yako. Mungu akasema, Sivyo, lakini Sara mkeo atakuzalia mwana wa kiume, nawe utamwita jina lake Isaka. Nami nitafanya agano langu imara kwake kuwa agano la milele kwa ajili ya uzao wake baada yake.” Mwanzo 17: 18-19

ii)            Mzaliwa wa kwanza wa Isaka aliitwa Esau na hakupata, ila Yakobo mzaliwa wa pili alipata.

“Akasema, Je! Hakuitwa Yakobo kwa haki, maana amejitia mahali pangu mara mbili hizi? Alichukua haki yangu ya mzaliwa wa kwanza, na sasa amechukua mbaraka wangu. Akasema, Je! Hukuniwekea na mimi mbaraka?” Mwanzo 27:36

iii)          Mzaliwa wa kwanza wa Yakobo aliitwa Reubeni na hakupata.

 “Yakobo akawaita wanawe, akasema, Kusanyikeni, ili niwaambie yatakayowapata siku za mwisho. Kusanyikeni, msikie, enyi wana wa Yakobo,Msikilizeni Israeli, baba yenu.

Reubeni, u mzaliwa wangu wa kwanza,Nguvu zangu, na malimbuko ya uwezo wangu.Umewapita wengine kwa ukuu na kwa nguvu.Umeruka mpaka kama maji, basi usiwe na ukuu,Kwa sababu ulikipanda kitanda cha baba yako,Ukakitia unajisi; alikipandia kitanda changu.” Mwanzo 49: 1-4

Reubeni alikuwa na nguvu na ukuu akiwazidi nduguze, yaani alikuwa mahiri, hata hivyo alikosa kwa sababu alikinajisi kitanda cha baba yake kwa kulala na mwanamke; baba yake alimnyang’anya ukuu.

Kwenye damu kuna vitu vinapokea kila neno. Baada ya Yakobo kumnyang’anya ukuu Reubeni, Yakobo akafariki, na hivyo Reubeni hakusomeka kuwa mtoto wa Yakobo. Ndugu zake kuanzia mzaliwa wa pili wakalinda nafasi zao ili Reubeni asiweze kuzichukua.

Neno: 1 Nyakati 5:1

Kwakuwa Reubeni alipoteza nafasi yake, haki yake ya mzaliwa wa kwanza walipewa watoto wa Yusufu.

Magonjwa mengi yanayowapata watu huwa yanarithishwa kupitia damu (DNA). Kwa jina la Yesu magonjwa ya kurithishwa kutoka kwa baba kwenda kwa mwana yanaondolewa.

Baba yetu siku zote hupenda kusaidia watu tangu zamani amekuwa akifanya hivyo. Muujiza wa mtu upo kwenye kufuata anachoambiwa.

3.    Nyumba ya Yoabu

Kuna namna ya rohoni ambapo unaweza kuitengeneza mtu usiweze kurithi tabia kutoka kwenye familia au kwenye ukoo. Ni kwa kushindana kwenye ulimwengu wa roho kwenye familia na kwenye ukoo ili uweze kuziondoa zisikupate wewe na uzao wako.

Kuna familia inayoathirika kwasababu ya maneno waliyotamkiwa ambayo yanaingia kwenye damu na kwa kadiri wanavyozaliana ndivyo matatizo yanazidi kuongezeka kwenye uzao wao. Namna ya kuweza kushinda tatizo hilo ni kwa kutumia Neno.

Neno: 2 Samweli 3:27

Kwa Kadiri familia za nyumba ya Yoabu walivyoendelea kuoa ndivyo matukio ya ukoma, ombaomba, ulemavu yalivyosambaa.

Hata hivyo Bwana huyabatilisha maneno yote tunayotamkiwa - Waebrania 4:12

Kuna tabia au matukio ambayo yapo kwenye familia ambayo ni tatizo kwenye maisha ya watu wa familia yako; namna ya kushinda tatizo au matukio hayo ni kutoroka na kwenda kwenye ukoo wa Yesu. Ukiwa ndani ya familia ya Yesu unakuwa mrithi wa tabia za Yesu na namna ya kuingia kwenye ukoo wa Yesu ni kupitia damu ya Yesu.

Sisi sote tumekombolewa kwa damu ya Yesu – 1 Petro 1:18-23

Damu inaweza kusajili tabia kutoka kwa mzazi Kwenda kwa mtoto. Tabia hiyo inaweza kuwa magonjwa, umasikini, ulevi au wizi, au tabia nyingine yoyote. Usifanye au kusema jambo lolote kwa ajili ya kujifurahisha wewe mwenyewe kwa sababu, jambo au neno hilo linaweza kuwa madhara kwenye uzao wako.

Neno: Waebrania 7: 9-10

Matukio katika ukoo yanaenda mpaka kwenye sadaka. Lawi alihesabika katoa sehemu ya kumi kwa sababu, wakati Ibrahimu akitoa sehemu ya kumi, Lawi alikuwa kwenye kiuno cha Ibrahimu (Lawi na baba yake hawakuwa wamezaliwa).

Kama jema au baya ulifanyalo, hilo linakuwa limesajiliwa kwenye damu yako na watoto wako au wajukuu wako au vitukuu vyako au mtu yeyote anayetokana na uzao wako atahesabika ametenda jambo hilo kwa sababu, wakati ukitenda jambo hilo, wao walikuwa kwenye kiuno chako. Damu iliyosajiliwa kwenye damu yako itasafiri mpaka kwa uzao wako. Tumtumikie Mungu kwa ajili ya uzao wetu.

Kuna mambo mema pia huenda kwa uzao wa mtu kupitia damu. Mtu anaweza kurithi imani kutoka kwa wazazi wake na mara nyingi imani ya kurithi inakuwa ni kali kuliko.

Neno: 2 Timotheo 1: 3-5

Namna ambayo matukio ya familia husafiri; -

1.    Mazindiko ya familia

Mazindiko yanatokea ikiwa mtu ambaye ni kiongozi wa familia anaikabidhi familia kwa shetani ili ilindwe. Ni mkataba wa shetani na wazee wa ukoo. Malipo kwa Shetani ni damu kutoka kwa mwana wa ukoo huo. shetani hutengeneza matukio mbalimbali kama vile magonjwa au ajali ili kupata damu.

Ikiwa, kutokana na mkataba wa kishetani ambao wazee wa ukoo wameingia na shetani, damu inapaswa kuchukuliwa kwa magonjwa, basi shetani hutengeneza aina fulani ya ugonjwa, mfano, shinikizo la damu, mshtuko wa moyo, au ugonjwa wowote, na huo ndiyo utakuwa utaratibu wa vifo vya wana wa ukoo huo.

Sambamba na mikatabo ya kishetani ya ukoo, kunakuwa na mashetani yaitwayo mizimu yanayolinda familia/ukoo/mikataba hiyo. Mashetani hayo yanakuwa vilevile kama kabila la ukoo huo lilivyo; mfano, kama ni kabila la kisukuma, mashetani yatafanania usukuma.

     “Mwivi haji ila aibe na kuchinja na kuharibu; mimi nalikuja ili wawe na uzima, kisha wawe nao tele.” Yohana 10:10

2.    Dhambi

Dhambi pia inaweza ikaleta tatizo kwenye familia yako kwa sababu ya dhambi ulizonazo. Dhambi inaleta kifo, unaweza kufanya jambo na usilimalize kwasababu ya dhambi. Dhambi husababisha matukio katika damu.

Kwa sababu ya dhambi, Mungu humuua mtenda dhambi.

“Yuda akamwoza mke Eri, mzaliwa wake wa kwanza, na jina lake huyo mke ni Tamari. Naye Eri, mzaliwa wa kwanza wa Yuda, alikuwa mbaya machoni pa BWANA; na BWANA akamwua.” Mwanzo 38:6-7

– Mzaliwa wa kwanza wa Yuda alitenda dhambi, Mungu akamuua.

Warumi 6:23 – Mshahara wa dhambi ni mauti.

3.    Kushiriki mambo ya mila na desturi

Mila na desturi huendeshwa na wakuu wa familia au ukoo, na ni sharti kuhudhuria. Huwekwa masharti kwa hao wasiohudhuria, mfano kutengwa na familia au ukoo.

Yesu anatuita twende kwake, tumtegemee Yeye kwakuwa ndani ya ukoo wa Yesu kuna kila kitu na tunapata ulinzi wa damu ya Yesu dhidi ya mambo ya ukoo wa kidunia.

Njoni kwangu, ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha.” Mathayo 11:28

Kwenye ukoo wa Yesu tunapata ndugu wengi na hakuna hata laana ya mzaliwa wa kwanza, kwa maana, kwa kupigwa kwake Yesu familia zetu zimekombolewa.

Isaya 53:5

Mafarisayo waliogopa kulitaja jina la Yesu kwa sababu ya mambo ambayo yangewatokea.

“akisema, Je! Hatukuwaamuru ninyi kwa nguvu, msifundishe kwa jina hili? Nanyi, tazameni, mmeijaza Yerusalemu mafundisho yenu, na mnataka kuileta damu ya mtu yule juu yetu.” Matendo ya Mitume 5:28

Ukilitaja jina la Yesu maana yake unaileta damu ya Yesu Kristo juu yako.

Yesu anatuita watu wote kutoka kwenye familia na koo zetu tulizonazo tuziache na tuingie kwenye ukoo wa Yesu. Kitendo cha kuhama kutoka kwenye koo zetu za kidunia tulizonazo na kuingia kwenye ukoo wa Yesu kinaitwa Kumpokea Yesu.

Ukoo wa Yesu hauchagui aina ya watu; hubeba watu wote, tajiri au masikini wa dini zote. Inakupasa leo kukubali kuwa ndani ya ukoo wa Yesu, nawe utakuwa umetoroka katika matukio kwenye familia. Unaposema damu ya Yesu Kristo unairuhusu damu iingie kwenye familia yako.`

BONYEZA HAPA KUANGALIA IBADA YA JUMAPILI

Post a Comment

0 Comments