google.com, pub-4324601895065941, DIRECT, f08c47fec0942fa0

Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MATUKIO YA KICHAWI

UFUFUO NA UZIMA CATHEDRAL
IBADA YA PASAKA 12.04.2026
ASKOFU DKT JOSEPHAT GWAJIMA
SOMO: MATUKIO YA KICHAWI

Ulimwengu una matukio mbalimbali; mfano, yapo matukio ya kijeshi ambapo nchi na nchi zinapigana. Kuna matukio ya kichawi. Yapo matukio ambayo unaweza kuyaona ni ya kawaida kumbe ni mambo ya kichawi.

Uchawi upo; Biblia takatifu na Quran vimethibitisha. Mfano, Biblia imeandika kuwa, usimwache mwanamke mchawi kuishi. Kuna matukio yanampata mtu ambaye anayatafsiri kuwa ni matukio ya kibinadamu lakini ni uchawi.

Mungu aliumba Malaika; baadhi ya Malaika waliasi na kutupwa duniani. Kwasababu hiyo, kuna Malaika wa aina mbili, yaani, Malaika watakatifu na Malaika waovu. Malaika watakatifu hutumwa na Mungu kutuhudumia watoto wake. Malaika waovu nao hutumwa na shetani kusababisha matatizo kwa watu.

Malaika waovu wana majina mengi ambayo hutofautiana sababu ya majukumu yao; wapo huitwa, mapepo, mashetani, majini, mizimu, vibwengo n.k., wote ni walewale. Mashetani ni watafiti. Mashetani wanaoufahamu wao uleule waliokuwa nao kabla ya kuasi na kutupwa. Mashetani wakitolewa ndani ya mtu huenda wakitafuta. Wana sifa zote za Malaika, lakini wao; -

-      Ni Malaika wa kuzimu: Ufufuo, 9:11

-      Ni Malaika wasioilinda enzi yao wenyewe, Yuda 1:6

-      Ni joka na Malaika zake, Ufunuo 12:7

-      Ni Ibilisi na Malaika zake, Mathayo 25:41

 “Kwa maana ikiwa Mungu hakuwaachilia malaika waliokosa, bali aliwatupa shimoni, akawatia katika vifungo vya giza, walindwe hata ije hukumu;” 2 Petro 2:4

Kwa ufahamu huu juu ya Malaika waovu, ni dhahiri kama isemavyo filosofia, huwezi kutatua tatizo bila kujua chanzo chake, na kama mtu akijaribu kutatua tatizo bila kujua chanzo cha tatizo atatengeneza tatizo tofauti na alilonalo. Mungu hutuma Malaika zake katika kila kazi yake, vivyo hivyo, shetani naye hutuma malaika zake ili kutenda uovu, mfano, Malaika Gabrieli alitumwa na Mungu kwa Daniel kuleta taarifa kuhusu kusikiwa maombi yake alivyosali na kufunga siku ishirini na moja, na kwa Mariamu kuhusu kuchukua mimba kwa uwezo wa Roho Mtakatifu. Malaika waovu hutumiwa na wachawi kuleta matatizo kwa watu.

Kanisa la Ufufuo na Uzima tunaamini kuwa kumtumikia Mungu ni kuwatumikia watu, hivyo kuwatumikia watu ni kupambana na Malaika waovu wawatoke watu, na siku ya leo tutaondoa Malaika waovu wote, kwa Jina la Yesu. Tatizo kubwa la mtu ni kuwa na tatizo lakini hajui chanzo zha tatizo lake.

Malaika waovu ni roho. Hawafanyi kazi mpaka watumwe na wachawi.

Sifa Za Malaika:

Wanaweza kujigeuza kuwa chochote; Malaika waovu wanaweza kugeuka kuwa mtu, mti, upepo, mnyama, wadudu, n.k. pia Malaika waovu wanaweza kuwa hali tofauti tofauti kama ugonjwa, ulemavu, matatizo, kifafa, ububu, ukichaa.

“Mtu mmoja katika mkutano akamjibu, Mwalimu, nimemleta mwanangu kwako, ana pepo bubu; na kila ampagaapo, humbwaga chini, naye hutoka povu na kusaga meno na kukonda; nikasema na wanafunzi wako wamtoe pepo, wasiweze. Akawajibu, akasema, Enyi kizazi kisichoamini, nikae nanyi hata lini? Nichukuliane nanyi hata lini? Mleteni kwangu.” Marko 9:17-26

Mtu anaweza kuwa na hali isiyo ya kawaida kumbe Malaika waovu wametumwa na wachawi wamuingie na kuleta hali hiyo. Mtu anaweza kuwa bubu, anaweza kuwa na hali ya kubwagwa chini, kukonda, kutoka povu, kuharibu biashara, kifafa, nuksi, balaa, kukosa kibali, n.k.

Mtu akishaingiwa na pepo aliyetumwa na wachawi, huonekana na ugonjwa fulani ambao hupewa jina la kisayansi, na kama mtu huyo asipojua chanzo cha ugonjwa huo, huishia kukubaliana na sababu za kisayansi na mwisho kurasimisha ugonjwa huo kwake.

Ukijua asili ya wachawi huogopi tena, na ukijua nguvu iliyo ndani ya damu ya Yesu huogopi mchawi kabisa. Yesu anasema mwenye hali/matatizo yoyote ALETWE KWAKE

“Akawajibu, akasema, Enyi kizazi kisichoamini, nikae nanyi hata lini? Nichukuliane nanyi hata lini? Mleteni kwangu.” Marko 9:19

Fungua moyo wako kwa Yesu naye atakutibu; Matendo ya Mitume 16:14, Mathayo 11:28. Roho Mtakatifu hushuka na kuyeyusha kamba zote za kichawi.

Mapepo, majini, vibwengo, mashetani n.k. wakimuingia mtu huweza kumfanya mtu ajipeleke mwenyewe kwenye hatari; mfano, unamuona mtu amening’inia kwenye chombo cha moto kwa namna ya kuhatarisha maisha yake lakini anaona ni kawaida kwake. Huitwa ajali ya kujitakia

 “Enyi Wagalatia msio na akili, ni nani aliyewaloga, ninyi ambao Yesu Kristo aliwekwa wazi mbele ya macho yenu ya kuwa amesulibiwa?” Wagalatia 3:1

Yesu hukemea kwa amri. Sisi pia tunayoamri ya kukemea pepo atoke na kumrudia yeye aliyemtuma; ni msaada utokao juu. Mara nyingi mtu akipata msaada shetani huzidisha tatizo la mtu ili akate tamaa; mfano, ustawi wa biashara ya mtu kuporomoka zaidi.

Mfano, Yesu alipomkemea pepo wa kifafa amtoke mtu, pepo akamtia kifafa sana mtu huyo na kumfanya aonekane amekufa, hata watu wengi wakasema amekufa (Marko 9:26). Machoni pa watu hali ya mtu huonekana kama amekosa msaada lakini yampasa mtu kutoacha kumfuata Yesu kwani bidii husababisha shetani kumuachia mtu.

Mashetani wanaweza wakamfanya mtu aonekane amekufa. Bahati mbaya zaidi hospitalini hawana kipimo cha kupima kifo; wao hupima viashiria tu kuwa mtu yawezekana amekufa, mfano, mapigo ya moyo, kucheza kwa macho n.k. Mashetani wanaweza kufanya vipimo kuonesha mapigo ya moyo yamesimama na macho hayachezi na hivyo mtu huyo kuthibitishwa kitabibu kuwa amekufa, kumbe ni kulogwa.

Wachawi ni watu ambao ni mawakala wa shetani. Wachawi hutumia roho ambazo ni Malaika wa giza ili kumloga mtu. Mchawi anaweza kuwa baba, mama, kaka, dada, shangazi, mjomba. Wachawi sio mapepo ni binadamu, wanaweza kuwa viongozi, mfano askofu, mchungaji, shehe, diwani, mbunge, au kiongozi wa ngazi yoyote; na wachawi wote ni kuwafyeka na akitokea tena fyeka zaidi “Usimwache mwanamke mchawi kuishi.” Kutoka 22:18

Sisi kwa mamlaka ya Jina la Yesu tunatumia upanga wa roho ambao kazi yake ni kufyeka (Waefeso 6:17); tunafyeka mchawi yeyoye. Mchawi akiwa; -

-      Baba mdogo, fyekaaaaa!

-      Shangazi, fyekaaaaa!

-      Baba, fyekaaaaa!

-      Kaka, fyekaaaaa!

-      Dada, fyekaaaaa!

-      Askofu, fyekaaaaa!

-      Shehe, fyekaaaaa!

-      Mtu yeyote, fyekaaaaa!

Kila kinachoonekana kimekufa Yesu anayo mamlaka na uwezo wa kukishika mkono na kukiinua nacho kikasimama; mfano, kazi, maisha, biashara, afya, huduma, n.k. Marko 9:27

Neno: Marko 1:21-23

Mashetani yanaelewa, yana utambuzi, yanaongea, yanaangamiza, na yanapotumwa na wachawi kwa mtu, yanamtambua vizuri mtu huyo ni nani. Mashetani ni wanajeshi kamili wa ufalme wa giza (Waefeso 6:12). Ili kuyazuia mashetani ni lazima yashindane na Majeshi ya Bwana.

Majeshi ya giza yakiwa mahali yanamiliki; akiingia Yesu utawala wao unakoma. Kwenye maisha yetu tunayo amri ya kumkemea pepo afumbe kinywa na atoke kwenye biashara, afya, kazi, huduma, n.k., kwa Jina la Yesu na anatii. Sisi hatuhitaji nywele, mafuta, kucha au kitu chochote ili kutoa pepo; sisi ni FUMBA KINYWA, TOKA kwa Jina la Yesu.

Tatizo la mtu lipo hapa; kutambua chanzo cha tatizo na utatuzi wake. Mchawi, msoma Nyota, mpiga ramli, mganga wa kienyeji ni walewale kama ilivyo wizara mbalimbali ndani ya serikali moja. Huwezi kutatua tatizo la kulogwa kwa kwenda kupata msaada kwa mganga wa kienyeji.

Utatuzi kwa tatizo la kulogwa na wachawi ni kumfuata Mtu wa Mungu, Mtu aliyetumwa na Mungu kufanya kazi ya Kimungu. Mungu hutuma watu kwenye maisha yetu. Chochote tunachokitaka kutoka kwa Mungu kipo kwa watu; Mungu alishashusha yote kwa watu. Ukimkosa Mtu aliyetumwa na Mungu, umemkosa Mungu.

Kidunia, kila familia huwa imezindikwa. Tunahakikisha leo wachawi wote wanapoteza wateja. Mizimu ni mashetani waliokaa kwenye ukoo kwa miaka mingi. Kila ukoo/kabila kuna mizimu inayomiliki ukoo/kabila hilo; mfano, kwa kabila la Wasukuma, kila ukoo una bibi wa ukoo ambaye kila salamu inamtaja.

Wanaukoo hutengenezwa na mizimu kuwa na tabia fulani. Wanaukoo huzuiwa mambo fulani; mfano, kuoa/kuolewa, kula aina fulani ya chakula, umasikini/umiliki unaopimwa. Ikitokea mwanaukoo kafanikiwa jambo fulani kinyume na tabia ya ukoo, mizimu huyaondoa mafanikio hayo.

Mizimu ya ukoo pia husafirisha tabia fulani au hali kutoka kizazi hadi kizazi. Mizimu ikivunjika tabia hizo zinaondoka katika ukoo huo. Ukitoka kwenye vifungo vya mizimu ya ukoo unakuwa huru na matatizo na taabu zote. Mashetani wako wa viwango tofauti, mfano, kuna wakuu wa giza, wafalme wa giza, na mamlaka za giza.

Mungu huwashika mkono watu. Unatakiwa kukubali kushikwa mkono na Mungu. Kuna watu wana Bahati ya kushikwa mkono na Mungu lakini hawashikiki; mfano, mke wa Ruthu alishikwa mkono na Mungu kumuepusha na moto mkali wa Sodoma na Gomora lakini hakuvumilia akageuka nyuma na kuwa jiwe la chumvi. Hatupaswi kumuogopa shetani auaye mwili. Yatupasa kumuogopa Mungu auaye mwili na roho.

Sala zote tunazosali sio mbaya; mfano sala ya Bwana, sala ya Bikira Maria, ama dua ya Quran. Ubaya wa sala hizi hazishughuliki na shetani. Sisi Ufufuo na Uzima katika sala tunashughulika na shetani; tunamuamrisha shetani atoke kwenye maisha yetu na hali zetu za maisha, kwa Jina la Yesu.

Kuna viumbe ndani ya mtu wanamwendesha mtu kufanya yale asiyopenda kufanya. Kuna familia hawaelewani kabisa wao kwa wao. Mambo haya yote yanatokana na tabia ambazo zinaongozwa na mizimu.

Pepo hutumwa na mtu. Bahati mbaya sana mtu huyo lazima awe anakufahamu. Pepo anapotumwa huwa na kazi ya kutimiza alichotumwa kufanya; mfano kuiba Nyota ya uso wa kibali au Nyota ya macho ya kuona fursa. Wachawi wakikuibia hutumia Nyota hiyo kuendesha mambo yao. Unapokuwa umeibiwa Nyota mfano, Nyota ya uso, kila anayekuona anakuwa havutiwi nawe.

“Amemeza mali, naye atayatapika tena; Mungu atayatoa tumboni mwake.”Ayubu 20:1

Ukimkemea shetani na Malaika zake wanahama katika maisha yako na hawatakuwako tena kwa sababu Jina la Yesu ni jina lipitalo majina yote. Kuna viumbe vinakuendesha bila wewe kujua na ukiviondoa viumbe hivyo kuna baadhi ya tabia zitaondoka kwako. Mungu amemuumba mtu na uso wenye kibali, mashetani wakichukua hicho kibali kila mtu anayekuona hataki kukuona tena kwa sababu umeibiwa Nyota ya uso wako.

Unazaliwa na akili ya kufikiri na uwezo mkubwa wakukumbuka lakini zikichukuliwa na wachawi wanazitumia kwa ajili ya kazi za kichawi. Majini na pepo wanapotumwa huja ili kuharibu lile kusudi maalum ambalo Mungu ameliweka ndani ya mtu; pia huweza kuharibu mifumo ya mwili wa mtu na kuleta magonjwa na mtu huyo akifa huonekana kama alikufa kutokana na ugonjwa fulani au shida fulani, kumbe ni moja ya matukio ya kishetani ambayo wanafanya ndani ya mtu huyo.

Ili mtu awe na nguvu za kushindana na mashetani hayo, ni lazima mtu huyo awe amempokea Yesu katika maisha yake (Waefeso 6:12). Mpokee Yesu akujaze nguvu za kuyashinda mashetani.

BONYEZA HAPA KUANGALIA IBADA YA JUMAPILI

Post a Comment

0 Comments