UFUFUO NA UZIMA
CATHEDRAL
IBADA YA PASAKA
05.04.2026
ASKOFU DKT GERSHOM
MWAKILA
SOMO: NGUVU YA UFUFUO
![]() |
Kibinadamu, watu husherehekea Pasaka kwa namna tofauti
tofauti; kupika chakula kizuri, wapo hunywa vileo na kutembelea sehemu
mbalimbali kufurahisha mioyo yao. Hawa wote hujiita Wakristo.
Je, Pasaka ni siku au sherehe ya Wakristo? Biblia imetaja
neno “Wakristo” mara moja tu, vilevile imetaja “Wana wa Mungu” mara sitini na
moja na “Mwana wa Mungu” mara arobaini na sita.
“hata alipokwisha kumwona
akamleta Antiokia. Ikawa kwa muda wa mwaka mzima wakakusanyika pamoja na kanisa
na kuwafundisha watu wengi. Na wanafunzi waliitwa Wakristo kwanza hapo
Antiokia.” Matendo ya Mitume 11:26
Hivyo basi, ili kuwa sahihi sana, Biblia kutaja “Wana
wa Mungu” na “Mwana wa Mungu” zaidi ya mara mia moja kwa pamoja imelenga
kuifanya Pasaka kuwa ni sherehe ya Wana wa Mungu kwasababu Wana wa Mungu wamekombolewa,
hawafi na wanarithi uzima wa milele. Wakristo hufa.
“isha baadhi ya Masadukayo
wakamwendea, wale wasemao ya kwamba hakuna ufufuo, wakamwuliza,” Luka 20:27
-
Wana
wa ulimwengu huu huoa/huolewa lakini Wana wa Mungu hawaoi/hawaolewi kwasababu
ni Wana wa Ufufuo.
Kilichozaliwa na mwanadamu kinaitwa mwanadamu na
kinachozaliwa na Mungu kinaitwa Mungu; kama ilivyo, mwana wa mbwa huitwa mbwa
na mwana wa ng’ombe huitwa ng’ombe. Kimsingi, Wana wa Mungu ni miungu katika
dunia hii kwa maana wamezaliwa na Mungu katika namna ya kiroho. Wana wa Mungu
ni watu ambao wamempokea Yesu, na wamefanyika kwa namna ambayo sauti zao zimejazwa
nguvu ya kusikilizwa kwa chochote watakachokifanya.
“Amin, amin, nawaambia, Saa
inakuja, na sasa ipo, wafu watakapoisikia sauti ya Mwana wa Mungu, na wale
waisikiao watakuwa hai.” Yohana 5:25
Sauti ya Mwana/Wana wa Mungu inasikika hata kwa
waliokufa na vilivyokufa. Chochote kilichokufa au ambacho kiko kwenye msafara
kuelekea kufa kikiisikia sauti ya Mwana wa Mungu hupata uhai/hakifi. Imani yetu
imejazwa katika kifo cha Yesu na kufufuka kwake; tunaamini hivyo. Tunamwamini muasisi
wa Imani yetu kama alivyozaliwa kimaajabu, akakua kimaajabu, akatenda kazi yake
kimaajabu, akashtakiwa kimaajabu, akafa kifo cha maajabu, akazikwa na kufufuka
kimaajabu. Kufufuka kwa Yesu kupo katika nguvu ya Mungu iliyomtoa kaburini,
ambayo inakaa ndani yetu. Nguvu hiyo hutuhuisha sisi kwa Roho Mtakatifu.
“Hata sabato ilipokwisha,
ikipambazuka siku ya kwanza ya juma, Mariamu Magdalene, na Mariamu yule wa
pili, walikwenda kulitazama kaburi. Na tazama, palikuwa na tetemeko kubwa
la nchi; kwa sababu malaika wa Bwana alishuka kutoka mbinguni, akaja
akalivingirisha lile jiwe akalikalia.” Mathayo 28:1-2
Nguvu ya Ufufuo:
Kufufuka kwa Yesu kumefanyika kwa Nguvu ya Ufufuo
ambayo kwayo mambo makuu ya rohoni ni dhahiri na hutokea kama ifuatavyo; -
1.
Ufufuo
una nguvu ya kusababisha tetemeko.
Kila mtu husikia bila kujua kuwa
kuna mtu wa rohoni ameshuka. Akili za kibinadamu na kisayansi haziwezi kuelewa
wala kusikia ila Wana wa Mungu pekee yaani, Wana wa Ufufuo.
Siku ya Ufufuo ni siku ya
tetemeko ulimwenguni kutetemesha kila kilicho kinyume na kazi ya Mungu. Tukikumbuka
Ufufuo tunaagiza tetemeko liende kwenye kila kaburi lililozika mambo yetu;
mfano, kaburi lililozika afya, kazi, hatma, Nyota, huduma n.k.
Kupitia Nguvu ya Ufufuo kila
kilichozikwa kwenye kaburi kinainuka na kuwa hai tena. Kuna viumbe wa rohoni ambao
ni Malaika wa Bwana, hushuka na kuleta tetemeko kwenye kaburi na kufufua kila
kilichozikwa.
2.
Ufufuo
una nguvu ya kuondoa lolote ambalo limewekwa na wanadamu kwa lengo la kuzuia
mpango wa Mungu.
“Hata ilipokuwa jioni akafika mtu
tajiri wa Arimathaya, jina lake Yusufu, naye mwenyewe alikuwa mwanafunzi wa
Yesu; mtu huyu alimwendea Pilato akauomba mwili wa Yesu. Ndipo Pilato
akaamuru apewe. Yusufu akautwaa mwili, akauzonga-zonga katika sanda ya
kitani safi, akauweka katika kaburi lake jipya, alilokuwa amelichonga
mwambani; akavingirisha jiwe kubwa mbele ya mlango wa kaburi, akaenda zake.” Mathayo
27:57-60
Yusufu, mmoja wa wanafunzi wa
Yesu, aliuomba mwili wa Yesu na kuuvingirisha sanda, akauweka kaburini, kisha akaweka
jiwe kubwa mlangoni mwa kaburi.
Kukawa na walinzi Mafarisayo
ambao waliweka muhuri kwenye jiwe kuzuia mtu/watu kuligusa jiwe hilo ili mwili
usitolewe na kudanganya kuwa Yesu amefufuka.
Mafarisayo walitenda kibinadamu
bila kuzingatia kuwa ilitabiriwa kutendeka kiroho, na Mbingu zina mpango wa
kutekeleza Ufufuo siku ya tatu (wakati ulionenwa utakapotimia).
Siku ya tatu ilipotimia, Mbingu
hazikusubiri mkono wa mwanadamu; Mbingu zilituma Malaika kwenda kuliondoa jiwe
na Yesu akafufuka.
Wakati binadamu wanaweka mpango
wa kukuzuia usiende kwenye muujiza wako, Mbingu zina mpango kinyume nao wa
kukufanya upenye katika ule wakati sahihi ambao Mbingu zimepanga ufanikiwe.
Mbingu hutuma mjumbe/wajumbe
wake/Malaika kututoa kwenye majaribu ya muovu/mkono wa kibinadamu.
Mbingu husikiliza Kanisa liseme tu
ili zitume mjumbe wake kuondoa vizuizi vyote vilivyowekwa na shetani kupitia watoto
wake/binadamu.
“Na tazama, palikuwa na tetemeko
kubwa la nchi; kwa sababu malaika wa Bwana alishuka kutoka mbinguni, akaja
akalivingirisha lile jiwe akalikalia.” Mathayo 28:2
Katika kalenda ya Bwana, ni saa
ya Ufufuo duniani, na ifahamike kwamba, kama Baba yetu mpendwa alivyotuambia, Pasaka
hii ni ya mwisho tunakula tukiwa na hali tuliyonayo; katika Pasaka hii tunajazwa
utele wa Bwana.
Mungu anafanya mambo yote kuwa
mapya katika Pasaka hii. Katika hili, Mungu ameachilia Malaika wake kuondoa
vizuizi katika maisha yetu; Yeye hutuwazia yaliyo mema siku zote.
Kila kizuizi angukaaaa, kwa Jina
la Yesu!
Kwetu sisi, Ufufuo ni Malaika wa
Bwana kuondoa vizuizi katika maisha yetu. Malaika wanatetea walio Wana wa Mungu
kwa kuwaondolea vikwazo vyao.
3.
Ufufuo
una nguvu ya kuwafanya walinzi wa maisha wafe.
Wana wa Mungu wanalindwa na Nguvu
za Mungu. Hakuna nguvu nyingine ya kutegemea ila ni kupitia nguvu za Mungu na
kuwa na ulinzi wa Mungu. Mungu huyatembelea maisha yetu. Nguvu ya Ufufuo; -
-
Inawafanya
watu wanaotaka kukuangamiza wafe.
-
Inawalaza
chini walinzi wote wanaokulinda ubaki kwenye shida.
-
Hukulinda
dhidi ya nguvu za giza.
Wana wa Mungu hawalindwi na
viumbe au vitu vyovyote kama chumvi, mafuta, sabuni, chupa, maji n.k., Wana wa
Mungu wanalindwa na Neno la Mungu. Chumvi, mafuta, sabuni, chupa, maji n.k.,
haviwezi kukukimbilia ili kukuokoa kwenye hatari ila Neno la Mungu, ambalo kwa
hilo; -
-
Mungu
halali wala hasinzii.
-
Ni
taa na lina macho.
-
Atulindae
ana miguu hivyo anatembea; Bwana hutembea kuja kututendea sawasawa na haja zetu;
kwa wachawi ni nyundo iangukayo kwenye vifua vyao, ni mkate au chakula cha
uzima, Neno linafyeka maana ndilo Upanga wa Roho, lakini vilevile Neno li
shahidi wa kazi njema za Mungu. Kwenye Biblia wachawi waliishia kupigwa.
Ufufuo una nguvu ya kufanya wote
watulindao kwenye matatizo wafe, kwa maana kutaka kwetu ndiko kutaka kwa Bwana.
Siku ambayo mtu anaenda kupokea miujiza ni siku ambayo kunakuwa na vizuizi
vingi ambavyo vinamzuia mtu asiende nyumbani mwa Bwana; ni kwa sababu kuna watu
wanakuzuia usiende.
“Na kwa kumwogopa, wale walinzi
wakatetemeka, wakawa kama wafu.” Mathayo 28:4
Wakati Yesu anakufa, maandiko
yanasema watu wengi walifufuka; -
“Nimesulibiwa pamoja na Kristo;
lakini ni hai; wala si mimi tena, bali Kristo yu hai ndani yangu; na uhai nilio
nao sasa katika mwili, ninao katika imani ya Mwana wa Mungu, ambaye alinipenda,
akajitoa nafsi yake kwa ajili yangu.” Wagalatia 2:20.
Wakati wa kufufuka kwa Yesu
walinzi, waganga, wachawi, wasoma nyota, wapiga ramli ni zamu yao kufa, kwa
Jina la Yesu.
4.
Ufufuo
una nguvu ya kukamilisha maneno yote yaliyosemwa juu ya mtu.
Bwana Yesu hakukubali kwenda kinyume
na kila alichoandikiwa bali alifuata kile kilichoandikwa na Mungu na vyote
alivyoandikiwa na Mungu alivitimiza.
-
Alizaliwa
kama ilivyotabiriwa.
-
Alienda
Misri kama ilivyotabiriwa.
-
Alienda
Bethlehemu, Galilaya, Yerusalemu n.k. kama ilivyotabiriwa.
-
Alisema
atasalitiwa na akasalitiwa kama ilivyotabiriwa.
Wakati Yesu akila chakula mara ya
mwisho pamoja na wanafunzi wake, alitabiri kusalitiwa kwake ambapo wanafunzi
wake walifadhaika sana mioyoni mwao kusikia utabiri wa Yesu kusalitiwa. Hata
hivyo, Bwana Yesu aliwatia moyo wale kumi na moja mara tu Yuda msaliti
alipokuwa hayupo.
Neno hili linatufundisha kuwa,
Yuda wa maisha ya mtu akiondoka, Yesu huzungumza na mtu kwa habari ya maisha
yake. Yuda yeyote aliyekuja/aliyepo kwenye maisha ya mtu leo tunamfyekaaa, kwa
Jina la Yesu!
Kuna wakati watu wanajifanya wanakupenda
sana ila mpango wao ni ishara ya kutaka kukuangamiza; hao tunawaitwa kuwa ni
Yuda wa maisha yako. Kama vile Petro alivyochomoa panga lake na kumfyeka Yuda,
kwa Jina la Yesu tunatwaa Upanga wa Roho ambao ni Neno la Mungu na tunakufyeka
Yuda yeyote uliye kwenye maisha yetu.
-
Mchawi
kwenye kazi, fyekaaaa!
-
Mchawi
kwenye familia, fyekaaaa!
-
Mchawi
kwenye ndoa, fyekaaaa!
-
Mchawi
unayezuia safari, fyekaaaa!
-
Mchawi
unayeiba Nyota, fyekaaaa!
5.
Nguvu
ya Ufufuo inathibitisha kuwa yote ni kweli.
Kupitia nguvu ya Ufufuo, ahadi za
Mungu zitatimia kwenye maisha yetu. Yesu alipopaa kwenda kwa Baba yake
alituahidi anakwenda kutuandalia makao ya milele, na atarudi tena. Yesu alisema
anatuachia Roho Mtakatifu kuwa msaidizi wetu, na ndivyo ilivyo.
Kama ambavyo yote yaliyotabiriwa
yalifanyika, kwa Nguvu ya Ufufuo tunaamini vilevile ahadi ya Yesu kwetu
itatimia. Kwakuwa tunaamini atarudi, kabla hajarudi lazima tuhakikishe
tunakomesha wachawi na kuzuia nguvu za ibilisi kwenye maisha yetu, kwa Jina la
Yesu.
Hatari kubwa ni kwa mtu
anayeambiwa Yesu atarudi tena ila mtu huyo bado hajampokea Yesu.
Yote yaliyotabiriwa yalitokea,
iweje mtu huyo asiamini kuwa Yesu atarudi? Ni heri leo mtu huyo ampokee Yesu,
na kwa kuzingatia kuwa leo ni Pasaka, basi itakuwa kumbukumbu nzuri sana kwa
mtu huyo kumpokea Yesu siku ya Pasaka.
Biblia inasema, mtu asiyempokea
Yesu maishani mwake, hawezi kuurithi ufalme wa Mungu.
Faida za kumpokea Yesu: -
-
Mungu
atakusamehe makosa yako yote,
-
Mungu
atafuta jina lako kwenye kitabu cha kifo,
-
Mungu
ataandika jina lako kwenye kitabu cha uzima wa milele,
-
Wewe
unakuwa mtoto wa Mungu,
-
Wewe
unakuwa rai awa Mbinguni, na
-
Mungu
anakuwa Baba yako na atawajibika kwenye mahitaji yako yote.
Mkiri Yesu mbele za watu naye
atakukiri mbele za Baba yake aliye Mbinguni;
“Basi, kila mtu atakayenikiri
mbele ya watu, nami nitamkiri mbele za Baba yangu aliye mbinguni.” Mathayo 10:32
“Nami nawaambia, kila
atakayenikiri mbele ya watu, Mwana wa Adamu naye atamkiri yeye mbele ya malaika
wa Mungu;” Luka 12:8.

.jpg)
0 Comments