UFUFUO NA UZIMA
CATHEDRAL
IBADA YA JUMAPILI 17.05.2026
ASKOFU DKT GERSHOM
MWAKILA
SOMO: KUFUTA KIAPO
CHA KICHAWI
![]() |
Tunashawishika kuamini kuwa, miongoni mwa mambo
yaliyofanyika kuzuia Danieli asipate taarifa kutoka kwa Mungu kuwa maombi yake
yalisikiwa tangu siku ya kwanza, ni ‘Kiapo cha Kichawi.”
Kiapo ni maneno ambayo mtu husema, au jambo ambalo
mtu analifanya ili kumaanisha kuwa kwenye hilo analosema ni kweli na
anamaanisha. Kiapo kina nguvu sana kwa sababu asili yake ni ya rohoni. Makusudi
ya kiapo yamebebwa kwenye ulimwengu wa roho; kiapo kinashikiriwa kwenye
ulimwengu wa kiroho kwa uzuri au kwa ubaya. Mtu anapoapa, anaapa kwa mamlaka ya
juu ya rohoni “Maana wanadamu huapa kwa yeye aliye mkuu kuliko wao; na
kwao ukomo wa mashindano yote ya maneno ni kiapo, kwa kuyathibitisha.” Waebrania
6:16.
Mojawapo ya mambo yanayofanya watu wasije kwenye maisha
ya mtu ni uwepo wa viapo vya kichawi. Kiapo ni hati miliki ya rohoni. Ukomo wa
mambo yote ni kiapo. Mtu akishaapa hayo mambo hayawezi kubadilika na nilazima
yatekelezwe vilevile kama yalivyoapwa. Ahadi za Mungu juu ya watu hutimia; ili
Mungu ahakikishe yale aliyotuahidi kuwa atafanya vilevile alivyosema, amefunga
ahadi zote kwa kamba ziitwazo kiapo. Kiapo cha Mungu akifunga huwa hakibadiliki.
Wale wanaobadilika badilika kwenda kinyume na kiapo
ambacho wameweka au Mungu ameweka, Mungu hutekeleza yaleyale yaliyofanyika kwa
kiapo
“Kila kutoa kuliko kwema, na kila
kitolewacho kilicho kamili, hutoka juu, hushuka kwa Baba wa mianga; kwake
hakuna kubadilika, wala kivuli cha kugeuka-geuka.” Yakobo 1:17.
Mfano ni kiapo cha Mungu na Musa kuwa Mungu atawatoa
wana wa Israeli utumwani; wana wa Israeli walipomuasi Mungu kwa kujifanyia
muungu awatoe utumwani, Mungu alitaka kuwaangamiza kwa uasi huo.
Musa alimkumbusha Mungu juu ya kiapo chake na wana wa
Israeli kuwa atawatoa utumwani na kuwapeleka nchi ya ahadi, na siyo
kuwaangamiza.
Mungu alikumbuka ahadi na kiapo chake, hakuwaangamiza
wana wa Israeli; Mungu akatekeleza ahadi yake bila kujali kuwa wana wa Israeli
walibadilika na kuasi
“Katika neno hilo Mungu, akitaka
kuwaonyesha zaidi sana warithio ile ahadi, jinsi mashauri yake yasivyoweza
kubadilika, alitia kiapo katikati;” Waebrania 6:17
Yale mambo ambayo Mungu ameahidi au ameweka ahadi
juu ya mtu, hakuna litakalodondoka bure au kubadilika; zitabadilika nyakati,
watabadilika watawala, yatabadilika masaa, lakini Mungu hatabadilika. Yale ambayo
Mungu amesema, lazima yatatokea, na ameyafunga kwa kiapo. Mifumo ya ulimwengu
itabadilika lakini ahadi za Bwana hazitabadiliki hata milele.
Mtu huapa kwa uovu au kwa wema; kwenye ulimwengu wa
roho kiapo hicho husajiliwa. Kwa kujua ama kwa kutokujua watu huteswa na viapo
walivyoviweka (Mambo ya walawi 5:4).
Kitabu cha Yeremia 4:2 kinatufundisha
namna ya kuapa. Imeandikwa, “nawe utaapa hivi, Kama BWANA aishivyo,
katika kweli, na katika hukumu, na katika haki ndipo mataifa watajibariki
katika yeye, nao watajitukuza katika yeye.” Mtu unapoapa unajifunga kwa
kifungo kuwa ulichosema hakitabadilika mpaka kitimie.
AINA YA VIAPO
Kuna aina tofauti za viapo; -
1.
Kiapo
cha Kitaaluma:
Wanataaluma fulani baada ya kutunukiwa hatua muhimu ya taaluma yao, huapa ili
wakafanyie kazi taaluma waliyoipata. Mfano ni Wanasheria (kiapo cha kutenda haki),
Madaktari (kiapo cha usiri bila upendeleo), Maaskari (kiapo cha utii kwa
mamlaka ya nchi), n.k.
2.
Kiapo
cha Viongozi:
Viongozi wapatapo madaraka, huapa kutumia nafasi zao kwa malengo sahihi ya
nafasi hizo.
3.
Kiapo
cha Ndoa:
Wanandoa wafungapo ndoa huapa kupendana kwenye hali yoyote, na kutoachana ila
kwa kifo tu.
4.
Viapo
vya Wachawi:
Wachawi wafanyapo uchawi wao huapa kutimiza adhma zao.
5.
Kiapo
cha Mungu: Kiapo
cha Mungu kinalinda Uungu wake (Mwanzo 22:16-18). “ akasema,
Nimeapa kwa nafsi yangu asema BWANA, kwa kuwa umetenda neno hili, wala
hukunizuilia mwanao, mwanao wa pekee” Aina zote za viapo huapa kwa jina
la mamlaka zao za juu za rohoni zinazowaongoza, isipokuwa kiapo cha Mungu tu. Mungu
huapa kwa nafsi Yake; Haapi kwa mamlaka nyingine yoyote kwakuwa hakuna mamlaka iliyo
juu zaidi Yake.
Kiapo cha Mungu kina nguvu ya
kufanya yale yasiyowezekana yakawezekana. Mfano; Baiolojia na sayansi kwa
ujumla inasema, kwa desturi ya wanawake, mwanamke mwenye umri sawa na umri wa
Sara mkewe Ibrahimu hawezi kupata mimba na kuzaa mtoto kwa maana tayari
alishapita ukomo wa kuzaa.
Kiapa cha Mungu ni zaidi ya
sayansi kwa maana Mungu kwa kiapo na ahadi yake kwa Ibrahimu na Sara ni
kuwapatia mtoto; kwa kiapo cha Mungu, Sara akiwa na umri wa miaka tisini
alimzaa Isaka.
Mungu ni Mungu wa ahadi na baraka zake juu ya mtu anazifunga
na kiapo. Mungu hana mbadala wa ahadi zake. Ahadi ya Mungu imehakikishwa (2
Samweli 22:31, Zaburi 18:30).
Ahadi za Bwana hazikawii wala hazichelewi; huja kwa
wakati ambao Bwana ameukusudia. Mungu alimtaka Ibrahimu amtolee sadaka, na akaahidi
kumbariki Ibrahimu akimtii. Ibrahimu, akiyaheshimu maneno ya Mungu, akamtoa
mwanaye Isaka kuwa sadaka kwa Mungu. Mungu akaapa kuwa, kwakuwa Ibrahimu amemtii
“akasema, Nimeapa kwa nafsi yangu
asema BWANA, kwa kuwa umetenda neno hili, wala hukunizuilia mwanao, mwanao wa
pekee, 17katika kubariki nitakubariki, na katika kuzidisha nitauzidisha
uzao wako kama nyota za mbinguni, na kama mchanga ulioko pwani; na uzao wako
utamiliki mlango wa adui zao; 18na katika uzao wako mataifa yote ya dunia
watajibarikia; kwa sababu umetii sauti yangu. ” Mwanzo 22:16-18
1. Atambariki,
2. Atauzidisha uzao wake kama nyota za
mbinguni na kama mchanga ulioko pwani,
3. Uzao wa Ibrahimu utamiliki
milango ya adui zao, na
4. Uzao wa Ibrahimu utajibarikia
wenyewe.
Ahadi ya Mungu kwa wana wa Israeli: Baraka za Mungu kwa
Ibrahimu zinaonekana kwa wana wa Israeli wakiwa utumwani. Kwa kiapo, Mungu
aliwapa wana wa Israeli nchi ya maziwa na asali (Yeremia 11:5). Hata
sasa, sisi pia tunamiliki nchi na vyote viijazavyo kwa kiapo. Mungu humtendea
mtu sawasawa na kiapo. Kiapo ni kufungo (Ezekieli 16:59).
Kiapo cha Mungu kimefungana na neno la Mungu; Mungu
ameapa na akatamka neno lake ili watu wote walitii, ya kwamba, kila goti
litapigwa mbele zake na kila ulimi utaapa (Isaya 45:23). Kiapo cha
Mungu kimeweka “inclusive criteria” kwa kila mtu na kwa yeyote kwenye kila
nafasi; wakuu wa nchi, wakuu wa dola, wakuu wa taasisi, viongozi, au mtu
yeyote, mwema na muovu, kupiga goti mbele za Bwana.
Kiapo ni tendo la rohoni. Mashetani nayo hujua nguvu
ya kiapo. Marko 5:6-7; mtu mmoja mwenye pepo alipomuona Yesu,
pepo akamuongoza kumkimbilia Yesu na kumsujudia, na mara moja pepo akamuapisha Yesu
kwa Mungu ili asimtese.
Maneno ya pepo yule, “… Nakuapisha kwa Mungu
usinitese.” Yanamaana kuwa; -
1. Pepo anaapa ili kukwepa mateso,
2. Ukiapishwa ukaapishika hutaweza
kumwajibisha au kumtesa pepo/adui.
Ni muhimu sana kuvunja kiapo kilichowekwa na adui
yako kwa sababu, ikiwa adui yako amekuwahi kwenye kiapo, mashambulizi yako kwake
hayampati.
Kiapo kinaambatana na majaribu, na ukikiuka kiapo
hicho adhabu ni kifo. Mfalme Sauli alijifunga kwenye kiapo yeye na watu
wake/majeshi kwenda vitani bila kula (kwa kufunga) ili kulipa kisasi. Majeshi yakaogopa
kukiuka kiapo hicho. Kule vitani walipokuwa mwituni kukawa na asali ikidondoka
na kuleta tamaa ya kula lakini hakuna aliyejaribu kula kwa sababu ya kiapo
“Nao watu wa Israeli walisumbuka
sana siku ile; lakini Sauli alikuwa amewaapisha watu, akisema, Na alaaniwe mtu
awaye yote alaye chakula cho chote hata jioni, nipate kujilipiza kisasi juu ya
adui zangu. Basi hakuna mtu miongoni mwa watu aliyeonja chakula.” 1 Samweli 14:24-28
Mwana wa Sauli aitwaye Yonathani ambaye hakuwepo
wakati Sauli akiwaapisha watu wake, akala asali ile, akatiwa nuru machoni na
kuwapiga Wafilisti sana. Hata hivyo kwa kukiuka kiapo, Yonathani alistahili
kufa. Kama unauhusiano na kiapo kilichowekwa, ukikiuka unauwawa “Ndipo
Sauli akamwambia Yonathani, Niambie ulilolifanya. Basi Yonathani akamwambia,
akasema, Ni kweli, mimi nalionja asali kidogo kwa ncha ya fimbo ile iliyokuwa
mkononi mwangu; na tazama, imenipasa kufa.” 1 Samweli 14:43-44.
Kuna viapo vya namna mbalimbali; -
1.
Kiapo
cha Maneno:
Mtu huongea maneno bila kujua
wala kujali nguvu iliyopo nyuma ya maneno hayo. Maneno kama, “naapa kabisa” au “I
swear” yanatengeneza kiapo. Maneno yana nguvu kwenye maisha ya mtu. Kuna maneno
yanatamkwa na mtu, na ndiyo inakuwa chanzo cha matatizo anayoyapitia yeye au
mtu aliyetamkiwa maneno hayo. Maneno hayo pengine ni ya uongo au ya laana ila
kwa sababu ni kiapo, yanatekelezwa na mamlaka ya ulimwengu wa roho sawasawa na yalivyotamkwa.
Wana wa Israeli, kwa agano la
amani na Wagibeoni, wakaapa kutowaua Wagibeoni. Yoshua alipojua kuwa Wagibeoni
hawakueleza ukweli, na kwamba agano lililofanyika limetokana na uongo,
aliwaongoza wana wa Israeli kutowapiga Wagibeoni kwa sababu wakuu wa mkutano
walikuwa wamekwisha kuwaapia kwa Bwana. Wagibeoni wakaachwa kuishi nchi ya
ahadi kama watumwa kwa ajili ya nyumba ya Mungu “Naye Yoshua akafanya
amani pamoja nao, na kufanya agano nao, ili kwamba waachwe hai; na wakuu wa
mkutano wakawaapia.” Yoshua 9:15-23.
Ndoa ya Isaka ilihusisha kiapo
cha maneno cha Ibrahimu baba yake ili Isaka asipate mke miongoni wa wanawake wa
Kanaani (Mwanzo 24:1-4).
Nyuma ya maneno kuna roho: Yohana
6:63, Ezekieli 3:24, Yeremia 1:12, Yohana 1:14.
Kiapo cha maneno kinauwezo wa kubeba laana kwa sababu ya roho iliyopo nyuma
yake. Unaweza ukaanza jambo vizuri lakini mwisho halifanikiwi.
Maneno huapizwa sehemu yoyote;
njia panda, kwenye miti, majini n.k., hivyo kiapo ni lazima kivunjwe na kubomolewa
kwa jina la Yesu.
2.
Kiapo
cha Kufunga:
Hiki ni kiapo cha kutokula. Wana wa
Mungu wanapofunga kwa mambo fulani kwenye maisha yao, wana wa ibilisi nao
hufunga kwa mambo yao. Adui na wachawi wanaweza wakaapa kwamba hawatokula hadi
watakapokamilisha kuharibu maisha ya mtu. Hiki ni kiapo kikali sana. Waingiapo kwenye
kiapo hiki, hufanya kwa haraka sana na kwa bidii sana; kwa kadili wanavyokuwa
na njaa ndivyo wanakuwa na hasira sana. Hata hivyo, Mungu alichokiahidi juu ya
maisha yako ni lazima yatimie kwa sababu Mungu alishaweka kiapo juu ya maisha
yako.
Wayahudi zaidi ya 40 wamepatana
kufunga kwa kutokula wala kunywa chochote mpaka wamuue Paulo (Matendo ya
mitume 23:12-14).
Yeye atulindaye halali wala
hasinzii wala haruhusu miguu yetu isogenzwe kwa jina la Yesu (Zaburi 121);
Hapana uchawi kwa Yakobo (Hesabu 23:23).
3.
Kiapo
cha Damu:
Watu wanaapa wakiwa wanamwaga damu.
Kuna kiapo cha urafiki ambacho watu wanachanja damu zao wanazichanganya au
wanakunywa damu ndivyo hivyo kwa wachawi wanaweka kiapo chao kwa kumwaga damu
yao au wanatoa kafara zao kwa ajili ya kupokelewa kiapo chao. Kupitia kiapo cha
damu, damu inakuwa inaongea kwa ajili ya kiapo walichokiweka kwenye maisha ya
mtu huyo, “Musa akaitwaa ile damu, akawanyunyizia watu, akasema, Hii
ndiyo damu ya agano alilolifanya BWANA pamoja nanyi katika maneno haya yote.” Kutoka
24:8.
Mambo ambayo Mungu ameyaweka juu yako
ni lazima yatimie hata kama maadui wametoa kafara zao. Kiapo cha Mungu ni
lazima kitimizwe.
Wachawi huapa kwa siri kwenye
sehemu za viapo vyao, lakini Mungu aliyeviumba vitu vyote yupo kila mahali
watakapoenda kuapia; Mungu huwaona na hivyo hakuna siri (Zaburi 91:10,
Yohana 10:10).


0 Comments