UFUFUO
NA UZIMA CATHEDRAL
IBADA
YA JUMAPILI 06.04.2025
ASKOFU
DKT JOSEPHAT GWAJIMA
SOMO:
ULICHOKIBEBA NDIO CHANZO CHA VITA YAKO
![]() |
“Nayo mavumbi kuirudia nchi kama yalivyokuwa, Nayo
roho kumrudia Mungu aliyeitoa.” Mhubiri 12:7
Baba
na mama wanapokutana wao hutengeneza dongo yaani mwili, lakini Mungu ndiye anayeweka
roho ndani ya hilo dongo. Ndani ya hiyo roho Mungu anakuwa ameweka jukumu
flani ambalo anataka huyo mtu akalifanye. Mungu mbinguni anakuwa ana jambo lake
ambalo anataka kulifanya hapa duniani, hivyo anamtuma mtu duniani ndani ya
dongo ambalo ni mwili ili aifanye hiyo kazi kwa niaba yake. Mtu huyo anakuwa mwakilishi
wa Mungu duniani katika nyanja mbalimbali. Ndio maana kuna maraisi, wahandisi, madaktari
na wengine ambao Mungu amewapa majukumu ya kumuwakilisha duniani.
“Kilichozaliwa kwa mwili ni mwili; na kilichozaliwa
kwa Roho ni roho.” Yohana 3:6
Mtu anapokuja duniani, huja akiwa amebeba kusudi ndani yake ambalo Mungu amemuwekea. Ndani yake Mungu anakuwa ameweka vitu vya kuweza kumfanya atimize lile kusudi alilomuwekea. Katika ulimwengu wa roho, wachawi wanauwezo wakuona vile vitu na lile jukumu ambalo Mungu amempa mtu na kuanza kumpinga asiweze kutimiza jukumu hilo. Kutokana na kusudi hilo la Mungu ndani ya mtu, mara nyingi husababisha vita kutoka kwa shetani ili ashindwe kutimiza jukumu hilo.
“Kwa maana kila kitu kilichozaliwa na Mungu
huushinda ulimwengu; na huku ndiko kushinda kuushindako ulimwengu, hiyo imani
yetu.” 1Yohana 5:14
Mtu
aliyebeba jukumu kutoka kwa Mungu anakuwa na neema inayo mwongoza na kumsaidia ili
kutimiza jukumu lake. Ukitaka uweze kufanikiwa, lazima utembee katika njia ile uliyoitiwa. Mtu aliyeitiwa jukumu flani na Mungu analindwa na Mungu kwa sababu
jambo analotakiwa kulifanya ni jambo la Mungu mwenyewe. Yeye anakuwa mwakilishi
tu, ila mwenye jukumu hilo ni Mungu mwenyewe.
“Naam, hatasinzia wala hatalala usingizi, Yeye aliye mlinzi wa Israeli.” Zaburi 121:4
Kuna
sehemu Mungu anataka upite ili uende kwenye kusudi lako. Ingawa njiani kuna watu
ambao wanataka kukuzuia, ila Bwana akiwa upande wako, hakuna kitu cha kukuzuia. Kuna mambo ambayo mtu anapitia, Mungu huruhusu ili kumtengeneza
na kumfanya kuwa imara ili aweze kutimiza kusudi alilomuitia.
“Hataogopa habari mbaya; Moyo wake u imara ukimtumaini BWANA.” Zaburi 112:7
Aliyetumwa hana nguvu sawasawa na aliyemtuma, ila aliyetuma humpatia nguvu aliyemtuma ili kazi yake itimie. Wachawi na waganga kwenye ulimwengu wa roho hushindana na mtu aliyetumwa na Mungu, lakini hawawezi kufanikiwa kwa sababu Mungu anamlinda aliyemtuma kwaajili ya kusudi lake. Hivyo, vita yake mtu huyo ni kubwa kwenye ulimwengu wa roho katika ufalme wa giza na silaha yao kubwa ni laana.
“Basi Yesu akapaza sauti yake hekaluni, akifundisha
na kusema, Mimi mnanijua, na huko nitokako mnakujua; wala sikuja kwa nafsi
yangu; ila yeye aliyenipeleka ni wa kweli, msiyemjua ninyi. Mimi namjua,
kwa kuwa nimetoka kwake, naye ndiye aliyenituma.” Yohana 7:28-29
Kuna baadhi ya mambo mabaya yanaruhusiwa na Mungu yampate mtu ili kumpeleka kwenye ukuu wake. Mungu ili kutimiza kusudi lake duniani hutumia vitu vyote kama watumishi wake. Hata wachawi ni watumishi wa Mungu pale inapobidi ili kusudi la Mungu lisimame.
“Tazama, nimepewa amri kubariki,Yeye amebariki, nami
siwezi kulitangua Hakutazama uovu katika Yakobo,Wala hakuona ukaidi
katika Israeli.BWANA, Mungu wake, yu pamoja naye,Na sauti kuu ya mfalme i
katikati yao. Mungu amewaleta kutoka Misri,Naye ana nguvu kama nguvu za
nyati.Hakika hapana uchawi juu ya Yakobo,Wala hapana uganga juu ya Israeli.Sasa
habari za Yakobo na Israeli zitasemwa,Ni mambo gani aliyoyatenda Mungu! Tazama,
watu hawa wanaondoka kama simba mke,Na kama simba anajiinua nafsi yake,Hatalala
hata atakapokula mawindo,Na kunywa damu yao waliouawa.Balaki akamwambia
Balaamu, Basi usiwalaani kabisa, wala usiwabariki kabisa. Lakini Balaamu
akajibu akamwambia Balaki, Je! Sikukuambia ya kwamba, Kila neno BWANA
atakalolisema sina budi kulitenda?” Hesabu 23:20-25
Hakuna
mchawi anayeweza kuzuia hatima ya mtu. Hatima yako inafahamika kwenye
ulimwengu wa roho katika ufalme za giza. Yapo mambo ambayo mtu ni lazima ayafanye ili
kuweza kumruhusu Mungu kumuongoza katika kulitimiza kusudi lake.
0 Comments