google.com, pub-4324601895065941, DIRECT, f08c47fec0942fa0

Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

KUFUTA KALENDA ZA KICHAWI

UFUFUO NA UZIMA CATHEDRAL
IBADA YA JUMAPILI 24.05.2026
ASKOFU DKT GERSHOM MWAKILA
SOMO: KUFUTA KALENDA ZA KICHAWI


Kalenda ina asili ya kiroho. Kalenda haikuanza na watu ila na Mungu. Kalenda ambayo dunia inatumia ni ya ulimwengu wote. Mungu alipokuwa akiumba, aliumba kalenda pia; aliumba dunia katika namna ambayo kalenda itapatikana.

Dunia ina wataalamu mbalimbali ambao katika usomaji wao shuleni, kila walichosoma kiliumbwa na Mungu. Mungu ndiye mtaalamu wa kila kitu. Kwa mfano, kulingana na Jiografia (elementary), dunia ni miongoni mwa sayari nyingi zilizopo ulimwenguni lakini sayari tisa pekee ndiyo huzungumzwa sana.

Wakati wanajiografia wanafanya utafiti kuhusu dunia, waliona dunia ina mizunguko miwili.

1.   Dunia kujizungusha kwenye mhimili wake (rotation); matokeo ya dunia kujizungusha kwenye mhimili wake tunapata majira ya usiku na mchana. Mzunguko huo hukamilika kwa masaa ishirini na nne (24).

2.   Dunia kulizunguka jua (revolution). Dunia huzunguka jua kwa muda wa siku 3651/4 au 366. Matokeo ya dunia kulizunguka jua tunapata majira ya mwaka. Majira haya ni ya aina nne, yaani, i) Kiangazi ii) Masika iii) Vuli, na iv) Kipupwe.

Majira yanasaidia mipango ya shughuli za kijamii. Majira huendana na shughuli fulani za kijamii; mfano, wakati wa Masika shughuli za kijamii ni kilimo, na Disemba wakulima huanza kuandaa mashamba. Imani ya mkulima ipo kwenye majira. Kiangazi ni wakati wa joto.

Mjinga asiyejua majira akiamua kulima wakati wa kiangazi, ataingia gharama kubwa sana kupata matokeo chanya. Mkulima hapandi mbegu ili kushawishi majira, ila majira ndiyo huongoza shughuli za watu.

Mfano: Hatuvai sweta ili iwe baridi, ila baridi husababisha tuvae sweta; hatuvui sweta ili iwe joto, ila joto husababisha tuvue sweta.

Majira katika uumbaji wa Bwana yameandikwa katika kitabu cha Mwanzo 1:14, yaani

Mungu akasema, Na iwe mianga katika anga la mbingu ili itenge kati ya mchana na usiku; nayo iwe ndiyo dalili na majira na siku na miaka;”

Mungu ndiye aliyeumba majira na akaweka shughuli ndani ya majira (Mhubiri 3:1).  Mambo yote chini ya mbingu yamewekwa kuakisi majira yake. Mfano: Lia kwenye majira ya kulia, na furahi kwenye majira ya furaha; utaonekana mtu wa ajabu sana kulia kwenye majira ya furaha na kufurahi kwenye majira ya kulia (kucheka kwa furaha msibani, na kulia kwa huzuni harusini).  Katika mambo yote, majira hayatakoma

“Muda nchi idumupo, majira ya kupanda, na mavuno, wakati wa baridi na wakati wa hari, wakati wa kaskazi na wakati wa kusi, mchana na usiku, havitakoma.” Mwanzo 8:22.

Hekima na akili kuliko zote ni kuwa na ufahamu wa nyakati na majira, na kujua cha kufanya na kwa wakati gani ukifanye. Hata majira haya ya mfungo wa siku 40, baba yetu ameweka mfungo huu kipindi hiki kwani majira ya watu kupenya kwenye biashara, ajira, kazi, ndoa, kwenye yale wayatafutayo kwa muda mrefu ni sasa, kwa jina la Yesu.

Majira yote yamepanga matukio. Wanadamu hupanga ratiba zao kulingana na majira (1 Mambo ya Nyakati 12:32). Kuna wepesi wa kufanya jambo ikiwa unalifanya katika nyakati na majira yake. Sisi tunaye baba anayejua nyakati na majira, na watu watende nini ili wapate wanavyovitafuta.

Yesu alilia akiangalia Yerusalemu na kusema, laiti ungelijua majira haya, usingetenda hayo utendayo; lakini yamefichwa machoni pako (Luka 19:41-44). Kalenda huwa inafichwa; usipojua kalenda za kichawi vizuri, adui atakuzunguka, atakujengea boma na atakuangusha wewe na watoto wako. Fanya likupasalo kufanya ili kuzijua kalenda za adui.

Kulogwa, kuharibu mimba, utasa, magonjwa, laana, mikosi, ajali, na mambo ya adui kama hayo, yamewekwa kwenye kalenda za kichawi. Wachawi hupanga kwenye kalenda zao ili muda ukifika uaibike, upate ajali, uumwe, upate hasara, n.k., na adui ana tabia ya kukamata ufahamu wa mtu ili asijue majira yake; hapo ndiyo adui anapata nafasi ya kutimiza mambo yaliyo kwenye kalenda yake ya kichawi. Wachawi huficha kalenda zao ili zisijulikane wazi kwa watu; huloga akili watu wasijue nyakati na majira (2 Wakorintho 4:4). Kile ambacho hakijasajiliwa kwenye akili, jicho haliwezi kukiona: Unapaswa kuzirarua, kuzichana na kuzifuta kalenda za kichawi, kwa jina la Yesu.

Kufanya kazi ndani ya majira kuna neema yake. Kuna mambo ya kufanya leo yana mahusiano na mambo yako ya kesho. Furaha ya leo ni kwa sababu ya yale tulitengeneza jana. Tunachotengeneza leo kina mahusiano na watoto, mafanikio, mega church, au chochote cha mafanikio ya mtu cha kesho. Futa kalenda leo ili yale ya kesho yatokee kama vile Mungu alivyoyakusudia kwako. Ukiziondoa kalenda za kichawi, unamuondolea nguvu adui yako.

Tunaomba ili tupate njia kwa Mungu, sisi na wote wanaotuhusu. Njia zinapatikana kwa kufuta kalenda za kichawi. Ukiondoa kalenda umeondoa matukio ya kichawi kwa sababu wachawi huloga ndani ya kalenda zao. Ukiondoa kalenda shetani na wachawi wanabaki wanamangamanga hawana ujanja.

Kuna kalenda za aina mbili; kalenda za Mungu na kalenda za kichawi.

1.   Kalenda za Mungu.

Mungu akitaka kufanya jambo lolote anafuata kalenda yake; haruki hata nukta ya kalenda yake. Mungu ana majira na nyakati ambazo ameweka kwa ajili ya kufanya kila jambo katika uso wa nchi.

Nguvu ya kalenda ya Mungu ipo pale ambapo mtu anakuwa anajua nini cha kufanya katika majira fulani. Usipojua nini cha kufanya, kalenda ya Mungu inakuwa haina nguvu juu ya maisha yako. Hivyo, siri ya nguvu ya kalenda ya Mungu katika maisha ya mtu ni akili na hekima ya kujua yakupasayo kufanya.

Nguvu ya mtu ipo kwenye maarifa ya mtu; nguvu kidogo, maarifa kidogo; nguvu nyingi, maarifa mengi (Hosea 4:6). Kalenda ya Mungu ina nguvu pale mtu aliyekusudiwa anapokuwa na maarifa juu yake.

Mifano ya Kalenda za Mungu:

a)    Kalenda ya kuwatoa wana wa Israeli utumwani.

“BWANA akamwambia Abramu, Ujue hakika ya kwamba uzao wako utakuwa mgeni katika nchi isiyo yake, watawatumikia watu wale, nao watateswa muda wa miaka mia nne. 14Hata na taifa lile, watakaowatumikia, nitawahukumu; baadaye watatoka na mali mengi.” Mwanzo 15:13-14

Wana wa Israeli kuwa utumwani kwenye nchi ya ugeni, majira yake yalipangwa na Mungu. Kwenye kalenda ya Mungu, aliwaona wana wa Israeli wengi wakati Ibrahimu hata hajamzaa Isaka.

Mungu alikuwa ameandaa mpango wa kuwatoa wana wa Israeli utumwani hata kabla ya wakati wa kutoka Misri kufika. Bwana huona mwisho wa jambo lolote mwanzoni, na huweka kwenye kalenda yake ili muda unapofika akutendee. Mafanikio yako, ushindi wako, kumiliki kwako, na kuwa na kila kitu unachohitaji, yapo kwenye kalenda ya Bwana.

Kabla taifa la Israeli kuwepo, Mungu alimwambia Ibrahimu atawatoa wana wa Israeli utumwani na kuwapeleka katika nchi ya ahadi. Mungu aliyaona mateso ya wana wa Israeli kabla hawajazaliwa, na alimuona Farao kabla ya utumwa. Hivyo, kalenda ya Mungu ya kuwatoa wana wa Israeli utumwani ilikuwepo tangu mwanzo kabla ya taifa la Israeli kuwepo.

b)   Kalenda ya Yusufu kuwa Waziri Mkuu wa Misri

Mungu alikuwa ameandaa mpango wa Yusufu mwana wa Yakobo kufika kwenye nafasi ya Waziri mkuu wa Misri. Mungu aliruhusu Yusufu auzwe Misri na ndugu zake; Yusufu akafika Misri bila kutumia ghaama yoyote. Kalenda ya Mungu iliruhusu Yusufu auzwe Misri.

Akiwa mtumwa Misri, Yusufu alisingiziwa kosa akapelekwa gerezani. Ulikuwa mpango wa Mungu kupitia kalenda yake kuwa, ili Yusufu afikie hatma yake ni lazima awe mfungwa gerezani. Mungu ana desturi ya kuruhusu baadhi ya mambo yakukute ili akufikishe kwenye hatma yako. Mungu akampa ndoto Farao kwa makusudi akijua gerezani yupo Yusufu mwenye uwezo wa kutafsiri ndoto ambaye alikuwa na mpango nae. Mungu akamuinua mtumishi wa Farao kumtaja Yusufu kwa Farao kuwa anaweza kutafsiri ndoto ya Farao. Kwa hiyo tunaona kila hatua aliyoipitia Yusufu ilikuwa na mahusiano ya kumfikisha kwenye hatma yake; kuuzwa na ndugu zake Misri, kufungwa gerezani na kutafsiri ndoto ya Farao zote zilikuwa ni njia kwenye kalenda ya Mungu kufanikisha hatma ya Yusufu kuwa Waziri mkuu wa Misri, na wana wa Israeli kufika Misri.

c)    Kalenda ya kuzaliwa, kufa na kufufuka kwa Yesu.

Miaka mia saba kabla ya Yesu kuzaliwa, nabii Isaya alioneshwa (Isaya 1:1) kuwa Yesu atazaliwa ili kuukomboa ulimwengu. Kuzaliwa kwake Yesu ilikuwa ni mpango wa Mungu; kabla hajazaliwa, hajafa, hajafufuka, hajatukuzwa Yesu, Mungu alijua yote imekwisha.

Katika maono yake, Isaya alimuona bikra akichukua mimba na kuzaa mtoto (Isaya 7:14). Ni kanuni ya Mungu kuwa, akiyaona huyasema hata kabla ya kutokea; yanatokea kwa sababu yamewekwa kwenye kalenda ya Mungu.

Isaya anaona serikali na kusema kabla haijakuwapo; miaka mia saba badae, serikali inatokea

“Maana kwa ajili yetu mtoto amezaliwa, Tumepewa mtoto mwanamume; Na uweza wa kifalme utakuwa begani mwake; Naye ataitwa jina lake, Mshauri wa ajabu, Mungu mwenye nguvu, Baba wa milele, Mfalme wa amani.” Isaya 9:6

Isaya anasema kuhusu, kuchukua masikitiko yetu na kuteswa kwa ajili yetu, na kwamba kwa hayo yote sisi tumeponywa, kabla hakujakuwako “Hakika ameyachukua masikitiko yetu,Amejitwika huzuni zetu; Lakini tulimdhania ya kuwa amepigwa,Amepigwa na Mungu, na kuteswa. Bali alijeruhiwa kwa makosa yetu,Alichubuliwa kwa maovu yetu; Adhabu ya amani yetu ilikuwa juu yake, Na kwa kupigwa kwake sisi tumepona.” Isaya 53:4-5

Miaka mia saba baada ya maono ya Isaya, ukafika utimilifu wa wakati ambapo Yesu akazaliwa kama ilivyotabiriwa/kama kalenda ya Bwana ilivyo (Wagalatia 4:4).

Maisha yamejaa maelekezo/kalenda za Mungu zimejaa maelekezo. Mungu alipanga Yesu azaliwe bethlehemu na akamuelekeza Yusufu ampeleke Mariamu huko; akamzaa katika zizi la ng’ombe. Baada ya muda mfalme Herode alitaka kumuua mtoto Yesu, na Mungu akamuelekeza Yusufu amtoroshe mtoto kwenda Misri. Baada ya mfalme Herode kufa, Mungu akamuelekeza Yusufu kwenda Nazareti, na badae ulipofika wakati wa kubatizwa, Yesu akabatizwa, na wakati wa kufa alikufa, na wakati wa kupaa kurudi mbinguni alipaa, na hakuna kilichomzuia kwa sababu kalenda ya Mungu ilikuwa imewekwa hivyo. Hapo tunaona mchoro mzima ulipangwa na Mungu hata kabla Yesu kuzaliwa.

Bwana hututukuza kwa kutupenda na kwa kutuchagua tangu asili (Warumi 8:30, Yohana 17:22). Bwana ametupa utukufu na heshima. Vyote alivyoviumba Bwana vinapaswa kutuheshimu. Tumewekwa kusimamia vyote kwa niaba ya Bwana, na mafanikio yatokee sawasawa na kalenda ya Bwana.

Watumishi wa Mungu ni wasimamizi wa kalenda ya bwana. Bwana amewachagua kusimamia yote ili watu wafanikiwe, watu warudishwe, watu waponywe magonjwa, wakupigwa wapigwe, wakubomolewa wabomolewe, wakutukuzwa watukuzwe.

Hata muda tulionao kuhubiri na kusema neno la Bwana upo kwenye kalenda ya Mungu. Mahubiri yana nyakati; hayatakuwepo wakati wote. Hii ni mbaya (Amosi 8:11-12).

Ukiona jambo linapatikana kwa wingi sana ujue lina thamani kubwa. Vile vitu vya umuhimu sana, Mungu amefanya vipatikane kwa urahisi sana. Vitu vya bure vina gharama sana; kama visingekuwa vinapatikana bure, ingekuwa ni vigumu sana kuvimudu. Mfano; hospitalini, dawa za kufubaza virusi vya ukimwi, ARVs, zinatolewa bure kwa sababu kama isingekuwa hivyo, gharama yake ni kubwa kwa kidonge kimoja na hivyo isingekuwa rahisi kumudu kwa walio wengi.

Kalenda ya Mungu huwa haibadiliki. Mungu amesema ataleta njaa ya neno lake majira hayo yakifika. Watu watalitafuta neno la Mungu lakini hawatalipata. Katika majira haya, neno linatusisitiza tulitafute sana maadamu linapatikana (Isaya 55:6). Mungu atupe akili ya kuyafahamu haya ili tusipate kiu ya neno majira yakifika wakati halipatikani, na kule litakakoenda tuweko.

2.   Kalenda za Kichawi

Wachawi huandaa mipango yao namna watakavyoleta uharibifu kwenye maisha ya mtu. Hupanga walete lini, mahali gani na kwa njia gani uharibifu wao. Huandaa mpango siku nyingi. Utekelezaji wa uharibifu huo huitwa pia siku ya uovu au siku ya mabaya (Waefeso 6:13, Zaburi 27:5).

Uharibifu ukiwekwa umpate mtu, utampata kama haukubatilishwa. Mfano; Hamani alipanga ubaya dhidi ya Mordekai na kutafuta majira sahihi ya kumuua Mordekai na Wayahudi wote. Hamani akamshawishi mfalme Ahasuero akakubali na nyaraka zikaandikwa na kusambazwa mikoa yote. Siku ya uovu ikapatikana kuwa tarehe kumi na tatu ya mwezi wa kumi na mbili.

Mordekai na Esta wakaazimia Wayahudi kufunga ili kubatilisha uovu unaopangwa na Hamani. Esta akamwendea mfalme kinyume na sheria na Wayahudi wakafanikiwa kubatilisha majira yaliyoandaliwa na Hamani kwa ajili ya uovu juu ya Mordekai na Wayahudi wote (Esta 3:3-15, 4:15-17). Bwana hutujibu kinyume cha sheria kupitia maombi tumwombayo. Sara alipata mimba na kuzaa kinyume cha sheria.

Bwana huigeuza siku ya uovu kuwa siku ya nuru, furaha, shangwe na amani kwa wana wa Mungu/majeshi ya Bwana. Bwana huitangua kalenda ya wachawi/uovu, na ule mti ulioandaliwa na wana wa uovu ili kuwatundika wana wa Mungu, utatumika kuwatundika wana wa uovu wenyewe 

"Naye Mordekai akatoka usoni pa mfalme, amevaa mavazi ya kifalme, ya rangi ya samawi na nyeupe, mwenye taji kubwa ya dhahabu, na joho ya kitani safi na rangi ya zambarau. Mji wa Shushani wakapaza sauti, wakashangilia. Ikawa nuru na furaha na shangwe na heshima kwa Wayahudi. Na katika kila jimbo, na kila mji, po pote palipowasili amri ya mfalme na mbiu yake, Wayahudi wakapata furaha na shangwe, karamu na sikukuu. Hata wengi wa watu wa nchi wakajifanya Wayahudi, kwa kuwa hofu ya Wayahudi imewaangukia."Esta 8:15-17

BONYEZA HAPA KUANGALIA IBADA YA JUMAPILI


Post a Comment

0 Comments