UFUFUO NA UZIMA
CATHEDRAL
IBADA YA JUMAPILI 03.05.2026
ASKOFU DKT GERSHOM
MWAKILA
SOMO: KUNYAMAZISHA
KAFARA YA DAMU
![]() |
Kila mamlaka ya kimwili imesimikwa na mamlaka ya rohoni. Jambo lolote linapoishinda mamlaka ya kimwili, mamlaka hiyo huirejea mamlaka ya rohoni kuomba msaada. Msaada utolewao ni uimarisho ambao hutolewa pale mamlaka ya kimwili ikitoa kafara.
Mamlaka ya rohoni inapokuwa imedhoofika nayo hutaka
sadaka ya kafara kutoka kwa mamlaka ya kimwili ili mamlaka ya rohoni iimarike. Nguvu
ya mamlaka ya rohoni inategemea kafara.
Kafara ni nini?
Kafara ni sadaka inayohitaji damu ya mwanadamu,
mnyama ama ndege. Kafara yoyote inahusisha damu. Kwenye biblia neno kafara limeandikwa
mara 19 na neno damu limeandikwa mara 369. Zipo mamlaka za kidunia kama
watawala, viongozi, wafanyabiashara, mke/mume, mchungaji, askofu, shehe au mtu yeyote
unayeongozana naye, zimesimama na kufanikiwa kuwa hapo zilipo kwa sababu ya kafara
ya damu. Kafara hiyo ni ama ya kutoka kwa Mungu au kwa shetani.
“Mambo yote yawatukia wote
sawasawa; kuna tukio moja kwake mwenye haki na kwake asiye haki; kwa mtu mwema
na kwa mtu mwovu; kwa mtu aliye safi na kwa mtu asiye safi; kwake yeye atoaye
kafara na kwake asiyetoa kafara; kama alivyo huyo mwema ndivyo alivyo mwenye
dhambi; yeye aapaye na yeye aogopaye kiapo.” Mhubiri 9:2, na 1 Wakoritho 10:20
Kafara ya damu hujulikana vilevile kama sadaka kwa
mashetani. Mungu hawapendi watu watoao kafara kwa mashetani au kushirikiana na mtu
anayetoa kafara. Wachawi hutoa kafara watu walio katika uzao wao. Mungu
anakataza kutoa kafara kwa mashetani ya kizazi chako chochote
“Nawe usitoe kizazi chako cho
chote na kuwapisha kwa Moleki, wala usilinajisi jina la Mungu wako; mimi ndimi
BWANA.” Mambo ya walawi 18:21.
Kwakuwa Mungu anakataza kutoa kafara, ipo adhabu kwa
wote watoao kafara, nayo ni kuuawa bila huruma (Mambo ya walawi 20:2,4).
Wapo watu wanaweza wakakwambia, “inakuhusu nini nikitoa kafara ya mtoto wangu,
kwani ni wako?”; hata kama mtoto ni wake, tayari ni maelekezo ya Mungu kumuua
(Kutoka 22:18).
Kama wenyeji wa nchi ama wale wapaswao kumuua
wasipomuua mtoa kafara kwa mashetani, Mungu atamkatilia mbali yeye na wote
wanaomuonea huruma “Tena kama wenyeji wa nchi wakimfumbia macho mtu huyo
kwa njia yo yote, hapo atoapo katika kizazi chake na kumpa Moleki, wasimwue;” Mambo
ya walawi 20:4.
Mtu yeyote katika familia, ukoo au katika jamii au
taifa akitoa kafara yapaswa auawe. Hauawi kwa namna ya mwilini bali kwa namna
ya rohoni na udhihirisho unakuwa mwilini. Mungu hajashindwa Yeye Mwenyewe
kumwua ila Mungu anatuagiza sisi na anaangalia utii wetu kwake. Mungu akikwambia;
-
-
Ng’oa,
lazima ung’oe;
-
Bomoa,
lazima ubomoe;
-
Haribu,
lazima uharibu;
-
Fyeka,
lazima ufyeke, n.k.
Mfano; Mfalme Sauli aliagizwa na Mungu amuue mfalme
Hagagi lakini hakumwua; Mungu akaweka hasira dhidi yake, lakini Mungu alimuagiza
Nabii Samueli kumuua Hagagi naye hakuzuia upanga wake, akakata kichwa cha
Hagagi kwa utii kwa Mungu.
Adui wa Mungu ni adui yetu. Nyanyua upanga wako kwa
adui yeyote. Huruma yako ikizidi kuliko huruma ya Mungu inakupeleka shimoni. Huruma
yako isizidi huruma ya Mungu, na wema wako usizidi wema wa Mungu.
Ukizungukwa na marafiki au watu washirikina,
wachawi, wezi na wewe baada ya muda utakuwa kama wao. Katika Agano la Kale, Mfalme
Suleiman pamoja na kuwa alifanya mambo makubwa kwa ajili ya Bwana, alizungukwa
na watu wengi watoa kafara kama mfalme wa Moabu; Mfalme Suleiman akajiingiza
kwenye kutoa kafara na likawa chukizo kwa Mungu (1 Wafalme 11:6-12).
Katika Agano Jipya, Moleki apokeaye sadaka za kafara
za watoto ametajwa pia. Moleki ni yaleyale mashetani yaliyotajwa kwenye Mambo
ya Walawi (Matendo ya mitume 7:43).
Yeremia 19:5 imeandika kuhusu kafara za watoto
kwa Baali kama sadaka za kuteketezwa kwa kuchomwa moto. Kafara pia inaonekana
katika Yeremia 7:31 na Ezekieli 20:25-28.
Kutoka 1:16 nayo imeandika kuhusu kuuawa kwa
watoto wa kiume ili wasiongezeke. Watoto wa kiume hubeba mbegu ya kuongezeka;
Farao alipambana na mbegu kwa kuua watoto wa kiume tu. Mbegu ikiwa imara
ongezeko ni lazima. Mfano; Ufufuo na Uzima kama Mega Church ilianza kama mbegu
ya mtu mmoja, ikapandwa, ikaoza, ikastawi; imeongezeka na kuenea Tanzania yote na
nje ya mipaka yake.
Mbegu inayozalisha hufichwa; Musa alitaka kuuawa
akiwa mtoto akafichwa. Musa alikula chakula cha wanaomtafuta, alikunywa maji ya
wanaomtafuta, akalelewa na kukuzwa na wanaomtafuta. Kwa kusudi la Mungu la
kuwaongoza wana wa Israeli kutoka utumwani, Mungu aliilinda mbegu (Musa) na
kuiongoza mbegu hiyo ili ichepuke.
Hekima ya Mungu ni ya ajabu sana. Farao ndiye alimlea
Musa, lakini Mungu akaona ni Musa ndiye astahiliye kumtandika Farao. Farao alikuwa
anatoa kafara kwa joka lililokuwa linakaa katika mto huko Misri. Hata katika
maisha yetu wapo watu hutulea na kutupa mahitaji ya kukua kwetu; wakati
mwingine na shule wanatusomesha lakini wao ndiyo huyafunga maisha yetu kwa
kafara.
Mungu anataka mtu mwenyewe amtandike Farao atoaye
kafara kuharibu maisha ya mtu. Mungu anaagiza Farao katika maisha ya mtu
atandikwe mpaka amuache mtu aende.
Kwa sheria ya Mungu, kila kilichozaliwa cha kwanza
ni cha Mungu ila watu wengine wanatoa wazaliwa wao wa kwanza kwa miungu ambayo
ni mashetani.
Kwanini wachawi wanatoa kafara ya
Damu?
“Akasema, Umefanya nini? Sauti ya
damu ya ndugu yako inanililia kutoka katika ardhi.” Mwanzo 4:10
- Damu inaongea;
- Damu hunyamazishwa;
- Damu inalia;
Damu ya mwenye haki inapolia Mungu huisikia sauti hiyo.
Damu ya kafara inapomwagwa mashetani huisikia.
Damu inapomwagwa inabeba maneno ya huyo mchinjaji na
mashetani wanasikia. Damu iliyomwagwa ikasababisha umasikini, magonjwa, au
chochote kibaya kwenye maisha ya mtu, inabidi inyamazishwe ili matatizo yakome.
-
Damu
ina uhai
Uhai wa mwanadamu upo katika damu yake (Mwanzo
9:4-6). Uhai wa mnyama pia upo katika damu ya mnyama huyo. Damu ya mtu ikimwagika
uhai wa mtu unamtoka.
Damu, kupitia madhabahu, ina upatanisho (Mambo
ya walawi 17:10-11). Tumepewa, juu ya madhabahu, damu ya Yesu
itupatanishayo na Mungu (Mathayo 26:28).
Damu ya Yesu inapokuwa kwenye madhabahu inaunganisha
nafsi ya mtu na Mungu. Wachawi nao hujiambatanisha na mashetani kwa kupitia
nafsi zao kwenye madhabahu zao kwa kupia kafara ya damu wanazozitoa kwa
mashetani.
Kwa nini watu wanatoa kafara ya damu?
1 Wafalme 16:31-34
Mahusiano ya mkuu wa nchi kati yake na Mungu au
shetani ndiyo huamua uhusiano wa nchi na mamlaka ya rohoni. Kuna misingi
imejengwa ya kutawala eneo hilo kwa kafara ya damu za watu. Viongozi tulionao,
kama asipokuwa na Mungu basi anakuwa na mganga wake; kama ana mganga wake,
lazima katoa kafara ya damu ili asimame kwa nafasi aliyonayo.
Ahabu alimuuzi Mungu kuliko wafalme wote wa Israeli waliomtangulia;
Ahabu alikuwa mchawi.
Wakati wana wa Israeli wanavuka mto Yordani kuelekea
Kanaani, Yoshua aliwaongoza kuangusha ukuta wa Yeriko, na akaweka agano na
Mungu kuwa alaaniwe mtu yeyote atakayeijenga yeriko waliyoiangusha.
Katika utawala wa Ahabu, Hieli Mbetheli akaijenga
Yeriko kwa kutoa kafara ya mzaliwa wake wa kwanza na laana ikawa juu yao.
Ahabu alizungukwa na wachawi na kuamini nguvu ya wachawi
kumtegemea mungu Baali. Ahabu mwenye kuamini wachawi wake 450 alikuwa mwenye
kiburi hata asimuheshimu nabii Eliya.
Eliya akaamua kukomesha uchawi kwa kushindanisha
nguvu za Mungu anayemwamini na nguvu za Baali anayeaminiwa na Ahabu na wachawi
wake 450. Nguvu za Mungu haziangalii ni wangapi wapo upande wake, hata mtu
mmoja anatosha kuangusha maelfu ya watu wasiomwamini Mungu.
Ili mamlaka ya kimwili ipate muunganiko na mamlaka
ya rohoni, ni lazima kuwepo na daraja ambalo ni kiunganishi kati ya mamlaka
hizo; Daraja hilo ni madhabahu. Wachawi 450 hawakufanikiwa kuzungumza na
kupatana na Baali kwasababu hawakulijenga daraja kati yao na Baali; tunaamini
vilevile kuwa nabii Eliya alikuwa amemfunga Baali (Mathayo 16:19,
Marko 3:27).
Eliya aliijenga madhabahu ya Bwana iliyokuwa
imevunjika na kumuita Mungu ajulikane kama kweli ni Mungu. Baada ya Mungu
kujulikana ndiye Mungu wa kweli, nabii Eliya akaamuru wale wachawi 450
wakamatwe (1 Wafalme 18).
Kwanini watu wanatoa kafara?
Wachawi hawapendi kujitoa wao kama kafara, na kafara
kubwa kwa mashetani ni wanapojitoa wao wenyewe kama kafara. Kwasababu hii watu
hutoa kafara kwa ajili yao.
Watu wanatoa kafara kwasababu wanaona mambo yao
hayaendi vizuri, au wanaona wanaelekea kushindwa kwenye mambo wanayoyashindania;
ni kama wanatoa rushwa ya rohoni ili waimarishwe, yaani, mtu asiyefaa na
wakushindwa anatoa kafara ili aimarike na kushinda.
Kafara inatolewa ili kufanikisha namna mbili; -
1.
Kumuimarisha
anayetoa kafara ambaye ni dhaifu ama amekuwa dhaifu. Watu wanapokuwa wameshindwa
au kuwa dhaifu kwenye mambo fulani wanayoyataka, hutoa kafara ili kufanya wawe wenye
nguvu au waongeze nguvu ya kuwashinda wanaoshindana nao;
2.
Anakuwa
anamdhoofisha adui yake ambaye ni imara kuliko yeye ili awe dhaifu na amshinde.
Wapo wanasiasa kwa ngazi tofauti kama vile udiwani, ubunge,
uraisi, na vyeo vingine, hutoa kafara kwa ajili ya mafanikio katika siasa zao. Biblia
imeandika, Mfalme wa Babeli (raisi wa nchi) anatumia uchawi kwa kutoa sadaka
kwa mashetani (Terafi) ili apate kura za Yerusalemu (Ezekieli 21:21).
Majeshi ya Bwana ndiyo kiboko ya wanasiasa wachawi. Bwana
anasema atakipindua kiti cha mwanasiasa mchawi na hakitakuwepo tena mpaka atakapokuja
ambaye ni haki yake, naye atampatia (Ezekieli 21:27).
Biblia imeandikwa kuwa Mfalme wa Moabu aliposhindwa
vitani aliamua kutoa kafara kwa mashetani ya mzaliwa wake wa kwanza, ambaye
ndiye alikuwa mrithi wa kiti chake (2 Wafalme 3:26-27).
Kafara inaweza ikamfanya mtu kuahirisha ahirisha
mambo. Hatma ya mtu inachorwa na Mungu ila kwasababu ya kafara ambayo wachawi wanatoa
kwa mashetani, inamfanya mtu kusitasita kwenda kwenye hatma yake ambayo Mungu
ameamua aende.
Ni kanuni ya rohoni kuwa mamlaka inayohusisha watu
inahitaji kafara. Kafara inaweza kufanya mtu awe maarufu sana hata kama anachokifanya
sio cha msingi; mambo au umaarufu huo unatokana na kafara ya damu iliyoambatana
na maneno yaliyonenwa wakati wa kumwaga damu hiyo. Kwa Kadiri damu inavyoongea,
inaongea maneno sawasawa na maelekezo yaliyotolewa kwa mashetani.
Sisi hatumwagi damu za wanyama; kafara yetu
ilifanyika pale msalabani. Yesu alitoa uhai wake na damu yake iliyomwagika
ndiyo tuitumiayo kumshinda shetani (Ufunuo 12:11). Damu ya
Mwana-kondoo inanena mema.
Kafara inawezakufanya taifa liwe kwenye kufungwa. Nyuma
ya shida ya mtu au umasikini wa mtu, ipo damu inanena. Kuna mwingine damu
imemwagwa ili akae kwenye vifungo. Kwa kadiri damu inavyozungumza kwenye
ulimwengu wa roho, mashetani wanasikia na kutekeleza.
Iko sauti ndani ya damu. Damu ya Yesu Kristo nayo
inazungumza (Waebrania 12:24). Damu ya Yesu inanyamazisha kafara
iliyotolewa ili mtu asipate. Damu ya Yesu ina nguvu ya kunyamazisha damu ya
kikafara inayozuia mtu asimiliki urithi wake kama mwana wa Mungu.
Lengo la kunyamazisha kafara ni kutaka Mungu wetu aabudiwe
na bendera Yake isimamae ili bendera nyingine zote zishushwe.


0 Comments