UFUFUO NA UZIMA
CATHEDRAL
IBADA YA JUMAPILI 31.05.2026
ASKOFU DKT GERSHOM
MWAKILA
SOMO: NDOTO YA
MAISHA YAKO
![]() |
Kwa vinywa vya mashahidi wa mwili, ndoto huthibitika. Ndoto ni halisia; ndoto ni bayana. Ndoto ya mtu ni hatima ya mtu, ndoto ya mtu ni utajiri wa mtu, ndoto ya mtu ni maisha ya mtu, ndoto ya mtu ni mafanikio ya mtu, ndoto ya mtu ni kushinda au kushindwa kwa mtu. Kwa njia ya ndoto unaweza ukapata, na kwa njia ya ndoto unaweza ukakosa.
Ndoto zipo kwa mtazamo wa aina mbili. Mtazamo wa
kwanza ni ndoto anayoota mtu kwa sababu amelala; hutokea mtu akiwa usingizini akaota
ndoto kuhusu tukio fulani. Mtazamo wa pili ni ndoto kwa namna ya matamanio ya
mtu; mtu kutamani aishi maisha fulani, amiliki nyumba ya namna fulani, awe na
mke wa namna fulani, n.k. haihitaji mtu kulala; Mfano wa ndoto ya namna hii ni mtu
kusema, “Nimepata kazi ya ndoto yangu”. Matamanio ya mtu kuhusu
jambo fulani, ni ndoto ya mtu.
Maarifa ya ndoto ni ya muhimu. Kuwa na matamanio kuhusu jambo fulani / ndoto / maono bila kuwa na maarifa ni jambo baya na ni tatizo. Ukikosa maarifa kuhusu ndoto au maono yako utaangamia, kama ilivyoandikwa katika Hosea 4:6 na
“Pasipo maono, watu huacha
kujizuia; Bali ana heri mtu yule aishikaye sheria.” Mithali 29:18.
Kama huna maono au ndoto, huwezi kujizuia;
kunaangamiza, kwa sababu unakuwa kwenye hatari ya kupata madhara kwenye kila
ufanyalo. Mwenye maono hujizuia kwenye mambo fulani ili aweze kulinda maono na
ndoto zake.
Ndoto inatafsiri nyingi. Maana halisia ya ndoto
inaweza ikaelezwa hivi; -
1.
Ndoto
ni kiashiria cha rohoni cha kuwa mtu atakuwa nani hapo badae.
2.
Ndoto
ni mfumo wa maisha unaomuongoza mtu na kuonesha mtu huyo ataishia wapi.
3.
Ndoto
ni lugha ambayo Mungu huitumia kuwasiliana na watu wake.
4.
Ndoto
ni hati miliki ya mtu kuhusu hatima yake. Hekima ni kupata hati miliki ambayo
ni maisha ya mtu.
5.
Ndoto
ni mawasiliano ya mtu ambaye ni roho, na ulimwengu wa roho; ni ama mtu
anawasiliana na Mungu au Ibilisi.
Mungu ndiye asili ya ndoto. Mungu alikuwa na
matamanio yake; hiyo ni ndoto ya Mungu. Mungu alitamani kuwa na mtu wa mfano
wake, hivyo, akamfanya mtu kwa mfano wake na kwa sura yake, na mwenye kutenda
kazi kama Mungu mwenyewe. Tumefanyika kuwa watu wa ndoto ya Bwana.
Mungu ndiye mwanzilishi wa mipango na Mawazo. Mawazo
yetu na mipango yetu haifanani kutokana na makusudi ya Mungu. Kila mtu amebeba
kusudi la Mungu juu yake, na hiyo ndiyo sababu ya kutofautiana kwetu, ambayo
ndiyo huitwa ndoto ya mtu.
Katika mpangilio wa vitabu vyote vya Mungu vilivyo
kwenye Agano la Kale na Agano Jipya, kitabu cha kwanza cha kila Agano (Mwanzo
na Mathayo) kimeanza na ndoto. Huu ni mpango wa Mungu.
Mfano1:
Katika kitabu cha Mwanzo 20:3, Mungu kamjia mfalme Abimeleki
katika ndoto ya usiku akimkemea kwa kumchukua mke wa Ibrahimu (Sara), na Mungu
katika ndoto hiyo akamwambia mfalme Abimeleki kuwa kwa jambo hilo atakufa.
Ndoto siyo za kupuuza kabisa kwa maana madhara ya
kupuuzia ndoto yanaathari kubwa sana kwenye maisha ya mtu. Watu wengi hudhurika
kwa sababu huota ndoto lakini wakiamka kutoka kulala kwao hawachukui hatua
kushughulika na ndoto walizoota.
Katika kitabu cha Mwanzo 20:8-9, mfalme
Abimeleki alipoamka tu kutoka usingizini alikoota ndoto kuwa atakufa, akaanza
kushughulika na ndoto ili kukwepa kifo alichoambiwa na Bwana ndotoni. Tunatakiwa
kufanyia kazi ndoto tunazoota kwa sababu, kwa kadili tunavyopuuzia ndoto, madhara
yake yanakuwa makubwa. Usiposhughulika na ndoto utaangamia (Mithali 29:1).
Mfano2:
“Yakobo akatoka Beer-sheba, kwenda Harani. Akafika mahali fulani
akakaa huko usiku kucha, maana jua lilikuwa limekuchwa; akatwaa jiwe moja la
mahali pale akaliweka chini ya kichwa chake, akalala usingizi pale pale. Akaota
ndoto; na tazama, ngazi imesimamishwa juu ya nchi, na ncha yake yafika
mbinguni. Tena, tazama, malaika wa Mungu wanapanda, na kushuka juu yake.” Mwanzo
28:10-22
Yakobo anakimbia baada ya Esau, ndugu yake, kumwibia
baraka zake. Akiwa kwenye kukimbia ardhi ya nyumbani kwao, mwenye kuchoka,
akaamua kupumzika kwenye kichaka na akapata usingizi.
Akiwa amelala kichakani, mahali pasipofaa, tena
hapana chochote cha thamani, Mungu akamjia Yakobo katika ndoto na kumwambia
kuwa amempa nchi ya mahali alipolala, yeye na uzao wake. Baraka ya maneno pekee
aliyotamkiwa na baba yake, Isaka, Mungu ameigeuza kuwa ndoto ya umiliki wa
nchi.
Jambo la muhimu pia, Mungu anajitambulisha kwa
Yakobo ndotoni; imeandikwa katika Mwanzo 28:13 kuwa, “Na
tazama, Bwana amesimama juu yake, akasema, Mimi ni Bwana, Mungu wa Ibrahimu
baba yako, na Mungu wa Isaka; nchi hii uilalayo nitakupa wewe na uzao wako.”
Kiuhalisia, Ibrahimu ni babu yake Yakobo; Isaka
ndiye baba yake Yakobo. Hii inatufundisha kuwa kwa Mungu hakuna babu, kuna baba
tu. Ulimwengu wa roho hauna babu bali una baba, kwa sababu, baba huwa anammilikisha
mwana. Mungu wa baba yake Yakobo amemmilikisha Yakobo ndotoni.
Na sisi tunaye Mungu wa baba yetu, ambaye tunamuomba
atumilikishe yale yote tuyaotayo ndotoni kwa habari ya kusudi la maisha yetu, kwa
jina la Yesu.
Ndoto imempa Yakobo umiliki ndotoni, kuongezeka
ndotoni, na uhakika wa ulinzi ndotoni, mpaka yote ambayo Mungu wa baba yake
ameyatamka, yadhihirike mwilini. Mungu hawezi kuruhusu mabaya yatupate kwa
sababu anawajibika na kusudi lake kwetu (Mwanzo 28:15, Zaburi
121).
Kama kuna ndoto yoyote ambayo Bwana amekuonesha
atahakikisha inatokea vilevile sawasawa na makusudi ya Mungu na mapenzi yake.
Ndoto haichagui mahali; hutokea mahali popote bila kujali mazingira ya mtu
alipo. Kitu cha msingi ni mtu alale tu.
Hatutakufa mpaka yale aliyosema Bwana katika ndoto
juu ya maisha yetu, yatokee. Unachokifanya baada ya Mungu kukuonesha ndoto ni
cha muhimu sana. Mahali popote ambapo Mungu anazungumza katika ndoto, yupo
mahali hapo; hapo huitwa Nyumba ya Mungu. Yakobo alipopewa nchi na Mungu
ndotoni, palikuwa pakiitwa Luzu, akapabadili jina na kupaita Betheli.
Mahali popote upewapo na Mungu, yakupasa upabadili
jina ili uweze kupaongoza kulingana na ndoto uliyopewa. Jina unalotoa, Mungu
hulisajili sawasawa na ndoto aliyosema. Mwenye kutoa jina ndiye mmiliki. Jina
litabadilisha tabia na mambo mengine ili yaendane na jina.
Majina ya mtu yanatokana na tabia ya mtu; mtu
anapokuwa na jina la ovyo na tabia ya mtu inakuwa ya hovyo. Ndoto ya mtu
inathibitisha mahali pa mtu. Usijidharau kwa maana ni Mungu huwaletea watu
ndoto.
Kwa sababu ndoto ya Yakobo ilihusika na kumpa
ulinzi, chakula na mavazi mpaka itimie, Yakobo akaweka nadhiri kwa Bwana ya
kumtolea fungu la kumi ikiwa ni kweli atammilikisha yale aliyomwambia katika
ndoto.
Tusipuuze ndoto, na tukiota ndoto tushughulike na
ndoto bila kujali ukubwa wa ndoto na uhalisia wa maisha yetu. Ndoto ya Bwana
haina uhusiano na halisia ya maisha ya mtu. Mungu husababisha jambo ili yale
tuotayo yatokee. Usijidharau kwa maana ni Mungu ndiye huleta ndoto. Mwenye
ndoto hatapeliwi; hata ikitokea anatapeliwa, Mungu hutokea na kumtetea.
Mwanzo 31:10 - 29
Maisha ni mchezo wa ndoto; Yakobo anatembea katika
ndoto tu. Mungu anawaona wote wanaocheza na ndoto aliyompa mtu. Labani
alijaribu kuchepusha ndoto ya Yakobo kwa kutengeneza utaratibu/kanuni za
kumbana Yakobo, lakini Mungu, kwa kumkumbusha Yakobo juu ya Betheli na nadhiri
ya Yakobo, akamlinda Yakobo na vyote alivyompa. Mungu ni Mungu ashikaye
maagano.
Kanuni na sheria zinaweza kutumika kuzuia ndoto ya
mtu, lakini Mungu huzitumia kanuni na sheria hizo hizo kumpatia mtu sawasawa na
ndoto yake. Kwa Kadili wanavyokuzuia ndivyo unanyoongezeka, kwa Jina la
Yesu.
Adui wa ndoto anayekuzuia kwenda mahali pa ndoto
yako, dawa yake ni kumtandika. Kuna wakati unaelekea kupata ila kuna adui
anakuzuia usiende kule ulipo kusudiwa; kwakuwa tunaye Mungu aliye hai, dawa ni
kumtandika. Mungu aliyemuahidi Yakobo kumlinda, alimkemea Labani katika ndoto
na kumuagiza asimsemeshe Yakobo la heri au la shari.
Ukiwa na baba, Mungu wa baba yako anazungumza na
adui zako na kuwakemea; Bwana huwapiga adui kupitia mikono ya watumishi wake
kwa maana yeye hutenda kazi ndani yetu (Wafilipi 2:14, 1
Samweli 2:10).
Baada ya mfungo huu, Bwana amesema iandike njozi
yako ifahamike (Habakuki 2:2).
Miradi ya Bwana inafadhiliwa na Mungu mwenyewe; Yeye
anasimamia mradi wa kuigeuza dunia kuwa koloni la Mwana-Kondoo. Mungu
anatuambia kuwa mambo hayo hayana budi kutokea, kwa jina la Yesu.
Mfano3:
1 Wafalme 3:4-28
Kuna sadaka ukitoa inamvuta Mungu aje kuzungumza na
wewe kupitia ndoto. Unapotoa sadaka inavuta moyo wa Mungu kwa uzuri au kwa
ubaya. Unapotoa kwa uzuri Mungu anakuwa anazungumza na wewe na anakupa chochote
unachokitaka. Ila kwa kadili unapokuwa hautoi sadaka kwa uaminifu, unaukwaza
Moyo wa Mungu.
Mtu anaweza kuomba ndotoni na kupewa majibu ndotoni.
Kwenye biblia, mfalme Sulemani alimtolea Mungu sadaka yenye kumfurahisha na
kumpendeza Mungu, naye Mungu akamtokea katika ndoto na kumwambia aombe chochote
anachotaka ili amtendee. Sulemani akaomba hekima akiwa ndotoni na akapatiwa
hekima akiwa ndotoni. Unaweza kupewa maelekezo kwa njia ya ndoto. Ndoto ina mahusiano
na mahitaji yako kama vile utajiri au umaskini, uponyaji wako au ugonjwa wako.
Unapotoa sadaka unajimilikisha ndoto hiyo, kwa jina la Yesu.
Sulemani alipoamka na kukuta ni ndoto, akaanza
kushughulika na ndoto. Akamtolea Bwana sadaka. Katika biblia, hakuna mtu
aliyepuuzia ndoto.
Mfano4:
Ndoto inaweza kusahaulika. Ndoto ikisahaulika haimaanishi kuwa haipo; ipo ila
imefichwa na wachawi. Mfalme Nebukadreza aliota ndoto iliyomtia hofu ila
alipoamka hakuikumbuka. Pamoja na kuwa Nebukadreza aliisahau ndoto aliyoota,
alipoamka alishughulika na ndoto. Mungu hutenda kazi vizuri kwenye changamoto
kubwa inayohitaji majibu ya ki Mungu. Danieli, mtu wa Mungu, peke yake aliweza
kumkumbusha ndoto yake na akatoa tafsiri ya ndoto hiyo (Danieli 4).
Biblia katika kitabu cha Ayubu 20:8,
inatufundisha pia kuwa ndoto inaweza kupaa.
Mambo ya hatari ambayo ndoto inawezakuleta kwenye
maisha ya mtu; -
1.
Ndoto
inaweza kukuletea maadui wa ndani;
Kwenye biblia Yusuph aliota ndoto
na kuwasimulia ndugu zake, na wale ndugu zake wakamchukia na kumuuza Misri. Ndoto
yako inaweza ikasababisha uchukiwe na ndugu zako, na jamaa zako, na watu wako
wa karibu (Mwanzo 37:5-8).
Hata ukichukiwa wewe endelea
kuota; usibadili ndoto na maono yako kwa sababu ya chuki za ndugu zako na chuki
za marafiki zako. Ndoto haiachwi kizembe; kuwa thabiti kwenye ndoto zako leo na
siku zote (Mwanzo 37:9).
Wazazi wanaweza wakakunyamazisha,
lakini kama ndoto inatoka kwa Bwana, haiwezi kunyamazishwa. Kupigwa vita, na
vizuizi kutoka kwa adui wa mtu haibadilishi ndoto ya mtu. Mungu humpa mtu ndoto
kwa sababu amemuona ni wa maana. Usibadilishe msimamo wako. Mungu aliyekuchagua
anakulinda (Warumi 8:29-30).
Hakuna silaha wala jambo lolote
kinyume na ndoto yako litakalofanikiwa, asema Bwana (Isaya 54:17).
2. Ndoto inaweza ikakufanya ufe
kabla ya wakati;
Usipojua cha kufanya/kutenda, unaweza
ukafa. Mungu anataka upenye na usife. Watu wengi wenye ndoto kubwa wasipojua
cha kufanya wanaweza wakafa kabla ya wakati. Ndugu wa Yusuph walifanya
mashauriano ili wamuuwe kwa sababu ya ndoto zake.
Ndoto ina tabia ya kuonekana
kutokea mbali. Hata ukiwa bado mdogo wachawi wanaweza kujua, nao wakakutengenezea
matukio ya kukuua. Lakini Bwana yeye anatulinda ili ndoto zetu zitimie (Zaburi
118:17).
Yesu alipozaliwa tu mamajusi wa
Mashariki ya mbali wakaona kutokea mbali ndoto ya Yesu kuwa atakuwa mfalme.
Naye nabii Isaya anaitangaza ndoto ya Yesu kabla Yesu hajazaliwa (Isaya
9:6). Wachawi wanaweza kumloga mtu mwenye ndoto kabla hajazaliwa ili
kukwambisha ndoto yake. Vita kubwa aipatayo mtu ni sababu ya wachawi wameiona
ndoto ya mtu kutokea mbali. Kama Mungu alivyomuokoa Yakobo, atatuokoa na adui
wote wanaopambana na ndoto zetu (Zaburi 68:20).
Kila ndoto ina adui wa ndoto. Mungu wa Yakobo ndiye
Mungu wangu; ameapa kunilinda mpaka yale yaliyo kwenye ndoto yangu yatimie. Mungu
wa baba yangu ndiye Mungu wa Yakobo. Adui wote watainama mbele zangu. Mamlaka
zote za rohoni zitainama.
Adui wa ndoto anaweza akatengeneza matukio kinyume
na ndoto ili kukwamisha ndoto isitimie. Mfano; kama ndoto ya mtu ni kuwa
askari, adui anaweza akasababisha matukio ya magonjwa kwa mtu ili kumuondolea
ukakamavu na utimamu wa akili.
Mwili hulala lakini roho ambayo ndiye mtu mwenyewe,
halali. Mwili ulalapo, roho huendelea na kuona (hiyo ndiyo ndoto). Kuamka kwa
mwili hakusimamishi matukio ya roho.
Ndoto ina mahusiano na kibali cha mtu. Kuota
unalishwa chakula ni mbaya sana kwa sababu maadui wa giza wanapomlisha mtu
vyakula ndotoni, wanakuwa wanaimarisha matatizo waliyoyaweka kwa mtu huyo.
Matatizo hayo huondoa kibali cha mtu. Kwa kulishwa vyakula ndotoni, mambo mengi
katika maisha yanaharibika na vifungo alivyofungwa mtu vinaimarika.
Unapokula chakula cha kichawi kuna tabia
zinabadilika na kuiona kazi ya Mungu ni ya kawaida, na kuifanya kazi ya Mungu
kwa ulegevu; na ndivyo unavyokosa kibali.
Kuna watu huota ndoto wakinyolewa nywele. Maana ya
kunyolewa nywele ndotoni ni kuwa kuna nguvu ya mtu inaondolewa kwenye maisha
yake. Kuna wengine wanaota wakichanjwa chale mwilini. Haya yote yanafanyika ili
kuimarisha matatizo ya mtu.
Kanuni ya usingizi ni ileile; ukilazwa ni ama unawekewa kitu au unaondolewa kitu. Mfalme Sulemani alipolala, Mungu alimuwekea hekima. Pambana sana kuondoa vizuizi kwenye maisha. Mungu huleta msaada kupitia maombi; omba sana mchana na usiku. Ni kwa sababu ya dhabihu na sadaka ya kueleweka, Mungu hummilikisha mtu mambo yote ya ndoto yake. Toa sadaka ambayo haitaleta ugomvi kati yako na Mungu. Toa kwa ukamilifu “Leteni zaka kamili ghalani, ili kiwemo chakula katika nyumba yangu, mkanijaribu kwa njia hiyo, asema BWANA wa majeshi; mjue kama sitawafungulia madirisha ya mbinguni, na kuwamwagieni baraka, hata isiwepo nafasi ya kutosha, au la.” Malaki 3:10
BONYEZA HAPA KUANGALIA IBADA YA JUMAPILI


0 Comments