google.com, pub-4324601895065941, DIRECT, f08c47fec0942fa0

Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

VITA YA MTU ANAYEKARIBIA KUPATA

UFUFUO NA UZIMA CATHEDRAL
IBADA YA JUMAPILI 14.06.2026
ASKOFU DKT GERSHOM MWAKILA
SOMO: VITA YA MTU ANAYEKARIBIA KUPATA

Mara nyingi mtu akipakwa mafuta kuwa masihi wa Bwana, hutazamia kapata hitaji lake au kuliishi lile kusudi la maisha yake. Kupakwa mafuta ni kutengwa kwa ajili ya kusudi maalumu; ni kitendo cha uhakika wa kupata kusudi.

Mafuta yanamlinda mtu asidhurike, asizuiwe na asiguswe. Unapopakwa mafuta unaelekea kupata. Unapoelekea kupata kuna vita inainuka kukuzuia usipate. Akili ni kumshambulia adui pale unapohisi anataka kukuzuia. Vita ipo kwenye kila kitu ambacho mtu anakitaka; lazima tupigane vita asubuhi, mchana, jioni na usiku. Vita ilikuwepo tangu enzi na ilianzia mbinguni ambapo mtesi wetu alitupwa ulimwenguni, hivyo yupo. Kwa Kadiri vita ya mtu inaonekana ni kubwa, ndivyo kile kilicho ndani ya mtu ni kikubwa, kwa maana hata Mungu ni Mungu wa vita.

Mtu aliyefunga siku arobaini ni lazima akutane na mitego ya shetani. Biblia inatufundisha kuwa, wale wote waliofunga siku arobaini, walipomaliza mfungo, shetani alijionesha kwao. Nabii Musa baada ya kufunga siku arobaini, aliposhuka katika mlima Holebu, aliona uasi kwenye kambi ya mji aliokuwepo.

Yesu alipomaliza kufunga siku arobaini, akiwa mlimani, alitokewa na shetani na akajaribiwa. Shetani anapokuja kwa watu waliofunga siku arobaini, huja kupambana na lile kusudi la kufunga kwao; shetani huja kile kipindi ambacho mtu anakaribia kupata, hivyo vita ya aliyefunga siku arobaini ni maalum (special). Sisi pia, baada ya kumaliza mfugo wetu wa siku arobaini, vita tunayopigana ni maalum kwa sababu tunaelekea kupata

“Na Yesu, hali amejaa Roho Mtakatifu, alirudi kutoka Yordani, akaongozwa na Roho muda wa siku arobaini nyikani, akijaribiwa na Ibilisi. Na siku hizo alikuwa hali kitu; hata zilipotimia, aliona njaa. Ibilisi akamwambia, Ukiwa ndiwe Mwana wa Mungu, liambie jiwe hili liwe mkate. Yesu akamjibu, Imeandikwa ya kwamba mtu hataishi kwa mkate tu. Akampandisha juu, akamwonyesha milki zote za ulimwengu kwa dakika moja. Ibilisi akamwambia, Nitakupa wewe enzi hii yote, na fahari yake, kwa kuwa imo mikononi mwangu, nami humpa ye yote kama nipendavyo. Basi, wewe ukisujudu mbele yangu yote yatakuwa yako. ”Luka 4:1-14

Uwapo kwenye mfungo wa siku arobaini au baada ya mfungo, yakupasa uwe makini sana kwa maana shetani huja kwa sura ya ufumbuzi wa hitaji lako, lakini huo ni mtego. Shetani hujua mahitaji yetu tuyaombayo kwa Bwana, hivyo, hutujaribu kwa sura ya kujibiwa maombi yetu, na unapoingia kwenye mtego huo, mwisho huwa ni mbaya. Kuna wakati mtu hufikiria kuwa Mungu anachelewa kujibu maombi, lakini biblia inatufundisha kuwa Mungu hawahi wala hachelewi ila hujibu wakati wa utimilifu wa wakati; unapokaribia utimilifu wa wakati, shetani hujitanguliza kuharibu kusudi la Mungu kwa mtu.

Shetani ni baba wa uongo; akiahidi kukupa chochote, hulenga kukukwamisha usiyapate yale Mungu ameahidi kukupa. Shetani anajua ya kuwa, kupitia uongo wake, aliiba milki yote ya ulimwengu, hivyo hutumia ujanja wake ili aendelee kubaki nayo; ni ahadi ya Mungu yenye utimilifu kwa yeyote kuwa mtu akifanikiwa kurudisha vile vilivyoibiwa na shetani, Mungu atalikuza jina la mtu huyo na atamzidisha katika dunia kwa sababu amefanikiwa kuirudisha asili ya Mungu na kusudi la uumbaji wake.

Njia ya Mungu kutimiza kusudi lililo ndani ya mtu, ni njia ngumu yenye sura ya kukatisha tamaa, lakini mwisho wake ni mwema na wenye kumiliki vyote. Yesu, ili aukomboe ulimwengu uwe koloni lake, lilikuwa ni kusudi la Mungu apitie mateso mengi na kejeli kwa ajili ya watu wote.

Njia ya shetani ni nyepesi na yenye kubembeleza. Yesu alijaribiwa na shetani kuwa “ukisujudu mbele yangu yote yatakuwa yako”; kwa sababu ahadi za Bwana ni za kweli, Yesu alichagua njia ngumu yenye mateso, nalo jina lake ni kuu, kubwa na lenye kuponya wote wenye uhitaji.

Kabla Mungu hajalikuza jina “Yesu” kuwa jina lipitalo majina yote, Yesu alipitia dhiki, kutengwa, kejeli, lakini alivumilia mateso hata akafa akazikwa na kufufuka kwa ajili ya wote watakaompokea wawe na uwezo wa kufanyika wana wa Mungu. Yeye akataliwaye na watu, ama ndugu zake au jamii yake, asikate tamaa kwa maana kuna mahali jina lake lina thamani na anasubiriwa; maumivu ni sababu ya kukataliwa.

“Alikuwako ulimwenguni, hata kwa yeye ulimwengu ulipata kuwako, wala ulimwengu haukumtambua. Alikuja kwake, wala walio wake hawakumpokea. Bali wote waliompokea aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa Mungu, ndio wale waliaminio jina lake;” Yohana 1:10-12

Kuna watu wanakuza majina yao kwa njia za mitandao na wengine wanatumia machawa lakini majina yao yanakuwa ya kawaida, ila ukiirudisha dunia katika njia ya Bwana Mungu anakupa jina lipitalo majina yote. Unapoamua kuichagua njia ya Bwana, kuna kukataliwa na familia, kutengwa na watu, kukejeliwa, kusengenywa ila mwisho wake ni mzuri. Jipe moyo, usikate tamaa kwa maana hata Yesu alienda kwa walio wake lakini hawakumpokea.

Biblia imejaa watu waliokataliwa. Wapo watu ambao wako na nia ya kupindisha kesho ya mtu au kupindisha njia ya mtu, lakini Mungu anayo njia ya kumrudisha mtu katika njia impasayo mtu kuiendea. Mtu awapo mgumu kwa Mungu, Mungu humvuta mtu huyo kwa njia ngumu. Hivyo ni afadhali ujilegeze kwa Mungu ili Mungu akupeleke kwenye kusudi lake kwa njio isiyo ngumu; Mungu kwa wapole anakua mpole, mnyenyekevu kwa wanyenyekevu, na mgumu kwa wagumu.

Mfano1; Paulo ambaye ndiye alikuwa Sauli, Mungu alitumia njia ngumu kumrudisha katika kusudi lake kwa sababu Sauli alikuwa mgumu. Mungu alimpiga Sauli na upofu ili kulegeza moyo wake arudi kwenye kusudi. Baada ya kuwa Paulo, watu waliomfahamu kama Sauli walimkataa, naye akaenda kwa mataifa.

Mfano2; Daudi mwana wa Yese alikataliwa na baba yake kwenye tukio la kutafuta mfalme wa nchi na masihi wa Bwana. Daudi alitengwa na familia ya baba yeke nyuma ya jangwa ili nabii Samweli mwenye pembe ya mafuta asiweze kukutana naye. Biblia inatufundisha kuwa, yeye aonekanaye kwa macho ya watu kuwa ndiye, sio lazima mbele za Mungu awe ndiye, na yule asiyeonekana anafaa machoni pa watu yawezekana kabisa ndiye anayefaa mbele za Mungu. Mungu haangalii kama wanadamu waangaliavyo; Yeye huangalia roho. Pamoja na kuwa nabii Samweli aliona watoto wa Yese (isipokuwa Daudi) wanasifa za mfalme, Mungu aliwakataa wote, na mbele za Mungu, ni Daudi peke yake mwenye kustahili kupakwa mafuta.

Daudi alifichwa nyuma ya jangwa lakini mafuta yalimtafuta. Nabii Samweli na familia ya Yese hawakula wala kunywa mpaka Daudi aliye nyuma ya jangwa afike sawasawa na kusudi la Bwana. Hata sisi zile siku tulizofunga ni sawa na tulikuwa nyuma ya jangwa; tumemaliza mfungo na sasa tumetoka jangwani tukiwa na mafuta, na tunaenda huko tunakosubiriwa kwa maana, huko kuna watu ambao hawali na hawanywi wala hawakai, wanatusubiria; wale wanaokataliwa sana, ndio hao wenye kesho kubwa sana, na ndio hao wenye jina kubwa sana, na ndio hao wanaosubiriwa sana, na ndio hao ambao mwisho wao ni mkubwa sana, kwa maana kwa Mungu hakuna kuchelewa na hakuna kuwahi ila kuna utimilifu wa wakati

“Hata ulipowadia utimilifu wa wakati, Mungu alimtuma Mwanawe ambaye amezaliwa na mwanamke, amezaliwa chini ya sheria,” Wagalatia 4:4

Ni vyema kuijua njia iliyo sahihi; imeandikwa katika Mithali 14:12, 16:25 kuwa, “Iko njia ionekanayo kuwa sawa machoni pa mtu, Lakini mwisho wake ni njia za mauti.” Njia isiyo sahihi ni moja tu lakini matokeo yake ni njia nyingi za mauti, mfano, ukiiendea njia ya shetani (njia moja yenye kuanza na mvuto) itazalisha njia nyingi za mauti kama mauti ya kazi, mauti ya ndoa, mauti ya biashara n.k., lakini ipo njia inayoanza kwa kutengwa, kukataliwa, kuwa na huzuni lakini mwisho wa njia hiyo ni mwema (njia ya Yesu).

Mtu achaguaye njia ya Yesu dhidi ya njia ya shetani atafanikiwa. Yesu aliwapa ahadi wanafunzi wake / Thenashara na watu wote kuwa yeyote aliyeacha mambo yake kwa ajili ya jina lake (Yesu), atapokea mara mia na ataurithi uzima wa milele (Mathayo 19:29). Ahadi hii ya Yesu ilionekana kuleta mashaka kwa baadhi ya wanafunzi wake, kwa mfano, Yesu anawaambia wanafunzi wake kuwa atateswa, atakufa, atazikwa na atafufuka siku ya tatu; inawezekana vipi kufa bila kutimiza ahadi ya kuwapa “mara mia” ya vyote walivyoviacha kwa ajili ya jina lake?

Kwa sababu mtu akikaribia kupokea sawasawa na kusudi lake, shetani hufanya hila ili kuharibu kusudi la Mungu, shetani akamwingia Yuda na kumwongoza kumsaliti Yesu kwa kumuuza kwa vipande thelathini vya fedha. Hili linatufundisha kuwa kuomba kunahitaji uvumilivu kwa maana Mungu hujibu wakati unapotimilika; unaweza ukamuomba Mungu akupatie kazi, ila wakati utimilifu wa ki Mungu wa kupata kazi uitakayo haujawadia, shetani anaweza akakuletea fursa ya kazi ambayo siyo ya uwezo wa Mungu, na ukiingia ndiyo inakuwa chanzo cha kuanguka kwako kwenye mauti nyingi. Shetani anaweza kabisa kumuingia mtu aliyekaribia kupata ili akate tamaa.

Mungu hufuata ukamilifu wa wakati; hakuna neno litokalo bure kutoka kwa Bwana (Isaya 55:11). Ahadi ya Bwana ya kupata “mara mia” ilikuwa ni kanuni ya ki Mungu iliyohaririwa kwa matukio ya ki Mungu. Yatupasa kuelewa litupasalo kufanya kwa wakati huo. Kanuni ya Mungu kwa Thenashara ilikuwa kuwapa mara mia baada ya Yesu kusulubiwa, kufa, kuzikwa na kufufuka siku ya tatu, ndiyo maana, wanafunzi wengine wa yesu walipata mara mia isipokuwa Yuda aliyemsaliti Yesu.

Yesu aliasisi njia yake kwa mateso na akaikamilisha ili ahadi ya kupokea mara mia iwapate watu wote. Alipomaliza kuitengeneza njia yake, akatuachia Roho Mtakatifu atusaidie kuenenda katika njia yake. Wanafunzi wa Yesu hawakuhitaji tena kupitia mateso ili wapate majibu ya mahitaji yao; jina la Yesu linatosha kutatua yote.

Biblia inatufundisha kuwa, siku ya Pentekoste upepo wa nguvu uliwaingia wanafunzi wa Yesu wawapo pamoja katika kusali, wote wakajazwa Roho Mtakatifu wakaanza kunena kwa lugha; majibu ya mahitaji yao/ile ahadi ya “mara mia” ikaanza kufanya kazi (Matendo ya Mitume 2:1-4). Wanafunzi wa Yesu walikabidhiwa jina la Yesu; hiyo ni fimbo waliachiwa (Yohana 14:13). Walitangaza jina la Yesu kwa wote wenye uhitaji, waliponya wagonjwa, waliwafungua wenye vifungo, walitumia fimbo yao kuwaongoza watu kwenye mahitaji yao; hawakuhitaji elimu au Hekima za kidunia kwa maana fimbo waliyopewa ni zaidi ya hivyo. Ukiwa pamoja na Yesu unafanya yale aliyoyafanya; tumia fimbo uliyopewa ili ufanye yale aliyofanya yye aliyekupa fimbo.

Wanafuzi wa Yesu walipokutana na kiwete hawakumpa fedha wala dhahabu ila kwa jina la Yesu wakamponya kiwete yule. Yule uliyenae ndivyo utakuwa wewe; wanafunzi wa Yesu walifanya yale aliyoyafanya Yesu, kwa sababu, alivyo baba ndivyo alivyo mwana. Ukitembelea mafuta ya anayekuongoza utafanya kama yeye.

 

Sisi tuna baba ambaye ametupa fimbo/mafuta tutumie kupata majibu ya mahitaji yetu.  Hatuoni aibu kutembea/kufanya yale afanyayo baba yetu kwa maana sisi na baba tu umoja (Warumi 1:16, Yohana 10:30). Kwa mafuta na moto wa baba, wengi tumefanikiwa. Kuna jambo moja ambalo yatupasa kujifunza ili kukamilisha kanuni ya mimi na baba tu umoja, nalo ni kutoa.

Mwenye kutoa hakaukiwi kupata, ila asiyetoa anaelekea uhitaji. Kutoa ni mlango wa kupokea. Kutoa ni kanuni ya Mungu; Mungu alimtoa mwanaye wa pekee ili aupate ulimwengu wote. Baada ya kumtoa mwanaye wa pekee, sisi sote tumekombolewa kwa damu ya mwana wa kwanza wa Mungu, Yesu. Kwa kipimo kile kile cha Yesu kuwa mwana wa Mungu, ndivyo sisi tumefanyika kuwa wana wa Mungu

“Tazameni, ni pendo la namna gani alilotupa Baba, kwamba tuitwe wana wa Mungu; na ndivyo tulivyo. Kwa sababu hii ulimwengu haututambui, kwa kuwa haukumtambua yeye.” 1 Yohana 3:1

Ibrahimu na Sara walikubali kumtolea Mungu Isaka, mtoto wao, naye Bwana akalikuza jina la Ibrahimu na kumzidisha katika dunia. Upenyo unakuwa kwenye kutoa cha pekee; kidogo ulichonacho, kimetoka kwa Bwana

“Mtumaini BWANA kwa moyo wako wote, Wala usizitegemee akili zako mwenyewe; Katika njia zako zote mkiri yeye, Naye atayanyosha mapito yako.” Mithali 3:5-6

Sadaka huwa haitolewi kwa watu au kwa walemavu; huo ni msaada siyo sadaka. Sadaka inatolewa kwa Mungu au miungu. Ukihitaji Mungu akutendee jambo lako ni lazima utoe sadaka. Ukipanda maombi utavuna maombi; usipande kunena kwa lugha ukategemea kuvuna hela, kama unahitaji fedha, lazima umtolee Mungu sadaka ya fedha; baraka ya fedha inakuja kwa kutoa fedha (Wagalatia 6:7). Shetani anaijua kanuni ya kupata, ndiyo maana anabana sana kwenye matoleo kanisani. Sadaka huvuta Roho wa Mungu; Sadaka ya Kornelio iliwavuta malaika waende kwake, na sadaka ya Habili ilimuinua.

Ni kanuni ya Mungu kumtolea zaka na dhabibu. Zaka na dhabihu lazima ziwe za ukamilifu, vinginevyo ni kuleta laana. Laana ni kinyume cha baraka, na ni mlango kwa mtu afikwe na mabaya yote. Tunatoa kwa Mungu kwa maana ndiye atoaye nguvu za kupata utajiri (Mithali 23:4). Mtu anaweza akawa amefunguliwa kwenye mambo yote, lakini hafanikiwi kwa sababu ya kukiuka kanuni ya Mungu ya utoaji. Usipotoa au ukatoa sadaka/zaka/dhabibu isiyokuwa ya ukamilifu, shetani hutushtaki kwa Mungu, Naye Mungu husimamia kanuni yake.

Binadamu humwibia Mungu na hivyo kupata laana kwenye yote wafanyayo. Laana inayotokana na kumwibia Mungu zaka na dhabihu, haitoki kwa kubadilisha unachofanya; badilisha nia, Mungu huponya laana. Upenyo wa mtu kwenye mambo ya fedha umelala kwenye kuijua kweli. Laana za wachawi au wazazi tukimwomba Mungu tunaziondoa, ila laana ya Mungu hakuna maombi yanayoweza kuiondoa.

Tunamtolea Mungu zaka na dhabihu ili nyumbani mwa Bwana kuwe na chakula. Chakula katika nyumba ya Bwana maana yake ni uponyaji. Hivyo, tunamtolea Bwana ili nyumba ya Bwana iwe na uponyaji. Mungu ameturuhusu tumjaribu kwa kumtolea; tumtolee Mungu kwa ukamilifu ili tusiwe na hatia mbele zake

“Je! Mwanadamu atamwibia Mungu? Lakini ninyi mnaniibia mimi. Lakini ninyi mwasema, Tumekuibia kwa namna gani? Mmeniibia zaka na dhabihu. Ninyi mmelaaniwa kwa laana; maana mnaniibia mimi, naam, taifa hili lote. Leteni zaka kamili ghalani, ili kiwemo chakula katika nyumba yangu, mkanijaribu kwa njia hiyo, asema BWANA wa majeshi; mjue kama sitawafungulia madirisha ya mbinguni, na kuwamwagieni baraka, hata isiwepo nafasi ya kutosha, au la. Nami kwa ajili yenu nitamkemea yeye alaye, wala hataharibu mazao ya ardhi yenu; wala mzabibu wenu hautapukutisha matunda yake kabla ya wakati wake katika mashamba, asema BWANA wa majeshi.” Malaki 3:8-11.

Kanuni ya fedha ina njia zake, na mojawapo ya njia hizo ni uaminifu kwenye kutoa fungu la kumi. Kama mtu siyo mwaminifu kwa Mungu kwenye kutoa, mtu huyo ni mwizi anayemuibia Mungu. Kumuibia Mungu ni mbaya sana kuliko kuwaibia watu; tubu uanze upya uaminifu na Bwana kwenye kumtolea zaka na dhabihu.

BONYEZA HAPA KUANGALIA IBADA YA JUMAPILI

Post a Comment

0 Comments