google.com, pub-4324601895065941, DIRECT, f08c47fec0942fa0

Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WAMEOGOPA HATIMA YAKO WAKAKUFICHA NYUMA YA JANGWA

UFUFUO NA UZIMA CATHEDRAL
IBADA YA JUMAPILI 12.07.2026
ASKOFU DKT JOSEPHAT GWAJIMA
SOMO: WAMEOGOPA HATIMA YAKO WAKAKUFICHA NYUMA YA JANGWA

Hatima ni utakavyomalizia maisha yako, au mustakabali wa maisha ya mtu. Kiswahili hakitoi maana timilifu ya neno hatima. Unaondoka duniani unapomaliza hatima yako. Somo hili kimsingi siyo mahubiri lakini ni maelekezo kutoka kwa Mungu ili kutusaidia kumaliza mbio zetu hapa duniani kwa nguvu na ushindi. “Wameogopa hatima yako wakakuficha nyuma ya jangwa” inamaanisha adui ameiona hatima na kusudi kubwa la mtu hapa duniani hivyo anamzuia mtu asiishi hatima hiyo kwa kumtenga na njia impelekayo mtu huyo kwenye hatima; jangwa, kama linavyotajwa kwenye somo, linawezakuwa pingamizi lolote la kuzuia hatima, mfano umasikini.

Nchi ya Israeli walilazimika kuchagua Rais kipindi cha utawala wa mfalme / Rais Sauli, lakini nchi nzima walikuwa wahajui Rais atakuwa nani. Kwa utaratibu wa kumpata kiongozi wa nchi kwa wakati huo, Mungu alikuwa anamtumia nabii aliyemchagua kummiminia mafuta masihi ili awe Rais. Kipindi cha utawala wa Sauli, nabii wa Mungu alikuwa Samweli aliyefunuliwa na Mungu kumpaka mafuta mtu mwingine awe Rais. Katika maisha ya sasa, kitendo hiki cha kummiminia mafuta mtu mwingine awe Rais wakati Rais yupo, kingetosha mtu kushitakiwa kwa kutenda kosa la uhaini.

Mungu alimtuma nabii Samweli abebe pembe ya mafuta na kwenda kwa familia ya Yese kumpaka mafuta masihi wake. Samweli akazungumza na Mungu kuhusu mfalme Sauli ikiwa atasikia kuwa anampaka mafuta mtu mwingine, lakini Mungu akamwambia Samweli aende kwa namna ya kutoa dhabihu, na Mungu atamuongoza na kumpatia nguvu.

Samweli akaenda kwa familia ya mzee Yese, na wakati huo, familia ya mzee Yese hawajui kama kuna mtu atakuwa Rais kutoka kwenye nyumba yao. Wakati mtu haijui hatima yake, Mungu anaweza akamtumia mtumishi wake mwenye uwezo wa kujua hatima ya mtu ili kumuelekeza mtu huyo kuiendea hatima yake.

Kwenye nyumba ya Yese, Samweli anamkuta mzee Yese na watoto wake saba wa ndoa wenye sifa za ukakamavu na ni wanajeshi; hata hivyo, hakuna kati yao ambaye Samweli, kwa macho ya mbinguni, alimuona anatakiwa kumiminiwa mafuta. Kwenye maisha, siyo mbio zako zinazoweza kukupa ushindi ila wakati na Bahati huwapata wote (Mhubiri 9:11). Samweli alipomuuliza mzee Yese kama kuna mtu mwingine kwenye nyumba yake, maana Samweli alijawa shauku kuwa masihi wa Bwana anatoka kwenye nyumba hiyo, mzee Yese akamjibu kuwa yupo mmoja mdogo mdogo ambaye hajamuita kwa sababu hata muonekano wake hauwezi kumfanya awe mfalme.

Makuhani wa Mungu huona hatima ya mtu; ni vyema kujionesha kwao, wakikuona wanakujua. Moyo wa mtu unafisha sana; namna mtu anavyojiona ndiyo au siyo, kwa Mungu ni tofauti. Unaweza ukajiona hufai kwa kazi fulani, lakini sivyo, kuna jambo lipo kubwa umebeba zaidi ya maisha uliyonayo; jambo la msingi ni kulijua. Kutokujua kunatupa maswali mengi sana, mfano; Nini thamani ya maisha? Je, tunaishi ili tuje kufa; Je, tunalala ili siku iishe? Hapana, hakuna kipya hapa duniani.

Wote tumetumwa ili tufanye kile ambacho Mungu angekuja kukifanya mwenyewe. Kuna kusudi ambalo Mungu ameliweka ndani ya mtu. Je, ni nini kinachofanya mtu aishi hadi muda huu? Ni nini kilitokea hadi sikufa nilipokuwa tumboni wakati wa mimba au kwenye ile ajali? Jibu ni kwamba, kuna kusudi lipo ndani ya mtu ambalo kama hautalitekeleza Mungu atakuhukumu.  Yampasa mtu aamke ili agundue kusudi lake na kulifanya; lazima kila mtu ajione ana kitu amebeba. Lazima mtu achambuke mwili na roho ili atende lile lililo la roho ambalo ametumwa kulitenda; CHAMBUKA!

Mfano wa ‘kuchambuka’ upo kwenye mfumo wa Kemia; Sodiamu (Sodium – Na) na Kloreni (Chlorine – Cl) zinapoungana kwa pamoja zinatengeneza chumvi tunayotumia kwenye chakula, lakini zinaweza kutenganishwa zikatengana na kila moja ikafanya kazi nyingine; vivyo hivyo, kuna roho na mwili ambavyo vikiungana anapatikana mwanadamu na vikitengana kuna mwili kurudi kwenye mavumbi na roho kurudi kwa Mungu. Kwahiyo, ni vizuri kuonekana kwa watumishi wa Mungu ili wakuone yale usiyoweza kuyaona (mambo ya rohoni).

Kwakuwa Daudi alifichwa nyuma ya jangwa, na Samweli kuwa na shauku, Samweli akasema hakuna kula wala kunywa mpaka Daudi aletwe. Hapa tunafundishwa kuwa, hata kama wamekuogopa sana wakakupeleka nyuma ya jangwa ili usionekane / usifikie hatima yako, watakufuata wao wenyewe. Alipofika Daudi na kuonwa na nabii Samweli, na kupangwa upya ili kujua nani anastahili kupakwa mafuta, hakuna kilichobadilika kwa wale saba; uwepo wa Daudi tu ukamfanya nabii Samweli kusema masihi wa Bwana yupo katikati yao, na akammiminia pembe ya mafuta.

Kwanini walimficha Daudi? Daudi alikuwa mtoto wa nje ya ndoa; wale watoto saba walizaliwa na mama mmoja isipokuwa Daudi, lakini wote walikuwa watoto wa mzee Yese (Zaburi 51:5, Zaburi 22:10). Hatima ya Daudi ilitoka kwa Mungu mwenyewe na hakuwepo wa kuizuia; umasikini hauwezi kuzuia hatima.

Hatukuanza siku ya kuzaliwa (Mwanzo 2:7); tulikuwepo kabla hatujazaliwa. Tulikuwepo ndani ya Mungu; wakati anaumba tulikuwa naye. Bibilia inatufundisha kuwa;

1.   “Mtu kwa mavumbi ya ardhi” ni mwili.

2.   “Mtu nafsi hai” ni roho.

Mimi siyo mtu kwa mavumbi ya ardhi; mimi ni mtu nafsi hai (Warumi 7:12, Waefeso 3:16). Mimi ni mtu wa ndani. Aliyenibeba ndiye “mtu kwa mavumbi ya ardhi” ambaye atarudi mavumbini, lakini mimi hakuna wa kunirudisha mavumbini kwa sababu sijatokea huko

 “kwa jasho la uso wako utakula chakula, hata utakapoirudia ardhi, ambayo katika hiyo ulitwaliwa; kwa maana u mavumbi wewe, nawe mavumbini utarudi.” Mwanzo 3:19.

Mimi nilitolewa kwa Mungu nikaingia ndani ya mwili kwa pumzi ya Mungu; nitarudi kwa Mungu (Mhubiri 12:7). Ninaweza nikawa kwenye hatari yoyote lakini siogopi kwakuwa hakuna wa kuniua kwa sababu mimi siyo mwili (Mathayo 10:28); yeyote unayenitafuta, HUNIUI (Zaburi 91:10). Aliyetolewa kwa Mungu atarudi kwa Mungu; Yesu alitolewa na Mungu, alipomaliza kazi yake akarudi kwa Mungu

“Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele.” Yohana 3:16.

Mtu wa kwanza (Adamu) hakuzaliwa wala hakunywa maziwa; alibuniwa na kuumbwa na Mungu. Alianza kwa kuwepo na kupuliziwa pumzi ya uhai. Wazo/fikra huzalisha itikadi; wazo/fikra duni huzaa itikadi dhaifu. Wakati Mungu akimuumba Adamu alikuwa na wazo/fikra bora zilizozaa itikadi imara. Mungu alipokuwa anaumba mwili wa kwanza, alizingatia kuwa hataumba miili mingine isipokuwa huo mwili anaouumba anaupa uwezo wa kutengeneza miili mingine. Mungu akaweka mbegu ndani ya mwili wa mwanaume ili miili itengenezeke, kisha Mungu akammega mwanaume na kumtengeneza mwanamke, na ndani ya mwanamke akaweka mayai yenye uwezo wa kurutubisha mbegu za mwanaume ili kupata miili.

Siku mbegu na yai zikikutana, mwili mpya unaanza kutengenezwa siku hiyo, na Mungu anamtuma mwanaye ambaye ni roho. Siku hiyo mbinguni ni kama send-off, ila unakuta siku yako ilipofika mwili ulio tayari upo kwa wazinzi kwenye baa; ndiyo unajikuta umezaliwa sehemu hiyo. Kuna waliotumwa kwa kusudi fulani, wakanyofolewa na adui wakiwa tumboni na kufichwa kwenye mashimo; wanasaidiwa na waliotumwa na Mungu kuwarudisha wote walionaswa kwenye mashimo ili wakakamilishe kusudi lao (Isaya 42:22).

Kusudi lazima litimie, haijalishi umeshukia wapi; muda ukifika wa kutimiza kusudi lako Mungu atakuongoza katika njia zake za kukutoa mautini (Zaburi 68:20). Yapo mahesabu ya kimbingu ambayo yanajua mahali fulani kuna hitaji fulani, na hivyo mbingu zimeweka kabisa muda na utimilifu wake. Jambo lililopangwa ili jasusi litumwe, lazima litimie na halitimizwi na aliyetumwa peke yake; Mungu hutuma majasusi wengine kushirikiana naye ili akamilishe. Popote litakaposhushiwa jasusi siyo tatizo kwa maana Bwana atamuongoza katika njia zake mpaka akutane na wenzake wenye nia moja.

Inatupasa tuchambuke; ukichambuka ukajijua na ukalijua kusudi lako utalitenda. Paulo ni mfano wa kuchambuka; kuna wakati aliongea yeye, na kuna wakati aliongea Bwana kupitia yeye (1 Wakorintho 7:12).

Kwenye kutekeleza jukumu haihitaji nguvu nyingi kwa sababu kitu hicho kipo ndani yako. Anayeshuka kutoka mbinguni ni roho, ni mtu kabisa (1 Wakorintho 15:47). Kama tulivyoona awali habari ya “mtu kwa mavumbi ya ardhi” na “mtu nafsi hai”, biblia inatupa maana zaidi kuwa;

1.   “Mtu wa kwanza” ndiyo huyo huyo “mtu kwa mavumbi ya ardhi” ambaye ni mwili, na

2.   “Mtu wa pili” ndiye huyo huyo “mtu nafsi hai” ambaye ni roho.

Mtu wa kwanza ndiye alianza kuumbwa na alipokamilika Mungu akamtoa mtu wa pili / akapuliza pumzi ya uhai kwa mtu wa kwanza. Mtu wa kwanza na mtu wa pili wana miili kabisa na wote hula. Chakula cha mtu wa kwanza kinafahamika, na chakula cha mtu wa pili pia. Mtu wa pili hula chakula cha roho (1Wakorintho 10:4). Wekeza kwa mtu wa pili; mlishe sana kila wakati ili amtawale na kumuongoza mtu wa kwanza, kinyume chake, ukimlisha sana mtu wa kwanza utamdhoofisha mtu wa pili kwa kuwa nia ya mwili ni mauti (Warumi 8:6).

Mfano wa mtu wa kwanza na mtu wa pili ni gari na dereva wa gari; mtu wa kwanza ni gari, na mtu wa pili ni dereva wa gari.

Biblia inafafanua tena kuwa kuna mwili wa asili na mwili wa roho (1 Wakorintho 15:44). Mwili wa asili ni mtu wa kwanza, na mwili wa roho ni mtu wa pili. Mfano wa uwepo wa mwili wa roho ni Yesu alipokufa msalabani na roho yake kwenda mpaka kuzimu kuhubiri na kuchukua funguo za kuzimu.

Mfano mwingine wa uwepo wa mwili wa roho ni wakati wa ujenzi wa mnara wa Babeli; Mungu ni roho (Yohana 4:24) lakini Mungu akiwa kwenye kikao cha mbinguni anasema washuke wakawachafulie usemi (Mwanzo 11:7). Popote walipo wa mwili wa asili, wa roho wanaweza wakafika tena bila kuonekana; watakachokipanga kututenda, tunaouwezo wa kuwafuata kwenye vikao vyao kwa namna ya miili ya roho na hawatuoni ila tupo.

Ibrahimu amekufa miaka mia tisa, badae Yesu akawepo ulimwenguni na kusema alimwona Ibrahimu, jambo lililowashangaza Wayahudi (Yohana 8:57); Yesu alikuwako mbinguni kabla ya Ibrahimu, kwa maana Yesu mwenyewe ndiye Mungu.

Ni desturi ya kushuka mtu, kuanza mwili wa asili kwanza halafu unafuata mwili wa roho. Mariamu anapashwa habari kuwa atachukua mimba kwa uwezo wa Roho Mtakatifu na atamzaa mtoto jina lake Yesu; ilianza mimba, akashuka Mungu mwenyewe. Wakati anashuka, Mamajusi wakamuona. Unaposhushwa unaonekana na wenye macho ya rohoni, kwa hiyo adui anaweza akakuficha ili lile kusudi lisitimie.

Wewe peke yako huwezi kuijua hatima yako; hata waliokuzunguka hawajui. Mungu huweka watu wanaoijua hatima yako. Hata kama wakufiche kwenye ganda la chuma ili usionekane, ganda litapasuka. Unatakiwa ukutane tu na Samweli wako. Usiogope kuanguka kwa maana mwenye haki huanguka na kuinuka tena; asiye haki / mwovu akianguka hainuki (Mithali 24:16, Mika 7:8, Warumi 7:19).

BONYEZA HAPA KUANGALIA IBADA YA JUMAPILI

Post a Comment

0 Comments