UFUFUO NA UZIMA
CATHEDRAL
IBADA YA JUMAPILI 28.06.2026
ASKOFU DKT JOSEPHAT
GWAJIMA
SOMO: AMESIMAMA
KUWA KIKWAZO CHA HATIMA
![]() |
Mungu anachagua watu na kuamua miisho yao kabla hawajazaliwa, kabla hawajafika shule, kabla hawajafika chuo kikuu, kabla hawajaingia kwenye ndoa na kabla miili yao haijazikwa. Kitendo cha Mungu kujua mwisho kabla ya mwanzo kitaalamu hujulikana kama ‘pre-destination’.
Watu hujiuliza, kama Mungu anajua mwisho kabla ya
mwanzo, si angetuwahisha huko mwisho kuliko kutuacha tukihangaika mwanzo na
mambo mengi ya hapa katikati. Matatizo aliyonayo mtu ni njia ya kumpeleka kwenye
hatima yake. Mungu hufanya kazi kwa kufuata utaratibu. Wakati Mungu akiwa
kwenye mchakato wa kumpeleka mtu kwenye hatima yake, huuona uzee wa mtu kabla hajazaliwa;
ukiwa mbishi unashangaza tu
“Nikarudi, na kuona chini ya jua,
ya kwamba si wenye mbio washindao katika michezo, wala si walio hodari
washindao vitani, wala si wenye hekima wapatao chakula, wala si watu wa ufahamu
wapatao mali, wala wenye ustadi wapatao upendeleo; lakini wakati na bahati
huwapata wote.” Mhubiri 9:11.
Kuna vitu mtu amepangiwa na kuna vitu mtu hajapangiwa.
Vile vitu Mungu amempangia mtu, mbele ya macho ya Mungu vilishakamilika;
azuiaye anajisumbua tu. Milima inayomfanya mtu aone mambo hayawezekani, ni
mchakato tu ambao mtu anapitia kuelekea kwenye hatima yake.
Mfano; familia inawezakuwa na watoto wengi waliozaliwa
katika mwili na mama mmoja, lakini tumbo la mama yao haliamui hatima zao; yule
aliyetoka mbinguni (roho) akaingia ndani ya mwili ndiye mwenye hatima. Bidii ya
mtu nayo huwekwa na Mungu ndani ya mtu ili mtu afikie hatima yake. Siku zote
hatima kubwa inakuwa na mzigo mkubwa, na hivyo, moyo wa mtu mwenye hatima kubwa
unakuwa hautulii sehemu moja au kwenye jambo moja.
Katika dunia, kuna watu wanawezakuwa masikini mpaka
siku ya mwisho. Dunia inakadiriwa kuwa na idadi ya watu wasiopungua bilioni
nane, ambapo wamegawanyika kwenye makundi tofauti; kuna matajiri sana, matajiri
wa kawaida, masikini, masikini sana na kuna fukara. Hata ikitokea watu wote
katika dunia, bila kujali hali zao za maisha, wakanyang’anywa kila
wanachomiliki na wakagawiwa hela au mali kwa usawa, baada ya muda fulani aliyekuwa
tajiri atarudi kuwa tajiri na aliyekuwa masikini atarudia umasikini. Hii ni
kwasababu, namna ya kufikiri ya tajiri na namna ya kufikiri ya masikini hutofautiana
sana. Tajiri huwaza kuongezeka, hivyo kufikiria namna ya kukizalisha
alichonacho kiongezeke; masikini huwaza kutumia kile alichonacho, na mara
nyingi mawazo yake hubadilika badilika. Masikini ni mbishi sana, huchelewa
kuanza jambo na ni rahisi kuacha akianza. Mtu mwenye mawazo ya umasikini
(poverty mentality), ukimwambia alete pendekezo (proposal) la biashara ili asaidiwe,
atachelewa tu (roho ya kusita sita).
Maisha ni kama mlango. Mlango hufungwa na
kufunguliwa. Mlango uliowazi leo sio lazima uwe wazi kesho. Mtu anayefikika
leo, sio lazima afikike kesho. Unachokiona mbele yako kikamate maana kuna
wakati utakitafuta hautakipata tena. Wachungaji waliochunga na Daudi kama
wangejua Daudi atakuwa mfalme wa Israeli, wangetamani kuambatana naye mapema
ili wakati wa ufalme wake wawe na nafasi ya kuzungumza naye. Utumie mlango
vizuri uwapo wazi kwa maana ukifungwa hautaweza kuufungua
“Nayajua matendo yako. Tazama,
nimekupa mlango uliofunguliwa mbele yako, ambao hapana awezaye kuufunga, kwa
kuwa unazo nguvu kidogo, nawe umelitunza neno langu, wala hukulikana jina
langu.” Ufunuo 3:8.
Mungu ni mwenye nguvu kuliko wote, aliyeumba dunia
kwa siku sita na siku ya saba akapumzika. Kwa sababu ni mwenye nguvu, tunaamini
angeweza kuumba vitu vyote mara moja maana anayajua yote. Hata hivyo, Mungu ni Mungu
wa utaratibu. Kwa kufanya uumbaji kwa siku sita, Mungu alitaka kutufundisha
kuwa jambo lolote la kufikia hatima, hufanywa hatua kwa hatua, siku kwa siku,
na badae hufikia hatima yenyewe. Ni vyema kuelewa jambo hili japo wapo watu
wasioelewa hata wakieleweshwa
“Na neno la nabii Isaya linatimia kwao,
likisema, Kusikia mtasikia, wala hamtaelewa; Kutazama mtatazama, wala hamtaona.”
Mathayo 13:14.
Kuna mambo yanashangaza. Yesu alizaliwa kwa Wayahudi
ila Wayahudi hawamkubali, na mpaka sasa wanasubiri Kristo azaliwe Bethlehemu
kama iliyotabiriwa na nabii Isaya (Yohana 1:11-12). Unabii wa Yesu
kuzaliwa (Isaya 9:6, Mika 5:2) ulitimia, Yesu akazaliwa
Bethlehemu lakini hakukaa huko; Mariamu alichukua mimba kwa uwezo wa Roho
Mtakatifu huko Nazareti, na kwa sababu ya sensa, Yusufu na Mariamu wakarejea
Bethlehemu ambako Yesu alizaliwa, lakini kwa hofu ya Herode, wakaondoka siku
hiyo hiyo kwenda Misri.
Hata walipotoka Misri, Yesu Kristo alienda Nazareti
na badae akaanza kazi huko Galilaya. Kwa mzunguko huu, Mungu aliamua kuwafunga macho
Wayahudi wasielewe kuwa aliyetabiriwa kuzaliwa Bethlehemu, ndiye huyo Yesu
ambaye yupo hata sasa. Kuna mambo mtu hayaamini hata kama yapo; huko ndiko
kufungwa macho. Mzunguko wote wa Yesu mpaka kufikia hatima yake hapa duniani,
ni mchakato ulioratibiwa na Mungu mwenyewe. Mungu anaweza akachanganya
vitu/mambo ili ampeleke mtu kwenye hatima yake. Sisi tunalindwa na Yesu kwa
imani, ila Wayahudi wanalindwa na silaha za mwili.
Unabii wa Isaya kuwa Yesu atazaliwa ulifanyika miaka
mia saba kabla ya Yesu kuzaliwa. Hata hivyo, ulipotimia wakati, kuna baadhi ya
watu walijua Masihi yupo duniani kama ilivyotabiriwa.
Mfano:
1. Mariamu alitokewa na Malaika
katika ndoto kuwa atachukua mimba kwa uwezo wa Roho Mtakatifu, naye atamzaa
mtoto Yesu. Mariamu, bila kujali aibu atakayopata aliikubali taarifa ya Malaika
ilikufikia hatima na hakuna silaha juu yake ingefanikiwa
“Kila
silaha itakayofanyika juu yako haitafanikiwa na kila ulimi utakaoinuka juu yako
katika hukumu utauhukumu kuwa mkosa. Huu ndio urithi wa watumishi wa BWANA, na
haki yao inayotoka kwangu mimi, asema BWANA.” Isaya 54:17.
2. Yusufu, mchumba wa Mariamu, alipewa
taarifa na Malaika juu ya mimba kwa uwezo wa Roho Mtakatifu, naye akachagua
kutomwaibisha Mariamu kwa kumuacha kwa siri. Malaika akamtokea Yusufu na kumpa
maelekezo asimuache Mariamu mkewe.
3. Mamajusi wa mashariki ya mbali,
kwa kuiona Nyota ya mtoto Yesu, walijua Mfalme wa Wayahudi amezaliwa
Bethlehemu. Hatima ya mtu inaokana sana kwa maadui zake. Adui hujua mtu atakuwa
nani badae ndio maana humshambulia ili kumzuia.
4. Elizabeth aliyekuwa na mimba
kumzaa Yohana Mbatizaji, alipotembelewa na nduguye, Mariamu, akajua kuwa Yesu
Kristo tayari yupo duniani kama ilivyotabiriwa.
5. Wachungaji wa kondeni, jeshi la
Malaika, na mzee Simeoni, wote walijua kuwa Yesu yupo duniani, amezaliwa
Bethlehemu, ila Wayahudi hawakujua.
Hata hivyo Wayahudi wametiwa upofu ili Yesu aenee
kwa mataifa mengine; wao siyo wakristo na wanamsubiri Kristo azaliwe. Wayahudi
wamefumbwa macho wasimtambue Kristo (Luka 24:16). Waliofanikiwa kufahamu
kuwa Yesu alizaliwa, baadhi hawakujua baada ya kuzaliwa alienda wapi; Mungu
alifanya hivi ili kumlinda Yesu na hatima yake.
Unawezakuwa na jambo kubwa linalosubiriwa lakini
akili yako ikakwambia siyo wewe mwenye hilo jambo (unajidharau). Mungu ana desturi
ya kufanya kazi kwenye hali ya kawaida kawaida na kutumia watu wa kawaida.
Hatima inapokaribia, hatari huongezeka. Daudi mwana
wa Yese, aliyepakwa mafuta na nabii Samweli, alipata wasiwasi wa kuuliwa na
Sauli kwa sababu Sauli alikuwa akimkimbiza mara kwa mara, hivyo asipokimbia,
ipo siku Sauli angemuua. Daudi akajiunga na adui wa Sauli, Akishi, ili kumkabili
Sauli.
“Ndipo Daudi aliposema moyoni
mwake, Siku moja, basi, mimi nitaangamia kwa mkono wa Sauli; hakuna jema zaidi
kwangu kuliko kukimbia mpaka nchi ya Wafilisti; naye Sauli atakata tamaa kwa
habari yangu, asinitafute tena mipakani mwote mwa Israeli; hivyo nitaokoka
katika mikono yake. Basi Daudi akaondoka, yeye na hao watu mia sita
aliokuwa nao, akamvukia Akishi, mwana wa Maoki, mfalme wa Gathi.” 1 samweli 27:1
Mungu anapompa mtu hatima, humpa na watu wa
kumfikisha mtu huyo kwenye hatima hiyo. Yampasa mtu awajue watu ambao ni wa
hatima yake. Kuna watu wanaweza kukushauri kwa nia nzuri ila kumbe shetani
anaweza kutumia njia hiyo kukuzuia usiende kwenye hatima yako.
“angu wakati huo Yesu alianza
kuwaonya wanafunzi wake ya kwamba imempasa kwenda Yerusalemu, na kupata mateso
mengi kwa wazee na wakuu wa makuhani, na waandishi, na kuuawa, na siku ya tatu
kufufuka. Petro akamchukua, akaanza kumkemea, akisema, Hasha, Bwana, hayo
hayatakupata. Akageuka, akamwambia Petro, Nenda nyuma yangu, Shetani; u
kikwazo kwangu; maana huyawazi yaliyo ya Mungu, bali ya wanadamu.” Mathayo
16:21-23
Ukiwa unaelekea kwenye hatima yako, yakupasa uwe
makini na kujua watu ambao Mungu amekuinulia; usijitenge na watu uliopewa na
Mungu. Usipomjua Mungu kwa neno basi jitahidi umjue Mungu kwa uumbaji wake. Jifunze
kanuni ya kipaumbele (law of priority). Mfano; moyo hutia mwili uhai kupitia
kusukuma damu kwenye mwili. Kupitia kanuni ya kipaumbele, kabla moyo
haujasukuma damu kwenda kwenye viungo vingine, hujipa damu kwanza wenyewe,
halafu huvipa damu viungo vingine vyenye umuhimu mkubwa kwenye mwili kama
ubongo, figo, ini, na badae husukuma damu kwenye viungo vingine.
Mungu hupanga watu ambao huwajui ili ufikie hatima
yako. Wajue watu muhimu kwenye maisha yako, kama moyo ujuavyo viungo muhimu vya
kupewa damu kwa haraka. Hatima ya mtu ilishaamuriwa. Mabonde na milima
anayopitia mtu ni mchakato tu kuelekea kwenye hatima. Kuna watu watajaribu
kuizuia hatima ya mtu kwa namna mbalimbali, lakini neno linatufundisha kuwa
watashindana na hawatashinda
“Kila silaha itakayofanyika juu
yako haitafanikiwa na kila ulimi utakaoinuka juu yako katika hukumu utauhukumu
kuwa mkosa. Huu ndio urithi wa watumishi wa BWANA, na haki yao inayotoka kwangu
mimi, asema BWANA.” Yeremia 20:11.


0 Comments